TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MDAHALO KUHUSU KUZINGATIA MAMBO MUHIMU KATIKA KATIBA INAYOPENDEKEZWA UTAKAOFANYIKA TAREHE 24 Januari 2015, KATIKA UKUMBI WA MCC MUSOMA.
Taasisi ya Mwalimu Nyerere imeandaa mdahalo kuhusu kuzingatia mambo muhimu katika Katiba Inayopendekezwa. Huu ni mfululizo wa midahalo na majadiliano kuhusu Katiba Inayopendekezwa. Mdahalo huu utafanyika siku ya Jumamosi tarehe 24/01/2015, kuanzia saa 8:00 mchana mpaka saa 12:00 jioni katika ukumbi wa MCC Musoma.
Mdahalo huu unalenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia mambo muhimu yaliyomo katika Katiba Inayopendekezwa, na kuwapa fursa wananchi kusikiliza na kuelewa mambo muhimu na ya msingi kabla ya zoezi la upigaji kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa. Ikumbukwe kuwa Taasisi ya Mwalimu Nyerere hailengi wala haikusudii kukosoa au kuanzisha malumbano na mtu wala Taasisi yoyote ile, bali lengo ni kutoa elimu ya uraia na kupanua uelewa wa Katiba Inayopendekezwa.
Kama ilivyo kawaida ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa midahalo iliyokwisha fanyika katika Jiji la Dar es Salaam na Mwanza, mdahalo huu utafanyika kwa njia ya amani, utulivu na bila hofu yoyote. Ni mdahalo wa wazi kwa kila mtu kuhudhuria.
Washiriki katika mdahalo huu ni pamoja na baadhi ya wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakiwemo Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume; wengine ni waliokuwa makamishina wa Tume ambao ni Ndugu Joseph Butiku, Prof. Mwesiga Baregu, Prof. Paramagamba Kabudi, Ndugu Humprey Polepole na Ndugu Ali Saleh kutoka Zanzibar. Vilevile wananchi na Viongozi kutoka taasisi na asasi mbalimbali zinazowakilisha jamii ya Watanzania ambazo ni pamoja na asasi za kiraia (NGOs), vyama vya siasa, madhehebu ya dini, wasomi, vyombo vya habari, taasisi za kitaaluma, vyama vya ushirika, vyama vya wafanyakazi, n.k. wanakaribishwa kushiriki.
Imetolewa na;
Taasisi ya Mwalimu Nyerere,
22 Januari 2015
GALLUS N. ABEDI
k.n.y: MKURUGENZI MTENDAJI
Nakala: Habari Maelezo Dar es Salaam
Vyombo vyote vya habari,
ITV, TBC, Star TV, Channel Ten,
Radio Sauti Fm, Radio One, Radio Free Africa (RFA),
Nipashe, Mwananchi, Majira, Tanzania Daima,
Majira, Uhuru, Mtanzania, Raia Mwema, Mawio
No comments:
Post a Comment