Habari za Punde

Akamatwa na mabomu manne ya kivita Z`bar


Na Rahma Suleimaan

Jeshi la Polisi Zanzibar limemkamata mtu mmoja akiwa na mabomu manne ya kivita ya kurushwa kwa mkono.

Moja kati ya mabomu hayo ni lililotumika darajani Juni 13 mwaka huu na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi kadhaa.

Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa, Kamishna wa Jeshi la Polisi, Hamdani Omar Makame, alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ni moja kati ya operesheni ya jeshi hilo ya kupambana na vitendo vya kihalifu ambavyo vimekuwa vikitokea nchini kwa kumwagiwa watu tindikali, milipuko ya mabomu na watu kuuawa kwa kupigwa risasi.

Hata hivyo, Kamanda Makame hakutaja jina la mtu huyo wala eneo alilokamatiwa.
"Ni katika mapambano hayo jeshi la polisi Zanzibar linamshikilia mtuhumiwa mmoja ambaye amethibitisha kujihusisha katika mtandao wa kuagiza, kuingiza na kuhifadhi mabomu ya kivita ya kurushwa kwa mkono ambayo yamekuwa yakitumika katika matukio mbalimbali ya kihalifu na uvunjifu wa amani katika maeneo mbalimbali hapa nchini," alisema.

Aliyataja matukio ambayo yametokea na yanahusishwa na mtandao huo ni pamoja na matukio ya milipuko ya mabomu Arusha, Mwanza, Zanzibar na Dar es Salaam.

Alisema kutokana na matukio ya kihalifu yaliotokea nchini, jeshi la polisi linaomba ushirikiano kutoka kwa wananchi wema kutoa taarifa zaidi zitakasaidia kuwabaini wahalifu miongoni mwa jamii yao.

"Wananchi wanapaswa kuwa makini na kujiepusha na watu wanaoweza kuwashawishi ili kujihusisha katika vitendo ambavyo vinahatarisha amani na usalama wa nchi yetu," alisema Hamdani.

Hata hivyo, aliwataka wananchi kutohusisha ukamataji wa watuhumiwa wa matukio na masuala ya kiimani na kusema mtu binafsi anapofanya uhalifu katika jambo lolote anashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi na wala sio kwa sababu ya dini au imani yake.

Alisema mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani visiwani hapa uchunguzi utakapomilika na akibainika kuwa anashirikiana na watuhumiwa waliokamatwa na matukio ya kigaidi atafikishwa katika mahakama jijini Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

3 comments:

  1. jamani mbona mnahatarisha usalama wa nchi

    ReplyDelete
  2. sijui nani tena keshapewa janga hilo

    ReplyDelete
  3. hiyo ndio ile dua waliyoisoma kule msikti wa kidongo chekundu wakachinja kila aina ya mnyama sasa matokeo yake ndio hiyo inafanya kazi na wala bado aMungu mkubwa na wala hachezewi

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.