Na Laylat Khalfan
Idadi ya watoto wanaoungua moto inaongezeka
kila mwaka, ambapo zaidi ya watoto 948 waliungua moto na kulazwa katika
hospitali kuu ya Mnazimmoja katika kipindi cha mwaka 2012 na 2013.
Akizungumza kwa huzuni na mwandishi wa
habari hizi, Katibu wa hospitali hiyo,
Hassan Makame Mcha, alisema watoto wanaoungua moto ni wale wenye umri wa
kuanzia miezi sita ambao wako katika hatua ya kutambaa.
Alisema watoto hao walilazwa katika
hospitali hiyo wakiwa na majeraha mabaya ya kuungua uji moto, maji, chain a
wengine kuungua moto wenyewe.
Alisema chanzo cha watoto wengi kuungua
moto, ni wazazi kutokuwa makini kuwaangalia watoto wao hasa katika hatua ya
kutambaa.
Alisema akina mama wengi ni wazembe na
wafuatilii nyenendo za watoto wao, ambao wanahitaji uangalizi wa karibu hasa
wakati wa kutambaa ili kuondoa hatari ya kuungua na kuwasababishia makovu ya
muda mrefu na wakati mwengine kupoteza maisha.
Alisema ili kukabiliana na wazazi wazembe,
serikali haina budi kuanzisha kitengo maalum kitakachotoa adhabu kali kwa
wazazi wazembe wasiowachunga watoto wao na kusababisha kuungua.
Aidha alisema ipo haja kwa wazazi kuwa
makini na kuwachunga watoto wao hasa katika umri wa kutambaa ili kuwanusuru na
matukio ya kuungua moto.
No comments:
Post a Comment