Habari za Punde

Mkutano wa 59 wa Kamisheni kuhusu Hadhi ya Wanawake wafanyika UN

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akiwa na wajumbe wa Tanzania waliohudhuria na kushiriki  Mkutano wa 59 wa Kamisheni  kuhusu  Hadhi ya  Wanawake ( CSW) mara baada ya kufungwa kwa mkutano huo wa wiki mbili jana Ijumaa.
 Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi akiwa na  wajumbe  kutoka Zanzibar  waliohudhuria mkutano wa  59 wa CSW

Na  Mwandishi Maalum

Mkutano wa 59 wa Kamisheni kuhusu  Hadhi ya  Wanawake umemalizika kwa kutoka na maazimio mbalimbali   likiwamo  linalobainisha kuwa  tofauti zote za usawa wa kijinsia zinamalizwa ifikapo mwaka 2030

Mkutano huo wa wiki mbili na ambao umehudhuriwa  na  mamia ya  wawakilishi  kutoka mataifa ambayo ni wanachama wa  Umoja wa Mataifa, Taasisi za UM na Asasi zisizo za Kiserikali pia ulipitisha kwa kauli moja  tamko la kisiasa ambalo  limeainsha na kuazimia mambo kadha kwa kadha yanayohusu  fursa  sawa za kijinsia na uwezeshaji wa mwanamke.
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huu,  uliongozwa na Mhe. Sophia Simba ( Mb), Waziri wa Maendeleo ya Jamii,  Jinsia na Watoto.

Kupitia mkutano huo wajumbe hao walijadiliana na kubadilishana mawazo  kuhusu  mafanikio  katika utelekezaji wa maazimio mbalimbali yaliyokubalika wakati  wa Mkutano wa kihistoria wa wanawake uliofanyika  Beijing mwaka 1995 pamoja na changamoto zake.

Akihitimisha mkutano huo Katibu Mkuu  Msaidizi Mwandamizi na Mkurugenzi Mtendaji wa UN- Women,  Bibi.  Phumbzile Malambo-Ngacuka  amesema mwaka 2030  lazima uwe hitimisho la utofauti wa kijinsia jukumu linalotakiwa  kufanyiwa kazi kuanzia ngazi ya familia,  kijamii,  kisiasa na kiuchumi.

Naye Mwenyekiti wa Kamisheni Bi Kandra Vajarabhaya  akizungumzia mwenendo mzima wa mkutano huo anamesema, kwa wajumbe  kupitisha kwa kauli  moja tamko la kisiasa, kamisheni hiyo  imerejea wajibu  wake  wa  kuchagiza na kufanikisha  upatikanaji wa fursa sawa za kijinsia, uwezeshaji wa wanawake pamoja na  kuhakikisha haki za wanawake na watoto wa kike.

 Akatoa pia tathimini ya utekelezaji  wa maazimio  pamoja na  Jukwaa la utekelezaji wa mkutano wa Beijing pamoja na  changamoto zilizobakia.

Kupitia mchakato huu   Bi  Vajarabhaya amesema wajumbe  wamemejifunza kwamba bado kuna changamoto , na kwamba   mkutano wa kamisheni hiyo umetoka na mapendekezo kadhaa ya  kuimarisha utendaji wa chombo hicho.

Pamoja na majadilianao  ya ajenda mbalimbali   mkutano huo  umepitisha  maazimio manne likiwano linalohusu namna ya kuwasaidia wanawake wa Palestina, azimio hilo lilipitishwa kwa kupigiwa kura ambapo kura 27 ziliunga mkono azimio hilo huku  mbili (  Israel na  Marekani ) zikilipinga.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.