Habari za Punde

Urafiki wa China tuuangalie vema

Na Salim Said Salim
 
KATIKA siku za karibuni  nimekuwa ninapata wasi wasi ninaposikia au kuona nchi yetu inawafungulia milango Wachina kama ndugu na marafiki tunaotarajia kuchangia maendeleo ya nchi yetu.
 
Hali hii haitokani na labda ninawachukia . Kwa lugha mwanana ya Zanzibar…laa hasha! Kinachonishitua ni mwenendo wa hawa Wachina wa siku hizi ambao ni tafauti na ulivyokuwa miaka michache iliyopita chini ya uongozi wa Mwenyekiti Mao Dze Dung.
 
Hii inatokana na Mchina wa leo sio tu kubadili  kivazi chao cha asili iliopita na ambacho kwa kiasi kikubwa kilikuwa sehemu ya utambulisho wao .
 
Hata wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Nyerere ambaye alikipenda kivazi kile na kukifanya kuwa miongoNi mwa vivazi vya kitaifa hapa kwetu.
 
Wachina wa siku hizi wamebadilika, tena sana na ukweli ni kwamba sio tu wameamua kuvaa suti na tai shingoni bali wamekuwa wakitumia  hizo tai kukaba roho za nchi ziliowaona marafiki zao wa karibu.
 
Masikini China ya leo sio ya zamani na mwenendo wa baadhi ya raia wa wake umekuwa na sura ya kutisha, hasa kwa nchi za Afrika!

Nilipata bahati ya kufanya kazi kwa karibu na Mchina tangu udogo wangu nilipoanza kazi ya uandishi wa habari  zaidi ya miaka 50 iliyopita Zanzibar .
 
Niliwaelewa Wachina kama watu waadilifu, wenye ukweli na mwenendo wa kujituma na kutumikia wengine kwa moyo safi, lakini tabia yao ile imekuwa sehemu ya historia.
 
Ama kweli waliosema dunia ya leo inakabiliwa na mabadiliko ya nchi hawakukosea, lakini yapo mabadiliko makubwa ya tabia ya watu na miongoni mwa watu waliobadilika sana katka miaka ya karibuni ni Wachina.
 
Kwanza walibadili mavazi yao na sasa siasa, uchumi , utamaduni na tabia zao.
 
Mwishoni mwa miaka ya 1960 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980 tuliwasikia viongozi wa nchi za Afrika waliojiita wajamaa  wakilamikia nchi za Magharibi kwa kuanzisha ukoloni mamboleo katika Bara la Afrika.
 
Lakini siku hizi tunaona “ Ukoloni mambo kesho” wa Mchina. Hili linaonekana kwa  kila baada ya muda mfupi kupata taarifa za wafanyabiashara  wa kichina na baadhi ya maofisa wa ubalozi wake kudaiwa kuhusika na kuangamiza utajiri wa wanayama pori, hasa tembo, katika bara la Afrika.
 
Katika kipindi cha miaka mitatu iliopita tumeona Wachina wakikamatwa, kushitakiwa na wengine kusukumwa gerezani katika nchi nyingi za Afrika kwa kuhusika na biashara ya pembe za ndovu.
 
Hivi karibuni tu tumeelezwa kuwa wakati wa ziara ya Rais wa China,  Xi Jinping, hapa nchini Desemba, mwaka jana, ilitumika kusafirishia magendo ya meno ya tembo kwa kutumia mifuko ya kidiplomasia ndani ya ndege ya Rais huyo.
 
Serikali yetu na ya China zimekanusha madai hayo na kueleza kuwa huo ni uzushi . Lakini ripoti ziliochapishwa nchi mbalimbali zimezusha gumzo kubwa na sintofahamu iliyokosa majibu ya kuridhisha mpaka sasa.
 
Hii ni kwa sababu Wachina wamesemekana kuhusika zaidi na biashara haramu ya meno ya tembo kuliko watu wa nchi nyengine yeyote ile duniani.
 
 Ni hali hii imesababisha baadhi ya watu kuuliza nini hasa kinachosababisha China kuwa karibu zaidi na bara la Afrika, wanashangaa urafiki huo ni mkubwa zaidi kuliko ule alionao kwa majirani zake huko  bara la Asia?
 
Kwa muda mrefu nchi yetu imekuwa na uhusiano mzuri na China na kwa kweli wamesaidia miradi mingi ya maenedeleo bara na visiwani. Hii ni pamoja na kujenga viwanda vingi na hata viwanja vya michezo.
 
Lakini katika siku za nyuma hatukusikia taarifa za hawa tunaowaita ndugu zetu wa China kuhujumu uchumi wetu wala kushiriki kutokomeza urithi wetu wa wanyama pori.
 
Kwa muda mrefu sasa Watanzania wamekuwa wakilalamikia ongezeko kubwa la raia wa China na baadhi yao kujihusisha na biashara zinazotia wasiwasi ikiwemo kuuza karanga, miwa, mahindi na nyinginezo ambazo kwa raia wa kigeni si rahisi kuzifanya
 
Ninaamini Watanzania watakaojihusisha na biashara kama hizo nchini China hawataruhusiwa kufanya hivyo kwa vile kwa wageni kufanya kazi hizo kunawapunguzia Wachina nafasi za ajira.
 
 Katika siku za karibuni viongozi wetu wengi wa Serikali ya Muungano na Zanzibar wamefanya ziara za mara kwa mara China na kusaini mikataba mbalimbali ya mradi ya maenndeleo.
 
 Wiki hii tu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alikuwepo China kwa wiki nzima  na alitumia nafasi hiyo kuwaalika wawekezaji wa nchi hiyo kuwekeza hapa kwetu.
 
 Hatua hiyo si mbaya, hasa ukitilia maanani maendeleo makubwa ya kiuchumi ambayo China imeyapata katika miaka ya karibuni.
 
 Lakini ni vizuri pia tukaangalia kwa makini mwenendo wa hao wawekezaji watakaokuja hapa kwetu kwani baadhi yao wamesemekana kushiriki katika nchi jirani kusafiriha meno ya tembo na hata baadhi ya kampuni zao kupigwa marufuku kufanya kazi katika nchi hizo.
 
 Kesi nyingi za kukamatwa kwa baadhi yao katika viwanja vya ndege na katika majumba yao wakiwa na meno ya tembo ni kielelezo cha mchezo mchafu wa baaadhi yao wanaofanya katika nchi za Afrika.
 
Kwa hili la ziara ya kingozi wa China  nchini kwetu kutumika kusafirisha meno ya tembo hatupaswi kulipuuza hata kidogo. Ni vizuri likafanyiwa  uchunguzi wa kina na kwa kuwa limechukua sura ya kimataifa basi hao wachunguzi nao watoke nje ili tusafishe jina la nchi yetu.
 
Kutokana na ujangili wa meno ya tembo kukithiri katika miaka ya 1970 na 1980 idadi ya tembo hapa nchini ilipungua kutoka 110,000 hadi 55,000 hivyo tuna kila sababu ya kusafisha jina letu.
 
 Hata hivyo, hatua ya kupiga marufuku biashara ya meno ya tembo katika mwaka 1989  idadi ya wanyama hawa iliongezeka kufikia 143,000  katika mwaka 2006, lakini tunaambiwa wanyama hawa wamepungua kwa karibu theluthi mbili katika miaka ya karibuni.
 
 Taarifa hii inatisha na kama hatujachukua hatua zinazofaa tutakuja kujijutia siku za usoni na tembo ambao wamekuwa kivutio kikubwa cha watalii hapa kwetu watapotea kama iivyotokea katika matifa mengine
 
Siku chache zilizopita tumepata taarifa za kusikitisha zinazoeleza kuwa hata Twiga sasa wamekuwa wakiuawa kwa kasi kubwa, si ajabu tukasikia na wanyama wengine nao wanauawa kwa kasi
 
Wakati umefika wa kuhakikisha hatupotezi utajiri wetu wa wanyama pori. Kama tukifanya mzaha tutakuja kujijutia na vizazi vijavyo havitatusamehe kwa kupoteza utajiri tuliorithi kwa waliotutangulia.
 
Tusikubali urafiki wetu na nchi yoyote ile  kuwa ndio leseni ya kupora utajiri wetu wa wanyama pori au madini mbali mbali yaliyopo nchini kwetu.
 
Chanzo : Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.