Habari za Punde

Hotuba ya Maalim Seif siku ya upandaji miti kitaifa


HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. MAALIM SEIF SHARIFA HAMAD SIKU YA UPANDAJI MITI KITAIFA KATIKA ENEO LA BARABARA YA JENDELE - CHEJU - UNGUJA UKUU, MKOA WA KUSINI UNGUJA TAREHE 20 APRIL, 2014

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama na Serikali
Waheshimiwa Wananchi, Mabibi na Mabwana
Assalm Alaykum.
Kwanza kabisa hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenye wingi wa rehema kwa kutujaalia neema ya uhai tukaweza kukutana hapa wakati huu  tukiwa wazima.
Pia napeda kuchukua fursa hii kuwashukuru nyote mlioshiriki katika kuandaa kampeni ya Upandaji Miti Kitaifa na kuamua kunialika mimi nije kujumuika nanyi katika tukio hili muhimu. Vile vile nawashukuru wananchi nyote mlioweza kufika hapa kwa wingi. Kuhudhuria kwenu katika shughuli hii ya upandaji wa miti kunaonesha ni jinsi gani mnavyo thamini juhudi za kuistawisha nchi yetu, ili iwe na mazingira mazuri, jambo ambalo ni muhimu sana kwa maisha yetu, vizazi vyetu na kwa maendeleo ya nchi yetu kwa jumla.

Waheshimiwa Viongozi na Wananchi
Tunasema kuwa siku ya leo ni muhimu sana kwa sababu ina lenga kutukumbusha hostoria ya visiwa vyetu vya Unguja na Pemba. Historia ya utajiri mkubwa wa miti ya asili na matunda ya aina mbali mbali. Lakini kutokana na tabia zetu mbaya sisi binaadamu zimepelekea matumizi mabaya ya rasilimali hizo na matokeo yake ni kupotea kwa miti mingi hapa nchini.
Wazee wetu nadhani bado mnakumbuka kwamba visiwa hivi vilikuwa vikijuilikana kama Visiwa vya Kijani. Hali hii ilitokana na ukweli kwamba visiwa vilikuwa vimepambwa kwa mandhari nzuri ya miti ya aina mbali mbali. Hivyo basi kila mgeni alitamani kutembelea na wakati mwengine kuamua kuishi hapa hapa, kutokana na utajiri huo mkubwa wa aina mbali mbali za miti na wanyama. 

Hata hivyo, nadhani tunakubalina sote kwamba hivi sasa hali hiyo imeanza kubadilika kwa kasi, kuna maeneo mengi ya visiwa vyetu miti imeadimika sana na mengine kutishiwa kuwa jangwa, kutokana na ukataji wa miti uliokithiri ambao unafanywa bila ya kuzingatia taratibu zozote.
Waheshimiwa Viongozi na Wananchi
Kuongezeka kwa mahitaji muhimu ya nishati kama vile makaa na kuni, majengo, ardhi kwa ajili ya makaazi na kilimo na shughuli nyengine za maendeleo kunazidisha kuongezeka kwa kasi ya ukataji wa miti na uharibifu wa misitu hapa nchini.
Takwimu za hivi karibuni za sensa ya miti zinaonesha wazi kwamba idadi ya miti inapungua sana. Zimeonesha kwamba maeneo mengi ya misitu pamoja na mashamba yamegeuzwa kuwa makaazi ya watu na hivyo kuendelea kukatwa kwa kasi. Miongoni mwa miti inayokatwa sana ni miti mikubwa, miti ya matunda na ya viungo.  Ardhi zenye rutba ambazo zimetengwa kwa kilimo hivi sasa ndizo zinazovamiwa kwa ujenzi na hivyo kupunguza zaidi idadi ya miti na uzalishaji wa matunda na chakula.
Takwimu hizo zimeonesha kwamba juzi tu, yaani mwaka 1997 visiwa vya Unguja na Pemba vilikuwa na miti yenye mita za ujazo wa 10.3 milioni, lakini kima hicho kilipungua hadi kufikia mita za ujazo 8.6 milioni mwaka jana wa 2013.


Waheshimiwa Viongozi na Wananchi
Hali halisi ni kwamba uwezo wa misitu na miti yetu ya kuzalisha rasilimali ambao ni mita za ujazo 485,532 (cm3) kwa mwaka, wakati ambapo mahitaji yetu mita za ujazo 1,340,067 (cm3) kwa mwaka. Hivyo basi kutokana na taarifa hizo, nchi yetu ina upungufu wa mahitaji ya rasilimali zitokanazo na miti, yaani kuni, makaa, mbao na majengo, za kiasi cha mita za ujazo 854,537 (cm3) ambazo zinabidi zifidiwe kutoka nje ya nchi. Hali hii haioneshi picha nzuri hata kidogo kwa mustakabali wa nchi, hasa ikizingatiwa kuwa mahitaji makubwa tuliyonayo ya miti kwa ajili ya nishati.

Waheshimiwa Viongozi na Wananchi
Siku ya upandaji miti Kitaifa imeteuliwa rasmi na Serikali ili kuwatanabahisha na kutoa changamoto kwa wananchi wa visiwa hivi kuhusu jukumu letu la kupanda na kuitunza miti na uhifadhi wa mazingira ya nchi yetu. Athari za mabadiliko ya tabia ya nchi si tatizo la Kiulimwengu pekee, bali hata nasi hapa Zanzibar tunaathirika sana na mabadiliko hayo ya hali ya hewa. Taathira tunazokabiliana nazo ni pamoja na kubadilika kwa miongo, mvua zisizo za uhakika, mafuriko, vimbunga, ukame, kuzuka kwa mioto, maradhi na athari nyenginezo. Matokeo yake ni pamoja na kupungua kwa mazao ya kilimo, nishati, kuni, miti ya kujengea na kuongezeka kwa maradhi ya binaadamu, wanyama na mimea.

Waheshimiwa Wananchi    
Miti husaidia kwa kiasi kikubwa kuhifadhi mazingira ikiwa ni pamoja na vyanzo vya maji, chemchem, mito, kujikinga na upepo mkali na kusaidia upatikanani wa mvua ambayo ni muhimu kwa shughuli zetu za kilimo na ustawi wa maisha yetu binaadamu na wanyama.
Aidha, miti ni chanzo cha pato la wananchi na Taifa kwa jumla, kwa mfano karafuu ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya fedha za kigeni kwa nchi yetu na pia inachangia nishati kuu ya kuni na makaa tunayotumia. Pia inatumika kwa shughuli za ujenzi wa nyumba, mbao, chakula na hata madawa ya asili. Tukumbuke kuwa misitu ndio makaazi na mazalia muhimu ya wanyama, ndege na samaki, hususan katika maeneo ya miti ya mikoko.

Waheshimiwa Viongozi na Wananchi
 Inabidi tuzidi kukumbuka kwamba maisha yetu kwa kiasi kikubwa yanategemea kuwepo kwa miti kwa ajili ya mahitaji yetu muhimu ya kila siku. Kuimarika kwa ardhi ya kilimo, yaani kuwa na rutba kunahitaji sana kuwepo kwa miti ambayo hutoa virutubisho ambavyo ndio chakula  cha mimea tunayoipanda. Chemchem za maji haziwezi kuimarika bila ya kuwepo kwa miti. Hivyo basi ni wajibu wetu kuendelea kuihifadhi, kuitunza na kuipanda kwa wingi, ili tuweze kuyanusuru maisha na mazingira yetu hivi sasa na siku zijazo.

Waheshimiwa Viongozi na Wananchi
Ulimwengu hivi sasa umehamanika kutokana na matatizo makubwa yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa. Uhifadhi wa mazingira yetu ni sehemu ya suluhisho la kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira ambazo zinasababisha mabadiliko ya hali ya hewa tusivyotarajia. Pale tutakapomudu kutunza vyema miti yetu ya asili na tunayoipanda, ikiwemo ya matunda na viungo basi ni dhahiri kwamba tutakuwa tumepiga hatua kubwa za kukabiliana na mabadiliko hayo ya hali ya hewa. 
Juhudi kubwa hazina budi kuchukuliwa katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu na thamani ya miti yetu kijamii, kiuchumi na kimazingira. Ni lazima tufahamu kwamba majanga mengi ya kimazingira yataendelea kutokea ikiwa tutaendelea kuikata miti hiyo ovyo na bila ya utaratibu.

Waheshimiwa Viongozi na Wananchi
Kwa upande wa Serikali mkazo mkubwa tumeuweka katika suala zima la upandaji wa miti nchini. Mkazo huu umewekwa katika upandaji wa miti aina mbali mbali kwani miti yote ina faida nyingi kama ambavyo niliwaeleza hapo awali. Hata hivyo suala zima la upandaji wa miti ya misitu, matunda, viungo na mikarafuu, Serikali nayo imelipa msukumo zaidi katika kipindi hichi.
Hakuna asiyefahamu umuhimu wa zao la Karafuu kwa uchumi wetu. Zao hili kwa kipindi kirefu limekuwa likikabiliwa na matatizo makubwa katika uendelezaji wake. Hali hii imechangiwa sana na kuporomoka kwa bei yake katika soko la Dunia. Uzalishaji mdogo pia umesababishwa na maradhi, kuzeeka kwa miti hiyo pamoja na matunzo hafifu, hali iliyopelekea miti ya mikarafuu kukatwa kwa wingi, na hata ile iliyosalia iliachwa hadi kufa bila ya kupata huduma zozote. Hali hii ilipelekea visiwa vya Zanzibar kuanza kupoteza sifa yake ya kuwa ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa karafuu zenye ubora unaosifika hapa Ulimwenguni.
Mbali na matatizo hayo katika uzalishaji wake, zao la karafuu linakabiliwa na tatizo jengine kubwa la kusafirishwa kwa magendo. Lakini pia jambo baya zaidi hivi karibuni kumezuka tabia ya baadhi ya watu kuitorosha kwa magendo miche ya mikarafuu na kuipeleka nje ya nchi. Kwa kweli hili ni janga kubwa ambalo halina budi kupigwa vita kwa nguvu zote. Serikali imeendelea kuwapa motisha wakulima wa mikarafuu ili kuinua uchumi na maisha yao na kuinua pato la Taifa kwa jumla. Pia Serikali inaendelea kutoa miche bure na vivutio vyengine, ili kuhakikisha wakulima wetu wanafaidika na jasho la kazi yao.

Waheshimiwa Viongozi na Wananchi
Tupandeni kwa wingi mikarafuu pamoja na mazao mengine yakiwemo ya viungo na matunda. Haiba na mandhari njema ya nchi hii yataendeela kuwa mazuri iwapo upatikanaji wa matunda mbali mbali na viungo utaendelea kushamiri. Hata Miji, Vijiji pamoja na barabara zetu zitazidi kupendeza ikiwa zitaendeela kutunzwa kwa kupandwa miti ya vivuli na ya matunda.
Uzinduzi tunaoufanya leo katika barabara hii ya Jendele hadi Unguja Ukuu ni muendelezo wa kampeni hii ya upandaji miti katika barabra na maeneo mengine ya jamii. Lengo letu kuu ni kuhakikisha tunapanda miti katika barabara zote za Unguja na Pemba na kuhakikisha kwamba tunaendeleza mandhari nzuri za barabara zetu, kama ilivyo katika baadhi ya maeneo kama vile Bungi, ambako kila mmoja wetu anafurahia kupita.
Napenda kutoa wito kuwa skuli zetu na hata vyuo vyetu vipangiwe program maalum ya kupanda na kutunza miti kwa wingi. Pengine kila mwanafunzi akipewa jukumu la kupanda, kulea na kutunza mti mmoja tu kwa mwaka, basi tutaibadili nchi yetu katika kipindi kifupi.
Pia wananchi washajiishwe kuacha tabia ya kukata miti katika viwanja wanavyokusudia kujenga nyumba zao. Badala yake wahakikishe kuwa nyumba wanazojenga zinazunguukwa na miti kwa kuihifadhi iliyopo na kupanda mingine.
Wakati mzuri wa kupanda miti ili istawi na kukua ni nyakati za misimu ya mvua. Hivyo tuzitumie mvua hizi kupanda miti kwa wingi kama itakavyo wezekana.

Waheshimiwa Viongozi na Wananchi     
Katika msimu huu wa mvua, Serikali kwa kushirikiana na wana jamii pamoja na vikundi vya kuhifadhi mazingira imedhamiria kupanda miti katika maeneo mbali mbali ikiwemo hayo ya barabara. Jumla ya kilomita 50 za barabara tayari zimepandwa miti katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.
Uongozi wa Wilaya hizo pamoja na Masheha kwa kushirikiana na wananchi wote wana jukumu la kushiriki kikamilifu katika kupanda miti, lakini pia kuihudumia miti hiyo. Uzoefu unaonesha mara nyingi huwa tunapanda miti mingi hasa katika kampeni kama hizi, lakini tatizo linakuja kwenye matunzo ya miti hiyo, ambapo mingi hushindwa kustawi.  

Waheshimiwa Viongozi na Wananchi
Kwa vile tumeshafanya kazi kubwa na muhimu ya kupanda miti katika barabara hii, nisingependa kutumia muda wenu zaidi, hivyo basi nachukua fursa hii kukushukuruni nyote kwa kushiriki katika Uzinduzi huu. Pia nakushukuruni sana kwa utulivu na uvumilivu wenu kwa muda wote nilipokuwa nikizungumza.

Ahsanteni sana.             



1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.