Na
Kija Elias, MWANGA
SERIKALI
inatarajia kuanzisha mradi mkubwa wa maji katika kijiji cha njia panda Kirya,
wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro, unaokadiriwa kugharimu shilingi bilioni
32.
Hayo yamesemwa
na Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe,wakati akizungumza na wakazi
wa kijiji cha njia panda Kirya katika
maadhimisho ya miaka 37 ya CCM, iliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Kirya
na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Alisema
mradi huo unatekelezwa na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya Falme za Kiarabu
(BADEA) na kwamba serikali kwa kutambua
tatizo la maji inaboresha miundombinu katika vyanzo vya maji ili wananchi
waweze kupata huduma hiyo, na kumaliza kero ya maji katika wilaya ya Mwanga,
Same na Korogwe.
Alisema
mradi huo ambao ni wa taifa, utahusisha ujenzi wa mtambo mkubwa wa maji katika
kijiji cha Njia panda Kirya ambapo serikali imepanga kuleta kampuni ya
kusambaza maji itakayofanya kazi ya kusukuma kutoka vyanzo vya maji hadi maeneo
yanayokabiliwa na tatizo hilo.
"Serikali imedhamiria kumaliza matatizo
ya maji, kwa hapa njia panda tunaleta
kampuni ya kusambaza maji kijijini kwenu, kuna mradi mkubwa wa maji wa taifa ambao
utaanzishwa hapa Mwanga na naamini tukifanikiwa tutakuwa tumetatua kero ya maji
kabisa," alisema.
Aidha
alisema maji hayo yatahifadhiwa katika tenki kubwa litakalofungwa mtambo wa
kusafisha maji kabla ya kuyasambaza katika vijiji vyngine vyenye mahitaji ya
maji.
Aliongeza
kuwa mkondo mwengine utasukuma maji hayo kutoka katika kijiji cha Njia panda
Kirya hadi Kisangara ambapo maji hayo yatapandishwa katika milima ya Kiverenge
na wakati huo huo kukiwa na mkondo mrefu ambao utafanya kazi ya kusukuma maji
hadi wilaya ya Same.
Alisema
vijiji ambavyo vinatarajia kunufaika na maji
safi na salama ni Handeni, Bora, Kagongo, Nyabinda Mvungu, Mangulai, Kirya, Kisangara, Makanya na Kisangara.
Aliwataka
wananchi kuchukulia miradi yote inayoanzishwa na serikali kama urithi wao huku
akihamasisha umuhimu wa kutunza mazingira kwa manufaa ya vizazi vya baadae.
Kwa
upande wake, mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa wa Kilimanjaro, Paul Matemu, alisema
vyama vya upinzani ni makundi ya wanaharakati na kamwe hayawezi kuingia ikulu
mwaka 2015 kama ambavyo yamekuwa yakijinadi katika mikutano mbalimbali nchini.
Alisema vyama hivyo haviwezi kufikia hatua
ziliyofikiwa na Chama Cha Mapinduzi
(CCM), kutokana na vyama vingi kujihusisha na
makundi ya wanaharakati ambayo yamekuwa yakiwashawishi vijana
kuhamasisha machufuko.
Alisema katika sherehe za kuadhimisha miaka 37
ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi, kinajivunia misingi imara ambayo
iliasisiwa tangu zamani na hayati Julius Kambarage Nyerere na hayati Abed Amani
Karume.
No comments:
Post a Comment