Khamis Amani na Madina Issa
BARAZA la Wawakilishi limeridhia kuunda Kamati Teule, kuchunguza wizi
wa nyaraka muhimu uliofanywa katika Idara ya Nyaraka na Makumbusho.
Hatua hiyo imekuja baada ya Wawakilishi kuonesha wasi wasi juu wa wizi
huo na masuala ya kuwepo harufu ya rushwa.
Spika wa Baraza la Wawakilishi alitangaza kuundwa Kamati hiyo, baada
ya Wawakilishi wengi kuunga mkono na kuwashinda wale waliopinga.
Hata hivyo, Spika alisema wajumbe wa Kamati hiyo na lini itaanza
kufanya kazi zake watatangazwa baadae ili kufanya uchunguzi kabla ya Mamkala ya
kupambana na rushwa nayo haijaaza kuchunguza tukio hilo.
Awali Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, alisema ana wasi
wasi kwamba kama Kamati teule haitaundwa ikaachiwa mamkala ya rushwa kufanya
kazi pekee, inaweza kusababisha Wawakilishi kushindwa kuhoji wizi huo baada ya
kesi kufikishwa mahakamani.
Alisema kwa kuwa taarifa ya Kamati teule haiwezi kuchukuliwa kama ushahidi mahakamani,
Wawakilishi wana haki ya kuunda kamati hiyo ili kujiridhisha na kuchukua hatua
zifaazo.
Mapema juzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara
maalum za SMZ, Mhe. Haji Omar Kheri, alikiri wizi huo kutokea, lakini aliwaomba
Wawakilishi kazi ya uchunguzi kuiachia mamlaka ya kupambana na rushwa, ombi
ambalo lilikataliwa na Wawakilishi.
Wakati huo huo, serikali inadaiwa shilingi
92,844,586 ikiwa ni fidia kutoka kwa wafanyakazi waliopata ajali wakiwa kazini.
Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Wanawake
na Watoto, Mhe. Zainab Omar Mohammed, aliwaambia Wawakilishi jana.
Hata hivyo, alisema kuwa wizara inaendelea na
juhudi za kulitatua deni hilo.
Alisema, katika kufanikisha suala hilo Kamati ya
Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Wanawake ya Baraza la Wawakilishi, iliandaa
kikao maalumu kulitafutia ufumbuzi tatito hilo.
Alisema Novemba 29 mwaka jana, kamati
ikiwajumuisha Makatibu Wakuu kutoka wizara hiyo nay a fedhana kuangalia
uwezekano wa kulipatia ufumbuzi deni hilo.
Katika kikao hicho wizara ya fedha iliahidi
kulilipa deni lote kufikia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu baada ya
kukamilisha baadhi ya taratibu, ikiwemo uhakiki wa madeni hayo.
Aidha alisema, wizara kwa kushirikiana na wizara
ya fedha itasimamia utekelezaji wa maamuzi mengine yaliyofikiwa ili kuwa na
utaratibu ulio bora zaidi wa kusimamia malipo ya fidia kwa wafanyakazi
wanaoumia au kupata madhara wakiwa kazini.
Mapema Mhe. Mohammed Mbwana Omar akiwasilisha
ripoti ya Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii ya Baraza la
Wawakilishi, alisema kamati inasimamia deni hilo kwa karibu kwa sababu fidia ni
haki ya kisheria kwa kila mfanyakazi kulipwa pindi anapopatwa na ajali akiwa
katika mazingira ya kazi.
Alisema, katika kipindi cha mwaka wa fedha
2012/2013 kwa upande wa Unguja deni lilikuwa shilingi 45,000,000 na matarajio
yalikuwa ni kupata shilingi 20,000,000 ili kupunguza deni hilo lakini fedha
zilizopatikana zilikuwa 11,000,000.
Katika hatua nyengine serikali imefungua akaunti
kwa ajili ya ununuzi wa dawa, kwa lengo la kuhakikisha dawa za matumizi ya
bianaadamu zinapatikana kwa wakati.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya, Mhe. Juma Duni
Haji, katika majumuisho ya michango mbali mbali iliyowasilishwa na Kamati na
wawakilishi katika kikao kilichopita.
Alisema serikali kupitia wizara ya afya katika
kuhakikisha upatikanaji wa dawa imetengeneza mfumo mpya wa wa ununuzi wa dawa
ambazo zitakuwa zikinunuliwa kupitia mfumo wa 'frame work contract' badala ya
kutegemea bohari kuu ya dawa pekee.
Alisema katika kuhakikisha suala hilo linapatiwa
ufumbuzi wizara imefungua akaunti ya dawa ambapo fedha kutoka serikalini na
fedha za DANIDA zinaingizwa katika akaunti hiyo.
Kamati ilibaini kuwa hakuna uhakika wa
upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na badala yake serikali hukaa
muda mrefu na hutoa fedha chache zisizokidhi haja na kuwategemea wahisani
wakiwemo DANIDA, ambao pia wamekuwa na masharti yasiyo na muelekeo mzuri wa
ufanisi kwa upatikanaji wa dawa muhimu kwa afya ya jamii.
Katika kulihakikisha hilo, alisema upande wa
fedha za wafadhili ambao ni DANIDA wamesisitiza kuwa hawataingiza fedha kwa
ajili ya ununuzi mpaka wahakikishe serikali inachangia fedha kwa ajili ya
ununuzi wa dawa hizo.
No comments:
Post a Comment