WALIOBAKWA na kisha kuozwa waume katika wilaya ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba, wamesema ndoa za ‘mkeka’, zinachangia kwa kiasi kikubwa kasi ubakaji katika jamii.
Walisema jamii
imekuwa na uharaka wa kuwafungisha ndoa mabinti zao wanapobaini kuwa na uhusiano
na wanaume, wakidhani kuwa ndio sulhu ya kutokomeza matendo hayo, lakini badala
yake wamekuwa wakichangia kuendelea.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi katika utafiti maalum wa kuangalia hali ya kupungua
kwa matendo ya ubakaji katika shehia sita wilayani humo, waathirika wa matendo
hayo walisema ndoa za papo kwa hapo sio suluhisho.
Walisema jamii
imekuwa na kawaida kuharakia sulhu ya ndoa hata kama shauri hilo
limeshafikishwa katika vyombo vya sheria, jambo ambalo huwapa jeuri na kiburi
wabakaji kuendelea na matendo hayo.
Mmoja kati ya
waathirika wa ubakaji na kisha kuolewa mwenye miaka (17), mkaazi wa shehia ya
Mchanga Mdogo wilayani humo, alisema binafsi baada ya kujihisi ameshapewa
ujauzito, alikimbilia kituo cha polisi na kisha muhusika kukamatwa.
Alisema awali,
alimueleza mpenzi wake kwamba ameshapata ujauzito na alipokataa, ndipo wazazi
wake walipokimbilia kituo cha polisi Wete, ingawa kesi hiyo haikufikishwa
mahakamani baada ya kufanyiwa suluhu.
‘’Mimi nilitaka kesi hiyo ifikishwe mahakamani, lakini
mama na kaka waling’ang’ania niolewe na kweli niliolewa, ingawa ndoa
yangu ilidumu kwa siku 18 tu na kuachwa,’’alisema.
Nae muathirika
mwengine wa matendo hayo, mkaazi wa shehia ya Mchangamdogo (18), ambae
alikatisha masomo alisema, mara baada ya kubainika na wazazi wake kwamba ana
ujauzito, harakati za kuolewa zilianza.
Alisema
aliwekewa mkazo na wazazi wake na hata baadhi ya marafiki, kwamba ni vyema
akakubali kuolewa na baada ya kujkifungua aliachwa.
Wazazi wa
vijana hao wa kike walikiri kufanya hivyo kutokana na kuogopa usumbufu katika
vyombo vya sheria na kisha kesi zao kutofikia pahala pazuri.
“Unaweza kuzifikisha mahakamani kesi hizo, lakini
kutokana na taratibu za ushahidi zilivyo, baadae unaweza kuwaona wabakaji wako
nje na sisi kuachiwa watoto wanaokosa matunzo,” alisema mzazi
mmoja wa waathirika hao.
Aidha mzazi
huyo alisema, wakati mwengine hulazimika kuwaozesha watoto wao kutokana na
kuvunjika kwa ndoa na baba kumuachia mama ulezi peke yake.
Kwa upande
wake Mratibu wa wanawake na watoto wa shehia hiyo, Mbeu Makame Bakari, alisema
chanzo cha matendo hayo ni kwa wakosaji kukosa kutiwa adabu inayofaa.
Alieleza kuwa
hata kama vyombo vya sheria vitafikishiwa makosa ya aina hiyo wamekuwa
wakiwashawishi wahusika kufanyiana sulhu ikiwa ni pamoja na kuwafungisha ndoa.
Alibainisha
kuwa, ili matendo hayo yaondoke ni vyema elimu kwa jamii ikaongezwa pamoja na
sheria za ubakaji kutumika ipasavyo.
Sheha wa
shehia ya Kinyikani wilaya ya Wete, Mussa Rashid Said alisema chanzo cha
matendo hayo ni kuondoka kwa malezi ya pamoja ambayo yalikuwa katika miaka ya
iliopita.
Alifafanua
kuwa, malezi ya pamoja yaliokuwa yakiambatana na adhabu hadharani yalisaidia
kwa kiasi kikubwa kwa vijana kuwa na nidhamu.
Mzazi katika
shehia ya hiyo, Said Khalifan Ali, alieleza kwa wakati umefika kwa ndoa za
mkeka kupigwa marufuku, kwani zimekuwa zikiwapa mbinu vijana wa kike na kiume
kufanya matendo hayo.
Nae Mratibu wa
wanawake na watoto wa shehia ya Mjini ole, Khadija Henop alisema, bado jamii
haijaona hilo kuwa ni tatizo.
Nae sheha wa
shehia ya Kangagani, Faki Omar Yussuf, alisema matendo hayo yanaweza kukoma,
pindi sheria ya kuwalinda watoto wa kike na matendo hayo itatumika.
Mwanafunzi wa
kidato cha pili skuli ya sekondari ya Kangagani, Rehema Juma Shaame (18),
alisema watoto wa kike wamekuwa wakibakwa kutokana na baadhi yao kujengwa na
tamaa ya maisha.
Afisa Elimu na
Mfunzo ya Amali mkoa wa kaskazini Pemba, Hassan Sheha Ali, alisema chanzo cha
matendo hayo, pia husababishwa na utukutu wa baadhi ya vijana wa kike.
Kwa upande wake
Afisa Ustawi wa Jamii wilayani humo, Haroub Said Hemed, alisema bado jamii
inahitaji elimu kwa umbapana zaidi ya athari ya ubakaji.
Afisa Mkuu wa
seksheni ya wanawake na watoto, Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Wanawake
na Watoto, Pemba Rabia Rashid Omar, alisema kuna mambo kadha yanayochangia
kuzorotesha jitihada za kutokomeza matendo hayo.
No comments:
Post a Comment