Na Mwashamba Juma
CHINA inatarajia kuinufaisha Zanzibar katika sekta ya viwanda na
utalii ili kuimarisha uchumi wake na kuinua uhusianao wakidugu baina ya nchi
hizo mbili.
Kauli hiyo imetolewa na ujumbe wa watu 21 kutoka China uliokuja
Zanzibar kwa ziara ya siku moja kwa lengo la kuanzisha uhusiano wa kibiashara
baina ya nchini mbili hizo hasa katika sekta za maendeleo ikiwemo uvuvi na
utalii.
Ujumbe huo ulikuwa ukizungumza na Waziri wa Fedha, Mhe. Omar Yussuf
Mzee ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar.
Kiongozi wa ujumbe huo, rais wa kampuni ya China Beobei International
Investment Group, Bian Hongdeng, alisema
ziara yao imewavutia zaidi katika uvuvi wa bahari kuu ya Zanzibar ambapo
wataleta meli kubwa za uvuvi na kujenga kiwanda cha samaki ili kukuza sekta ya uvuvi nchini.
Akizungumzia sekta ya utalii, alisema Zanzinar ni kisiwa kizuri kwa
utalii hivyo tayari wamezungumza na shirika la ndege la Hainan la China ili
kuleta watalii wengi Zanzibar watakaoingia moja kwa moja wakitokea China.
Alisema pia wanatarajia kujenga hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano
itakayotoa huduma zinazolingana na utamaduni wa China, sambamba na kutoa nafasi
10 kwa Wazanzibari kwenda China kusoma kichina kwa ajili ya kufanyakazi na
wachina wakiwa Zanzibar.
Ujumbe huo pia umezungumzia ujenzi wa chuo cha utalii kitakachotoa
taaluma ya utalii kwa Wazanzibari ili kuimarisha sekta hiyo.
Wakizungumzia maendeleo mengine, walisema wanatarajia kujenga bandari ndogo katika
kijiji cha Unguja Ukuu, ambako walipata tetesi ya kukaliwa na Wachina katika
karne zilizopita.
Kujengwa kwa bandari hiyo kutarudisha hisroria zilizopita pamoja na
kuimarisha uhusiano wa kirafiki baina ya Zanzibar na China.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Mhe. Omar Yussuf Mzee, alisema miradi
hiyo itakapotekelezwa Zanzibar itapiga
hatua kubwa kimaendeleo na kukuza uchumi wake.
Alisema serikali itapunguza ushuru kwa sekta ya viwanda ili kuwapa
nafasi wawekezaji wengi kuwekeza katika sekta hiyo.
Alisema ni wajibu wa serikali kutafuta nafasi za uwekezaji nchini kwa
maendeleo na maslahi ya nchi na watu wake.
Ujumbe huo ulikuja kufuataia ziara ya Mhe. Rais wa Zanzibar, Dk. Ali
Muhamed Shein aliyoifanya China mwaka uliopita.
No comments:
Post a Comment