Na Said Ameir, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza dhamira ya kweli ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya mfumo wa umoja wa kitaifa ya kuwatumikia wananchi kwa kuimarisha ustawi wao na kuendeleza amani, utulivu na mshikamano. Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Balozi wa Marekani nchini anayemaliza muda wake,Alfonso Lenhardt ambaye alifika Ikulu kumuaga.
“Ningependa kurejea tena dhamira yangu binafsi na ya serikali ninayoiongoza ambayo imo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa kuwa lengo letu ni moja -kuwatumikia wananchi. Hivyo tutaendelea kufanya kazi kwa pamoja kutimiza lengo hilo,” alimueleza Balozi Lenhardt.
Alisema uhusiano kati ya serikali na wananchi wa nchi mbili hizo hizo sio tu kuwa una historia kubwa lakini pia umekuwa wa karibu na mafanikio mengi.
Alimpongeza Balozi Lenhardt kwa jitihada zake binafsi wakati wote alipokuwa nchini katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya serikali na watu wa pande mbili hizo.
“Tumeshuhudia mafanikio mengi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya ushirikiano kati ya nchi zetu. Mafanikio haya ni matokeo ya jitihada za pamoja lakini lazima nieleze kuwa jitihada zako binafsi zilitoa mchango mkubwa katika mafanikio hayo,” alisema.
Alisema katika kipindi cha miaka minne ya utumishi wa Balozi Lenhardt, Tanzania imeshuhudia viongozi wakuu wa Marekani wakitembelea na ziara hizo zilichangiwa na jitihada binafsi za balozi huyo.
Alimueleza Balozi huyo kuwa serikali na wananchi wa Zanzibar wanathamini misaada inayotolewa na serikali na wananchi wa Marekani.
“Tunathamini sana misaada tunayopewa na serikali na watu wa Marekani kwani tunaelewa fika kuwa misaada hiyo inatokana na kodi zinazolipwa na wananchi wa nchi hiyo hivyo ujumbe wetu kwao ni kuwa tutaitumia vizuri ili itoe matokeo mazuri yaliyokusudiwa na kwa muda mrefu,”alisisitiza.
Aidha alisema misaada inayotolewa na watu wa Marekani imesaidia kuchangia maendeleo na ustawi wa watu wa Zanzibar na kuutaja msaada katika sekta ya elimu kuwa unasaidia kujenga mustakbala wa nchi.
“Msaada huu wa elimu kwa watoto na vijana wetu unaiandalia Zanzibar viongozi wake wa baadae na watu wa kuijenga nchi yao, hivyo ni msaada muhimu katika kujenga mustakbala wa nchi yetu,” alisema.
Alimhakikishia Balozi huyo kuwa serikali na wananchi wa Zanzibar watampa kila msaada na ushirikiano Balozi mpya wa nchi hiyo kama ambavyo wamefanya kwake wakati wote wa utumishi wake nchini.
Nae Balozi Lenhardt alisema Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Serikali na watu wa Zanzibar kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana katika miradi inayoshirikiana nayo inakuwa endelevu.
“Tutaendelea kushirikiana ili kuhakikisha kila tunachokifanya kinakuwa endelevu. Hatutaki kuona ugonjwa kama wa malaria baada ya mafanikio makubwa unarudi kama zamani,” alibainisha.
Alielezea kuridhishwa kwake na ushirikiano alioupata kutoka serikali na wananchi wa Zanzibar katika kutekeleza miradi mbalimbali ambayo nchi yake inashirikiana na Zanzibar.
“Nimefurahi kuona kuwa nchi yetu imepewa fursa ya kuchangia maendeleo ya watu wa Zanzibar na naamini tumefanya vizuri, tumeshirikiana katika sekta ya nishati, afya, miundombinu, kilimo na elimu ikiwemo kuzipatia huduma za mtandao skuli za msingi na hata katika kukabiliana na majanga,” alisema.
 

 
 
.jpeg) 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment