HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA
BARAZA LA MAPINDUZI, MHE. DK. ALI
MOHAMED SHEIN,
KATIKA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA
MIAKA 50 YA
MAPINDUZI YA ZANZIBAR , UWANJA WA AMAAN
TAREHE 12 JANUARI, 2014
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein Akihutubia sherehe Mapinduzi Amaan.
Mawaziri wa Nchi Rafiki
mliohudhuria hapa leo,
Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ;
Mheshimiwa Dk. Mohamed Gharib
Bilal,
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ;
Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter
Pinda,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif
Hamad,
Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar ;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi,
Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar ;
Mheshimiwa Mzee Ali Hassan Mwinyi,
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ;
Mheshimiwa Benjamin William Mkapa,
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ;
Mheshimiwa Dk. Salmin Amour Juma,
Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi;
Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume, Rais
Mstaafu wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Viongozi Wakuu Wastaafu
Mliohudhuria;
Waheshimiwa Mawaziri
wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ;
Mheshimiwa Mama Anne
Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ;
Mheshimiwa Pandu
Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ;
Mheshimiwa Othman
Chande Mohamed, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ;
Mheshimiwa Omar
Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar ;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi
wa Mashirika ya Kimataifa;
Mheshimiwa Abdalla Mwinyi, Mkuu wa
Mkoa wa Mjini Magharibi;
Waheshimiwa Viongozi wa Serikali na
Vyama vya Siasa;
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Assalaam Alaykum,
Kwa unyenyekevu mkubwa, namshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba
Mbingu na Ardhi na vyote vilivyomo ndani yake, kwa kutujaalia uhai na uzima wa
afya, tukaweza kukusanyika hapa leo kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu
ya Zanzibar , ya
tarehe 12 Januari, 1964. Namuomba Mola wetu aibariki shughuli yetu hii iwe ya
mafanikio.
Kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar ,
natoa shukrani zangu za dhati kwako Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,
Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuungana nasi katika sherehe zetu
hizi adhimu na muhimu. Vile vile natoa shukrani
kwa wageni wetu wote kutoka nje ya nchi yetu akiwemo Mheshimiwa Yoweri Kaguta
Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Dk. Ikililou Dhoinine, Rais wa Muungano
wa Comoro, na Mjumbe Maalum, Waziri wa Makaazi na Maendeleo Miji na Vijiji
Mheshimiwa Jiang Weixin anayemwakilisha Rais Xi Jinping wa Jamhuri ya Watu wa
China. Kadhalika, natoa shukrani kwa
viongozi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, waliopo madarakani na waliostaafu, Mabalozi wa nchi
mbali mbali, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa dini na vyama
vya siasa na wananchi wote kwa kuhudhuria kwa wingi kwenye sherehe hizi.
Kuwepo pamoja nasi wageni wetu mbali mbali kunatupa faraja
kubwa sana . Kuja kwenu kunatudhihirishia kuwa Mapinduzi
yetu yanaheshimika na yanapewa taadhima kubwa ndani na nje ya nchi yetu. Tuna kila sababu ya kujivunia uhusiano wetu
na kuja kwenu ni uthibitisho wa juhudi zetu za pamoja za kuyaenzi Mapinduzi
yetu.
Waheshimiwa
Viongozi na Ndugu Wananchi,
Leo ni siku muhimu sana
katika historia ya wananchi wa Zanzibar ,
ambapo miaka 50 iliyopita walikata minyororo ya utawala wa Kisultani na ukoloni
wa Kiingereza uliodumu kwa miaka 132.
Wananchi walikataa kwa vitendo kudharauliwa, kunyanyaswa, kubaguliwa na kutoheshimiwa
katika nchi yao .
Ukombozi wa watu wa Zanzibar
ulifanywa na Chama cha Afro-Shirazi, ambacho kilianzishwa tarehe 5 Februari,
1957, kwa madhumuni ya kuikomboa Zanzibar
kutokana na madhila ya wakoloni, mabwanyenye na mabepari. Madhila haya walitendewa wananchi kwenye
mambo yote muhimu katika maisha ya binadamu, kama
vile kubaguliwa katika kupata elimu, huduma za matibabu, makaazi, chakula,
ubaguzi kwenye kazi, ubaguzi na dhulma kwenye matumizi ya ardhi, ubaguzi katika
kupata haki, na kadhalika.
Leo tunapoadhimisha sherehe za Mapinduzi kutimiza miaka 50,
hatuna budi kuwakumbuka na kuwashukuru wazee wetu Waasisi wa Chama cha
Afro-Shirazi walioongozwa na Rais wake wa Kwanza ,
Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Tunawakumbuka na tunawashukuru kwa ushujaa wao na jitihada zao za
kupigania haki, kuleta usawa na maelewano na kuondoa kila pingamizi walizokuwa
wakizipata wananchi wa Unguja na Pemba .
Kwa hivyo, leo ni siku ya kumbukumbu ya ushindi wa Chama
cha Afro-Shirazi na ushindi wa wananchi wa Zanzibar na kwamba
Mapinduzi yaliinua na kusimamisha utawala wa wanyonge na yaliweka usawa na
kuwakabidhi tena wafanyakazi na wakulima wa Zanzibar, heshima yao na ubinadamu
wao katika nchi yao.
Namuomba Mwenyezi Mungu amrehemu Jemadari wa Mapinduzi yetu
Matukufu ya tarehe 12 Januari, 1964 Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na
waasisi wengine wa Mapinduzi hayo waliotangulia mbele ya haki na awape umri
mrefu wale wote ambao wapo hai. Siku
zote tutawakumbuka, tutawaenzi na tutawashukuru kwa kujitoa muhanga kwa ajili
ya kutukomboa. Kutokana na jitihada zao na mapenzi kwa nchi yao , hivi sasa tupo huru
na tunasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi yetu na tutaendelea kuwa huru wakati
wote. Hatutokubali kutawaliwa,
kudhulumiwa, kubaguliwa na kudharauliwa katika nchi yetu.
Waheshimiwa
Viongozi na Ndugu Wananchi,
Leo tunafikia kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 50
ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 ni siku ya furaha kubwa na ya
kusherehekea kwa vifijo na hoi hoi kama tulivyokaribishwa katika uwanja huu wa Amaan na
tulivyojionea wenyewe muda mfupi uliopita.
Hata hivyo, sherehe hizi zinatukumbusha umuhimu wa kuendelea kuyalinda,
kuyatetea na kuyadumisha mapinduzi yetu kama tulivyofanya katika kipindi cha miaka 50 iliyopita,
kwa mafanikio makubwa.
Tunaposherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya tarehe 12
Januari, 1964, vile vile tunasherehekea umoja wetu uliotokana na muungano wa
nchi mbili zilizokuwa huru; Jamhuri ya Tanganyika
na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuzaliwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,
tarehe 26 April, 1964. Muungano wetu umetokana na sera sahihi za vyama viasisi
vya TANU na ASP na sasa CCM pamoja na uongozi bora na thabiti wa waasisi wa
nchi yetu Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid
Amani Karume na viongozi wa awamu nyengine waliofuata baadae.
Wakati tunasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi, ni wazi
kwamba tunasherehekea amani, umoja na maendeleo yaliyopatikana. Kwa hivyo, tunapaswa kuuenzi na kuuendeleza
umoja na mshikamano wetu ambao ndio siri kubwa ya kuendelea kuwepo kwa hali ya
amani na utulivu yenye kuimarisha maendeleo yetu.
Kwa msingi huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeiweka kauli mbiu ya maadhimisho
haya isemayo: “Tudumishe amani, umoja na
maendeleo ambayo ni matunda ya Mapinduzi yetu – Mapinduzi Daima”.
Nafarijika sana kuona wananchi wa Zanzibar wameungana na
Serikali yao katika kipindi cha miaka 50 kwa kuyatekeleza madhumuni na malengo
pamoja na shabaha ya Mapinduzi yetu na kupatikana maendeleo ya kisiasa,
kiuchumi na kijamii.
Katika kipindi cha miaka 50, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , imeweza
kuyatekeleza na kuyaendeleza madhumuni, malengo pamoja na shabaha ya
Mapinduzi. Katika kipindi chote hicho, Serikali ilipanga
mipango yake na iliitekeleza kwa mafanikio makubwa. Kwa hivyo, ni wazi kwamba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar
imefanya mambo mengi ya maendeleo kuliko yale yaliyofanywa na wakoloni, kwa
muda wa miaka 132 ya utawala wao.
Maelezo nitakayoyatoa yanadhihirisha ukweli huo.
Waheshimiwa
Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, nchi yetu imepitia
katika mifumo miwili ya kisiasa na
demokrasia kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Mara tu baada ya Mapinduzi ya 1964, nchi yetu ilikuwa na mfumo wa chama
kimoja cha siasa hadi mwaka 1992 uliporejeshwa mfumo wa vyama vingi vya siasa
nchini. Mfumo wa vyama vingi vya siasa
umetanua demokrasia kwa kuwapa fursa wananchi kujiunga na chama chochote cha
siasa na kuchagua viongozi wanaowataka.
Tangu kurejeshwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, jumla ya
chaguzi nne (4) zimeshafanyika ambapo wananchi walikichagua Chama cha Mapinduzi
kuiongoza nchi yetu.
Katika kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa
wananchi, mwaka 2010, Zanzibar ilifanya
mabadiliko ya 10 ya Katiba yake ya mwaka 1984, iliyoviwezesha vyama vya siasa
vyenye uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi kushirikiana katika kuiongoza Zanzibar . Hatua hii iliiwezesha Zanzibar kuunda Serikali yenye Muundo wa
Umoja wa Kitaifa ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuimarisha umoja wetu na
mshikamano na kuchangia katika kuongeza kasi ya maendeleo.
Tunasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi yetu, wakati nchi yetu
ikiwa imepiga hatua kubwa za mafanikio katika kuimarisha suala la Utawala Bora
na Haki za Binaadamu. Zanzibar
ina Katiba yake ya mwaka 1984 iliyoundwa kwa misingi ya kusimamia na kuendeleza
malengo ya Mapinduzi.
Nchi yetu inafuata mfumo wa mgawanyo wa madaraka kati ya Mamlaka tatu; Mamlaka ya
Utendaji (Serikali). Mamlaka ya Kutunga Sheria na Kusimamia Utekelezaji wa
Shughuli za Umma (Baraza la Wawakilishi) na Mamlaka ya Kutekeleza Utoaji Haki
(Mahakama). Mfumo wa aina hii haukuwepo
kabla ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964.
Baraza la Wawakilishi liliundwa mwaka 1980 na Tume ya
Uchaguzi ilianzishwa mwaka 1993 kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Taasisi hizi zinatekeleza vyema majukumu yao na kupelekea wananchi
kutumia haki zao za kidemokrasia kwa mujibu wa sheria. Katika kusimamia suala la kupambana na
rushwa na uhujumu uchumi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Mamlaka ya Kuzuia Rushwa
na Uhujumu Uchumi katika mwaka 2012 na imeanza kazi zake vizuri.
Tunapotathmini suala la Utawala Bora, katika kipindi hiki
cha miaka 50 ya Mapinduzi ni dhahiri kwamba mafanikio makubwa yamepatikana
kwenye Mahakama zetu kwa kuwa na Mahakimu na Majaji wengi zaidi ambao wote ni
wananchi na wameendelea kutoa hukumu kwa kuzingatia misingi ya haki. Aidha, ndani ya kipindi hiki sheria kadhaa
zimepitiwa na kurekebishwa na nyengine mpya zimetungwa zikiwemo za kulinda haki
za watoto na kuanzishwa kwa Mahakama ya Watoto mwaka 2012. Zaidi ya hayo, wananchi wanaelimishwa kwa
njia mbali mbali ili kuelewa umuhimu wa kutii sheria, kujiepusha na vitendo
visivyofaa katika jamii na kuishi kwa uadilifu.
Katika kipindi cha miaka 50 ya Mapinduzi, Serikali imechukua
juhudi za kuimarisha uchumi wa nchi yetu.
Mafanikio makubwa yamepatikana katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali
ambapo kwa wastani yameongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mwaka wa fedha 2012/2013 mapato
yalifikia TShs. bilioni 266.2 kutoka
TShs. milioni 59.67 mwaka 1964/1965.
Vile vile, uchumi wetu umekuwa ukikua kila mwaka na kwa
mwaka 2012/2013 umefikia asilimia 7.0 na kwa mwaka 2013/2014 unatarajiwa kukua
kwa asilimia 7.5. Pato la Taifa limekuwa
likiongezeka kutoka thamani ya TShs. bilioni 16.6 mwaka 1990 na kufikia thamani
ya TShs. bilioni 1,352 kwa mwaka 2012.
Kadhalika, pato la mtu binafsi nalo limekuwa likiongezeka
kutoka TShs. 726,000 (US$462) mwaka 2010 na kufikia TShs. 1,003,000 (US$ 656) mwaka 2012, kiwango ambacho
kimevuka maelekezo ya Ilani ya CCM ya 2010-2015 ya kufikia TShs. 884,000
ifikapo mwaka 2015.
Mfumko wa bei umeendelea kudhibitiwa na hadi Disemba, 2013
umefikia asilimia 5.0 kutoka asilimia 9.4 mwaka 2012.
Tunaposherehekea miaka 50 ya Mapinduzi, vile vile,
tunajivunia kuimarika kwa sekta ya fedha.
Hivi sasa idadi ya benki za biashara imefikia 10 kutoka benki mbili (2)
zilizokuwepo kabla ya Mapinduzi.
Kuhusu Mipango ya Maendeleo, kabla ya Mapinduzi hapakuwepo
mipango ya aina hiyo iliyokuwa rasmi.
Katika kuimarisha Mipango ya Maendeleo Tume ya Mipango ya kwanza
iliundwa 1977 ambapo Mpango wa Maendeleo wa miaka mitatu 1978/79 – 1980/1981,
uliandaliwa.
Utaratibu wa kuwa na Tume ya Mipango umeendelea hadi hivi
sasa. Katika mwaka 2000 Dira ya
Maendeleo ya Zanzibar 2020 ilizinduliwa na utekelezaji wake ulianza. Mpango wa kwanza wa utekelezaji wa Dira
ulikuwa ni Mpango wa Kupunguza Umasikini uliotekelezwa mwaka 2002 hadi
2005. Mpango huo ulifuatiwa na Mpango wa
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA I) mwaka 2007/2010 na baadae (MKUZA
II) 2010/2015.
Mipango yote hii inalenga katika kuimarisha uchumi na
kupunguza umasikini wa kipato, kuimarisha huduma na ustawi wa jamii pamoja na
kuimarisha utawala bora na Umoja wa Kitaifa, ambapo utekelezaji wake umeleta
mafanikio makubwa.
Dhamira ya kuimarisha maisha ya wananchi wa Zanzibar iko
wazi na lengo la Dira 2020 liko pale
pale ili nchi yetu iwe katika uchumi wa kiwango cha kati. Tutaendelea kufanya kila jitihada ili uchumi
uweze kukua kwa asilimia 8-10, ifikapo mwaka 2020. Lengo hili litaweza kufanikiwa ingawa uchumi
wetu unakabiliwa na changamoto nyingi.
Sekta ya biashara ni miongoni mwa sekta muhimu katika
maendeleo ya ukuaji uchumi hasa ikizingatiwa kuwa nchi yetu ni kisiwa chenye
eneo dogo kwa kuendeleza kilimo na mambo mengine yanayohitaji ardhi kubwa. Kwa kuzingatia umuhimu huo, mara baada ya
Mapinduzi hadi leo hatua mbali mbali zimechukuliwa ili kuimarisha mazingira ya
ufanyaji wa biashara.
Kwa hivyo, mwaka 1963, Serikali ya kikoloni iliendeleza
utaratibu wa kusafirisha bidhaa na kununua bidhaa, bidhaa zenye thamani ya
TShs. milioni 117.960 zilisafirishwa na bidhaa zenye thamani ya TShs. milioni 122.920
ziliingizwa nchini.
Biashara ya usafirishaji na uingizaji wa bidhaa imeweza
kuimarika ambapo usafirishaji hasa wa karafuu na mwani umeongezeka kutoka TShs.
milioni 17,907 mwaka 2010 hadi TShs. milioni 67,390.5 mwaka 2012, ongezeko la
asilimia 276.3. Bidhaa zenye thamani ya
TShs. milioni 271,273.1 zimeagizwa, mwaka 2012 kutoka TShs. milioni
129,137 mwaka 2010. Biashara hii
imefanyika kutokana na mazingira mazuri yaliyopo.
Serikali inaendelea kusimamia biashara ya karafuu kupitia
Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) lililoanzishwa mwaka 1966, na
biashara hio inaendelea vizuri. Wakulima
wa karafuu wanalipwa asilimia thamanini (80) ya bei ya soko na ununuzi
unaendelea vizuri, ambapo bei ya kilo moja inanunuliwa na ZSTC kutoka kwa
wakulima, kwa TShs. 14,000, hivi sasa, bei hii ni kubwa kuliko miaka iliyopita.
Kwa mfano, mwaka 2008 ilikuwa TShs. 2,500 kwa kilo. Serikali inafanya jitihada
ya kuliimarisha zao la karafuu kwa kuzifanyia karafuu za Zanzibar utambulisho
maalum (branding). Hatua nzuri
zimefikiwa katika utekelezaji wa mpango huu.
Serikali imeandaa sera ya maendeleo ya viwanda ambapo
umiliki na uendeshaji wa viwanda kupitia sekta binafsi umehamasishwa na
umeimarishwa na viwanda kadhaa vimeanzishwa na tayari sera hio imeanza kutekelezwa. Eneo Maalum la Uwekezaji (EPZ) lililotengwa
na Serikali huko Fumba limeanza kutumika na kiwanda kikubwa cha maziwa kimejengwa
na mwekezaji wa ndani na wawekezaji wengine wameonesha nia ya kuwekeza.
Ndugu Viongozi na
Ndugu Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi huduma za utalii hazikuwa katika msimamo
madhubuti na zilifanywa na watu wachache ambao hawakujali uhusiano baina ya
watalii na wananchi wa Zanzibar. Shabaha
yao ilikuwa ni kuingiza fedha mikononi mwao tu.
Katika jitihada za kuimarisha huduma za utalii, Serikali
ilijenga hoteli mpya tano (5), Unguja na Pemba na ililiimarisha Shirika la
Utalii kwa kupewa nyenzo, vifaa na wafanyakazi.
Idadi ya watalii waliokuja Zanzibar mwaka 1986 ilikuwa 29,211 na
iliongezeka hadi kufikia watalii 143,282 mwaka 2007. Idadi hii ni ongezeko la takriban mara 5. Kwa mwaka 2012, idadi ya watalii iliongezeka
na ilifikia 169,223 na mwaka 2013 idadi ya watalii iliongezeka na kufikia watalii 181,242. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 7.10.
Asilimia 72 ya Wawekezaji wote wanawekeza katika sekta ya utalii hapa
Zanzibar na hivi sasa zipo hoteli zenye vyumba 7995 na kati ya hoteli hizo, 26
ni za nyota tano. Sekta ya utalii ni
sekta kiongozi kutokana na MKUZA II, inakuwa kwa asilimia 6 na inachangia Pato
la Taifa kwa asilimia 27 na Serikali inapata asilimia 80 ya fedha za kigeni
kutokana na utalii. Serikali inaendelea
kuwashajiisha wawekezaji na imeweka mipango madhubuti ya kuongeza watalii
ili ifikapo 2015 idadi ya watalii ifikie
500,000.
Kabla ya Mapinduzi elimu ilikuwa ikitolewa kwa ubaguzi na
ilikuwa ya kulipia. Watoto wa wananchi
waliowengi, ambao ni maskini hawakuwa na uwezo wa kupata elimu. Baada ya Mapinduzi, tarehe 23 Septemba, 1964,
Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, alitangaza rasmi elimu kutolewa bure; bila ya
malipo na bila ya ubaguzi wowote kwa wanafunzi
wa Unguja na Pemba.
Yalipofanyika Mapinduzi, tarehe 12 Januari, 1964, wakoloni
walituachia skuli mbili tu za Maandalizi (Nursery) na hivi sasa zipo skuli 278
zenye wanafunzi 30,912. Kwa upande wa
skuli za msingi zilikuwepo skuli 62 tu
zilizokuwa na wanafunzi 19,106 kwa Unguja na Pemba. Hivi sasa, zipo skuli za msingi 342 zenye
wanafunzi 247,353.
Kuhusu elimu ya sekondari, hivi sasa zipo skuli za
sekondari 252 zenye wanafunzi 84,096 ikilinganishwa na skuli za sekondari za
Serikali nne (4), zilizokuwa na wanafunzi 734 hadi mwaka 1963.
Kwa upande wa mafunzo ya Amali, ilikuwepo skuli moja
tu. Hivi sasa zipo skuli tano (5) zenye wanafunzi 1,125.
Leo tunaposherehekea miaka 50 ya Mapinduzi, Zanzibar inavyo
vyuo tisa (9) vya masomo mbali mbali (colleges) na kabla ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari,
1964, Zanzibar ilikuwa na chuo kimoja tu cha ualimu (Teacher Training
College). Hivi sasa, Zanzibar ina vyuo
vikuu vitatu navyo ni, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Chuo Kikuu cha
Zanzibar na Chuo cha Elimu Chukwani na
kwa mwaka huu wa masomo vyuo hivi vina jumla ya wanafunzi 4485. Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kimeanzisha
skuli mbali mbali, na Septemba, 2013 ilianzishwa skuli ya masomo ya udaktari (school of
medicine) yenye jumla ya wanafunzi 33.
Lengo la mpango huu ni kujitosheleza kwa madaktari, mbali na mpango
maalum uliopo sasa wa masomo ya udaktari yanayoendeshwa kwa kushirikiana na
Serikali ya Cuba.
Ni dhahiri kwamba, Serikali ya Mapinduzi imefanya kazi
kubwa ya kuimarisha elimu na katika kuwasomesha, kuwaandaa na kuwaendeleza
watalaamu wake kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar, jambo ambalo halikufanyika
katika miaka yote ya utawala wa kikoloni.
Ingawa zipo changamoto mbali mbali zinazotokana na kuimarika kwa elimu,
hata hivyo, Serikali imeandaa mipango mbali mbali ya kuzipatia ufumbuzi
changamoto hizo.
Ndugu Viongozi na
Ndugu Wananchi,
Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Serikali ilifanya
juhudi kubwa na za makusudi za kuzipanua huduma za afya ambazo zikitolewa kwa
ubaguzi na hazikutosheleza mahitaji ya wananchi. Mwaka 1965 ilitangazwa rasmi kwamba
huduma za afya zitatolewa bure. Mipango madhubuti ya kuziendeleza huduma za
kinga na tiba iliandaliwa kutokana na Mpango wa Mwanzo wa Afya wa mwaka 1965 na
Sera ya Afya ya 1999, ambapo ulifanywa uamuzi wa kuzipeleka huduma za afya
karibu na wanakoishi wananchi, kuongeza
upatikanaji wa vifaa, nyenzo na dawa, mafunzo ya wataalamu mbali mbali wa afya,
ujenzi wa hospitali na vituo vya afya.
Hivi sasa huduma za afya zinatolewa katika hospitali
tofauti 12 badala ya hospitali 5 na vituo vya afya 134 badala ya 36 kabla ya
Mapinduzi. Vile vile huduma zinatolewa
na hospitali za vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Idara Maalum za SMZ,
taasisi za Watu Binafsi, mpango ambao kabla ya Mapinduzi haukuwepo.
Kuwepo kwa vituo vingi vya afya kunatoa nafasi kwa
mwananchi kupata huduma za afya kwa kwenda chini ya kilomita tano. Zaidi ya asilimia 95 ya wananchi wanaishi
ndani ya mzunguko wa kilomita 5 za huduma za afya.
Katika jitihada za kuwasomesha wataalamu wake, Serikali inatoa
mafunzo katika fani mbali mbali za afya katika kiwango cha Stashahada na hivi karibuni
chuo hiki kitaunganishwa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Uwezo wetu umeimarika sana wa kupambana na maradhi ya
kuambukiza na yasiyoyakuambukiza kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani na
Washirika wetu wa Maendeleo. Hivi sasa
uwiano wa daktari kwa idadi ya watu ni 1:18,982. Hata hivyo, mnamo mwezi wa
Agosti mwaka huu Serikali inatarajia kuwaajiri madaktari 38 watakaomaliza
masomo yao yanayoendeshwa na Chuo cha Madaktari cha Mathansas, Cuba, kwa
kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, madaktari wengine 12 watakaomaliza
masomo yao mwaka ujao katika utaratibu huo pamoja na wale wanaomaliza masomo
yao katika vyuo vya udaktari vya Tanzania Bara na viliopo nchi za nje,
wataajiriwa. Kwa hivyo, katika miaka
michache ijayo, tatizo la upungufu wa madaktari litapungua sana.
Kadhalika, jitihada zetu za kupambana na maradhi ya Malaria
zimefanikiwa sana kwa kushirikiana na Taasisi mbali mbali duniani. Kiwango cha malaria na kasi ya kuenea kwake
kimepungua na kimefikia asilimia 0.3
ikilinganishwa na asilimia 45 miaka ya tisini na asilimia 12 mwaka 2005.
Mipango madhubuti imeandaliwa ili mafanikio haya yaliyopatikana yawe endelevu
na kiwango chake kiendelee kupungua. Jitihada zetu za kupambana na UKIMWI
zimepata mafanikio ya kuridhisha na wanaoishi na virusi vya UKIMWI ambao
wanatumia ARVs afya zao zimeimarika.
Jitihada hizi zinaendelezwa kwa kushirikiana na washirika wetu wa
maendeleo.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji safi na
salama, mara baada ya Mapinduzi, Serikali ilitilia mkazo katika kuimarisha
sekta ya maji. Katika mwaka 1964, hali
ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama kote nchini ilikuwa ni asilimia
27 tu. Upatikanaji wa huduma hizi za
maji ni muhimu kwa maisha ya watu na umefikia wastani wa asilimia 76 kwa
wananchi wa mjini hadi mwaka 2010 na asilimia 60 vijijini. Jitihada mbali mbali za kuimarisha huduma
hizo zinaendelea kuchukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na Washirika wetu wa
Maendeleo ili upatikanaji wa huduma za maji ufikie asilimia 95 mjini na
asilimia 80, kwa vijijini ifikapo mwaka 2015 kwa kuzingatia Ilani ya CCM ya
Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010-2015 na MKUZA II.
Serikali imechukua mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya
Afrika kwa lengo la kuimarisha huduma za maji katika mji wa Wete, Chake Chake
na Mkoani kwa upande wa Pemba na Wilaya
ya Kati kwa upande wa Unguja na vijiji
kadhaa viliomo katika Wilaya hizo vitafaidika na mradi huo. Hadi sasa visima vyote vimeshachimbwa,
mabomba yamelazwa na yamefungwa na matangi ya maji yamejengwa na uchunguzi wa
maji umefanyika katika miji yote mitatu ya Pemba. Kadhalika, Serikali ya Ras Al Khaimah imetoa
msaada kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uchimbaji wa visima 50
kwenye maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.
Visima hivyo tayari vimeanza kuchimbwa katika maeneo mbali mbali na kazi
inaendelea vizuri. Jitihada za
kuimarisha huduma za maji kwa Mkoa wa Mjini Magharibi nazo zinaendelea vizuri
kwa kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa JICA, mkopo kutoka Benki ya Maendeleo
ya Afrika na visima 21 vitachimbwa kwa msaada wa Serikali ya Ras Al Khaimah. Jitihada hizi ambazo Serikali imezichukua
zina lengo la kupunguza tatizo la maji Unguja na Pemba kwa madhumuni ya
kutekeleza malengo ya Mapinduzi ya 12 Januari, 1964 ya kuwapatia wananchi
huduma za maji safi na salama. Serikali
inawaomba wananchi waendelee kuwa na subira wakati jitihada zinafanywa za
kulipunguza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama na baadae liondoshwe
kabisa.
Kabla ya Mapinduzi, ardhi ilimilikiwa na wakoloni na watu
waliokuwa na uwezo, wanyonge wa Zanzibar
hawakupewa nafasi ya kuitumia ardhi yao iliyochukuliwa kutokana na unyonge na
umasikini wao. Tarehe 8 Machi, 1964,
Marehemu Mzee Abeid Amani Karume alitangaza rasmi kwamba ardhi yote ni mali ya
Serikali na iligaiwa kwa wananchi wote bila ya kujali rangi, dini wala
kabila. Vile vile, tarehe 11 Novemba,
1965 aliuzindua mpango wa kugawa ardhi na aliwagawia wananchi eka tatu tatu
hapo Dole. Hadi mwaka 1973, jumla ya eka
24,000 ziligaiwa kwa wananchi wa Unguja na Pemba na ugawaji huo uliendelezwa
katika kipindi cha miaka 50.
Wakati tunasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi, ni jambo la
fakhari kuona kwamba wananchi wanaitumia vizuri ardhi waliyopewa kwa kuendeshea
maisha yao. Katika kipindi hiki, sheria
mbali mbali zinazosimamia ardhi zimetungwa pamoja na sera ya Ardhi na Mahkama
ya Ardhi imeanzishwa kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi.
Kuhusu matumizi endelevu ya ardhi, Idara ya Mipango Miji na
Vijiji imeanzishwa na Mpango Mkuu wa Matumizi ya Ardhi wa Zanzibar wa 2013
umetayarishwa. Kadhalika, katika kipindi
hiki, Serikali imewapimia wananchi viwanja katika maeneo mbali mbali Unguja na
Pemba, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na uwekezaji na katika mwaka 2010-2013 peke yake viwanja
1393 vilitolewa.
Waheshimiwa
Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi Matukufu wanyonge hawakuwa na uwezo wa
kuishi kwenye nyumba bora. Baada ya Mapinduzi, Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar iliamua kuwajengea wananchi makaazi bora ya kisasa bila ya ubaguzi wowote.
Katika azma ya kuwajengea wananchi nyumba bora na za
kisasa, ujenzi wa nyumba za kisasa za ghorofa ulianzishwa na Marehemu Mzee
Abeid Amani Karume tarehe 11 Agosti, 1964. Ujenzi huo ulianza Kikwajuni, baadae
Kilimani, Michenzani na Mombasa. Aidha, nyumba kama hizo zilijengwa huko Pemba
katika mji wa Wete, Micheweni, Chake Chake, Mkoani na Kengeja. Kadhalika, nyumba hizo za maendeleo
zilijengwa Makunduchi, Bambi na Chaani.
Jumla ya fleti 2928 zilijengwa na kupewa wananchi. Baadae ujenzi wa
nyumba za vijijini ulianzishwa katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba.
Kutokana na kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar, wananchi
wengi wamepata uwezo wa kujenga nyumba zao wenyewe. Hivi sasa wananchi wanajenga nyumba bora na
nzuri kuliko wakati wowote wa miaka iliyopita.
Katika kuendeleza malengo ya Mapinduzi ya kuwapatia wananchi
makaazi bora, Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itaanzisha Shirika la Nyumba hivi karibuni ambalo litakuwa linasimamia
ujenzi na upatikanaji wa makaazi bora na ya kisasa kwa wananchi wa Zanzibar
zitakazojengwa kwa ushirikiano na taasisi za watu binafsi na kuuzwa kwa
wananchi kwa bei nafuu.
Ndugu Viongozi na
Ndugu Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi, wakoloni walitumia ardhi, zaidi kwa
kilimo cha mazao ya biashara ya karafuu na nazi kwa lengo la kusafirisha
nje. Uzalishaji wa mazao ya chakula kama
vile mpunga na matunda kwa ajili ya mahitaji ya ndani hayakupewa umuhimu
mkubwa.
Baada ya Mapinduzi, Serikali ilikiimarisha kilimo kwa
kuanzisha mashamba ya mpunga na mazao mengine na juhudi hizo zililenga katika
kupunguza uagiziaji wa vyakula muhimu vinavyohitajiwa na wananchi kutoka nje ya
nchi.
Waheshimiwa
Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kuimarisha kilimo, mara tu baada ya Mapinduzi,
Serikali iliagiza matrekta kwa madhumuni ya kuwafanya wananchi
waache kutumia jembe la mkono katika
kilimo cha mpunga. Sambamba na kununua
matrekta, kilianzishwa kiwanda cha kutengenezea matrekta huko Mbweni kwa lengo
la kuyahudumia matrekta hayo. Vile
vile, wakulima walisaidiwa pembejeo za
kilimo ambazo zilisaidia sana kuliimarisha shamba la Cheju na Upenja.
Jitihada za kutekeleza mapinduzi ya kilimo zilizoanzishwa
hivi karibuni zimefanikiwa kwa kuagiza matrekta mapya na zana nyengine za
kilimo, kutoa ruzuku katika pembejeo mbali mbali za kilimo cha mpunga kwa
asilimia 75 na kuongeza kiwango cha mbolea kutoka tani 30 hadi 1500. Dawa za kuulia magugu, kiwango chake
kimeongezeka kutoka lita 12,000 hadi kufikia lita 30,000 katika mwaka
2010-2013. Kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji, katika mabonde mbali mbali
kinaendelezwa na hekta 720 zimeshatayarishwa kati ya hekta 8,521
zilizotengwa. Taasisi ya utafiti wa
kilimo Kizimbani imeimarishwa kwa nyenzo, vifaa na wataalamu na Maabara mpya
imezinduliwa katika sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi.
Chuo cha Kilimo cha Kizimbani nacho kimeimarishwa na
mafunzo ya Stashahada ya Kilimo yameanza kutolewa. Mafunzo kwa skuli za wakulima mashambani
yameendelezwa na skuli za wakulima zenye kuhudumia kaya 24,000 zimeanzishwa.
Ndugu Viongozi na
Ndugu Wananchi,
Katika kuimarisha zao la karafuu ambalo lina mchango mkubwa
kwenye uchumi wetu, Serikali imechukua juhudi za kuliendeleza zao hili na
imeongeza uzalishaji wa miche kutoka 500,000 mwaka 2012 na kuongeza kiwango cha
miche hadi kufikia miche 1,000,000 kwa mwaka 2013/14 ambayo inatolewa kwa
wakulima bure. Lengo la Serikali ni
kutoa miche milioni moja kwa kila mwaka katika miaka mitatu ijayo. Katika
kutekeleza Mapinduzi ya Kilimo, Serikali inaimarisha mazao ya chakula, matunda
na mazao ya viungo mbali mbali kwa ajili ya biashara. Serikali inawapongeza wakulima wote kwa
jitihada zao za kuimarisha kilimo na kuhakikisha kwamba wakati wote tunakuwanacho
chakula cha kutosha. Kwa wakulima wa
karafuu tunawapongeza kwa kuuza karafuu zao ZSTC. Takwimu za mauzo zinadhihirisha uamuzi
wao. Hongereni sana. Kadhalika pokeeni pongezi za Serikali kwa
kutuunga mkono kwenye mapambano yetu dhidi ya wafanya magendo ya karafuu.
Ndugu Viongozi na
Ndugu Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi huduma za ufugaji hazikuendelezwa sana
na hata mifugo haikuwepo ya kutosha na ilibidi iagiziwe kutoka nchi za nje.
Baada ya Mapinduzi ya 12 Januari, 1964 Serikali iliipa umuhimu mkubwa sekta ya
ufugaji. Wafugaji walipewa taaluma za
namna bora ya kufuga. Aidha, walipouza mifugo yao kama vile ng’ombe, kuku na
kadhalika, walipewa bei za juu.
Mashamba ya ufugaji kuku wa Serikali na mazizi ya ng’ombe
kwa ajili ya nyama na maziwa yalifunguliwa katika maeneo mbali mbali. Vile vile, vituo zaidi kwa matibabu ya
wanyama vilifunguliwa huko vijijini katika maeneo waliyoishi wafugaji.
Katika miaka ya hivi karibuni jitihada kubwa zimechukuliwa
za kuwaendeleza wafugaji kupitia programu mbali mbali, ikiwemo programu ya
kuimarisha huduma za mifugo (ASDP-L) yenye kutoa taaluma ya ufugaji bora. Katika mwaka 2011/2012, vikundi vipya vya
skuli za wafugaji 335 vya Unguja na Pemba vilipewa mafunzo. Aidha, wafugaji 3200 walitembelewa na kupewa
ushauri wa kitaalamu.
Vile vile, katika kuimarisha huduma za utafiti na utibabu
wa wanyama, matengenezo makubwa yamefanywa kwenye maabara ya Maruhubi Unguja na
Chake Chake Pemba pamoja na kuimarisha vituo vya mifugo viliopo sehemu mbali
mbali.
Jitihada
hizi za Serikali zimesaidia sana kuyainua maisha ya wafugaji katika kupambana
na umasikini.
Ndugu Viongozi na Ndugu
Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi Zanzibar haikuwa na wataalamu wa
uvuvi. Kwa hivyo, mwaka 1965 Serikali
iliwapeleka vijana wake nchi za nje ili kusomea uvuvi. Idara ya Uvuvi na Shirika la Uvuvi (ZAFICO)
lilianzishwa ili kuendeleza uvuvi.
Katika kipindi chote Serikali imefanya jitihada kubwa za kuuimarisha
uvuvi kwa kuwashajiisha wavuvi wadogo wadogo wanaoishi pembezoni mwa mwambao wa
bahari. Kutokana na juhudi hizo kiwango
cha samaki kilichovuliwa kimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni. Wastani wa
tani 30,500 zilivuliwa mwaka 2012 ikilinganishwa na tani 28,759 mwaka
2011. Uzalishaji wa mwani vile vile
umeongezeka kutoka tani 12,259 mwaka 2011 hadi tani 13,844 mwaka 2012, Zanzibar
ikiwa ni ya pili baada ya Thailand kwa kuzalisha mwani kwa wingi. Wavuvi wameendelea kuwezeshwa kwa kuwapa
mafunzo ya uvuvi bora unaozingatia uhifadhi wa mazingira na matumizi bora ya vifaa vya kisasa. Mafunzo kwa wavuvi juu ya udhibiti wa mazingira
ya baharini yamefanywa na mradi wa MACEMP ambao
ulilenga kuyaendeleza maeneo ya ukanda wa pwani ya Unguja na Pemba.
Jumla ya TShs. 163.6 milioni zilitolewa kwa kuwaendeleza wavuvi wa Unguja na
Pemba.
Kutokana na jitihada zilizochukuliwa na Serikali, mchango
wa sekta ya uvuvi katika Pato la Taifa umepanda kutoka asilimia 6.1 mwaka 2011
hadi 6.7 mwaka 2012.
Waheshimiwa
Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi yetu ya 1964, wananchi wengi waliokuwa
wakiishi sehemu za vijijini walikuwa wakipata shida ya usafiri kwa sababu
hakukuwa na barabara za maana, zilikuwa chache za lami na nyingi za udongo na
kifusi. Kabla ya Mapinduzi barabara za Zanzibar zilikuwa na urefu wa km 408
ambapo Unguja ilikuwa ni km 210 na Pemba ni km 198.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mara tu baada ya
Mapinduzi ilianza ujenzi wa barabara za lami na madaraja, mashamba na mjini. Leo tunaona fakhari kwamba hivi sasa barabara za Zanzibar zina urefu wa
km. 680.70; Unguja km. 450.25 na Pemba km 230.45. Barabara zote hizi ni za lami
na za kisasa.
Vile vile, barabara za Kaskazini Pemba zimejengwa upya kwa
msaada wa Shirika la MCC la Marekani na ziko katika hatua ya mwisho kumalizika
na zinatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
Hivi sasa, Zanzibar ina mtandao bora wa barabara na ni dhahiri zitatoa
mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wetu na kuwahudumia wananchi katika
maisha yao ya kila siku.
Ndugu Viongozi na
Ndugu Wananchi,
Huduma za Bandari baada ya Mapinduzi ziliimarishwa sana na Bandari
ya Malindi ilibadilishwa muundo wake wa zamani uliojengwa kabla ya
Mapinduzi. Bandari hio imejengwa upya kwa msaada wa Umoja wa Nchi za
Ulaya. Bandari hiyo hivi sasa inahudumia
abiria na makontena mengi zaidi. Kwa mfano mwaka 2012 yamepokelewa makontena
39,821 kutoka 39,293 mwaka 2011.
Ongezeko hili ni asilimia 27.
Serikali imeimarisha bandari hiyo kwa kununua mashine za kisasa mbali
mbali. Majengo mapya ya kupumzikia
abiria yamejengwa na Kampuni ya Azam Marine kwa kushirikiana na Serikali. Kwa upande wa Pemba, gati mpya ya Mkoani
imejengwa, huduma za bandari zimeimarishwa pamoja na jengo la abiria.
Katika hatua za kuimarisha usafiri wa anga, Serikali
imechukua hatua ya kukiimarisha na kukiendeleza kiwanja cha ndege cha Kimataifa
cha Abeid Amani Karume, ambapo njia ya kurukia na kutulia ndege imeongezwa
urefu hadi mita 3022 na upana umeongezwa hadi mita 45. Hivi sasa uwanja huo una
uwezo wa kuhudumia ndege za aina zote kubwa. Ujenzi wa “taxiway” mpya na
“apron” umekamilika na ujenzi wa jengo jipya la abiria katika eneo la pili
(terminal 2) unaendelea. Kwa upande wa uwanja
wa Pemba, jitihada kama hizi zitaendelezwa hivi karibuni kwa kuupanua uwanja na
kujenga jengo jengine la abiria. Utiaji
taa katika njia ya kurukia ndege utaanza hivi karibuni.
Waheshimiwa
Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika jitihada za kupunguza tatizo la usafiri wa baharini
baina ya Zanzibar na Tanzania Bara na sehemu nyengine, Serikali imeshafunga
mkataba na Kampuni ya Korea ya Kusini kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya ya
abiria ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukuwa abiria 1,200 na mizigo tani 200.
Meli hiyo inategemewa kufika nchini mwezi Juni, mwaka 2015.
Waheshimiwa
Viongozi na Ndugu Wananchi,
Huduma za umeme ni miongoni mwa sekta muhimu kwa ajili ya
maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ingawa Zanzibar ni miongoni mwa nchi za
mwanzo Barani Afrika kuwa na huduma za umeme, tangu mwaka 1880, lakini kabla ya
Mapinduzi huduma hizo ziliishia katika baadhi ya sehemu za mjini Unguja tu, kwa
wale waliokuwa na uwezo. Aidha, huduma hizo hazikuwa na mchango mkubwa katika
kustawisha au kuinua hali za wanyonge. Ndiyo maana, mara tu baada ya Mapinduzi,
tarehe 6 Juni, 1964, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianzisha Shirika la
Mafuta na Nguvu za Umeme ambalo hivi sasa linajulikana kwa jina la Shirika la
Umeme la Zanzibar (ZECO). Lengo la
shirika hili ni kusambaza huduma zake ili ziwafikie wananchi katika sehemu
mbali mbali wanazoishi mijini na vijijini.
Mahitaji ya umeme kwa Zanzibar kabla ya mwaka 1980 yalikuwa
ni Megawati 3.5 uliotokana na majenereta na umeme huo ulikuwa ukikatika katika
na kusababisha matatizo mbali mbali na ndipo Serikali ikalazimika kununua waya
wa umeme uliopitishwa chini ya bahari kwa kuunganishwa na gridi ya Taifa. Kiwango cha umeme cha waya huo kilikuwa ni
Megawati 45.
Waheshimiwa
Viongozi na Ndugu Wananchi,
Hivi sasa tunaposherehekea miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu
ya 1964, mafanikio makubwa yamepatikana kwa kuwa na kiwango cha umeme cha
Megawati 100 kwa Unguja na Megawati 20 kwa Pemba. Mafanikio haya yamepatikana kwa msaada wa
Serikali ya Marekani kwa Unguja na Serikali ya Norway kwa Pemba. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilichangia jitihada hizo. Kiwango hichi cha umeme kinapatikana kupitia
waya uliolazwa baharini na kuunganishwa na gridi ya Taifa baina Ras Kilomoni na
Fumba kwa Unguja na baina ya Tanga na Ras Mkumbuu kwa Pemba. Usambazaji wa umeme vijijini umefikia hatua
kubwa sana na katika kipindi cha miaka mitatu (3) iliyopita usambazaji huu
umefikia asilimia 87.5 ya vijiji vyote vya Unguja na Pemba. Hii ni hatua kubwa sana katika kuwapelekea
umeme wananchi. Haya ni mafanikio
makubwa yaliyofikiwa katika kuwahudumia wananchi walioko vijijini.
Waheshimiwa
Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika sherehe hizi za miaka 50, tunafurahia mafanikio
makubwa tuliyoyapata katika sekta ya Habari, Utamaduni na Michezo. Tumepiga hatua kubwa katika sekta ya habari,
kwa kutekeleza malengo ya Mapinduzi katika kuwaelimisha wananchi. Sauti ya Tanzania Zanzibar ambayo ilipewa
jukumu la kuifanya kazi hiyo, iliwapa wananchi habari za ndani na nje ya nchi na kuimarisha na
kuamsha msimamo wao wa kisiasa. Katika
nyakati tafauti, Serikali ilinunua mitambo ya redio ya kutangazia, muda wa
matangazo uliongezwa na jengo jipya la kutangazia la Rahaleo lilijengwa. Hivi
sasa Shirika jipya la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) limeundwa na linatoa
matangazo yake saa kwa 24 kwa Radio na Televisheni.
Ndugu Viongozi na
Ndugu Wananchi,
Utamaduni wetu ni suala la msingi katika maisha ya kila
siku ya watu wa Unguja na Pemba. Kwa
hivyo, baada ya Mapinduzi ya 12 Januari, 1964, tunaendelea kuutunza na
kuuendeleza utamaduni wetu. Tumeziimarisha sanaa na ngoma zetu za asili, lugha
yetu ya Kiswahili na michezo. Mipango ya
kuwakumbuka na kuwaenzi wasanii wetu waliovuma na kuipatia sifa Zanzibar kama
vile Marehemu Bibi Siti binti Saad, Marehemu Bi. Fatma binti Baraka (Bi. Kidude),
Marehemu Bwana Bakari Abeid imeandaliwa.
Taasisi ya kumuenzi Mwanaharakati Bibi Siti binti Saad imeanzishwa na
tarehe 7 Januari, 2014, ilizinduliwa rasmi.
Lugha ya Kiswahili
inaendelezwa na hivi sasa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, kinatoa
elimu ya kiwango cha Stashahada na
Shahada zote. Kadhalika, michezo inaendelea kuimarishwa na kushajiisha
mazoezi ya viungo kwa makundi mbali mbali ili kuimarisha afya za wananchi. Natoa wito kwa wananchi wote wafanye mazoezi
kwani ni muhimu kwa ajili ya afya zetu. Mazingira mazuri ya michezo
yameimarishwa kwa lengo la kuwawezesha wanamichezo kushinda katika mashindano
hayo.
Ndugu Viongozi na
Ndugu Wananchi,
Wakati huu tunapoadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi,
tunajivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika jitihada za Serikali za kuwahudumia
wazee na hatua zinaendelea kuchukuliwa za kuziimarisha huduma zote muhimu kwa
ajili ya maisha yao. Aidha, kwa azma ya kulinda haki za watoto, Serikali
imeanzisha sheria mpya ya kumlinda mtoto ya mwaka 2011 na masuala ya vitendo
vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto yanashughulikiwa na yamewekewa mikakati
madhubuti.
Katika kipindi hiki tunafurahia mafanikio ya juhudi zetu za
kupambana na umasikini kwa kuwawezesha kiuchumi vijana na kinamama. Jumla ya vikundi 257 vya Unguja na Pemba na
wajasiriamali 1,738 wamewezeshwa kwa kupewa mikopo. Jumla ya TShs. milioni 2,344.7 zilitolewa
kutoka kwenye mifuko iliyoanzishwa na Serikali.
Jitihada hizi zitaimarisha upatikanaji wa ajira.
Vile vile, jitihada mbali mbali zimechukuliwa katika
kuwasaidia watu wenye ulemavu. Mipango
na mikakati imepangwa kupitia Idara ya Watu wenye Ulemavu na katika mwaka 2012,
Serikali imezindua mfuko maalum wa kuwasaidia.
Zoezi la kuwasajili watu wenye ulemavu limefanyika katika Wilaya mbali
mbali ili uratibu wa shughuli zao ufanyike kwa ufanisi.
Kwa kuzingatia umuhimu wa masuala ya mazingira na jinsi
yalivyopewa kipaumbele duniani kote, Serikali ilitunga sera ya mazingira ya
1992. Sera hii ilifanyiwa mapitio na
sera mpya ilitungwa mwaka 2013. Sera hii
inatilia mkazo elimu ya mazingira kwa wananchi, kuhusu umuhimu wa uhifadhi na
utunzaji wa mazingira. Mapambano dhidi ya matumizi ya mifuko ya plastiki
yameendelezwa na tani 288 za mifuko hiyo zimekamatwa na wahusika kuchukuliwa
hatua. Miradi ya vitega uchumi hufanyiwa
ukaguzi wa mazingira na miradi 160 ilikaguliwa.
Suala la mabadiliko ya tabia nchi linashughulikiwa kwa kufanya tafiti za
athari yake kwa uchumi wa Zanzibar na jumla ya maeneo 165 yaliyoingia maji ya
chumvi yameorodheshwa. Hivi karibuni,
kikosi kazi maalum kimeandaliwa ili kushughulikia maeneo yanayochimbwa mchanga,
mawe na kifusi.
Pamoja na mafanikio makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii
ambayo nchi yetu imeyapata, zipo changamoto nyingi ambazo zinatukabili katika kuiletea maendeleo nchi
yetu. Changamoto kubwa inayotukabili ni
namna gani tutaweza kuyatunza na kuyaendeleza mafanikio tuliyoyapata ambayo leo
nimeyaelezea kwa furaha kubwa. Ni dhahiri
kwamba jukumu letu ni kuhakikisha kwamba amani na utulivu ndio jawabu peke yake
la kutatua changamoto hio na lazima tufanye kila jitihada ili tuiimarishe amani
na utulivu kwa madhumuni ya kupata mafanikio zaidi.
Bila ya shaka yoyote, hali hiyo tutaifikia tu tukiwa
makini, watiifu, waadilifu na tulioamua kuwa kwa maendeleo ya nchi yetu. Utiifu
wa sheria ni hatua moja muhimu katika kuyafanikisha hayo. Ni jukumu la viongozi
wote wa Serikali, wanasiasa, viongozi wa
dini na viongozi wengine katika jamii, sote kwa pamoja tutekeleze wajibu wetu huo
kwa kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinadumishwa na sheria za nchi
zinafuatwa. Ni wajibu wetu kuyalinda,
kuyaenzi na kuyadumisha Mapinduzi yetu na
kuuendeleza na kuudumisha Muungano wetu.
Muungano wetu pamoja na Mapinduzi yetu ndizo nguzo zetu kubwa za maendeleo na ndivyo vilivyotufikisha
hapa hivi sasa na ndivyo vitakavyotufikisha tunakokusudia kwenda katika miaka
mingi ijayo.
Napenda niwahakikishie wananchi wote kwamba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika kuendeleza Muungano wetu, kuuimarisha na
kuwatumikia wananchi. Katika kuuimarisha
Muungano wetu, sote tumetimiza wajibu kwa kutoa maoni yetu kwa ajili ya
kuandaliwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba Mpya imetimiza
wajibu wake na imefanya kazi kubwa na tayari wamemkabidhi Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Rasimu ya Pili ya Katiba kama sheria iliyoelekeza. Hatua zilizobakia nazo
zitakamilishwa kwa kuzingatia sheria iliyopo ili hatimae tupate Katiba Mpya
itakayoliongoza Taifa letu na kuimarisha Muungano wetu. Kwa mara nyengine tena
nampongeza Mwenyekiti wa Tume hio Jaji Mstaafu Mheshimiwa Joseph Sinde Warioba
na wajumbe wote wa Tume kwa kazi kubwa waliyoifanya, tena kwa wakati. Napenda
nimshukuru na nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk.
Jakaya Mrisho Kikwete kwa kusimama imara katika mchakato wa upatikanaji wa
Katiba mpya. Vile vile, nampongeza kwa
kuutetea na kuuendeleza Muungano wetu na kwamba siku zote yuko tayari
kuzizungumzia changamoto zinazoukabili Muungano wetu na kutafuta njia za
kuzipatia ufumbuzi kila zinapotokea.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuuendeleza na kuudumisha
Muungano kwa manufaa ya nchi zetu mbili. Hivi sasa tumemaliza miaka mitatu
tangu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa
imeingia madarakani. Tumepata mafanikio
ya kuridhisha, hata hivyo, bado ipo kazi kubwa mbele yetu ambayo inahitaji
jitihada zetu za pamoja.
Napenda kuwahakikishia wananchi wote kuwa Serikali
itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na sheria kwa kuilinda amani,
utulivu, mali na maisha ya watu. Hivi
sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko salama na Zanzibar iko salama kutokana
na kazi nzuri inayofanywa na vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama. Kwa hivyo, nchi yetu itaendelea kuwa salama
wakati wote.
Kwa mara nyengine natoa shukurani, kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwa nasi katika
maadhimisho ya sherehe zetu za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vile vile
natoa shukurani kwa wageni wetu Rais Yoweri Museveni wa Jamhuri ya Uganda, Dk. Ikililou Dhoinine,
Rais wa Comoros na Mhe. Jiang Weixin Mjumbe anayemwakilisha Rais wa Jamhuri ya
Watu wa China. Kadhalika natoa shukrani
kwa viongozi wengine wote waliohudhuria walioko madarakani na waliostaafu. Shukurani maalum ziwaendee Makamu wa Kwanza
wa Rais, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais,
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa ushauri wao wa kunisaidia kuiongoza
Zanzibar. Zaidi ya hayo shukrani zangu
nazitoa kwa nchi marafiki, Jumuiya za Kimataifa na Washirika wetu wa maendeleo
na wote waliotuunga mkono katika kipindi cha miaka 50 na tukaweza kushirikiana.
Napenda niishukuru na niipongeze sana Kamati ya Halmashauri
ya Sherehe na Maadhimisho kwa mwaka huu wa 50 wa Mapinduzi inayoongozwa na
Makamu wa Pili wa Rais. Mnastahiki
pongezi kwa kazi nzuri mloifanya katika kufanikisha sherehe zetu ambazo
zilifana sana na zitaingia kwenye historia ya nchi yetu. Hongereni sana. Natoa shukurani maalum kwa makamanda na
wapiganaji wetu wa vikosi vyote kwa namna walivyofanikisha sherehe hizi kwa
gwaride lililopendeza pamoja na vijana wetu wa halaiki, mlivyotia fora.
Nawashukuru na nawapongeza wafanyakazi wote wa Serikali kwa
jitihada zenu za kuwatumikia wananchi.
Ni matumaini yangu kwamba mtaendelea kuongeza juhudi zenu ili tuweze
kuyatekeleza malengo ya Dira 2020 ambayo hivi sasa tumebakiwa na miaka sita
kabla ya kumaliza muda uliopangwa.
Tujitahidi ili Zanzibar iwe miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati. Sote tudhamirie kwamba mwaka huu uwe wa
kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na nidhamu na tusifanye kazi kwa mazoea.
Namalizia kwa kutoa pongezi za dhati kwa wananchi wote kwa
kushiriki katika shughuli mbali mbali za
kusherehekea Mapinduzi yetu kutimiza miaka 50.
Kwenu nyote nasema ahsanteni sana. Aidha, nawashukuru wale wote
walioshiriki katika maandamano na waliotupa burudani. Vile vile, shukurani ziwaendee waandishi wa
vyombo habari kwa kuzitangaza shughuli na sherehe zetu kwa ufanisi tangu pale
tulipozizindua sherehe zetu tarehe 15 Agosti, 2013. Nasema hongereni sana.
MAPINDUZI DAIMA
MUNGU IBARIKI
ZANZIBAR
MUNGU IBARIKI
TANZANIA
MUNGU IBARIKI
AFRIKA
Ahsanteni kwa
kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment