Habari za Punde

Hotuba ya Mwenyekiti wa kamati ya Katiba, Sheria na Utawala

HOTUBA YA MWENYEKITI WA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA UTAWALA YA BARAZA LA WAWAKILISHI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA NCHI OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ 2014/2015

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kunijaalia afya njema na uzima wa kuweza kusimama mbele ya Baraza lako tukufu katika  kutekeleza majukumu ya kulijenga taifa letu. Aidha napenda kwa moyo wa dhati nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii muhimu ya kutoa maoni ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kwa mwaka wa fedha 2014/2015.

Mheshimiwa Spika, Napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Haji Omar Kheir mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Tumbatu pamoja na watendaji wake wote kwa juhudi zake anazozichukua na hatimae katika muda mfupi tu tokea ateuliwe  matunda ya juhudi zake yameanza kuonekana.

Mheshimiwa Spika, Kamati katika kipindi cha utekelezaji wa majukumu yake ilifanya kazi nzuri ya kuzipitia bajeti za Wizara husika na kutoa maelekezo yenye lengo la kuleta ufanisi wa majukumu ya kila siku ambapo Wajumbe wote walitoa ushirikiano wa hali ya juu katika kutekeleza wajibu wao wa kuikosoa Serikali pale panapohitajika.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru Wajumbe wote wa Kamati kwa umakini wao wakati wa Kazi za Kamati. Shukurani hizo pekee hazitatosha iwapo sitowataja wajumbe wa Kamati hii kwa majina yao, Pai naomba kuchukua nafasi hii kumkaribisha rasmi Mjumbe mpya wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki ambae ameletwa katika Kamati hii.

Mheshimiwa Spika, Wajumbe wa Kamati hii naomba kuwataja kama ifuatavyo:

  1. Mhe. Ussi Jecha SImai                                   Mwenyekiti
  2. Mhe. Abdalla Juma Abdalla                            Makamo Mwenyekiti
  3. Bikame Yussuf Hamad                                   Mjumbe
  4. Mhe. Mahmoud Thabit Kombo                        Mjumbe
  5. Nassor Salum Ali                                           Mjumbe
  6. Mhe. Suleiman Hemed Khamis                        Mjumbe
  7. Mhe. Wanu Hafidh Ameir                                Mjumbe
  8. Ndg. Aziza Wazir Kheir                                    Katibu
  9. Ndg. Khamis Hamad Haji                                 Katibu

 

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ ni miongoni mwa Wizara za Serikali ambazo zina majukumu mazito ya kutoa huduma kwa wananchi ambao wana mahitaji mengi ya msingi yanayohitaji kutekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, Wananchi waliowengi kipato chao ni duni na hivyo mahitaji yaio mengi ya msingi wanategemea kuyapata kupitia huduma zinazotolewa na baadhi ya taasisi za Serikali ambazo zinahusika na utoaji wa huduma hizo ambapo watumishi9 wa Serikali wanapaswa kutumia utaalamu na ujuzi wao wote kwa lengo la kuisaidia Serikali kufikisha huduma hizo kwa wananchi.

IDARA YA MIPANGO, SERA NA UTAFITI

Mheshimiwa Spika, Pamoja na majukumu mengine ya msingi, kazi kubwa ya Idara hii katika mwaka huu wa fedha ni kuandaa na kuhakikisha kuwa mpango wa kupunguza umaskini unatekelezeka. Aidha Idara ina wajibu wa kusimamia utekelezaji wa sera na sheria mbali mbali zilizo chini ya Wizara hii kwa lengo la kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na huduma zinazotolewa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa kuendeleza miradi mikubwa na midogo midogo ya maendelea katika ngazi za Serikali za mitaa ni mizuri, hata hivyo Kamati inaishauri Wizara kutekeleza mipango hiyo kwa kasi zaidi na kwa wale wananchi ambao wanakiuka amri halali za Serikali katika utekelezaji huo wachukuliwe hatua za kisheria.

Mheshimiwa Spika, Malengo makubwa kwa mwaka ujao wa fedha ni kuanzisha na kuzindua kamati ya uratibu wa shughuli za mipango katika ofisi. Kamati inakubaliana na wazo hilo la kuanzisha kamati amabyo itakuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa shughuli zote za Wizara zinatekelezwa kama zilivyopangwa jambo amablo litasaidia kuondoa baadhi ya kero zinazowakabili wananchi hivi sasa. Aidha Kamati inazidi kusisitiza kuwa Idara ina wajibu wa kuhakikisha kuwa inafuatilia utekelezaji wa kila robo mwaka wa Bajeti kwa upande wa Pemba ili malengo yaliyopangwa kwa kila mwaka yaweze kutekelezeka.

IDARA YA UENDESHAJI NA UTUMISHI

Mheshimiwa Spika, Idara hii ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa Wizara inaimarisha mipango yake ya upatikanaji wa rasilmali watu ambao watakua na ujuzi wa kutosha ambao wataisaidia Wizara kutekeleza mipango yake iliyojipangia kwa ufanisi mkubwa. Aidha Idara inawajibu wa kuhakikisha inatoa mafunzo ya muda mfupi yanayowajengea uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao. Aidha, Kamati inaishauri Idara kuweka mazingira mazuri ya kiutawala ambayo yatasaidia kuwa na maelewano baina ya wafanyakazi.

IDARA YA URATIBU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

Mheshimiwa Spika, Suala kubwa ambalo kamati inataka kusisitiza hapa ni ushirikiano baina ya viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao ni kiungo kikubwa katika maeneo yetu. Aidha Kamati imekubaliana na mpango wa Wizara uliowekwa kwa mwaka ujao wa fedha wa kuandaa vikao baina ya viongozi hao. Vikao hivyo vitasaidia kujua changamoto zilizopo baina ya viongozi hao ambao ni chachu ya maendeleo katika Serikali zetu za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, kumekua na changamoto kubwa hivi sasa ya kuibuka kwa bandari bubu katika baadhi ya maeneo mbali mbali ya Mikoa yetu. Hivi sasa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wananchi kuzitumia bandari hizo kwa kuwasafirisha wananchi kutoak sehemu moja kwenda nyuengine kwa kutumia majahazi na maboti ambayo hayajasajiliwa kuoakia abiria kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, jambo hili limekuwa ni chanzo cha kusafirishia silaha na magendo mbali mbali wakiwemo wanyama kutoka bara kuja hapa Zanzibar. Hali hiyo pia inahatarisha usalama wa afya za wananchi wetu kutokana na hao wanyama wanaosafirishwa kutofanyiwa uchunguzi wa kina hatimae kuingiza maradhi mbali mbali hapa nchini. Hivyo Kamati inaitaka Serikali kupitia Wizara kuzifunga shughuli zote zisizoruhusiwa katika bandari hizo, Kamati inaona kufanya hivyo kutaepusha mambo mengi ya kihalifu ambayo yamekuwa yakijitokeza hivi sasa hapa nchini likiwemo tukio la hivi karibuni la kukamatwa kwa silaha iliyoingizwa katika bandari ya Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini A.

Mheshimiwa Spika, Baadhi ya vipaumbele na mipango ya utekelezaji tunayoipanga na kuamua katika chombo hiki haitekelezeki siyo kwa sababu ya ufinyu wa bajeti peke yake, bali mengine inakwamishwa kutokana na aidha utendaji kazi uliochini ya kiwango na kutojali kwa baadhi ya watumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao ya msingi na ukaidi wa baadhi ya wananchi ambao mara nyingi wanapopewa amri na Serikali hukataa kuitii amri hizo.

Mheshimwa Spika, Uporomokaji huu wa maadili kwa baadhi ya watumishi wa Serikali umechangiwa sana na mifumo yetu mibovu ya uajiri huko nyuma na baadhi ya wananchi kutegemea viongozi wanaowajua ambao mara nyingi huwatetea Serikalini. Kamati inashauri Wizara kupitia bajeti ya mwaka huu kufanya kampeni maalumu na kuchukua hatua za lazima inapobidi kwa mujibu wa sheria, kuwashughulikia watumishi wa umma wasiozingatia maadili ya utumishi na wananchi wote wanaokataa kutii mari ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Sera na Kanuni za Serikali za mitaa ndio miongozo inayotumika katika utekelezaji wa mipango yote inayopangwa katika Taasisi hizo, hivyo ni wajibu wa Idara kuhakikisha kua inatoa mafunzo maalum kwa wananchi na taasisi zinazohusika kuhusiana na sera na kanuni hizo, kwa lengo la kuhakikisha kuwa mipango inayopangwa kwa wananchi inatekeleza bila kikwazo cha aina yoyote. Aidha Kamati inachukua nafasi hii kuipongeza Wizara kwa taarifa iliyoipatia Kamati kuwa wanategemea kuleta Mswada wa dharura wa marekebishio ya Sheria za Serikali za mitaa ambazo ni Mswada wa Sheria ya Tawala za Mikoa, Mswada wa Sheria ya Serikali za Mitaa na Mswada wa kuanzisha Shirika la Ulinzi la JKU. Kabla ya hapo kumekua na kilio cha muda mrefu ambacho Kamati kila Wilaya na Mkoa inaoupita inapewa malalamiko ya kuwepo kwa mgongano wa tafsiri za Kisheria ambazo zimekuwa ni kikwazo cha utekelezaji wa baadhi ya mipango ya Mikoa na Wilaya. Hivyo kuletwa kwa Miswada hiyo ya kisheria Kamati inaamini kuwa itaondosha migongano ya kisheria iliyokuwepo

TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

Mheshimiwa Spika, Kamati yetu kabla ya kupitia bajeti ya Wizara na kuipitisha ilipata nafasi ya kufanya kazi zake za kawaida na ilipata nafasi ya kukagua baadhi ya Wilaya na Mikoa ya kisiwa cha Unguja ukiwemo Mkoa na Wilaya ya Kusini Unguja, Hlmashauri ya Wilaya ya Kaskazinia “A”, Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “B” , na Halmashauri ya Wilaya ya Kati . Katika ziara hizo Kamati ilipata nafasi ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Bajeti na kuelezwa mambo mbali mbali zikiwemo changamoto ambazo nyingi kati ya hizo changamoto zinasababishwa na ufinyu wa bajeti. Kamati ilielezwa kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa usafiri wa uhakika kwa wafanyakazi, hali hiyo inasababishwa na bajeti finyu inayopelekwa ambayo haikidhi haja na hatimae wanashindwa kununua hata gari ya Ofisi.

Mheshimiwa Spika, Kamati pia ilipata changamoto ya malipo madogo ya wazee wanayolipwa kupitia Mikoa yao kila mwisho wa mwezi, Kamati ilielezwa kuwa posho la wazee hao ni shilingi elfu tano kwa mwezi wanayopatiwa ambayo Kamati inahisi kuwa kimo hicho ni kidogo na inaishauri Serikali ifanye utaratibu wa kuwaongezea wazee hao wanaoishi katika mazingira magumu angalau fehda hizo ziwe shilingi elfu hamsini kwa mwezi.

Mheshimiwa Spika, Kamati pia ilipata taarifa katika kila Mkoa na Wilaya iliyokua inakaguliwa kuwa Sheria nyingi zilizopo hivi sasa za Serikali za Mitaa zimepitwa na wakati, aidha sheria hizo hizo pia zinagongana na sheria za taasisi nyengine jambo ambalo limekua linazikosesha mapato Halmashauri zetu. Hivyo Kamati inapenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Wizara kwa uamuzi wake huo wa busara ambao utasaidia kuondoa changamoto zilizopo kama tulivyoeleza mwanzo katika hotuba hii.

Mheshimiwa Spika, Kamati inazipongeza Wilaya na Mikoa yote katika jitihada zao za kuhakikisha kuwa suala la ulinzi na usalama linaimarika kwa pia inazidi kusisitiza kuwa ulizni shirikishi ni suala la msingi ni vyema likazidi kuekewa mkazo kwa kuwashirikisha wananchi kila panapohitajika.

Mheshimiwa Spika, katika ziara za Kamati ilipotembelea Baraza la Manispa ilipatiwa changamoto mbali mbali zinazolikabili Baraza hilo ikiwemo changamoto ya uchache wa wafanyakazi jambo ambalo linapunguza kasi ya utendaji kazi hasa kazi ya uzoaji wa taka taka. Aidha Katika suala zima la kuweka mazingira ya maeneo yetu katika hali ya usafi, Kamati ilisikitishwa sana na taarifa kuwa kuna baadhi ya wananchi wamekua na tabia ya kukaidi amri ya kuzihifadhi taka taka katika maeneo ya kuwekea taka hizo. Hali hiyo imekua ikizorotesha juhudi zinazofanywa na Baraza hilo na kusababisha kuzagaa ovyo kwa taka hizo. Kutokana na hali hiyo Kamati inaishauri Wizara na Serikali kwa ujumla kuweka utaratibu maalum wa kuizuia hali hiyo na ikiwezekana mtu yeyote atakayevunja amri ya kuzihifadhi taka zake atozwe faini au adhabu yoyote itakayofaa ichukuliwe dhidi yake. Kamati inaipongeza Serikali kwa uwamuzi wake wa kuwaingiza wafanyakazi wa Baraza la Manispaa katika “Vote” ya mishahara ya Serikali jambo amablo litasaidia fedha wanazozikusanya kutoakana na vyanzo mbali mbali vya mapato kununulia vitendea kazi.  Aidha Kamati inapenda kuchuku nafasi hii kuipongeza Serikali kwa mpango wake wa kutaka kuliendeleza eneo la Darajani kwa kujenga maduka ya kisasa ambayo yatakuwa ni chachu ya maendeleo katika nchi yetu.

 

AFISI YA USAJILI NA KADI ZA UTAMBULISHO

Mheshimiwa Spika, Bado kuna umuhimu mkubwa wa Idara kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na umuhimu wa Vitambulisho ambapo baadhi ya wananchi hadi hii leo hawana vitambulisho hivyo. Hali hii inatokana na uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi ambao baadhi yao vitambulisho vyao hadi hii leo kwa taarifa za awali hawajaenda kuvichukua. Aidha Kamati inapenda kuchukua nafasi hii kuwahamasisha wananchi wale ambao hawana vitambulisho kufuata taratibu na kwenda kuchukua vitambulisho ambavyo ni utambulisho wa Taifa. Aidha katika kikao cha kupitisha Bajeti Kamati ilipewa taarifa kuwa Idara haikukadiriwa mapato yake kutokana na mjadala uliokuwepo hivi sasa juu ya suala la ada ya vitambulisho vya wageni ambapo suala hilo hivi sasa kutokana na Kanuni zake kutokamilika hivyo suala hilo litakaa sawa hapo mjadala wa Kanuni hizo utakapokamilika. Vile vile Idara inakusanya ada ya wanaopoteza vitambulisho ambapo Kamati ilipotaka maelezo juu ya suala hilo ilipewa taarifa hiyo na Kamati iliridhika.

IDARA MAALUM ZA SMZ

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inapenda kuchukua nafasi hii kuzipongeza Idara Maalum zote za SMZ kwa juhudi wanazozichukua katika kutimiza wajibu wao pamoja na changamoto nyingi wanazokabiliana nazo. Aidha Kamati wakati inafanya ziara zake katika baadhi ya Idara hizo ilijionea changamoto ya ukosefu wa makaazi ya kudumu ya watumishi hao ambapo baadhi ya nyumba wanazoishi hazifai kwa makaazi ya binaadamu, kutokana na hali hiyo Kamati inaishauri Wizara kuliangalia suala hilo kwa umakini mkubwa kwa kuhakikisha kuwa makaazi ya watumishi hao yanajengwa ili waweze kutimiza wajibu wao kwa umakini zaidi.

Mheshimiwa Spika, Suala la ubunifu kwa Idara Maalum ni suala la kupigiwa mfano kutokana na miradi mingi ya maendeleo inayobuniwa na Idara hizo ambapo mingi ya miradi hiyo endapo itatengewa bajeti za kutosha itaimarika na kuziimarisha Idara hizo kutokana na fedha zitakazopatikana katika miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilipokua katika ziara zake za kikazi katika Kikosi cha Valantia, ilikagua kiwanda cha kutengenezea viatu ambacho kinatengeneza viatu hivyo kwa uimara wa hali ya juu pamoja na hali ngumu iliyopo kiwandani hapo. Hivyo Kamati inaiomba Wizara ifanye mpango wa kukiendeleza kiwanda hicho kwa kuhakikisha kuwa anaajiriwa mtaalamu mwenye uwezo wa hali ya juu kutokana na mtaalamu anayetumika hivi sasa kutoajariwa na Idara hiyo na anafanya kazi ya kuwafundisha vijana waliopo pale kwa makubaliano maalum, aidha Kamati inaishauri Wizara kuwatafuta wafadhili hata nje ya nchi kwa ajilia ya kuwaendeleza vijana waliopo katika kiwanda hicho ili wakajifunze mbinu nyengine nzuri zaidi ambazo zitawezesha kukiendeleza kiwanda hicho.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilipata nafasi ya kukagua mradi wa ujenzi wa skuli ya ufundi ya JKU iliyopo Mtoni ambayo ujenzi wake umefikia hatua nzuri hadi hivi sasa. Kukamilika kwa mradi huo kutaisaidia jamii yetu kupunguza tatizo kubwa liliopo hivi sasa la ukosefu wa ajira kwa vijana wetu ambao wengi wao hawana ajira za kudumu, hata hivyo katika bajeti ya mwaka huu fedha za maendeleo katika Idara hii zilizotengwa ni kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga, pamoja na umuhimu wake kilimo hicho suala la ujenzi wa skuli hiyo pia ni muhimu zaidi, hivyo Kamati inatoa ushauri kuwa Serikali ifanye juhudi zake zote kuhakikisha kuwa skuli hiyo inakamilishwa hasa tukizingatia kuwa ujenzi wa mnara wa miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar fedha zake zilipatikana japokuwa hazikuainishwa katika bajeti iliyopita.

 Mheshimiwa Spika, Chuo cha Mafunzo ni miongoni mwa Idara zinazokumbwa na changamoto kubwa ya kutoa huduma kwa wananchi hasa wale wanowekwa katika magereza yetu, hivyo Kamati inaishauri Serikali inapopanga bajeti za kila Wizara ihakikishe kuwa inatoa kipaumbele kwa Idara hii kutokana na huduma za msingi zinazohitajika katika Idara hii ikiwemo ya malazi, makaazi na chakula. Kamati inazidi kusisitiza kuwa ujenzi wa gereza jipya la Hanyegwa Mchana ni wa lazima na Serikali haina budi kuhakikisha kuwa inatafuta wafadhili watakaoweza kutusaidia kukamilisha ujenzi wake.

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inapenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Idara ya Chuo cha Mafunzo kwa juhudi zake za kuanzisha mradi wa ujenzi wa maduka ambayo kukamilika kwake na mapato yake yataisaidia Idara hiyo kukwamua baadhi ya changamoto zilizopo.

Mheshimiwa Spika, Wito wa Kamati yangu kwa Serikali katika mwaka huu wa fedha ni kuitaka ihakikishe inatekeleza malengo waliyojipangia, ikiwa ni pamoja na kukamilisha mapitio ya huduma za sheria ya Idara Maalum, Sheria Namba 6 ya 2007 na Kanuni zake. Aidha Kamati inasisitiza kuwa Idara Maalum zote ikiwemo Idara ya Zimamoto na Uokozi, Kikosi cha Kuzuia Magendo, ni muhimu sana katika ustawi wa taifa letu hivyo Serikali ina wajibu wa kuwawekea mazingira mazuri ya kazi ili vijana wetu waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inaendelea kusisitiza suala la kuwalipa mishahara mizuri watendaji wa Idara Maalum zote kutokana na kazi nzito wanazozifanya na zinazolingana na wenzao wa Taasisi za Muungano ambao wanalipwa vizuri zaidi ukilinganisha na wao. Aidha Kamati haijaridhishwa na hali hii ya watumishi wa Idara Maalum kulipwa kiwango kidogo cha mishahara na inapendekeza hatua za haraka zichukuliwe na Serikali kukaa tena na Uongozi wa Wizara kujadiliana tena viwango vipya vya Mishahara inayolingana na wenzao wa Tanzania bara.

TUME YA UTUMISHI YA IDARA MAALUM

Mheshimiwa Spika, Tume hii ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa Idara Maalum za SMZ zinafanya zoezi la uajiri pamoja na kuweka mazingira bora yatakayoimarisha mazingira ya Utumishi kwa watendaji wa Idara hizo.

 Kamati yangu inazidi kuisisitiza Tume kusimamia zoezi zima la uajiri kwa haki ili kuepusha malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wananchi kipindi cha uajiri kinapofika. Kumekuwa na taarifa zisizoridhisha kinapofika kipindi cha uajiri ambapo kumekua na baadhi ya maafisa wasiokuwa waaminifu kuwalaghai wananchi kuwa watawapatia ajira kwa urahisi na kinachotakiwa ni wananchi hao kutoa fedha kwa ajili ya kuwafanyia mipango hiyo, malalamiko hayo yamekuwa ni mengi sana, hivyo Kamati inatoa agizo kwa Afisa yeyote atakayepatikana na kadhia ya kufanya kitendo hicho achukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo ambazo zimekuwa ni kikwazo na zinachafua jina la taasisi zetu.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Wizara kupitia Tume ya Utumishi ya Idara Maalum za SMZ kwa uamuzi wake wa kuwafundisha wapiganaji pamoja na maofisa wake Sheria mbali mbali za nchi ikiwemo Sheria ya Utumishi wa Umma pamoja na masuala ya Utawala na Uongozi ili kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, Mwisho naomba nichukue fursa hii kukushukuru wewe pamoja na Wajumbe wako wote wa Baraza hili tukufu kwa kunisikiliza kwa utulivu na umakini mkubwa.

Mheshimiwa Spika, Nawaomba wajumbe wako waichangie bajeti hii, watoe mapendekezo yao panapohitajika na hatimaye kuipitisha baada ya kuafikiana kwa hoja mbali mbali watakazoibua wakati wa mjadala.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

 

………………………………………..

Ussi Jesha Simai,

Mwenyekiti,

Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala,

Baraza la Wawakilishi,

Zanzibar.

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.