Na Kija Elias, Same
Mbunge wa Same Mashariki,Anne
Kilango Malecela, amesema atapeleka malalamiko Sekretarieti ya Baraza la
Maadili ya Viongozi wa Umma, kupinga hatua ya Mkuu wa wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya,
Dk. Michael Kadeghe, kupeperusha bendera ya taifa kwenye gari lake akiwa wilaya
ya Same ambayo haiongozi.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Kilango alisema atamshtaki Kadeghe kwa Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji
Mstaafu, Hamis Msumi kutafuta haki kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria na
taratibu za nchini.
Mgogoro huo ulianza wiki iliyopita
baada ya Kilango na Dk. Kadeghe kuingia kwenye mtafaruku jimboni huo.
Wakati Kilango akikagua
barabara zinazojengwa kwa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete alikutana ana kwa ana na
Mkuu huyo wa wilaya akipeperusha bendera kwenye gari lake na kuanza kurushiana
maneno.
Kilango anadai kwamba, Dk.
Kadeghe, akiwa na gari lake lenye namba za usajili STK 3764 aina ya Land
Cruiser, alifanya kosa hilo kwa minajili ya kuwatisha wananchi wa jimbo lake
ili wamwamini anafaa kuwa mbunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu ujao,
unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
“Nitakutana na Mwenyekiti wa
Sekretarieti ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma ili kutafuta haki.
Haiwezekani wewe siyo DC wa Same upeperushe bendera kwenye wilaya ambayo
huiongozi? huko ni kuwatisha wananchi lakini pia asitake abebwe,”alisema.
Alisema ingawa Kadeghe hana
ubavu wa kumng’oa kwenye kiti chake, lakini pia hapaswi kumkejeli katika
kipindi ambacho anatekeleza ilani ya uchaguzi ya chama chake, kuelekea uchaguzi
mkuu na badala yake anatakiwa kuvuta subira hadi filimbi itakapopulizwa rasmi.
Mkuu huyo wa wilaya hiyo,
alipotafutwa kutoa ufafanuzi wa madai ya Kilango, alisema hajawahi kufanya
vikao vya siri vya chama kwa ajili ya kuendesha kampeni ya kumng’oa kwenye ubunge,
lakini pia bendera hiyo ilikuwa ikifanyiwa usafi na wala haikuwa inapepea kama
ambavyo inadaiwa.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2005, Kilango alimshinda Dk. Kadeghe kwa kura 389 dhidi ya kura 46 alizoambulia
kwenye uchaguzi wa ndani wa CCM na mwaka 2010, Kilango pia alimpiga mwereka mpinzani wake huyo kwenye kura
za maoni kwa kupata kura 7,900 dhidi ya kura 2,200 alizoambulia Kadeghe.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya
ya Same, Herman Kapufi alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu mgogoro huo, alisema
taratibu zipo wazi kwamba Mkuu wa wilaya akishavuka nje ya mipaka yake ya
utawala kwa mujibu wa madaraka ya ukuu wa wilaya chini ya sheria ya tawala za mikoa
namba 19 ya mwaka 1977 na sheria ya serikali za mitaa namba 7 na 8 za mwaka 1982,
Dk. Kadeghe amekosea kupeperusha bendera
kwenye wilaya ambayo si ya kwake.
No comments:
Post a Comment