Habari za Punde

Balozi Seif: Kero za Muungano hazitoweza kupatiwa suluhisho endapo mchakato wa Katiba mpya utakwama

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifunga Kongamano la Maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika  na Zanzibar kutimia miaka 50 lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort  Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 Baadhi ya Washiriki wa Kongamano la Maadhimisho wa Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lililofanyika Zanzibar Beach Resort na kushirikisha watu wa Taasisi na Jumuiya tofauti za Elimu,Dini, Siasa na Utamaduni Nchini.
Baadhi ya Washiriki wa Kongamano la Maadhimisho wa Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lililofanyika Zanzibar Beach Resort na kushirikisha watu wa Taasisi na Jumuiya tofauti za Elimu,Dini, Siasa na Utamaduni Nchini.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

                                              
Na Othman Khamis Ame, OMPR

Wazanzibari na Watanzania wametanabahishwa kwamba baadhi ya mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa  kwa muda mrefu na Zanzibar  yatokanayo na kero za Muungano yanaweza kushindikana kurekebishwa kisheria endapo mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ya Muungano hautafikia lengo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitanabahisha hilo wakati akilifunga Kongamano la siku moja la Maadhimisho ya Miaka 50 ya Muungano  wa Tanganyika na Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort iliyopo Mazizini Nje kidogo ya Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alilitolea mfano Suala la Mafuta na Gesi ambalo Zanzibar inataka litolewe  kabisa katika mambo yaliyomo ndani ya Muungano linaweza lisifikie usuluhishi kwa vile ni suala linalohitaji marekebisho ya kina ya Kisheria.

Alisema masuala yaliyojitokeza ndani ya mjadala wa Bunge Maalum la Katiba Tanzania na kupelekea baadhi ya Wajumbe wa Bunge hilo kuamua kususia mjadala huo yanaweza yakaikosesha fursa Zanzibar katika mchakato mzima wa kujiimarisha kiuchumi.

Alisema Taifa tayari limeshatumia gharama kubwa katika kuandaa mchakato huo wa Kupata Katiba Mpya ya Tanzania lakini baadhi ya Watu zaidi wakiwa wanasiasa wanajaribu kutafuta mbinu za makusudi za kukwamisha mchakato huo muhimu katika Historia ya Taila la Tanzanai ndani ya Kipindi cha Miaka 50 tokea kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar Tarehe 26 Aprili Mwaka 1964.

“ Yale mambo ambayo yamelalamikiwa na Zanzibar kwa muda mrefu kuhusu kero za Muungano hasa lile suala la Mafuta na Gesi yatashindwa kurekebishwa kisheria kupitia mchakato huo kama utakwama “. Alifafanua Balozi Seif.


Akizungumzia Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema suala la Elimu ya Muungano na umuhimu wake bado lina uzito mkubwa katika Jamii hasa Kizazi kilicho hivi sasa.

Alisema inashangaza kuona baadhi ya Watu hasa wanasiasa wamebeba bango la kuhoji uhalali na faida za Muungano huo visingizo vinavyoleta hofu kiasi kwamba umuhimu huo wa Elimu ya Muungano inastahiki ili jamii iepuke kupotoshwa na watu wa aina hiyo.

Alifahamisha kwamba Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa Zanzibar imefaidia vilivyo na Muungano uliopo kwa vile tayari umeshalitangaza Taifa hili kwa upana zaidi ulimwenguni.

Alieleza kwamba Wananchi wengi wa Zanzibar  zaidi ya Laki Nane sawa na asilimia 62% ya Wazanzibari wote wanaendelea kufaidika Kijamii na Kiuchumi upande mwengine wa Jamuhuri  hiyo huko Tanzania Bara.

Balozi Seif alisema kuwa Uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla umeimarika kutokana na Mataifa, mashirika na Taasisi za Kimataifa kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika harakati zake za kujiletea maendeleo.

“ Mataifa mbali mbali Duniani yanaiona Tanzania watu wake ni wenye msimamo katika kuimarisha  Umoja na kudumisha amani, msimamo ambao umewavutia wawekezaji wengi na kutamani kuwekeza miradi tofauti ya kiuchumi Nchini “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwamba ni wajibu wa Jamii Nzima  ya Wanzania kuendelea kuwakumbuka waasisi wa Muungano huo Marehemu Mzee Abeid Amani  Karume na Marehemu Mwalimu Julius K ambarage Nyerere kwa mchango wao mkubwa uliofanikisha maendeleo yaliyopo hivi sasa.

Alisema fikra sahihi za waasisi hao zinapaswa kudumishwa na kuimarishwa ndani ya Muungano unaoendelea hivi sasa ili kuijenga Tanzania iliyostawi kwa maslahi ya wananchi wote,vizazi vya sasa ni vile vijavyo.

Balozi Seif aliwanasihi wnanchi wote kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar katika dhana nzima ya kudumisha na kuimarisha Muungano huo.

Akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kulifunga Kongano hilo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan  alisema kwamba utekelezaji wa kero za Muungano uliohusisha pande zote mbili umefikia hatua nzuri.

Waziri Samia alisema Kamati ya pamoja na Viongozi waandamizi wa pande hizo mbili Chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imemaliza kazi ya kutanzua kero kumi kati ya 13 zilizowasilishwa kwenye Kamati hiyo.

“ Utekelezaji wa Kero za Muungano zilikuwa 13 zilizowasilishwa kwenye Kamati yetu na tayari tumeshazifanyia kazi. Hivi sasa zimebakia Tatu lakini ni sawa na kusema imebakia moja ile kubwa ya Kiuchumi “. Alifafanu Waziri Samia Suluhu Hassan.

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 50 ya Muungano wa Tannganyika na Zanzibar  inasema “ Utanzania wetu ni Muungano wetu, Tuulinde, Tuuimarishe na Kuudumisha “.


6 comments:

  1. Ushajilimbikizia mashamba kule Tanganyika sasa unataka kutuletea story za faida ya muungano....tuache bana !

    ReplyDelete
  2. huyu mzee si juzi tu kule dodoma alisema kuwa hata kama ukawa wamejitoa lakini bado wako na wajumbe wa kutosha katika bunge la katiba.....kama ni hivyo basi iandikeni hiyo katiba ya CCM....halafu tuone kama kutakuwa na Tanzania tena):

    ReplyDelete
  3. ungeyajua hayo ungewakemea mawaziri na wawakilishi walokuwa wakiwatukana wapemba

    ReplyDelete
  4. Si peke yake banaaaa na wakina mabalahau pia wanayo tangu Muheza hadi Ntwara. Kifo cha jamaa arusi.

    ReplyDelete
  5. aibabaishe watu huyu ni mamluki wa tanganyika , muda umefika muungano uishe sasa , hatutaki kutawaliwa na yoyote yule

    ReplyDelete
  6. Propaganda za uongo. Wanafikiria Wazanzibari hawafahamu wala hawana uwezo wa kuchambua yanayojiri bungeni na katika nchi. Amkeni viongozi msifikiria kuwa matadangaya watu milele.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.