Na Fatuma Kitima, DAR ES SALAAM
WAANDISHI wa habari 101 wameteuliwa kuingia kwenye
kinyang’anyiro cha kuwania tuzo za umahiri wa uandishi wa habari Tanzania
(EJAT) 2013 ambapo kilele chake kinatarajiwa kuwa Machi 14 mwaka huu katika ukumbi
wa Mlimani City Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Katibu
Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, alisema idadi ya
wateule imeongezeka ambapo ni sawa na asilimia 24.6 ikilinganishwa na mwaka
jana.
Alisema kwa mwaka huu idadi ya waandishi wa habari
wanawake walioteuliwa imeongezeka na kufikia 18 ikilinganishwa na mwaka
uliopita ambao walikuwa 11 kwenye kinyang’anyiro hicho, ikiwa ni sawa na
ongezeko la asilimia 63.6.
Alisema waandishi wa magazeti wako 46, radio 39 na
televisheni 16.
“Wakati wateule kwenye magazeti wameongezeka kwa
wateule watano ikilinganishwa na mwaka jana ambapo walikuwepo wateule 41,
kwenye radio wameongezeka hadi kufikia 39 ikilinganishwa na 21 wa mwaka
uliopita,” alisema.
Aidha alisema kwa upande wa televisheni idadi ya
wateule imepungua kutoka 19 mwaka hadi kufikia 16.
Wakati mashindano hayo yalipoanza kulikuwa na makundi
tisa ya kushindaniwa ambapo mwaka uliofuata yaliongezeka kufikia 16 na mwaka
2011 yalifika makundi 19.
Alisema jopo la majaji lilianza kupitia kazi za
waandishi tangu Februari 10 na kumaliza kazi Februari 16 chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa majaji,
Gervas Moshiro.
Sambasamba na EJAT jopo la wataalam wa tunzo za maisha
ya mafanikio katika uandishi (LAJA) wamewasilisha pia majina ya wateule ambao
watatangazwa katika tamasha hilo .
Aliwataja baadhi ya wateule hao kuwa ni Grace Kiondo, Rahma
Ally, Husna Mohamed, Mwantanga Ame kutoka Zanzibar
na Sam Mahela ITV na Gervas Hubile TBC kutoka Dar es Salaam .
Katika tamasha hilo la utoaji tuzo za EJAT 2013 mgeni
rasmi anatarajiwa kuwa rais wa mahakama ya Afrika Mashariki, Jaji Harold
Nsekela.
No comments:
Post a Comment