Na Kadama Malunde,Shinyanga
Mwenyekiti CCM mkoa wa
Shinyanga, Khamis Mgeja, aliwataka wananchi katika manispaa ya
Shinyanga,kuwapuuza waliokuwa madiwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),waliohamia
CCM na baada ya miezi sita kurudi tena Chadema.
Alisema hayo wakati akizungumza
kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika siku mbili katika kata ya Masekelo na
Ngokolo mjini humo.
Kata hizo zilikuwa zikiongozwa
na madiwani kutoka Chadema, Sebastian Peter na Zacharia Mfuko kabla ya
kujiuzulu na kuhamia CCM kabla ya kurejea tena CHADEMA.
Alisema kutokana na madiwani
hao kukosa nidhamu ya kisiasa, wananchi wanapaswa kuwapuuiza.
Alisema shutuma zilizotolewa na
madiwani hao ni za uchonganishi zinazolenga kusababisha uvunjifu wa amani.
“Nawataka wananchi wa manispaa ya Shinyanga na
taifa kwa ujumla kuwapuuza madiwani wa Chadema, waliohamia CCM na kurudi tena
Chadema, huku wakitoa kashfa zenye shutuma za mauaji kwenye mikutano ya
hadhara,maneno ambayo ni ya kichonganishi na kutaka kuvuruga amani ya Tanzania,”
alisema.
“Kipindi madiwani hao walipokuwa
wakihamia CCM, walitoa shutuma za mauji, kuwa viongozi wa Chadema taifa ndio
waliomuua Philip Magadula SheLembi, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa
wa Shinyanga ,kutokana na kutaka madaraka ya ngazi ya juu,” alisema.
“Na waliporudi tena Chadema,
wakatoa shutuma za mauaji, kuwa viongozi wa CCM wakiongozwa na Mbunge wa jimbo
la Shinyanga mjini Steven Masele,
waliwapa pesa madiwani hao kwa ajili ya kuitungua ndege ya Dk. Wilbroad
Slaa mjini Shinyanga, hamuoni maneno hayo kama ni uchonganishi,”alihoji.
Akijibu shutuma hizo, Mbunge wa Shinyanga mjini, Steven Masele, alikanusha
na kusema hazina ukweli wowote na kwamba ni propaganda za kisiasa, zenye uchonganishi
za kukosa sera za kuwaambia wananchi nini sababu za kuhama kwenye chama chao na
kwenda kingine.
Naye Mbunge wa jimbo la Kishapu,Suleimani
Nchambi, alisema madiwani hao walikuwa wanasumbuliwa na njaa, huku akiwataka
wananchi kuepukana na watu wanaofanya siasa kama biashara.
Madiwani hao walijiuzulu nyazifa zao Februari
25, na Februari 26 wakapokelewa rasmi na
kujiunga na CCM, mbele ya Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi CCM Taifa , Nape
Nauye na Julai 30 mwaka huu wakabwaga
manyanga na kurudi tena Chadema.
No comments:
Post a Comment