Habari za Punde

Hotuba wa mapato na matumizi Wizara ya Uwezeshaji, ustawi wa jamii,vijana ,wanawake na watoto

MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA

2014/2015 - Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii,

Vijana, Wanawake na Watoto

 
 
UTANGULIZI:
 
1.                  Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu likae kama Kamati ya matumizi ili liweze kupokea, kujadili na kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
 
2.                  Mheshimiwa Spika, Naomba kuchukua fursa hii adhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia kwa mara nyengine kukutana hapa leo, tukiwa wazima wa afya. Aidha, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia mimi mwenyewe afya njema na uzima, nikaweza kusimama hapa leo kuwasilisha mbele ya Baraza lako Tukufu, Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
 
3.                  Mheshimiwa Spika, Kwa niaba yangu na Wafanyakazi wa Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jami, Vijana, Wanawake na Watoto, nachukua fursa hii adhimu kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa  kutuongoza vyema katika safari yetu ya kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Uongozi wake mahiri, thabiti na makini umeendelea kuwa dira katika utendaji wa kazi zetu. Tunaomba Mwenyezi Mungu azidi kumjaalia afya njema, maarifa na hekima katika kuiongoza nchi yetu, ili tuweze kufikia matarajio na malengo tuliyojiwekea katika kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
 
4.                  Mheshimiwa Spika, Pia napenda nichukue nafasi hii kuwapongeza Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharrif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi kwa kumshauri na kumsaidia kwa karibu Mheshimiwa Rais wa Zanzibar katika utekelezaji wa majukumu yake. Aidha, nachukua fursa hii kukushukuru wewe binafsi   Mheshimiwa Spika kwa kuendelea kuliongoza Baraza hili Tukufu kwa hekima, busara na uadilifu. Umahiri wako katika kuliendesha Baraza hili, umewezesha kuwepo kwa mijadala makini, ambayo imesaidia sana kuimarisha utekelezaji wa majukumu yetu ndani ya Serikali.
 
 
5.                  Mheshimiwa Spika, Napenda kuchukuwa fursa hii kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wote kwa kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Sherehe za maadhimisho haya zilitupa fursa ya kutathmini mafanikio tuliyoyapata kupitia sekta mbali mbali katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Aidha, zilitupa fursa ya kutafakari changamoto tunazopaswa kuzifanyia kazi, ili kuleta maendeleo endelevu kwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii. Napenda sana kumpongeza Mhe. Makamu wa Pili wa Rais na Wafanyakazi wake wote kwa kuratibu Sherehe hizi kwa ufanisi mkubwa, na hivyo kuweza kudhihirisha maendeleo ya kupigiwa mfano yaliyopatikana katika miaka hii 50 ya Mapinduzi. 
 
6.                  Mheshimiwa Spika, Napenda pia kuzipongeza Serikali zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuandaa na kufanikisha sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Aidha, sote tunapaswa kujipongeza kwa kuweza kuudumisha Muungano huu hadi kufikia miaka 50 na huku tukiendeleza amani na mshikamano katika nchi yetu. Sherehe zilionesha namna gani tumejizatiti kuendelea kuudumisha Muungano wetu, ambao ni wa kipekee na wa mfano Barani Afrika. Napenda kuwapongeza viongozi wetu mahiri Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa mafanikio hayo.
 
7.                  Mheshimiwa Spika, Nachukua fursa hii kuishukuru Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii ya Baraza lako Tukufu chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma, pamoja na wajumbe wake wote kwa ushirikiano, mawazo na michango waliyotupa, ambayo imeisaidia Wizara kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake. Ni matarajio yangu kwamba tutaendelea kushirikiana kwa pamoja katika kuimarisha utekelezaji wa majukumu yetu, ili kuleta mabadiliko yanayotarajiwa ya hali za wanawake, vijana, watoto, wazee na jamii kwa ujumla. Pia, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza lako tukufu kwa miongozo na michango yao, iliyotuwezesha kutekeleza majukumu ya Wizara kwa ufanisi. Aidha, napenda pia nichukue fursa hii kumpongeza Mhe. Mahmoud Thabit Kombo kwa kuchaguliwa kuwa Mwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki na kujiunga nasi katika shughuli za Baraza hili.
 
8.                  Mheshimiwa Spika, Utakumbuka kwamba mwaka jana nilisoma mbele ya Baraza lako tukufu Hotuba ya Bajeti kwa Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto. Mabadiliko ya baadhi ya Wizara yaliyofanywa mwezi Agosti 2013, yalipelekea kuanzishwa kwa Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto. Napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kuniamini na kuniteua kuiongoza Wizara hii.
 
MWELEKEO WA BAJETI KWA MWAKA 2014/2015
 
9.                  Mheshimiwa Spika, Bajeti na shughuli zilizopangwa kutekelezwa na Wizara yangu kwa mwaka wa fedha 2014/2015 zimezingatia Mipango Mikuu ya Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ni Dira ya Maendeleo ya 2020, Mkakati wa Kukuza  Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA II – 2010-2015), Malengo ya Milenia 2015, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2010-2015, Mwelekeo wa Sera za CCM 2010-2020, Mwelekeo wa Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2014/2015, Sera za Kisekta pamoja na Mpango Mkakati wa Wizara. Aidha, matumizi ya Wizara yataelekezwa zaidi katika kuimarisha programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi, hifadhi ya jamii kwa wazee na watu wanaoishi katika mazingira magumu zaidi, maendeleo ya vijana, mapambano dhidi ya udhalilishaji wa wanawake na watoto, pamoja na kushajiisha usawa na uwiano wa kijinsia.
 
10.              Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kipindi cha mwaka 2014/2015 imejipangia kutekeleza malengo makuu yafuatayo:
 
1.      Kuimarisha hali za kiuchumi na kijamii za Vijana, Wanawake, Watoto, Wazee, makundi yanayoishi katika mazingira magumu na jamii kwa ujumla;
 
2.      Kuhakikisha kuwa mapungufu ya sera na sheria katika masuala ya uwezeshaji na yanayohusu watoto, wanawake, vijana, wazee na makundi yanayoishi katika mazingira magumu yanafanyiwa kazi;
 
3.      Kuimarisha ubora wa huduma na upatikanaji wa hifadhi ya jamii kwa watoto, wanawake, vijana, wazee na makundi yanayoishi katika mazingira magumu;
 
4.      Kuhakikisha kuwa taarifa zinazohusu masuala ya wanawake, vijana, watoto, wazee, hifadhi ya jamii na uwezeshaji wananchi kiuchumi zinakusanywa na kutumiwa katika kuandaa na kuimarisha sera, mikakati na programu;
 
5.      Kukuza uwelewa wa jamii juu ya dhana, misingi na kanuni za Ushirika; na
 
6.      Kuimarisha uwezo wa Wizara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
 
 
MUHTASARI WA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2013/2014
 
11.              Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2013/2014,Wizara ilipangiwa kukusanya mapato ya jumla ya Shilingi Milioni Kumi (Tshs. 10,000,000) kutokana na usajili na huduma za ukaguzi wa vyama vya ushirika. Hadi kufikia mwezi wa Mei 2014, jumla ya Shilingi Milioni Tano, laki Tisa na Elfu Thamanini na Tano (Tshs. 5,985,000/=) zilikuwa zimekusanywa, sawa na asilimia 60 ya makadirio kwa mwaka 2013/2014.
 
12.              Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014, Wizara ilitengewa  Shilingi Bilioni Tatu, Milioni Mia Mbili Arobaini na Tisa, Laki Sita na Elfu Ishirini na Mbili (Tshs. 3,249,622,000/=) kwa matumizi ya kazi za kawaida, ikiwa ni pamoja na mishahara. Hadi kufikia mwezi wa Mei, 2014, fedha zilizotolewa ni Shilingi Bilioni Mbili, Milioni Mia Nne na Tisini na Tano, Laki Tatu na Hamsini Elfu (Tshs.2,495,350,000/=) ambayo ni sawa na asilimia 77 ya fedha zilizotengwa. Aidha, Wizara ilitengewa jumla ya Shilingi Bilioni Moja, Milioni Mia Nane na Themanini (Tshs.1,880,000,000/=) kwa kazi za maendeleo. Fedha zilizotolewa kwa kazi hizo mpaka kufikia mwezi Mei, 2014 ni Shilingi Milioni Mia Tano Arobaini na Mbili, Laki Mbili na Elfu Tisini na Mbili (Tshs.542,292,000/=), ambazo ni sawa na asilimia  29 ya fedha zilizotengwa (Angalia Kiambatanisho Namb. 1a na 1b).
 
UTEKELEZAJI WA MALENGO YA WIZARA KWA MWAKA 2013/2014
 
13.              Mheshimiwa Spika, Majukumu ya Wizara hii yanatekelezwa kupitia Idara zake nane na Ofisi kuu Pemba kama zifuatazo:
 
1.      Idara ya Mipango, Sera na Utafiti;
 
2.      Idara ya Uendeshaji na Utumishi;
 
3.      Idara ya Uendelezaji na Uratibu wa Programu za Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi;
 
4.      Idara ya Ushirika;
 
5.      Idara ya Mikopo;
 
6.      Idara ya Ustawi wa Jamii,
 
7.      Idara ya Maendeleo ya Vijana; na
 
8.      Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto.
 
9.      Ofisi Kuu Pemba inasimamia shughuli zote za Wizara, ikiwemo majukumu ya Idara hizi kwa Pemba.
 
Utekelezaji wa malengo ya Wizara kupitia Idara hizi kwa mwaka 2013/2014 na malengo kwa mwaka 2014/2015 ni kama ifuatavyo:
 
IDARA YA MIPANGO, SERA NA UTAFITI
 
14.              Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2013/2014, Idara hii ilijipangia kutekeleza malengo yafuatayo:
 
1.      Kusimamia uingizwaji wa masuala ya jinsia na mtambuka katika mipango, bajeti, programu/miradi na sera za kisekta na Wizara;
2.      Kusimamia uandaaji wa tafiti mbili zinazohusu masuala ya jinsia na maendeleo ya vikundi vya wanawake;
3.      Kuimarisha uratibu, uandaaji na ukusanyaji wa taarifa, ufuatiliaji na tathmini ya mipango, programu na bajeti ya Wizara;
4.      Kuimarisha mashirikiano ya kitaifa, kikanda na kimataifa ili kuleta maendeleo na ustawi wa wanawake, vijana, wazee na watoto; na
5.      Kusimamia utekelezaji wa miradi ya Wizara.
 
Utekelezaji wa malengo ya Idara ya Mipango, Sera na Utafiti kwa mwaka 2013/2014:
 
15.              Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa majukumu ya Idara ya Mipango, Sera na Utafiti ni kusimamia uandaaji wa sera, ili kujenga mfumo mzuri wa utekelezaji wa shughuli inazozisimamia. Katika hili, Wizara tayari imekamilisha Sera ya Maendeleo ya Ushirika na Sera ya Hifadhi ya Jamii, ambazo zimeshapitishwa rasmi na ziko tayari kutumika. Sera hizi zitakuwa ndio dira na miongozo katika uendeshaji wa vyama vya ushirika na usimamiaji wa mipango ya hifadhi ya jamii Zanzibar.
 
16.              Mheshimiwa Spika, Wizara pia imeandaa rasimu ya Sera ya Jinsia ambayo ipo tayari kujadiliwa katika kikao cha Kamati ya Makatibu Wakuu. Sambamba na hilo, Wizara inaandaa Mpango wa utekelezaji wa Sera hiyo. Rasimu ya Sera ya Maendeleo ya Vijana nayo imekamilika na matayarisho yanafanywa ili kuiwasilisha katika vikao vya maamuzi. Pia Wizara imo katika hatua ya kutayarisha Sera ya Uwezeshaji, ambapo rasimu ya mwanzo ipo tayari, inasubiri kujadiliwa katika Kikao cha Kamati ya Uongozi ya Wizara na hatimae kuwasilishwa katika ngazi nyengine za maamuzi.
 
17.              Mheshimiwa Spika, Wizara imefanya mapitio ya Mpango Mkakati wake ili uendane na mabadiliko yaliyofanywa kuhusiana na majukumu yake na kushughulikia changamoto mpya zilizojitokeza. Mpango Mkakati huo umekamilika na umetumika katika uandaaji wa Mpango wa Matumizi wa Muda wa Kati kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015.
 
18.              Mheshimiwa Spika, Wizara imetayarisha na kuwasilisha kunakohusika ripoti mbali mbali zinazohusiana na utekelezaji wa majukumu yake. Taarifa hizo ni pamoja na zinazohusu utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na Wizara, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2005) na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa  Wizara.  Aidha, ziara za ufuatiliaji zimefanywa ili kuangalia utekelezaji wa programu za Wizara.
 
19.              Mheshimiwa Spika, Wizara imo katika hatua ya kukusanya Taarifa za Hali ya Kijinsia (Gender Profile) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali. Kuwepo kwa taarifa hizo kutasaidia uandaaji wa Sera na Mipango ya Kitaifa inayozingatia masuala ya kijinsia.
 
20.              Mheshimiwa Spika, Ili kuimarisha uzingatiaji wa masuala mtambuka katika sera, mipango na program za Wizara, mafunzo yametolewa kwa wajumbe wa Kamati ya Wizara inayoshughulikia masuala mtambuka kwa upande wa Unguja. Mafunzo hayo ni pamoja na yaliyohusu uzingatiaji wa masuala ya kijinsia katika bajeti, mipango, sera na programu na masuala ya uwezeshaji na ujasiriamali. Kwa upande wa Pemba, wafanyakazi na familia zao wamepatiwa mafunzo ya kujikinga na maambukizo ya virusi vya UKIMWI na vifo vitokanavyo na UKIMWI, pamoja na kuhimiza utendaji wa kazi kwa kuzingatia jinsia.
 
21.              Mheshimiwa Spika, Kamati 18 za Shehia Pemba na 10 Unguja za kupinga vitendo vya udhalilishaji zimefuatiliwa ili kutathmini utekelezaji wa shughuli zao na kupewa ushauri na maelekezo ya kuwasaidia kuimarisha kazi zao. Aidha, jumla ya vijana 120 kutoka Mikoa 3 ya Unguja na 80 kutoka Mikoa miwili ya Pemba walipatiwa mafunzo ya kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na kuepukana na mimba na ndoa za utotoni. Vile vile, Wizara imesimamia uundwaji wa kamati kumi na moja (11) za Shehia za kupambana na udhalilishaji wa kijinsia katika Wilaya ya Chake Chake, Pemba. Aidha, Kamati hizo zilipewa maelekezo na kujengewa uwezo wa kusimamia shughuli zao kwa kushirikiana na Masheha na Waratibu wa Wanawake na Watoto wa Shehia.
 
22.              Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa taarifa mbali mbali kupitia vyombo vya habari ili kuielewesha jamii juu ya shughuli inazozitekeleza. Jumla ya taarifa 17 za matukio mbali mbali ya Wizara zilirushwa hewani kupitia vyombo vya habari. Pia vipindi vitatu (3) vya redio na televisheni kwa ajili ya kushajiisha jamii kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia viliandaliwa na kurushwa hewani. Vile vile, makala mbili (2) zilizozungumzia masuala ya haki za wanawake na kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ziliandaliwa na kutolewa katika Gazeti la “Zanzibar Leo”. 
 
Utekelezaji wa Programu zinazosimamiwa na Idara ya Mipango Sera na Utafiti
 
23.              Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika kipindi cha mwaka 2013/2014 imesimamia utekelezaji wa Programu mbili zifuatazo:
 
Programu ya Jinsia Zanzibar
 
24.              Mheshimiwa Spika, Programu hii inatekelezwa kwa  kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu (UNFPA). Madhumuni ya programu hii ni kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzingatia masuala ya kijinsia katika sera, mipango na bajeti, pamoja na kuzijengea uwezo taasisi mbalimbali na wananchi katika kupambana na udhalilishaji wa kijinsia.
 
25.              Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2013/2014, Wizara kupitia programu hii imetekeleza yafuatayo:
 
  • Imetayarisha miongozo kwa viongozi wa dini mbili kuu, ya Kiislamu na ya Kikristo, kwa ajili ya kuwafundisha waumini wao juu ya masuala ya kupinga udhalilishaji wa kijinsia. Miongozo hii imeshafanyiwa majaribio na marekebisho na ipo tayari kwa kutumika.
 
·         Imeandaa Taarifa ya Utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) kwa upande wa Zanzibar. Taarifa hiyo inayozungumzia utekelezaji kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2011 hadi 2014, itajumuishwa na ile ya Tanzania Bara kwa ajili ya kuwasilishwa katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika mwezi Septemba 2014.  
 
·         Imezijengea uwezo Kamati  za kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia za Mkokotoni, Mahonda na Kinyasini Unguja na Micheweni na Konde Pemba ili ziweze kufanya kazi zao kwa ufanisi. Jumla ya Wajumbe 140 wa kamati hizo wamepatiwa mafunzo ya ushauri nasaha, Sheria na taratibu za kukuza mwitiko dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na ufuatiliaji wa kesi.
 
·         Imefanya tathmini ya mapungufu yaliyopo katika Sheria ya Usajili wa Ndoa  ya mwaka 1966 sura ya 91 na 92, ambapo tathmini hiyo iligundua kwamba Sheria hii imejikita zaidi katika masuala ya usajili na haikugusia masuala muhimu yanayohusu ndoa, ikiwemo suala la haki na wajibu wa wanandoa, umri wa kuingia katika ndoa, tafsiri ya ndoa na suala la matunzo ya watoto baada ya kuvunjika kwa ndoa. Aidha, ripoti ya tathmini hiyo ilieleza kuwa kuna umuhimu wa kuandaliwa Sheria maalum ya ndoa, lakini itanguliwe na uandaaji wa Sera ya Kuimarisha Familia.
 
·         Imeandaa Muhtasari (Fact Sheet) juu ya hali halisi ya udhalilishaji  wa kijinsia ambao utatumika kushajiisha jamii kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya udhalilishaji. Vile vile, Wizara imeandaa mchezo wa kuigiza, wenye sehemu 25, kwa ajili ya kuelimisha jamii juu ya athari ya ukatili wa kijinsia kupitia redio. Mbali na hayo, Wizara imetayarisha filamu ya ushuhuda wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar, ambayo itatumika katika programu za kuelimisha jamii juu ya athari za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
 
Programu ya Kukuza usawa wa Kijinsia na Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi
 
26.              Mheshimiwa Spika, Programu hii inatekelezwa kwa mashirikiano na Shirika la UN- Women kwa lengo la kusaidia jitihada za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Kupitia programu hii, Wizara katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 imetekeleza yafuatayo:
 
·         Imefanya utafiti wa kuvitambua vikundi vya uzalishaji na vya kiuchumi vya wanawake katika Wilaya zote 10 za Unguja na Pemba. Utafiti huu utaweza kutambua aina ya biashara zinazofanywa na kinamama, uimara wa vikundi vyao, mitaji waliyonayo ya kuendesha biashara zao na maeneo vilipo vikundi hivyo,
 
·         Imetoa mafunzo ya kuvijengea uwezo vikundi vya wanawake vya Mkoa wa Kaskazini Unguja, jumla ya wanawake 60 wamenufaika na mafunzo hayo  na kwa upande wa Pemba jumla ya wanawake 60 wa Wilaya ya Micheweni na Mkoani wamenufaika na mafunzo hayo. Mafunzo hayo yalihusu utengenezaji wa bidhaa, ufungashaji, ufugaji wa kuku wa kisasa na kienyeji, utengenezaji wa unga wa lishe, ulimaji wa mboga mboga, utengenezaji wa sabuni na utafutaji wa masoko.
 
·         Pia kupitia mradi huu, watendaji wawili wa Wizara ilihudhuria mkutano wa 58 wa Tume ya Umoja wa Mataifa Juu ya Hadhi ya Wanawake, uliofanyika New York, Marekani ambapo ujumbe wa mwaka huu ulikuwa ni ‘Changamoto na Mafanikio katika Kutekeleza Malengo ya Milenia kwa Wanamke na Watoto wa Kike’.  Mkutano huo uliweka azimio la kuweka lengo mahsusi linalohusu usawa wa kijinsia katika Agenda ya Maendeleo ya Baada ya Mwaka 2015, pamoja na mambo mengine mkazo uliwekwa katika kumuwezesha mwanamke kiuchumi na kupiga vita vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia. Aidha, ilisisitizwa kuwa malengo mengine yote yaliyobaki yazingatie usawa wa kijinsia.
 
27.              Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2014/2015 Idara ya Mipango, Sera na Utafiti imekusudia kutekeleza malengo yafuatayo:
 
1.      Kusimamia uingizaji wa masuala mtambuka, ikiwemo masuala ya jinsia katika sera, mipango, program na bajeti za kisekta na Wizara;
2.      Kusimamia uandaaji wa utafiti wa kuangalia athari za utalii na mmonyoko wa maadili kwa vijana;   
3.      Kusimamia uandaaji wa Mpango wa Utekelezaji wa Sera ya Hifadhi ya Jamii, Sera ya Watoto, Sera ya Uwezeshaji na Sera ya Maendeleo ya Vijana;
4.      Kuimarisha uandaaji, uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya mipango na programu za Wizara;
5.      Kuimarisha mashirikiano ya kitaifa, kikanda na kimataifa ili kuleta maendeleo na ustawi wa wanawake, vijana, wazee, watoto na wananchi wanaoishi katika mazingira magumu zaidi; na
6.      Kuratibu utekelezaji wa programu na miradi inayosimamiwa na Wizara.
 
28.              Mheshimiwa Spika, Ili Idara ya Mipango, Sera na Utafiti iweze kutekeleza malengo yake iliyojiwekea kwa mwaka wa fedha 2014/2015, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Milioni Mia Moja na Elfu Sitini na Tano  (Tshs 165,000,000/=) kwa ajili ya matumizi ya Kazi za Kawaida na Shilingi Bilioni Mbili, Milioni Mia Mbili na Nne, Laki saba na Elfu Thalathini na Tano  (Tshs 2,204,735,000/=) kwa Kazi za Maendeleo.
 
IDARA YA UENDESHAJI NA UTUMISHI
 
29.              Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2013/14, Idara hii ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
 
1.      Kusimamia shughuli za kila siku za Uendeshaji na Utumishi za Wizara, ikiwemo Sheria na Kanuni za Utumishi Serikalini na kuhakikisha wafanyakazi wanafuata Sheria na Kanuni za Usimamizi wa fedha na manunuzi ya Vifaa vya Ofisi;
2.      Kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Wizara kwa kuwasaidia malipo ya ada ya masomo ya muda mrefu na muda mfupi kwa kuzingatia mahitaji ya Wizara;
3.      Kuimarisha utendaji kazi kwa kusimamia ununuzi wa vifaa muhimu vya kutendea kazi;
4.      Kuimarisha Wizara kwa kuajiri wafanyakazi wapya kumi na nane (18) Unguja na wanane (8) Pemba; na
5.      Kuendelea kuviimarisha vitengo vya manunuzi, uhasibu na ukaguzi wa ndani.
 
Utekelezaji wa malengo ya Idara ya Uendeshaji na Utumishi kwa mwaka 2013/2014
 
30.              Mheshimiwa Spika, Katika kusimamia uendeshaji wa shughuli za kila siku, Wizara imeshughulikia upatikanaji na utunzaji wa vifaa mbali mbali vya Ofisi, huduma za mawasiliano na usafiri, pamoja na kuvifanyia matengenezo vyombo ya usafiri na vifaa vya ofisi Unguja na Pemba. Aidha, Wizara imenunua vespa mbili (2) ili kuimarisha huduma za usafiri kwa ufuatiliaji wa shughuli za kazi.
 
31.              Mheshimiwa Spika, Wizara imeajiri wafanyakazi wapya 13 (4 wanaume na 9 wanawake) katika fani za Uchumi, Utawala, Katibu Muhtasi, Udereva, Ufundi, Ushoni na Upishi Unguja na Pemba. Nafasi hizi zimejazwa kutokana na kuachwa wazi na wafanyakazi waliostaafu kazi kisheria na wengine kufariki dunia. Aidha, Wizara imepokea wafanyakazi wawili (2) kwa njia ya uhamisho kutoka taasisi nyengine za Serikali na wafanyakazi tisa (9) walipewa uhamisho wa kwenda kuendelea na kazi katika Wizara nyengine. Pia, wafanyakazi kumi (10) walistaafu kazi kisheria, wafanyakazi wawili (2) waliacha kazi kwa hiari yao na wafanyakazi watatu (3) walifariki dunia (Angalia Kiambatanisho Namb.2a)
 
32.              Mheshimiwa Spika, Wizara imewapatia mafunzo ya muda mfupi wafanyakazi 4, (2 Unguja na 2 Pemba) katika kada ya Ukaguzi wa Hesabu za Ndani, Uandishi wa Kumbukumbu, Habari na Mawasiliano. Pia, Wizara imewasaidia ada ya masomo wafanyakazi 33 (Unguja 23 na Pemba 10) wanaochukua masomo ya muda mrefu katika vyuo mbali mbali nchini Tanzania. Wafanyakazi hao wanasomea fani za Ustawi wa Jamii, Uchumi, Sheria, Maendeleo ya Jamii, Ushirika, Mipango na Uongozi, Uongozi wa Fedha na Ujasiriamali, Utunzaji Kumbukumbu na Ukatibu Muhutasi (Angalia Kiambatanisho Namb. 2b).
 
33.              Mheshimiwa Spika, Wizara imefanya vikao kumi (10) vya Kamati Tendaji na vikao vitatu (3) vya Kamati ya Uongozi. Miongoni mwa yaliyojadiliwa katika vikao vya Kamati hizo ni pamoja na rasimu za Sera ya Hifadhi ya Jamii, Sera ya Maendeleo ya Vijana na Sera ya Maendeleo ya Ushirika, pamoja na taarifa za utekelezaji wa programu mbali mbali zinazosimamiwa na Wizara.
 
34.              Mheshimiwa Spika, Ili kuendana na mabadiliko yaliyofanywa katika muundo wa Wizara, Bodi ya Zabuni na Kamati ya Ukaguzi wa Ndani ya Wizara zimeundwa upya. Bodi ya Zabuni imefanya vikao viwili (2) ambavyo, pamoja na mambo mengine,  vilijadili na kupitisha Mpango wa Manunuzi kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2005 na Ripoti za Manunuzi. Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu za Ndani pia imefanya vikao viwili (2) ambavyo vilipitia na kujadili Ripoti za Ukaguzi wa Ndani zilizowasilishwa.
 
35.              Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Kitengo cha Ukaguzi wa Hesabu za Ndani ilifanya ukaguzi wa mahesabu na matumizi ya Wizara katika Idara, Miradi na Programu zake mbali mbali Unguja na Pemba. Lengo ni kuhakikisha kuwa fedha na mali nyengine za Wizara zinasimamiwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha na Manunuzi za mwaka 2005.
 
36.              Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 Idara ya Uendeshaji na Utumishi imejipangia kutekeleza malengo yafuatayo:
 
1.      Kufanya tathmini ya mahitaji ya uwezo wa rasilimali watu katika Wizara;
2.      Kuimarisha uwezo wa utendaji kwa kusimamia upatikanaji wa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wafanyakazi 10 (Unguja 8 na Pemba 2) na kuajiri wafanyakazi wapya 76 (Unguja 55 na Pemba 21);
3.      Kuimarisha mfumo wa mawasiliano wa Wizara kwa kununua mtambo na vifaa muhimu vya mawasiliano vitakavyowezesha kujiunga na mfumo wa Serikali wa mtandao (E–government), pamoja na kuweka simu za mezani;
4.      Kuimarisha utendaji kazi kwa kusimamia ununuzi wa vifaa mbalimbali vya ofisi;
5.      Kuendelea kusimamia nidhamu, wajibu, na upatikanaji wa haki, maslahi, fursa, na motisha kwa wafanyakazi wa Wizara Unguja na Pemba; na
6.      Kuimarisha Mfumo wa habari na uhusiano wa Wizara.
                                                                                            
37.                               Mheshimiwa Spika, Ili Idara ya Uendeshaji na Utumishi iweze kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Milioni Mia Tatu na Sitini   (Tshs. 360,000,000/=) kwa kazi za kawaida na jumla ya Shilingi Bilioni Moja, Milioni Mia Saba na Tano, Laki Moja na Elfu Sitini na Nne (Tshs. 1,705,164,000/=) kwa ajili ya Mishahara, Mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Posho za wafanyakazi Unguja.
 
IDARA YA UENDELEZAJI  NA URATIBU WA PROGRAMU ZA  UWEZESHAJI  WANANCHI  KIUCHUMI 
 
38.              Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 Idara hii ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:
1.             Kujenga utamaduni wa ujasiriamali na kuimarisha uwezo wa wajasiriamali, hususan vijana, katika wilaya 10 za Zanzibar;
2.             Kuimarisha usimamizi, huduma za ushauri, ufuatiliaji na tathmini shirikishi ya shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi;
3.             Kutanua soko la bidhaa za wajasiriamali wadogo wadogo; na
4.    Kuijengea uwezo wa kiutendaji Idara ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.
 
Utekelezaji wa malengo ya Idara ya Uendelezaji na Uratibu wa Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi 2013/2014:
 
39.              Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2013/2014, utekelezaji wa malengo kwa Idara hii ulikuwa kama ifuatavyo:
 
·         Idara ilipanga kutoa mafunzo kwa awamu sita juu ya ujasiriamali kwa watu 250 (150 Unguja na 100 Pemba) hususan vijana, lakini kutokana na uhaba wa fedha imeweza kutoa mafunzo kwa vijana 50 kutoka Mikoa miwili ya Pemba. Mafunzo hayo yalikusudia kuimarisha utamaduni wa ujasiriamali kwa vijana ili waweze kujiajiri kwa kuanzisha biashara mbali mbali. Pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo yamesaidia vijana kubuni mipango ya biashara kulingana na fursa zilizopo katika maeneo yao. Kati ya vijana waliopatiwa mafunzo, vijana 11 (7 wanawake na 4 wanaume) wameweza kujiajiri kwa kuanzisha shughuli za biashara, kilimo, ufugaji na ushoni.
 
·         Idara imetoa mafunzo ya awamu 4 kwa wajasiriamali wadogo wadogo 120 (90 Unguja na 30 Pemba) baada ya kufanya utafiti mdogo wa kubaini mahitaji yao. Pia imewapatia mafunzo wanavikundi 30 wa Wilaya ya Magharibi katika vijiji vya Maungani, Kisauni na Bweleo. Baada ya mafunzo hayo, wanavikundi hao wameunganishwa na wataalamu mbali mbali kulingana na mahitaji na changamoto zinazowakabili, kama vile masoko, upatikanaji wa vifaa vya kilimo na upatikanaji wa mashine ya kutotolea vifaranga na mayai inayotengenezwa kwa kutumia teknolojia rahisi na rasilimali zilizopo nchini.
 
·         Mafunzo ya awamu 4 juu ya Uandishi wa Mpango wa Biashara (Business Plan) yalitolewa kwa wajasiriamali 45 (30 Unguja na 15 Pemba). Kutokana na mafunzo hayo, jumla ya Mipango ya Biashara  15 ya wajasiriamali vijana kutoka Mikoa miwili ya Pemba imetayarishwa na kuwasilishwa katika Idara ya Mikopo kwa ajili ya kufanyiwa tathmini juu ya uwezekano wa kupatiwa fedha za mitaji kupitia njia ya mkopo. Pia Idara inatarajia kupokea Mipango ya Biashara 30 kutoka Mikoa mitatu ya Unguja kwa kuiwasilisha Idara ya Mikopo kama ilivyofanywa kwa upande wa Pemba.
 
·         Jumla ya wajasiriamali wadogo wadogo 100 (wanawake 70 na wanaume 30) wameshiriki katika maonesho ya Wiki ya Uwezeshaji yaliyofanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Wizara Mwanakwerekwe na Kisonge. Maonesho hayo yamebainisha kwamba wajasiriamali wadogo wadogo wanahitaji kujengewa uwezo zaidi katika kuimarisha ubora wa bidhaa zao, viwango na vifungashio ambayo ndiyo changamoto kubwa inayowakabili katika kumudu ushindani wa soko la ndani na la Afrika ya Mashariki.
 
·        Kupitia makongano (clusters), Idara imefanya uchanganuzi wa masoko ya ndani ya wajasiriamali wadogo wadogo katika Mikoa mitatu ya Unguja, ili kubaini changamoto katika uzalishaji na uuzaji wa mazao/bidhaa zao. Katika uchanganuzi huo, Idara imeweza kujua aina mbali mbali za bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wadogo wadogo, ubora na wingi wa bidhaa hizo, mitaji na faida inayopatikana, maeneo ya uzalishaji na uuzaji wa bidhaa hizo na changamoto zinazowakabili. Miongoni mwa changamoto zilizobainika ni pamoja na uhaba wa bidhaa zinazozalishwa kulingana na mahitaji ya soko, kutokuwepo kwa uendelevu katika uzalishaji, kukosekana kwa vifungashio vya bidhaa za wajasiriamali na ubora unaokubalika wa bidhaa. Changamoto hizo zinaendelea kufanyiwa kazi na Wizara.
 
·         Kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara na Viwanda, Wizara imeweza kuwasaidia wajasiriamali 50 kushiriki katika maonesho ya 14 ya Juakali/Nguvu kazi ambayo kwa mwaka 2013/2014 yalifanyika Nairobi, nchini Kenya.
 
·        Katika kuratibu shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi, Wizara imefanya mikutano miwili ya Kamati za Uwezeshaji za Wilaya ya Kusini na Kaskazini A Unguja. Pia imeandaa  mikutano miwili  na washirika wengine wa taasisi za Serikali ili kujadili utekelezaji wa  programu na shughuli mbali mbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi wanazozitekeleza. Mikutano hiyo pia imewashirikisha Waratibu wa programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi, ikiwemo TASAF; Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani Bidhaa na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF); na Programu ya Kukuza Mazingira ya Biashara. Aidha, mikutano hii imesaidia kubadilishana taarifa juu ya utekelezaji wa programu hizo na kupeana uzoefu juu ya mikakati iliyoleta mafanikio.
 
·         Idara imefanya ziara 3 (2 Unguja na 1 Pemba) za ufuatiliaji wa vikundi vya kiuchumi na mjasiriamli mmoja mmoja, ambapo jumla ya vikundi 20 (10 Unguja na 10 Pemba) na wajasiriamali 20 (kumi na tano Unguja na watano Pemba) walitembelewa na kupatiwa huduma za ushauri, ili kukuza biashara zao  (Angalia Kiambatanisho Namb. 3). Ziara hizo zimesaidia kuona udhaifu na kubaini matatizo yanayovikabili vikundi na wajasiriamali hao. Aidha, mafunzo ya papo kwa papo yalitolewa ili kutatua baadhi ya changamoto zilizobainika.
 
·         Katika kujenga uwezo wa Idara ili iweze kuyamudu vyema majukumu yake, Wizara imemgharamia mfanyakazi mmoja wa Idara hiyo kutoka Pemba, kushiriki katika  mafunzo ya wiki mbili juu ya masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi huko Tanzania Bara.
 
40.              Mheshimiwa Spika, Katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, Wizara pia imekuwa ikishirikiana na taasisi mbali mbali za Serikali na zisizo za Serikali. Wizara kwa kushirikiana na washirika wengine wa masuala haya imo katika maandalizi ya kuanzisha Kituo cha Kulelea Wajasiriamali katika Chuo cha Karume cha Sayansi na teknolojia, Mbweni. Kamati maalumu imeundwa kusimamia uanzishwaji wa kituo hicho. Kamati hiyo inahusisha wawakilishi kutoka Chuo kikuuu cha Taifa (SUZA), Jumuiya ya wafanya Biashara, Viwanda na Wakulima, Chuo cha Karume, Mamlaka ya vyuo vya Amali, Benki ya Watu wa Zanzibar, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Habari, Wizara ya Mawasiliano, Wizara ya Kilimo na Maliasili na Shirika la Kazi Duniani. Kituo hicho kitapokamilika kitatoa taaluma kwa vijana juu ya masuala  ya ujasiriamali, ikiwemo kuwasaidia kuibua na kuendeleza mawazo yao ya biashara pamoja na kuwaunganisha na huduma za fedha na masoko.
 
41.              Mheshimiwa Spika, Pia Wizara, kwa msaada wa Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Tanzania (COSTECH) imepata Mtaalaamu wa kujitolea kutoka nchini Canada, ambaye atasaidia katika masuala ya uimarishaji wa makongano (clusters) ya wajasiriamali. Mtaalamu huyo, kwa kushirikiana na Chuo cha Karume cha Sayansi na Teknolojia, Mbweni ametengeneza mashine ya kukaushia mwani na matunda kwa kutumia nguvu ya jua. Lengo ni kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo kuweza kutumia teknologia ya nishati ya jua kwa kuhifadhi bidhaa zao zisiharibike.
 
Malengo ya Idara ya Uendelezaji na Uratibu wa Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi  kwa mwaka 2014/2015
 
42.              Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi cha mwaka 2014/2015, Idara hii imekusudia  kutekeleza malengo yafuatayo:
 
1.      Kuandaa mafunzo ya ujasiriamali katika maeneo tofauti kwa vijana 200 wakiwemo wahitimu wa vyuo na vikundi vya kiuchumi;
2.      Kuanzisha Mtandao wa Wajasiriamali utakaohusisha taasisi zinazotoa huduma za kifedha na huduma za biashara;
3.      Kukuza mashirikiano na taasisi nyengine zinazohusika ili kuhakikisha upatikanaji wa masoko kwa bidhaa za wajasiriamali;
4.      Kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi;
5.      Kukamilisha uanzishaji wa Kituo cha Kutotoa Wajasiriamali (Incubation Center) Unguja; na
6.      Kutoa huduma za kibiashara kwa wajasiriamali wadogo wadogo kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko.
 
43.              Mheshimiwa Spika, Ili  Idara  ya Uendelezaji na Uratibu wa Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi iweze kutekeleza malengo yake kwa mwaka 2014/2015, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Milioni Sitini na Moja, Laki Tano na Elfu Sabini na Tano (Tshs. 61,575,000/=) kwa matumizi ya kazi za kawaida.  
 
IDARA YA USHIRIKA
 
44.              Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2013/14, Idara ya Ushirika ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:
 
  1. Kuongeza uelewa wa wanachama 3,000 juu ya Wajibu, Haki na ushiriki katika vyama vya ushirika;
2.      Kusimamia utekelezaji wa Sheria katika uendeshaji wa vyama vya ushirika 1,200;
3.      Kuwezesha uanzishwaji wa vyama viwili vya ushirika vya uzalishaji vinavyohusisha vijana;
4.      Kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa kuendeleza vyama vya ushirika;
5.      Kuimarisha utendaji wa vyama vikuu 6 na Shirkisho la Vyama  vya Ushirika (CUZA);
6.      Kuimarisha mahusiano na washirika wa sekta ya ushirika; na
7.      Kuimarisha mazingira ya kazi, ikiwemo mafunzo kwa wafanyakazi na upatikanaji wa vifaa.
Utekelezaji wa Malengo ya Idara ya Ushirika kwa mwaka 2013/2014.
 
45.              Mheshimiwa Spika, Idara ya Ushirika katika mwaka 2013/2014 imetekeleza yafuatayo:
·         imetoa mafunzo juu ya mbinu za ubunifu, ushindani, wajibu na haki za wanachama pamoja na dhana ya Ushirika kwa jumla kwa wanachama 2,372 (Wanawake 1,569 na Wanaume 803). Wanachama hao walitoka kwenye vyama vya ushirika 209 (Unguja 157 na Pemba 52). Kati ya vyama vilivyopatiwa mafunzo hayo, 67 ni SACCOS na 142 ni vyama vya uzalishaji na utoaji huduma.  Mafunzo hayo yamesaidia kuongeza uelewa wa wanachama hao juu ya haki zao na kwa kiasi fulani yametoa msukumo kwa wanachama kufuatilia shughuli za vyama vyao. 
 
·         Katika kusimamia utekelezaji wa Sheria kwenye vyama vya ushirika, Wizara imefanya ufuatiliaji, ukaguzi wa kawaida na kutoa mafunzo ya vitendo kwa vyama vya ushirika 629 (360 Unguja na 269 Pemba). Hii ni miongoni mwa juhudi za kuhakikisha kuwa vyama vya ushirika vinatunza vitabu vya hesabu na kuweka kumbukumbu nyengine kwa usahihi, kwa mujibu wa Sheria na Katiba za vyama husika.
 
·         Vyama vya ushirika 135 (99 Unguja na 36 Pemba) vimefanyiwa ukaguzi wa hesabu, ambapo kati yao 18 ni SACCOS na 117 ni vyama vya uzalishaji mali na utoaji huduma. Lengo la ukaguzi huo ni kutambua hali ya mahesabu ilivyo kwenye vyama hivyo na kutoa maoni na ushauri wa kitaalamu juu ya hali halisi ya fedha kwa vyama hivyo. Matokeo ya ukaguzi huo yameonesha ukuwaji wa wastani wa mitaji kwa baadhi ya vyama vya ushirika. Hata hivyo, elimu zaidi inahitajika ili kuimarisha udhibiti wa rasilimali na kuleta tija kwenye vyama vya ushirika.
 
·         Vyama viwili (2) vya Ushirika vya vijana wenye taaluma ya elimu ya juu vimeanzishwa, kimoja kinajishughulisha na kilimo cha mboga mboga na chengine kinashughulika na kutoa huduma za kitaalamu kwenye vyama vya ushirika. Vyama hivyo ni; Zanzibar Professionals Cooperative (ZAPROCO) chenye wanachama 21 (wanawake 10 na wanaume 11) kilichopo Dole, na Zanzibar Fresh Vegetable Production chenye wanachama 14 (Wanawake 10 na Wanaume 4) kilichopo Maungani, Wilaya ya Magharibi. Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) imepanga kuvijengea uwezo vyama hivyo kupitia programu za ajira kwa vijana, ili viwe mfano kwa vijana wengine kuwapa hamasa ya kujiajiri.
 
·         Jumla ya vyama vya ushirika 41 (Unguja 34 na Pemba 7) vimepatiwa mafunzo shirikishi ya kuandaa mipango ya biashara. Miradi iliyoandikiwa mipango ya biashara inajumuisha ya kilimo cha mboga mboga, ushoni, ufugaji wa samaki, ufugaji kuku, ukaushaji samaki, usagaji wa nafaka, uvuvi, upandaji miti, ufugaji nyuki, ufyatuaji matofali, useremala, kazi za mikono na ufundi umeme. Vikundi hivyo vimeunganishwa na taasisi za kifedha ili viweze kupatiwa mikopo kwa utekelezaji wa mipango yao ya biashara.
 
·         Juhudi za kuimarisha uendeshaji wa Vyama Vikuu na Shirikisho la Vyama vya Ushirika Zanzibar (CUZA) zimeendelea. Ziara za ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu kwa mujibu wa Mipango Mikakati ya Vyama Vikuu hivyo na CUZA zimefanywa. Aidha, vikao viwili baina ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika na Bodi ya CUZA vimefanyika ili kujadili na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa lengo la kurekebisha kasoro za utendaji zilizobainika. Hatahivyo, Wizara inaendelea kutoa mafunzo na ushauri zaidi kwa vyama hivyo ili viweze kufanya shughuli zake ipasavyo.
 
·         Wizara iliandaa maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani, ambayo huadhimishwa Jumamosi ya mwanzo ya mwezi Julai kila mwaka. Maadhimisho hayo yalijumuisha mkutano wa wadau wa kujadili maendeleo na namna ya kukabiliana na changamoto kwenye vyama vya Ushirika. Aidha, Tamko Rasmi la Waziri kuhusiana na maadhimisho ya siku hiyo lilitolewa. Vile vile, kipindi maalum kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC - TV) kiliandaliwa. Maadhimisho haya pia yalilenga kuwashajiisha wananchi juu ya umuhimu wa Sekta ya Ushirika kwa maendeleo ya watu, hasa wenye kipato cha chini.
 
·         Ili kuimarisha mashirikiano na wahusika wengine wa masuala ya ushirika, watendaji wawili (2) wa Wizara walishiriki katika Mkutano uliofanyika Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara, Moshi. Mkutano huo ulijadili hali ya maendeleo ya ushirika nchini pamoja na changamoto za upatikanaji wa huduma za mikopo. Pia watendaji hao walibadilishana mawazo na uongozi wa Chuo Kikuu cha Ushirika juu ya uwezekano wa Chuo hicho kushirikiana na Vyuo vilivyopo Zanzibar ili kutoa mafunzo na elimu ya Ushirika.
 
 
 
Malengo ya Idara ya Ushirika kwa mwaka 2014/2015
 
46.              Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi cha mwaka 2014/ 2015, Idara ya Ushirika imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:
 
1.      Kukuza uwezo wa ushindani wa vyama vya ushirika 10 ili vitoe huduma kwenye soko la utalii ifikapo Juni 2015;
2.      Kuongeza uelewa kwa wanachama na viongozi  3,000 juu ya maadili, kanuni za ushirika, na mbinu za utendaji bora kwenye vyama vya ushirika ifikapo Juni 2015;
3.      Kusimamia utekelezaji wa Sheria katika uendeshaji wa vyama vya ushirika 1,400 ifikapo Juni 2015; 
4.      Kuimarisha mashirikiano na washirika ili kubadilishana taarifa na kujifunza mambo mapya ya kuendeleza sekta ya Ushirika ifikapo 2015;
5.      Kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya maendeleo ya vyama vya ushirika ifikapo Juni 2015; na
6.      Kuimarisha mazingira ya kazi ikiwemo mafunzo kwa wafanyakazi na upatikanaji wa vifaa.
47.              Mheshimiwa Spika, Ili Idara ya Ushirika iweze kutekeleza majukumu yake kwa mwaka 2014/15, naliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi Milioni Arobaini na Tisa, Laki Tisa na Elfu Thelathini na Nane (Tshs. 49,938,000/=) kwa matumizi ya kazi za kawaida.
 
 
IDARA YA MIKOPO
 
48.              Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/2014, Idara hii ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:
1.Kutoa mikopo 1,000 kwa vikundi vya kiuchumi na watu binafsi/mjasiriamali mmoja mmoja yenye thamani ya Tshs. 300,000,000/=;
2.Kuongeza kiwango cha marejesho ya Mikopo kutoka asilimia 85 hadi zaidi ya asilimia 95;
3.Kuimarisha uwekaji wa kumbukumbu za mikopo; na
4.Kuimarisha mashirikiano na uratibu wa shughuli za mikopo nafuu hapa nchini.
 
Utekelezaji wa Malengo ya Idara ya Mikopo 2013/2014
 
49.              Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 Idara ya Mikopo ilitekeleza yafuatayo:
 
·         Imetoa mikopo 550 (Unguja 328 na Pemba 222) kupitia Mfuko wa Kujitegemea, yenye thamani ya Shilingi Milioni Mia Mbili Tisini na Nne, Laki Nane na Elfu Sabini na Saba (Tshs. 294,877,000/=). Kati yafedha hizo,  Shilingi Milioni Mia Mbili Kumi na Moja, Laki Nane na Elfu Sabini na Saba (TShs. 211,877,000/=) zilitolewa kwa wakopaji wa Unguja na Shilingi Milioni Themanini na tatu (Tshs.83,000,000/=) zilitolewa kwa wakopaji wa Pemba.  (Angalia Kiambatanisho Namb. 4). Aidha, Wizara imetoa mafunzo  kwa Wakopaji 550  kuhusiana na uwekaji wa kumbukumbu za hesabu, faida za kutumia huduma za kibenki kwa wakopaji, umuhimu wa  kujiwekea akiba na utafutaji wa masoko. Mafunzo haya yalitolewa ili kuwawezesha wajasiriamali kuzitumia fedha za  mikopo vizuri na kwa malengo yaliyokusudiwa, pamoja na kusimamia vizuri biashara zao. 
 
·         Imeendelea kufuatilia marejesho ya mikopo ya Mfuko wa JK/AK, ambapo jumla ya Shilingi Milioni Thelathini, Laki Sita Elfu Themanini, Mia Nne na Sabini na Nane (Tshs. 30,680,478/=) zimekusanywa katika kipindi cha kuanzia Julai 2013 hadi Machi, 2014. (Angalia Kiambatanisho Namb. 5). Idara pia imefanya ziara za ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo katika Wilaya zote za Unguja na Pemba. Ziara hizo zililenga kuangalia maendeleo ya miradi ya wakopaji na changamoto zao, pamoja na kuwashauri juu ya namna bora ya kuendesha biashara zao, ili waweze kupata tija na kulipa mikopo yao kama inavyotakiwa.
 
·         Idara imeanzisha mtandao wa taasisi zinazotoa huduma za kifedha kwa wajasiriamali wadogo ili kubadilishana taarifa za wakopaji na kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchukuaji na urejeshaji mikopo. Mtandao huo  umejumuisha taasisi mbalimbali za kifedha, zikiwemo WEDTF; YOSEFO; CRDB; CHANGAMOTO; Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar; na SACCOS mbalimbali za mijini na vijijini.  Kupitia mtandao huo, imeripotiwa kuwa hadi kufikia mwezi wa Aprili 2014, Jumuiya ya WEDTF imetoa mikopo 196 yenye thamani ya Shilingi Milioni Sitini na Moja (Tshs. 61,000,000/=); SACCOS kubwa 16 zimetoa mikopo 216 yenye thamani ya Shilingi Milioni Arobaini na Mbili (Tshs.42,000,000/=); na CRDB kupitia Mfuko wa Vijana imetoa mikopo kwa vikundi 116 yenye thamani ya Shilingi Milioni Mia Mbili Arobaini na Tano (Tshs.245,000,000/=).
 
·         Idara imefanya mikutano kadhaa na Mamlaka za Wilaya na Shehia kuhimiza urejeshwaji wa fedha za mkopo. Mikutano hii pia ilitumika kuwaelewesha washiriki juu ya madhumuni ya Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, pamoja na Muongozo wa uendeshaji wake, ikiwemo taratibu za uombaji na utoaji wa mikopo. Aidha, mikutano hiyo ilisaidia kuongezeka urejeshwaji wa fedha za mikopo, ambapo hadi kufikia mwezi wa Aprili 2014, jumla ya Shilingi Milioni Mia Moja na Kumi na Moja, Laki Moja, Elfu Tano na Mia Moja (T.shs 111,105,100/=) zimerejeshwa katika Mfuko wa Kujitegemea Unguja na Pemba. Kati ya fedha hizo, Shilingi Milioni Themanini na Tatu, Elfu Hamsini na Nane na Mia Sita (TShs. 83,058,600/-) zilirejeshwa kutoka kwa wakopaji wa Unguja na Shilingi Milioni Ishirini na Nane, Elfu Arobaini na Sita  na Mia Tano (Tshs. 28,046,500/=) kutoka kwa wakopaji wa Pemba (Angalia Kiambatanisho Namb. 6).  
 
·         Ili kujifunza uzoefu wa taasisi nyengine katika masuala ya mikopo, Idara imefanya ziara za kujifunza kwa taasisi bora zinazotoa mikopo huko Tanzania Bara. Taasisi zilizotembelewa ni Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (National Economic Empowerment Council) na  BLUE Finance zilizoko Dar es Salaam. Pia ziara mbili kwa wafanyakazi wa Idara baina ya Unguja na Pemba zilifanyika, ambapo waliweza kujifunza na kubadilishana uzoefu katika uwekaji wa kumbukumbu za mikopo.
 
·         Idara imeendelea kufuatilia ahadi za uchangiaji wa fedha zilizotolewa na taasisi, wafanyabiashara na wananchi mbali mbali kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. ambao ulizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, tarehe 21 Disemba, 2013. Katika uchangishaji huo, ahadi za jumla ya Shilingi Bilioni Moja, Milioni Ishirini na Tatu, Laki Nne na Elfu Tisini (Tshs. 1,023,490,000/=) zilitolewa. Hadi sasa jumla ya Shilingi Milioni Mia Tisa Sitini na Moja, Laki Nane na Elfu Tisini (Tshs. 961,890,000/=) fedha taslim zimekusanywa ambazo ni sawa na asilimia 94 ya ahadi zote. Zoezi la kufuatilia ahadi zilizobaki linaendelea. Naomba nichukue fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya Rais ya kusimamia uchangiaji wa Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, kwa kazi nzuri waliyoifanya. Chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Haroun A. Suleiman, Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais) Kazi na Utumishi wa Umma, Kamati hii imefanya kazi kubwa na nzuri ya kupigiwa mfano. Aidha, nachukua fursa hii kutoa shukurani maalumu kwa taasisi, wafanyabiashara na wananchi mbali mbali ambao wamechangia fedha kwa ajili ya kutunisha Mfuko huu. Nataka niwaahidi kwamba Wizara yangu itasimamia vyema Mfuko huu ili, kuhakikisha unafikia malengo yake ya kuwawezesha wananchi wa Zanzibar wenye kipato cha  chini, kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu, ili waweze kujiajiri kwa shughuli za kiuchumi na kujikwamua kutoka kwenye umasikini.
 
·         Ili kuimarisha utendaji, wafanyakazi watatu (Unguja mmoja na Pemba wawili) wamegharamiwa kuendelea na mafunzo ya muda mrefu katika fani ya mikopo na ujasiriamali, usimamizi wa masoko na usimamizi wa rasilimali watu. Mafunzo hayo yatasaidia kuongeza idadi ya wafanyakazi wenye taaluma, jambo ambalo ni muhimu katika kuleta ufanisi kwenye utendaji wa shughuli za Idara.
 
50.              Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2014/2015, Idara hii imepanga kuendelea kutekeleza malengo yafuatayo:
 
1.Kutoa mikopo 1,000 yenye thamani ya Shilingi 500,000,000/= kupitia vikundi vya kiuchumi na Mjasiriamali Mmoja Mmoja katika sekta za kiuchumi;
2.Kuongeza kiwango cha marejesho ya mikopo kutoka asilimia 85 hadi asilimia 95;
3.Kuanzisha fursa mpya za mikopo na kuwaelewesha wananchi juu ya  Muongozo wa Uendeshaji wa Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi;
4.Kuimarisha uwekaji wa kumbukumbu za wateja wa mikopo;
5.Kuendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili uendelee kuwasaidia wajasiriamali wengi zaidi;
6.Kuimarisha mashirikiano na uratibu wa shughuli za mikopo nafuu hapa nchini; na
7.Kuimarisha uwezo wa watendaji ili kuongeza ufanisi wa kazi.
 
51.              Mheshimiwa Spika, Ili Idara ya Mikopo iweze kutekeleza malengo yake kwa mwaka wa fedha 2014/2015, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Milioni Thamanini na Nne, Laki Tisa na Elfu Arobaini (T.shs 84,940,000/=) kwa matumizi ya kawaida.
 
IDARA YA USTAWI WA JAMII
 
52.              Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Idara ya Ustawi wa Jamii ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:
 
1.      Kuimarisha Mfumo wa Hifadhi ya Mtoto;
2.      Kuimarisha uratibu na kufuatilia masuala ya malezi na makuzi ya awali ya watoto kuanzia miaka 0-8;
3.      Kuimarisha Hifadhi ya Wazee;
4.      Kusimamia ulipaji wa fidia kwa Wafanyakazi waliopata ajali kazini; na
5.      Kuimarisha shughuli za kuwapatia wanajamii misaada ya kiustawi.
 
Utekelezaji wa Malengo kwa Idara ya Ustawi wa Jamii kwa mwaka wa fedha 2013/2014
 
 
53.              Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2013/204, Idara ya Ustawi wa Jamii imetekeleza shughuli zifuatazo:
 
·         Imekusanya taarifa za udhalilishaji wa watoto kutoka Wilaya za Unguja na Pemba na kuziingiza katika mfumo wa kuhifadhi taarifa. Aidha, Vituo vyengine viwili vya Mkono kwa Mkono vimeanzishwa katika Hospitali za Wete na Micheweni kwa ajili ya kurahisisha ushughulikiaji wa kesi za udhalilishaji katika maeneo hayo. Pia, mkutano mmoja (1) umefanywa ili kuwakutanisha wafanyakazi wa Vituo vya Mkono kwa Mkono vya Hospitali ya Mnazimoja, Kivunge na Makunduchi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili mafanikio pamoja na changamoto zinazowakabili katika kutoa huduma hizo. Pamoja na hayo, Kitengo cha Hifadhi ya Mtoto cha Mkoa wa Kaskazini Unguja kimeimarishwa kwa kupatiwa vifaa vya kufanyia kazi, ikiwemo kompyuta, printa, fotokopi na samani. Hadi kufikia mwezi wa Machi 2014, jumla ya malalamiko 2,356 (2,258 Unguja na 98 Pemba) ya udhalilishaji wa watoto yaliripotiwa na kushughulikiwa katika vituo vya Mkono kwa Mkono (Angalia Kiambatanisho Namb. 7a na 7b).
 
·         Kwa kushirikiana na Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Hifadhi ya Watoto, Idara imefuatilia kesi 20 za watoto waliodhalilishwa zilizoripotiwa katika kipindi cha miezi sita (Agosti - Januari). Aidha, Mkutano mmoja wa kuratibu na kujadili changamoto zinazozikabili Kamati za Hifadhi ya Mtoto za Wilaya zote za Unguja na Pemba umefanyika.  Vile vile, familia 10 zimepatiwa msaada wa kisaikolojia, ushauri nasaha na kupatiwa rufaa kwenda vituo vya Mkono kwa Mkono kwa kupata huduma za afya. Kwa upande wa Pemba, kamati zimefuatilia katika Vyombo vya Sheria jumla ya kesi 60 za udhalilishaji wa watoto. Pia, Idara imeandaa mikutano ya Kamati za Hifadhi ya Mtoto kwa Wilaya nne za Pemba na ya Kamati ya Kitaifa ya kushughulikia masuala ya Hifadhi ya Mtoto, ili  kujadili changamoto, matatizo na jinsi ya kukiimarisha kitengo cha hifadhi ya mtoto Pemba.
 
·         Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka Mahkama mbali mbali Unguja, jumla ya kesi Themanini na Tano (85) za udhalilishaji zimeripotiwa katika kipindi cha Julai 2013 hadi Aprili 2014 Unguja; kati ya kesi hizo, kesi za kubakwa ni Sitini na Saba (67) ambapo kesi nne (4) zimeshatolewa uamuzi, kesi (mbili (2) zimefutwa, kesi mbili (2) zimehukumiwa kifungo na Kesi Sitini na Tatu (63) zinaendelea kusikilizwa. Kesi za kutorosha watoto ni tatu (3) ambazo zote zinaendelea kusikilizwa na kesi za kulawiti ni kumi na tano (15), ambapo kesi mbili (2) zimetolewa uamuzi wa kufutwa na kesi kumi na tatu (13) zinaendelea kusikilizwa. Kwa upande wa Pemba jumla ya kesi 24 zimeripotiwa kutoka Mahkama za Mkoa katika kipindi cha mwezi wa Julai 2013 hadi Aprili 2014. Kati ya hizo kesi za kubaka ni kumi na tatu (13), kulawiti tano (5), kutorosha nne (4) na shambulio la aibu mbili (2). Miongoni mwa hizo, kesi tatu (3), zote za kubaka, zimeshatolewa hukumu.
 
·         Katika kuimarisha ufuatiliaji wa masuala yanayohusu hifadhi ya watoto, hususan masuala ya ubakaji, Wizara imefanya mikutano miwili ya Kamati ya Hifadhi ya Mtoto  inayohusisha Viongozi wa Juu (Mawaziri na watendaji wakuu wa Serikali kutoka Taasisi zinazohusika), ambayo ilijadili mikakati mbalimbali ya kuwalinda watoto dhidi ya udhalilishaji. Vile vile, Wizara imefanya mkutano wa kujadili Kitini cha Kufundishia Masuala ya Hifadhi ya Mtoto na pia kuwajengea uwezo Maafisa Ustawi, Maafisa Wanawake na Watoto na Masheha juu ya jinsi ya kuripoti kesi za udhalilishaji, Unguja na Pemba.
 
·         Kamati za Shehia za kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi katika Shehia mbili za Pemba (Kiuyu Kigongoni na Minungwini Wilaya ya Wete Pemba) zilifuatiliwa na kupatiwa mafunzo juu ya namna ya kuwatambua na kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Aidha, utambuzi wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi katika maeneo hayo ulifanyika. Pia, ili kuimarisha upatikanaji wa taarifa, Wizara kwa kushirikiana na ‘Measure Evaluation’ imeandaa Mpango Kazi wa miaka mitatu wa ufuatiliaji na tathmini ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi.
 
·         Idara imeendelea kuhudumia Nyumba ya Kulelea Watoto Mazizini yenye jumla ya watoto 38. Watoto hao walipatiwa huduma za chakula, afya, vifaa vya skuli na nguo. Aidha, Wizara imeendelea kutoa misaada ya kijamii kwa watu wasiojiweza na watu wanaoishi katika mazingira magumu zaidi katika jamii, wakiwemo wazee 163 wanaoishi katika nyumba za wazee Sebleni na Welezo Unguja na Limbani na Makundeni Pemba. Pia, familia 75 Unguja na 55 Pemba zinazoishi katika mazingira magumu zaidi zimepatiwa misaada ya fedha za kujikimu.
 
·         Idara imeanza kufanya utambuzi wa wazee wote wa Zanzibar ili kujua idadi yao halisi na kuweza kupanga mipango bora kwa mujibu wa mahitaji yao. Aidha, Idara iliandaa maadhimisho ya Siku ya Wazee duniani tarehe 01.10.2013 Unguja na Pemba. Katika maadhimisho hayo, Wizara ilisisitiza umuhimu wa jamii kutunza na kuwaenzi wazee, na kuwa jukumu la Serikali ni kuwahudumia wazee ambao hawana wa kuwahudumia kabisa. Pamoja na hayo, Wizara ilizika maiti nane (8) zisizokuwa na wenyewe zilizoripotiwa katika hospitali na maeneo mbalimbali.
 
·         Idara inaendelea na kazi ya kupokea madai na kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaopatwa na ajali wakiwa kazini, ambapo kwa mwaka 2013/14 jumla ya wafanyakazi 11 (10 Unguja na mmoja Pemba) walilipwa.  Aidha, Wizara bado ina deni kubwa la fidia lililofikia TShs. 96,808,293/= kwa wafanyakazi 89 wa Unguja na Pemba. Fedha hizo zimeshapatikana na watu wote wanaodai madeni hayo wameanza kulipwa. (Angalia Kiambatanisho 8a na 8b).
 
54.              Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Idara ya Ustawi wa Jamii imejipangia kutekeleza malengo yafuatayo:
1.      Kuimarisha mfumo wa Hifadhi ya Mtoto ifikapo mwaka 2015;
2.      Kuratibu na kufuatilia masuala ya malezi na makuzi ya watoto;
3.      Kuimarisha Hifadhi ya Wazee ;
4.       Kuendeleza  utoaji wa misaada ya kiustawi kwa wananchi wanaoishi katika mazingira magumu zaidi ;
5.      Kuimarisha Mfumo wa hifadhi ya Jamii ifikapo mwaka 2015; na
6.      Kusimamia ulipaji wa fidia kwa watu wanaopatwa na ajali kazini.
55.              Mheshimiwa Spika, Ili Idara ya Ustawi wa Jamii iweze kutekeleza vyema malengo yake kwa mwaka 2014/2015, naliomba Baraza lako Tukufu liiidhinishe jumla ya Shilingi Milioni Mia Mbili Tisini na Moja na Laki Tano (Tshs. 291,500,000/=) kwa kazi za kawaida.
 
IDARA YA MAENDELEO YA VIJANA
 
56.              Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2013/2014, Idara ya Maendeleo ya Vijana ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:
 
1.      Kuratibu uanzishwaji wa Baraza la Vijana;
2.      Kuratibu Mpango wa Mikopo kwa Vijana na kuwahamasisha kujiunga na vyama vya ushirika na mikopo;
3.      Kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Elimu ya Stadi za Maisha kwa Vijana walio nje ya Skuli;
4.      Kuratibu Mbio za Mwenge wa Uhuru na Wiki ya Vijana Kitaifa;
5.      Kufanya uratibu, ufuatiliaji na uhamasishaji wa vikundi vya vijana;
6.      Kuimarisha mashirikiano na uhusiano wa Taasisi za Vijana ndani na nje ya nchi; na
7.      Kuendeleza na kuimarisha miundo mbinu ya uzalishaji wa mazao ya kilimo cha rossela na mbogamboga kwa vijana Unguja na Pemba.
 
Utekelezaji wa malengo ya Idara ya Maendeleo ya Vijana kwa mwaka 2013/2014
 
57.              Mheshimiwa Spika, Katika kufanikisha malengo iliyojiwekea, Idara ya Maendeleo ya Vijana  katika mwaka 2013/2014 imeweza kutekeleza yafuatayo:
 
·         Iliendelea na taratibu za Kisheria za kuanzisha Baraza la Vijana la Zanzibar. Sheria ya kuanzisha Baraza hilo tayari imepitishwa na Baraza lako Tukufu na mchakato wa kuandaa kanuni kwa ajili ya utekelezaji wa Sheria hiyo unaendelea.
 
·         Imeshiriki katika kuratibu Mbio za Mwenge wa Uhuru na Wiki ya Vijana Kitaifa, ambapo kilele chake kiliadhimishwa tarehe 14/10/2013 Mkoani Iringa. Jumla ya miradi ya maendeleo 1,229 yenye thamani ya Shilingi Bilioni Mia Moja Thamanini na Nne, Milioni Mia Tano Thamanini na Saba, Laki Sita Sitini na Saba, Mia Sita Kumi na Tatu na Senti Arobaini (Tshs. 184,587,667,613.40/=) ilikaguliwa, kuzinduliwa au kuwekewa mawe ya msingi  Tanzania nzima. Kati ya hiyo, miradi 78 ilikuwa ya Zanzibar, ambapo kati yao 38 ilikaguliwa, 21 iliwekewa mawe ya msingi na 19 ilizinduliwa. Aidha, jumla ya fedha taslimu kiasi cha Shilingi Milioni Sitini na Sita, Elfu Tisini na Nne, Mia Sita na Arobaini (Tshs.66,094,640/=) zilikusanywa wakati wa Mbio za Mwenge katika Mikoa ya Zanzibar, kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi iliyozinduliwa (Angalia Kiambatanisho Namb. 9 na 10).   
 
·         Kupitia Idara hii, Wizara imeshirikiana na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ya SMT katika kufanya maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, uliofanyika tarehe 02/05/2014 katika Wilaya ya Bukoba, Mkoani Kagera. Ujumbe Mkuu wa mwaka huu ni “Katiba ni Sheria Kuu ya Nchi”, chini ya kauli mbiu “Jitokeze kupiga kura ya maoni tupate Katiba mpya iliyo bora”. Sambamba na ujumbe huo mapambano dhidi ya UKIMWI, Dawa za Kulevya, Rushwa na Malaria umekuwa ni ujumbe wa kudumu unaoendelea kutolewa wakati wa Mbio za Mwenge.
 
·         Idara iliendelea kuratibu utoaji na urejeshaji wa mikopo ya Mfuko wa Vijana, ambapo mikopo 116 imetolewa yenye thamani ya Shilingi Milioni Mia Mbili Arobaini na Tano (Tshs.245,000,000/=) Unguja na Pemba. Aidha, fedha zote zilizokopwa zimesharejeshwa. Hata hivyo, kulijitokeza changamoto ya ucheleweshaji wa marejesho ya mikopo kwa upande wa Pemba, hali iliyopelekea Wizara kwa kushirikiana na Benki ya CRDB kuandaa ziara maalumu, ambayo ilifanikisha kurejeshwa kwa fedha za mikopo iliyocheleweshwa, yenye thamani ya Shilingi Milioni Ishirini na Sita (Tshs. 26,000,000/=).  
 
·         Katika jitihada za kukuza ajira kwa vijana, Idara imendelea na juhudi za kuwahamasisha vijana Unguja na Pemba kujiunga katika vyama vya ushirika na kuanzisha miradi ya kiuchumi katika sekta za kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara na ufundi wa aina mbali mbali. Kufuatia juhudi hizo, vikundi 30 vimeanzishwa katika Wilaya ya Chake Chake na viongozi wake kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali. Aidha, mafunzo yalitolewa kwa vijana 60 (40 Unguja na 20 Pemba) katika nyanja za ukuzaji biashara, masoko, utawala na usimamizi wa miradi, ili kuimarisha uzalishaji katika vikundi vyao. Pia, jumla ya vikundi 103 vya Vijana vilitembelewa na kupewa ushauri na maelekezo ya jinsi ya kuendesha miradi yao (Angalia Kiambatanisho Namb. 11).   Vilevile, kwa kushirikiana na SACCOS ya Vijana Pemba, jumla ya vikundi 55 vya ujasiriamali vya vijana vilihamasishwa juu ya umuhimu wa kujiunga na SACCOS hiyo ili waweze kupata mikopo yenye masharti nafuu, kwa lengo la kuweza kuimarisha na kuendeleza shughuli zao za uzalishaji (Angalia Kiambatanisho Namb. 12).   
 
·         Katika kuimarisha mashirikiano na uhusiano wa Taasisi za Vijana ndani na nje ya nchi, Vijana wanne (4) wameshiriki katika Mikutano ya Vijana huko Austria na Misri. Aidha, kwa kushirikiana na Shirika la UVIKIUTA, vijana wa Zanzibar kwa kushirikiana na vijana wa Tanzania Bara, walipatiwa mafunzo ya uongozi wa kambi za kimataifa za vijana, ambazo madhumuni yake ni kuhamasisha vijana juu ya uzalendo na kuipenda nchi yao, kubadilishana mawazo juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana na namna ya kukabiliana nazo. Kupitia makambi haya, vijana hushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa katika miradi ya jamii kama vile ujenzi wa skuli, vituo vya afya na uhifadhi wa mazingira.
 
·         Wizara kwa kushikiana na Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) na Tume ya UKIMWI Zanzibar, imeandaa Kitini na Muongozo wa Mafunzo ya Stadi za Maisha kwa Vijana. Kitini na Muongozo huo vimefanyiwa majaribio kwa maandalizi ya mwisho ya kutumika rasmi. Muongozo huu utasaidia kutoa elimu kwa vijana, itakayowasaidia kujitambua na kuepukana na changamoto wanazokabiliana nazo.
 
·         Ili kuyaimarisha mashamba ya mauwa na mbogamboga ya vijana Tunguu, Unguja na Mbuzini, Pemba, Wizara kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana, imeendelea na taratibu za uwekaji wa miundo mbinu. Hii ni pamoja na kuweka miundombinu ya umwagiliaji majii kwa kutumia mfumo wa “drip irrigation”, pamoja na “green house” mbili kwa Unguja.  Kwa upande wa Pemba, Wizara inaendelea na hatua za uimarishaji miundo mbinu, ambapo imeweza kumalizia utiaji wa milango na madirisha ya kibanda cha kuwekea pampu ya maji. Lengo kwa upande wa Pemba ni kuweka “green house” kama Tunguu. Kwa hivi sasa vijana wanalitumia shamba hilo la Mbuzini kwa kulima mpunga.
  
58.              Mheshimiwa Spika; Kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Idara ya Maendeleo ya Vijana imepanga kutekeleza Malengo yafuatayo:
 
1)      Kuratibu utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Vijana;
2)      Kuratibu na kufuatilia uanzishwaji wa Baraza la Vijana;
3)      Kuratibu mbio za Mwenge wa Uhuru na Wiki ya Vijana kitaifa;
4)      Kuwahamasisha, kuwaandaa na kuwaunganisha vijana na fursa mbali mbali za kiuchumi  zilizopo;
5)      Kuratibu utekelezaji wa Kitini na Muongozo wa Stadi za Maisha kwa Vijana walio nje ya Skuli;
6)      Kufanya ufuatiliaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii za Vijana; na
7)      Kuimarisha ushirikiano na taasisi zinazoshughulikia masuala ya Vijana ndani na nje ya nchi.
59.              Mheshimiwa Spika; Ili Idara ya Vijana iweze kutekeleza majukumu yake naliomba Baraza lako tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Milioni Sabini na Tatu, Laki Tano na Elfu Thelathini na Tatu (Tshs. 73,533,000/=) kwa kazi za kawaida.
 
IDARA YA MAENDELEO YA WANAWAKE NA WATOTO
 
60.              Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/2014, Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:
 
1.      Kuratibu na kusimamia haki  za wanawake na watoto;
2.      Kuratibu na  kufuatilia utekelezaji wa Sera na Sheria ya Mtoto;
3.      Kuimarisha uratibu wa shughuli za kiuchumi na maendeleo ya wanawake na watoto;
4.      Kuimarisha mashirikiano ya kitaifa, kikanda na kimataifa kwa mambo yanayohusu wanawake na watoto.
 
Utekelezaji wa malengo ya Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto kwa mwaka 2013/2014
 
61.              Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa malengo ya Idara hii kwa mwaka 2013/2014 ulikuwa kama ifuatavyo:
 
·        Katika kuratibu na kusimamia, haki za wanawake na watoto, Kamati ya kupambana na vitendo vya  udhalilishaji  dhidi ya  watoto imeanzishwa. Kamati hiyo imejumuisha wawakilishi 30 kutoka katika taasisi za Serikali na zisizo za Serikali. Tayari Kamati hiyo imeanza kazi na imekuwa ikiendesha mikutano ya kujadili masuala mbali mbali yanayohusu hali na ustawi wa watoto wa Zanzibar.
 
·         Wizara kupitia Idara hii, imetayarisha nyenzo za mawasiliano za masuala ya udhalilishaji wa watoto na kuzifanyia mapitio kwa kuwashirikisha wadau wa masuala ya watoto wakiwemo wanafunzi, walimu na  wazazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja. Pia, Wizara imetayarisha Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ambao utasaidia upatikanaji wa taarifa na takwimu zinazohusu haki za watoto.
 
·         Idara imeendelea kuyapokea, kuyashughulikia na kuyapatia ufumbuzi malalamiko yanayohusu wanawake, ambapo kwa mwaka 2013/2014 jumla ya malalamiko 119 (Unguja24 na Pemba 95) yalipokelewa na kupatiwa ushauri na maelekezo yanayofaa. Malalamiko hayo yalihusu kupigwa, kupewa ujauzito, kubakwa, kutelekezwa na mume, kuunguzwa moto, madai ya fedha na madai ya nyumba (Angalia Kiambatanisho Namb.13a, 13b).
 
·         Idara iliratibu maandaalizi ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo mwezi wa Machi. Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2014 ilikuwa ni “ONGOZA MABADILIKO KWA MAENDELEO YA WANAWAKE”. Kwa upande wa Zanzibar, maadhimisho hayo yalihusisha shughuli mbali mbali zikiwemo: Kuandaa vipindi vya redio na Televisheni; Kufanya usafi wa mazingira  katika nyumba za wazee Sebleni; Kuendesha makongamano katika Wilaya za Kusini na Mjini; Maonesho ya kazi za Sayansi kwa wanafunzi wanawake; na Kufanya uhamasishaji wa  upimaji na uchangiaji wa damu salama. Siku ya Kilele (tarehe 08 Machi, 2014), kuliendeshwa Kongamano la Wanawake,  ambapo washiriki walipata fursa ya kujadiliana juu ya  hali ya Wanawake katika nyanja za kuchumi, kisiasa, kijamii na afya, pamoja na udhalilishaji wa kijinsia.
 
·         Katika  kupiga vita vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake, Umoja wa Mataifa umeweka siku 16 maalum (kuanzia tarehe 25 Novemba hadi tarehe 10 Disemba ya kila mwaka) kwa nchi wanachama kufanya kampeni na kuhamasisha jamii juu ya kupambana na vitendo hivyo. Kwa Unguja, kampeni hiyo iliendeshwa kwa kuandaa kongamano la siku moja lililowashirikisha  wadau kutoka taasisi za Serikali na zisizo za Serikali. Kwa upande wa Pemba, Wizara ilishirikiana na SOS kuandaa maandamano na mkutano wa hadhara iliyohusisha, pamoja na mambo mengine, mabango yenye ujumbe wa kupinga udhalilishaji, michezo ya kuigiza na hotuba za viongozi.  Kwa mwaka 2014, kampeni hii iliendeleza ujumbe unaosema “AMANI YA DUNIA HUANZA NYUMBANI; TUPINGANE NA VITENDO VYA UTUMIAJI WA NGUVU DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO.
 
·         Idara imeratibu uanzishwaji wa Mabaraza ya Watoto 38 ya Shehia (Unguja 29 na Pemba 9) ili kuinua ushiriki wa watoto katika mambo yanayowahusu. Kwa Unguja Mabaraza  hayo yameanzishwa katika Wilaya za Kaskazini B (8),  Kaskazini A (1), Mjini (10) na  Kati (10) na kwa Pemba yameanzishwa katika Wilaya za Wete (3) na Mkoani (6). Mabaraza haya yanasaidia watoto kujua haki zao na kusaidia kuripoti matukio mbali mbali yanayohusu watoto. Mabaraza mawili ya watoto ya Wilaya ya Magharibi katika maeneo ya Mwanakwerekwe na Welezo yamekaguliwa ili kuangalia utendaji wao. Hali ya Mabaraza ya Watoto imeonesha kuwa yamekuwa yakikosa ushirikianao kutoka kwa viongozi, wakiwemo Madiwani, Wabunge na Wawakilishi katika maeneo yao. Aidha, kwa upande wa Pemba Mabaraza kumi na moja (11) yametembelewa kuangalia utendaji wake, ambapo ilibainika kuwa yanaendelea vizuri, watoto wanasaidiana  na wanatoa taarifa juu ya mambo yanayohusu watoto yanayotokezea katika shehia zao.
 
·         Katika  Kuratibu na  kufuatilia utekelezaji wa Sera na Sheria ya Mtoto, Idara imeendesha mafunzo juu ya ushughulikiaji wa masuala ya  watoto wanaokinzana na Sheria. Mafunzo hayo yalitolewa kwa watendaji 53 kutoka taasisi za Serikali na zisizo za Serikali zinazoshughulikia masuala ya watoto. Lengo ni kuhakikisha kuwa watoto wanaokinzana na sheria wanashughulikiwa katika ngazi ya jamii, badala ya utaratibu wa kimahkama uliopo sasa, ikizingatiwa suala zima la kulinda haki zao za msingi kama ilivyoelekezwa katika Mkataba wa Haki za Mtoto.
 
·         Idara pia imesimamia uandaaji wa Mkakati wa Haki za Mtoto (2013-2018) pamoja na Mpango wa Utekelezaji kwa mwaka 2014. Uandaaji wa Mkakati huo pamoja na Mpango wake wa utekelezaji ulishirikisha taasisi nyengine zinazohusika, zikiwemo Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Mahkama, Vyuo vya Mafunzo, Polisi, na Taasisi zisizo za Serikali. Aidha,  Wizara imeandaa kanuni kwa ajili ya uendeshaji wa Mahkama ya Watoto kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa haki za watoto.
 
·         Kwa kushirikiana na UNICEF, Wizara imo katika hatua za kuandaa Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Masuala ya Haki za Kisheria za Mtoto (Child Justice Monitoring and Evaluation Framework). Mfumo huu, pamoja na mambo mengine, utawezesha Wizara kufahamu kesi za watoto zilizopo na hatua zilizofikiwa katika Mahkama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Polisi. Aidha, utawezesha kujua kama mfumo wa sheria unazingatia ipasavyo masuala ya haki za watoto, kama yalivyoainishwa katika Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto na Mkataba wa Afrika kuhusu haki za Watoto.
 
 
·         Kupitia Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto, juhudi za kuviimarisha vikundi vya kiuchumi vya wanawake zimeendelezwa. Jumla ya vikundi 70 vilitembelewa kwa lengo la kutathmini mahitaji na maendeleo yao, pamoja  na kuona  changamoto zinazowakabili ili kuwapatia ushauri unaofaa kwa ajili ya kuimarisha shughuli zao za kiuchumi (Angalia Kiambatanisho Namb. 14). Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko imeviwezesha vikundi 49 vya wajasiriamali wanawake (42 Unguja na 7 Pemba) kushiriki katika Maonesho ya 36 ya Sabasaba, kwa lengo la kutangaza biashara zao. Vile vile, mafunzo ya ujasiriamali na namna ya kutafuta masoko yametolewa kwa  Waratibu wa Shehia 99 wa shughuli za  wanawake na watoto katika Wilaya za Kaskakazini A, Magharibi na Kati Unguja, ili waweze kutoa mafunzo kwa vikundi vilivyopo katika maeneo yao. Kwa upande wa Pemba, tathmini ya vikundi vya ujasiriamali vya wanawake imefanywa katika Shehia 33 za Mkoa wa Kaskazini (21 Wete na 11 Micheweni) kwa lengo la kupata taarifa sahihi za vikundi hivyo.  Taarifa hizo zitatumika katika kuandaa mipango ya kuviimarisha vikundi hivyo (Angalia Kiambatanisho Namb. 15). 
 
62.              Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015, Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:
 
1.      Kuratibu na kusimamia haki  za wanawake na watoto;
2.      Kuratibu na  kufuatilia utekelezaji wa Sera na Sheria ya Mtoto;
3.      Kuimarisha uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za kiuchumi, kijamii na maendeleo ya wanawake na watoto;
4.      Kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa Mabaraza ya Watoto;
5.      Kuimarisha mashirikiano ya kitaifa, kikanda na kimataifa kwa mambo yanayohusu wanawake na watoto; na
6.      Kuratibu na kusimamia mapambano dhidi ya udhalilishaji wa wanawake na watoto.
63.              Mheshimiwa Spika, Ili Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto iweze kutekeleza malengo yake kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Milioni Sitini, Laki Saba na Elfu Sitini na Tatu (Tshs. 60,763,000/=) kwa kazi za kawaida na Shilingi Milioni Mia Moja Tisini  na Tano na Laki Sita  (Tshs.195,600,000/=) kwa kazi za Maendeleo.             
 
OFISI KUU PEMBA
64.              Mheshimiwa Spika, Ofisi kuu Pemba inasimamia shughuli zote za Wizara kwa upande wa Pemba, ikiwemo utekelezaji wa majukumu ya Idara mbali mbali za Wizara. Hivyo, utekelezaji wa majukumu  kwa mwaka 2013/2014 pamoja na malengo kwa mwaka 2014/2015 kwa Ofisi hii, ni kama ilivyoainishwa katika Idara husika, ambazo maelezo yake yamehusisha pia na Pemba.  
 
65.              Mheshimiwa Spika, Ili Ofisi Kuu Pemba iweze kutekeleza majukumu yake kwa mwaka wa fedha 2014/2015, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Milioni Mia Tatu Thelathini na Nane, Laki Tano na Elfu Hamsini (Tshs. 338,550,000/=) kwa Kazi za Kawaida na Shilingi Milioni Mia Nne Hamsini na  Thelathini na Sita Elfu (Tshs. 450,036,000/=) kwa ajili ya mishahara, mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na maposho ya wafanyakazi.
                                                                                      
 
HITIMISHO
 
66.              Mheshimiwa Spika, Tunatambua na kuthamini sana michango ya Washirika wa Maendeleo katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Napenda nichukue nafasi hii adhimu, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya zanzibar, kuwashukuru sana washirika wetu wa maendeleo kwa mashirikiano waliyotupa katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kuimarisha ustawi na maendeleo ya vijana, wanawake, watoto, wazee na wananchi wanaoishi katika mazingira magumu zaidi. Washirika hao ni pamoja na nchi wahisani, ikiwemo Umoja wa Ulaya, India na Jamhuri ya Watu wa China na Mashirika ya Kimataifa, ikiwemo UNFPA, UNICEF, UNESCO, UNDP, ILO, SAVE THE CHILDREN, FHI, Tunajali Program, CHAI, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, pamoja na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Jumuiya ya Madola;
 
67.              Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza majukumu yake, Wizara pia ilishirikiana na Wizara na taasisi nyengine za Serikali pamoja na zisizo za Serikali, ikiwemo sekta binafsi. Napenda kuchukua fursa hii kuzishukuru taasisi hizo kwa mashirikiano waliyotupa na naziomba tuendelee kushirikiana, ili kwa pamoja tuweze kufikia malengo tuliyopanga kwa maslahi ya wananchi na Taifa letu kwa jumla.
 
68.              Mheshimiwa Spika, Natoa shukrani maalum kwa Ofisi za Mikoa, Wilaya na Shehia kwa mchango wao katika usimamizi na ufuatiliaji wa masuala mbali mbali yanayohusu Wizara kwenye maeneo yao, ikiwa pamoja na masuala ya kupiga vita udhalilishaji wa wanawake na watoto. Pia natoa shukrani kwa taasisi za kiraia ambazo zimechangia katika juhudi za Serikali za kuimarisha ustawi na maendeleo ya vijana, wanawake, watoto, wazee na wanaoishi katika mazingira magumu zaidi. Taasisi hizo ni pamoja na ZAYEDESA, ZACA, ZAIADA, ZAWDO, ZAFELA, ZAWCO, ZAMWASO, ZANGOC, ZLSC, COWPZ, PIRO, UVIKIUTA, UWT, ACTION AID, WEDTF, TAWLA, TAMWA, CHANGAMOTO, PRIDE, TMC na TGNP. Shukurani zangu pia ziende kwa  taasisi za kifedha, ikiwemo BOT, PBZ, CRDB, FBME, na Benki ya Posta kwa mashirikiano yao mazuri kwa Wizara, hususan kwenye program za uwezeshaji wananchi kiuchumi.
 
69.              Mheshimiwa Spika, Vyombo vya habari navyo vimetoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa shughuli zetu, ikiwemo kutangaza matukio mbali mbali yaliyohusu Wizara, pamoja na kuelimisha jamii juu ya masuala ambayo Wizara inayafanyia kazi, ikiwemo programu za kupinga vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto. Hivyo, nachukuwa fursa hii kuwapongeza viongozi na watendaji wa vyombo hivyo vya habari, vikiwermo redio, televisheni na magazeti kwa mashirikiano yao kwa Wizara.
 
70.              Mheshimiwa Spika, Yote ambayo nimeyaeleza yametekelezwa kwa shirikiano mkubwa wa Watendaji Wakuu na Wafanyakazi wote wa Wizara. Napenda kuwashukuru na kuwapongeza Wafanyakazi wote wa Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto kuanzia Katibu Mkuu Nd. Asha Ali Abdulla, Manaibu Katibu Wakuu Nd. Ali Khamis Juma na Nd. Msham Abdalla Khamis, Wakurugenzi, Ofisa Mdhamini pamoja na Maafisa wafanyakazi wa ngazi zote kwa kufanya kazi kwa umakini na juhudi kubwa. Mashirikiano haya yamepelekea kutekeleza malengo na majukumu yetu kwa ufanisi mkubwa. Aidha, nawaomba waendeleze umoja, mashirikiano, mshikamano, upendo na nidhamu ili tuweze kufanikisha vyema malengo yetu kwa mwaka wa fedha unaokuja na itakayofuata.
 
71.              Mheshimiwa Spika, Ili Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto iweze kutekeleza malengo na majukumu yake kwa mwaka wa fedha 2014/2015, kwa heshima na taadhima nawaomba Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati yako wapokee, wajadili, watupe ushauri na maelekezo na hatimae wapitishe na kuidhinisha matumizi ya jumla ya Shilingi Bilioni Saba, Milioni Mia Tano Sabini, Laki Sita na Elfu Sabini (Tshs. 7,570,670,000/=). Kati ya hizo, Shilingi Bilioni Mbili, Milioni Mia Moja Hamsini na Tano na Laki Mbili (Tshs. 2,155,200,000/=)  ni kwa ajili ya mishahara, michango ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na maposho maalum kwa wafanyakazi; Shilingi Bilioni Moja, Milioni Mia Nne Thamanini na Tano  na Laki Nane (Tshs. 1,485,800,000/=) ni kwa matumizi mengineyo; Shilingi Bilioni Moja, Milioni Mia Tano na Elfu  Ishirini na Nne (Tshs. 1,524,000,000/=) ni kwa kazi za Maendeleo na Shilingi Bilioni Mbili, Milioni Mia Nne na Tano, Laki Sita na Elfu Sabiini (Tshs. 2,405,670,000/=) ni fedha zilizoahadiwa kutolewa na Washirika wa Maendeleo (Angalia Kiambatanisho Namb. 16). Pia naomba idhini ya kukusanya mapato ya Shilingi Milioni Kumi (Tshs. 10,000,000/=) kupitia usajili na ukaguzi wa vyama vya ushirika kwa mwaka 2014/2015.
 
 
72.              Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja.
 
 
 
 
                                                         Ahsanteni

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.