Na Mwantanga Ame
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka wafanyabiashara
kuacha kutumia vibaya vibali wanavyopewa kwa kusafirisha biashara mbaya
zinazoitia aibu nchi.
Aliyasema hayo wakati akifungua tamasha la biashara Zanzibar , ikiwa ni sehemu ya kuadhikisha miakia 50 ya
Mapinduzi ya Zanzibar yaliofanyika viwanja vya
Maisara mjini Zanzibar .
Alisema inasikitisha kuona katika siku za hivi karibuni
kumekuwepo taarifa zinazolitia aibu
taifa, kutokana na baadhi ya
wafanyabiashara kutumia vibaya vibali wanavyopewa kwa kusafirisha bidhaa haramu.
Alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la watu kukamatwa ndani
na nje ya nchi wakijihusisha na zisizoruhusiwa kisheria.
“Napenda kutabanaisha
kuwa vitendo hivyo vinavyofanywa na wafanyabiashara wachache vinaathiri
na kuharibu kwa kiasi kikubwa maendeleo ya biashara nchini na kuitia doa nchi
yetu pamoja na kujenga mazingira magumu kwa wafanyabiashara wengine na wananchi
kwa jumla hasa wanaposafiri nje,” alisema.
Alisema vitendo hivyo vinaiharibia sifa nchi hii, kwani
vinaweza kuyafanya mataifa wanayoyatumia kutowaamini pale watapopeleka biashara
zao.
Alisema serikali haiwezi kuacha hali hiyo iendelea na
itahakikisha inavisimamia vyema vyombo vya ulinzi ili kuwakabili watu hao kabla ya hawajaondoka nchini.
Alisema nia ya serikali ni kuona wafanyabiashara wanaopewa
vibali wanafuata taratibu za kisheria pahali popote.
Alisema serikali imeandaa
mazingira mbali mbali ya kufanya biashara, ili kuwawekea unafuu
wananchi, lakini moja ya tatizo kubwa linaloendelea ni kwa baadhi ya watu
kushindwa kuwatendea haki wananchi kutokana na kuwaongezea bei.
Alisema hali hiyo inasababisha kuwapo mfumko wa bei unaojitokeza
mara kwa mara hasa katika mwezi wa Ramadhani, licha ya serikali kupunguza
ushuru kwa baadhi ya bidhaa.
Alisema hali hiyo inachangia kuharibu uhusiano mabaya kati
ya wananchi na serikali yao ,
na ni vyema wafanyabishara wakazingatia maadili mema, uadilifu na sheria
ziliopo.
Akizungumzia hali ya biashara nchini, alisema kumekuwa na
mabadiliko mwaka hadi mwaka, kwani usafirishaji wa bidhaa umeongezeka kutoka
bidhaa zenye thamani ya shilingi 21,177.7 milioni kwa mwaka 2007, na kufikia
shilingi 67,390.5 milioni kwa mwaka 2012 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia
318.2.
Alisema usafirishaji huo, umeongezeka zaidi katika zao la
karafuu na mwani, huku upande wa uagizaji bidhaa zenye thamani ya shilingi
271,273.1 milioni kwa mwaka 2012, kutoka bidhaa zenye thamani ya shilingi
107,689 milioni kwa mwaka 2007 ikiwa ni sawa na asilimia 251.9.
Kutokana na ahali hiyo, alisema ipo haja kwa wazalishaji
wa ndani kujitahidi zaidi kuzalisha bidhaa mbali mbali zikiwemo za viungo ili
kuyafikia masoko ya nje badala ya kuendelea na utaratibu wa sasa wa kuwa
waagiziaji zaidi.
Alisema serikali katika kuandaa mazingira bora ya biashara
tayari imefanya mabadiliko mbali mbali ya sheria ikiwemo ya mwaka 1989 na
sheria ya leseni na kuanzisha mfumo wa
nambari za utambulisho wa bidhaa ambao ni muhimu kwa ushindani wa masoko ambao
tayari unaongezeka duniani.
Alisema kwa vile katika maonyesho hayo kuna ushiriki wa
mataifa mbali mbali duniani ni vyema wananchi walioshiriki kuyatangaza maeneo yao ya biashara.
Alisema kazi kubwa wanayotakiwa kuifanya ni wanawapa
maelezo sahihi washiriki hao ikiwa ni hatua itakayotanua wigo na ushirikiano
huku wakikumbushana wajibu wa
wafanyabiashara kuimarisha uchumi wa nchi.
Alizishukuru baadhi ya nchi zilizojitolea kushiriki
maonesho hayo kwani zitasaidia kuifanya Zanzibar
kujifunza mengi ikiwa na pamoja kuzalisha bidhaa bora.
Nae Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Mhe. Ahmeid
Nassor Mazrui, alisema maonesho hayo yametoa mwamko mkubwa kwa wananchi
kutokana na idadi kubwa ya washiriki wanaojitoleza.
Alisema hapo awali walipanga washiriki wa maonesho hayo watakua
120 lakini hadi jana walifikia 160, wakitoka mataifa mbali mbali duniani
ikiwemo Syria , Kenya ,
Indonesea, Uturuki na Tanzania Bara.
Alisema ushiriki huo umeiwezesha Wizara hiyo, kuona
umuhimu wa kuandaa maonesho hayo kila mwaka, ikiwa ni hatua itayosaidia kukuza masoko
ya wafanyabiashara.
Nae Mkurugenzi TANTRADE, Nd.Jaquiline Maleko, alisema
taasisi yao imeamua kufungua tawi Zanzibar ili kuhakikisha
inawapatia fursa wananchi kuweza kuimudu vyema sekta ya biashara ndani ya nchi
na duniani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara, Nd. Julian Rafael,
alisema maonesho hayo ni sehemu itayokuza utalii na yanapaswa kuendelezwa kama
inavyofanyika katika mataifa mengine duniani ikiwemo Dubai .
Tamasha hilo
la biashara limewashishirikisha viongozi mbali mbali wa Serikali akiwemo Makamu
wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, ambapo Dk. Shein, na viongozi hao
walitembelea na kukagua bidhaa mbali mbali za wafanyabiashara hao.
Maonyesho hayo yanatarajiwa kufungwa Januari 13, mwaka
huu.
No comments:
Post a Comment