Habari za Punde

Wanawake 87 wakeketwa

Na Jumbe Ismailly,Ikungi
LICHA ya kuwepo sheria ya kuzuia vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia hususani ukeketaji kwa wanawake,wilaya ya Ikungi,mkoani Singida imebainika kuwa bado inaendeleza vitendo hivyo ambapo kwa mwaka 2013 pekee wanawake 87 walikeketwa.

Hayo yamebainishwa na Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Ikungi, Dk. Abas Kashindye, katika mjadala kuhusu ushawishi juu ya sheria ya makosa ya kujamiiana ya mwaka 1998 wilayani Ikungi,iliyofanyika mji mdogo wa Ikungi.

Alisema wanawake hao waliokeketwa ni kati ya wanawake 1,317 waliofika kujifungua katika vituo vya afya vya nje na makao makuu ya  wilaya ya Ikungi wakati kwenye kituo cha afya Ikungi pekee wanawake 375 walijifungua.

Alisema kati ya wanawake 375 waliojifungua kituo cha afya Ikungi katika kipindi hicho, 87 waligundulika wamekeketwa,sawa na asilimia 23 na kwamba kati ya hao,55 sawa na asilimia 63 walikuwa na umri kati ya miaka 16 na 20.

Alisema cha kusikitisha mabinti hao walikeketwa wakati sheria ya mwaka 1998 tayari ikiwa inatumika.


Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa semina hiyo iliyoandaliwa na asasi isiyo ya kiserikali ya Singida Inter Africa Committee (SIAC),walisema ni vigumu kuwagundua watu wanaojihusisha na mila hiyo potofu.

Akichangia mada, diwani wa viti maalumu wanawake (CHADEMA),tarafa ya Ikungi,Tedy Daghau, alisema  mwaka 1984 wakati akiwa darasa la kwanza mama yake mzazi alikuwa ngariba.

“Niliona kabisa kwa macho yangu wasichana wakubwa tu wakiwa wanakeketwa,nilijaribu kumwambia mama yangu wakati nikiwa mdogo darasa la kwanza,mama mbona unawanyanyasa hivi watoto wa kike,kwa kweli miaka inayoendelea mama yangu akawa amebadilika akaacha lakini mangariba bado wapo,”alisisitiza.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Ikungi (CHADEMA), Machemba Mjengi, alisema watu wanaoendeleza mila hizo wamekuwa wakifanya vitendo hivyo siri kubwa kutokana na kuogopa sheria zinazosimamia na kukataza vitendo vya ukeketaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.