Habari za Punde

Sitta: Tunapokea maoni hatubadili rasimu

Na Mwantanga Ame, Dodoma
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta, amesema mapendekezo yanayotolewa na makundi tofauti, hayatabadili rasimu ya Katiba iliyopo, bali yanalenga kuweka msisitizo wa kutambulika mahitaji ya makundi hayo kwani Bunge la Katiba halipokei maoni mapya.
Mhe. Sitta, aliyasema hayo jana wakati akipokea mapendekezo ya kundi la Wasanii wa Tanzania, wakiwemo wa Zanzibar, huko Mjini Dodoma, ambapo vikao vya Bunge Maalum la Katiba vinaendelea kufanyika katika kamati 12 za Bunge hilo.
Maoni hayo yaliwasilishwa na kundi la Wasanii wa kazi za Muziki wa kizazi kipya, Wasanii wa Filamu, Wasanii wa kazi za Sanaa Ufundi na Maonyesho.
Wiki iliyopita Bunge hilo lilipokea maoni yaliyotoka katika makundi ya wakulima, wafugaji na wavuvi, baada ya makundi hayo kukabidhi waraka rasmi uliokuwa una mambo mbalimbali yaliyokuwa yakiyahusu makundi hayo.
 
Mhe. Sitta alisema amelazimika kuweka wazi hilo kwa vile Ofisi yake inachokifanya ni kupokea mitazamo ya makundi hayo kwa dhamira ya kuona ni vipi yataweza kuzingatiwa na Wajumbe wa Bunge hilo, wakati wakiendelea na kazi zao ndani ya Kamati.
 
Alisema mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya imeweza kuzingatia mambo mengi ikiwemo sura ya nne inayoyahusu makundi ya kijamii ambapo baadhi yake yameonekana kusahaulika kwa baadhi ya mambo.

Alisema kwa vile rasimu hiyo bado sio msahafu ndio maana Wajumbe wa Bunge hilo wamelazimika kuwapo hapo ili kuifanyia kazi kwa kuona ni vipi wataweza kuzingatia mambo ya msingi kuwamo ndani ya Katiba mpya.
Alisema Tanzania hivi sasa, vijana wake wengi wamekuwa wakifanya kazi za usanii jambo ambalo ni la msingi kuzingatiwa ndani ya mchakato huo ili kuona ni vipi wataweza kufanikisha mambo yao.Alisema ni kweli Katiba iliyopo tayari imeshapitwa na wakati, na maamuzi ya kutunga Katiba mpya yachukuliwe kuwa ni rafiki kwa Wananchi wa kawaida, kwa vile kuna maeneo ambayo ni muhimu kuangaliwa na kuzingatiwa kwa faida ya jamii.
Akiyataja maeneo hayo alisema ni yale ambayo yamekuwa yakihusu suala la haki hasa kwa vile Katiba ya sasa imekuwa ikiizingatia zaidi mali isiyohamishika huku mali isiyoshikika ikiwa haitambuliki.
Alisema hilo ni tatizo na ni lazima Bunge hilo, lione umuhimu wa kuzingatia m aoni ya makundi tofauti kwa vile ni sehemu itayoweza kupatikana kwa Katiba bora.
Nea Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Mhe. Samia Suluhu Hassan, alisema kitendo cha makundi tofauti kuamua kutoa maoni yao, imekuwa ikilipa moyo Bunge hilo ili liweze kuendelea vizuri kufanya kazi zake.
Alisema mchakato wa Katiba umekuwa unachukua mambo muhimu na ya msingi na maoni ya makundi yasioshikika yanauwezo wa kuifanya kazi hiyo vizuri.


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.