Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na
Balozi wa Ujerumani Nchini Tanzania Bwana Egon Kochanke ofisini kwake vuga
Mjini Zanzibar
Balozi wa Ujerumani
Nchini Tanzania Bwana Egon Kochanke akibadilisha mawazo na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif katika jitihada za kuimarisha ushirikiano
kati ya Ujerumani na Zanzibar.
(Picha na Hassan Issa OMPR).
Balozi wa
Ujerumani Nchini Tanzania Bwana Egon Kochanke alisema amani na usalama ndio
njia pekee na ya msingi itakayoyavusha salama Mataifa mbali mbali ya Bara
la Afrika katika kuimarisha uchumi na usawi wao.
Bwana Egon
alieleza hayo wakati akijitambulisha rasmi alipokuwa na mazungumzo yake
na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake
Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Egon Kochanke
alisema mataifa mengi ya Bara la Afrika yamekosa fursa ya kuendelea na harakati
za kujiletea maendeleo kwa kukumbwa na wimbi la vurugu na vita.
Alizitolea mfano Nchi
za Somalia, Sudani ya Kusini pamoja na Nigeria ambazo zimekosa utulivu wa
kisiasa kutokana na kukumbwa na vitendo vya uvunjifu wa amani likiwemo suala la
Ugaidi linaloonekana kuitishia amani ya Dunia.
Balozi wa Ujerumani
Nchini Tanzania alipongeza na kuridhika na mazingira mazuri ya Rasilmali
na uwekezaji yaliyomo ndani ya Visiwa vya Zanzibar jambo ambalo alisema
atatumia nafasi yake ya Kidoplomasia Kuitangaza kwa Makampuni na mashirika ya
Uwekezaji vitega uchumi ya Nchini kwake.
“ Nitachukuwa juhudi
kama Balozi kujaribu kuyashawishi Makampuni na Mashirika ya Kijerumani
kulitumia Soko la Zanzibar katika kuendeleza miradi yao kiuchumi na kibiashara
“. Alisema Balozi huyo wa Ujerumani Nchini Tanzania.
Balozi Egon
alifahamisha kwamba Zanzibar inaeleweka vyema Nchini Ujerumani kutokana na
uzalishaji wake wa vyakula na bidhaa za Viungo ambavyo hupendwa na kuwa na
watumiaji wengi duniani.
Katika kuunga mkono
juhudi za Zanzibar katika kujinasua kiuchumi pamoja na kuimarisha soko la Ajira
Balozi Egon alifahamisha kwamba Serikali ya Ujerumani itaandaa mipango maalum
wa kutoa mafunzo ya kazi za amali kwa vijana wa Kizanzibari.
Alisema mpango huo
utakaoendeshwa Nchini Ujerumani utajengewa mazingira ya kwenda sambamba
na kuwaalika wataalamu wa sekta mbali mbali Zanzibar kupata fursa ya kutangaza
mazingira na vivutio vya uwekezaji vya Visiwa vya Zanzibar kwa
taasisi na makampuni ya Nchi hiyo.
Akitoa shukrani zake
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliiomba
Ujerumani kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika
harakati zake za kuimarisha uchumi na maendeleo ya ustawi wa Jamii.
Balozi Seif alisema
Serikali hivi sasa inaendelea kuimarish miundo mbinu katika sekta mbali mbali
za kiuchumi ikilenga zaidi uimarishaji wa kilimo ambacho huchukua zaidi ya
asilimia 80% ya wananchi wote Nchini Tanzania.
Alisema ili
kufanikisha sekta hiyo zana za kisasa kama Matrekta yatahitajika katika
kuwawezesha wakulima wengi hasa vijijini kuongeza uzalishaji utaozingatia
taaluma ya kisasa kwa lengo la kuondokana na kilimo cha asili chenye mapato
madogo.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar kupitia Balozi huyo wa Ujerumani Nchini Tanzania aliwaomba
wawekezaji, mashirika na Taasisi za Ujerumani kujenga viwanda mbali mbali
vitakavyookoa mazao ya kilimo mashambani.
Alisema Zanzibar ni
kituo kikubwa cha biashara ndani ya ukanda wa Bara la Afrika ambacho
wawekezaji hao wanaweza kukitumia jambo ambalo pia watapunguza wimbi la ukosefu
wa ajira kwa vijana wengi wanaomaliza masomo yao.
No comments:
Post a Comment