STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 16.1.2015

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein leo ameongoza mazishi ya marehemu Mzee Makame
Mzee Suleiman aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Zanzibar.
Mazishi ya
Marehemu Mzee Makame Mzee Suleiman yalifanyika Mgenihaji, Wilaya ya Kati Mkoa
wa Kusini Unguja na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Naibu Katibu
Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuali Ali Vuai, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis
Haji, Mawaziri, Wawakilishi na viongozi wengine wa serikali, vyama vya siasa pamoja
na viongozi wa dini na wananchi.
Mapema Alhaj Dk.
Shein alishiriki katika sala ya kumsalia
Marehemu Mzee Makame Mzee Suleiman iliyofanyika huko katika Msikiti Mkuu wa Mgenihaji.
Akisoma wasifu wa
Marehemu, Katibu wa CCM, Wilaya ya Kati, Bwana Ali Yussuf alisema kuwa Marehemu
Mzee Makame Mzee Suleiman kifo chake kimetokea usiku wa tarehe 16 Januari, 2015
nyumbani kwake Amani, mjini Unguja.
Alieleza kuwa
Marehemu Makame Mzee Suleiman alizaliwa tarehe 14 Aprili, 1926, katika kijiji
cha Mitakawani, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini, Unguja na kupata Elimu ya
Msingi katika Skuli ya Uzini mwaka 1936.
Aidha,
alijiendeleza na masomo ya Qur-an katika kijiji hicho cha Mitakawani ambapo
mnamo mwaka 1945, marehemu alijiendeleza na elimu ya Sekondari.
Marehemu Mzee
Makame Mzee, alijiunga na Chama Cha Afro Shirazi Party (ASP) mwaka 1957 na ni
miongoni mwa Waasisi wa Chama cha Mapinduzi kilichozaliwa mwaka 1977,akiwa
katika Tawi la Mitakawani.
Katika uhai wake,
marehemu aliwahi kushika nyazifa mbali mbali ndani ya Chama na Serikali. Kwa
upande wa Chama na kutokana na uhodari, uwezo na weledi mkubwa wa masuala ya
kisiasa, Chama Cha ASP kilimteua kushika nafasi za uongozi zikiwemo Mwenyekiti
wa ASP Tawi la Mitakawani mnamom mwaka 1957-1977.
Mwaka 1961-1977
aliteuliwa kuwa Katibu wa ASP wa Wilaya ya Kati pamoja na kuwa Mjumbe wa
Mkutano Mkuu wa ASP Taifa. Pia, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Sekretarieti ya
Wilaya, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM wa Wilaya na Mkoa wa Kusini
Unguja.
Kwa upande wa
Serikali, marehemu alibahatika kushika nyadhifa mbali mbali ikiwa ni pamoja na
kuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi mnamom mwaka 1964-1972, Mkuu wa Wilaya ya
Kati, Unguja mnamo mwaka 1972-1974, Mkuu wa Wialaya ya ChakeChake, Pemba mnamo
mwaka 1974-1978 pamoja na kuwa Mshauri wa Rais wa Mambo ya siasa mwaka 1978.
Kwa kutambua
mchango wake mkubwa katika uongozi na Utumishi wa Umma, mwaka 2014, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein,
alimtunuku marehemu Nishani ya Miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Katibu huyo wa
CCM Wilaya ya Kati alieleza kuwa Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake
kinaungana na wanafamilia, ndugu na marafiki wa marehemu na kuwaomba wawe na
moyo wa subra katika wakati huu mgumu wa maombolezi ya Mzee Makame Mzee
Suleiman. Aidha, alieleza kuwa kifo cha marehemu kimeacha pengo kubwa kwa
Taifa.
Hadi kufariki
kwake, marehemu Mzee Makame Mzee Suleiman
alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar.
Marehemu ameacha
vizuka wawili na watoto ishirini (20). Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu
mahala pema peponi. Amin.
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment