Na Miza Othman –Maelezo
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekiri kuwa Skuli nyingi za Zanzibar zinaupungufu wa walimu wa masomo hasa ya Sayansi na Hesabati.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Zahra Ali Hamad huko Chukwani katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi wakati alipokuwa akijibu suala la Mh. Saleh Nassor Juma
Amesema katika kukabiliana na tatizo hilo Serikali imekuwa ikitumia mbinu mbali mbali katika kuongeza idadi ya walimu wa masomo ya Sayansi na Hesabati ikiwemo kuomba msaada wa walimu wa kujitolea kutoka mataifa na mashirika ya kujitolea kutoka mataifa mbali mbali.
Baadhi ya nchi na mashirika yaliyojitokeza kusaidia ni pamoja na Shirika la VSO la Uingereza, Peace Corps la Marekeni, JICA la Japani, Koica la Korea na Serikali ya Nigeria kupitia “Technical Aids Corps” ambalo lilikubali kuleta walimu 14 kufundisha masomo hayo
.
“Kutokana na kubadilishana uzoefu na ujunzi katika ufundishaji wa masomo ya Sayansi na Hesabati kati ya walimu wa kigeni na walimu wazalendo, kumepelekea ufaulu wa wanafunzi wengi katika mitihani ya kidato cha nne katika miaka ya hivi karibuni”, alisema Naibu Waziri.
Hata hivyo ameeleza kuwa Wizara yake inakusudia kutumia huduma za mtandao wa mawasiliano katika kusomeshea na kufundishia masomo mbalimbali kwa kutumia uwezo mkubwa wa mkongo wa Taifa wa mawasiliano wa simu uliopo hapa Zanzibar.
Aidha amesema hadi hivi sasa ni taasisi chache tu za elimu ndizo zilizounganishwa na mkongo wa taifa ikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibzr, Chuo cha Kiislamu Mazizini, Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia na Skuli ya Sekondari ya Kiembe Samaki.
Skuli hizo zimeunganishwa na mtandao kupitia kampuni ya Simu ya Zanztel. Pia Chuo Kikuu cha Taifa Cha Zanzibar kwa ufadhili wa Benki ya Dunia imepata fedha kwa ajili ya kuandaa maabara ya kurikodia vipindi mbalimbali vya masomo ya Sayansi na Hesabati.
No comments:
Post a Comment