Habari za Punde

Balozi Seif: Vyombo vya dola vitakuwa makini kuhakikisha amani inakuwepo nchini

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanbzibar Balozi Seif akijibu maswali aliyoulizwa na Wanahabari wa Shirika la Magazeti ya Serikali la Zanzibar leo Hafsa Golo aliyepo Kati kati na Tatu Makame wa kwanza kushoto.


Ripota wa Shirika la Utangazaji Tanzania {TBC } Marine Hassan akiporomosha maswali kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa mahojiano yao kuhusu maadhimisho ya Miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis Ame, OMPR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitegemei kuona kura ya Maoni ya Katiba Mpya ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu  unakumbwa na vurugu  zinazoweza kuepukwa mapema.

Akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania { TBC } mapema wiki hii Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba vyombo vya Dola vitakuwa makini muda wote kabla na baada ya matukio hayo mawili katika kuhakikisha amani inaendelea kudumu muda wote.

Balozi Seif Ali Iddi alisema suala la ulinzi na usalama ndani ya Taifa hili linamgusa kila Mwananchi  anayepaswa kuwajibika muda wote kwa kuwafichua watu au vikundi vinavyoashiria kutaka kujiandaa kufanya vurugu kwa kuchafua amani inayohitajika na  kila mtu.

Alisema kura ya maoni sambamba na uchaguzi mkuu unaofanyika kila baada ya miaka mitano n mambo ambayo yamo ndani ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania yakitekelezwa katika lengo la kuimarisha Utawala Bora  kwa mujibu wa Maazimio ya Umoja wa Mataifa Tanzania ikiwa ni Mwanachama wake.

Akizungumza pia na Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar { Zanzibar Leo } Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika kuimarisha miundo mbinu ya kiuchumi ndani ya Kipindi cha Miaka mitano iliyopita.

Balozi Seif alisema miradi ya Bara bara zilizomo ndani ya mpango wa ujenzi Unguja na Pemba hivi sasa zimekamilika na juhudi zinaelekezwa zaidi katika kuimarisha huduma za maji safi na salama katika baadhi ya maeneo ya Mijini na Vijijini ambayo bado yanakabiliwa na upungufu huo.

Alifahamisha kwamba zipo baadhi ya changamoto ikiwemo Bajeti ndogo ambayo haikidhi mahitaji halisi katika kukamilisha baadhi ya miradi ya Maendeleo hasa katika sekta za Elimu, Huduma za Maji pamoja na miradi ya Jamii.

Akijibu Swali la Mafuta na Gesi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Suala hilo linasubiri Katiba Mpya ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inayopendekezwa ambalo limetolewa katika Mambo ya Muungano.

Alisema endapo Katiba hiyo itapita kwenye Kura ya Maoni inayotarajiwa kupigwa baadaye mwaka huu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatengeneza Sera na Sheria inayohusu mambo ya Mafuta na gesi ili kuweka wazi uanzishwaji wa miradi itakayotokana na Sekta hiyo.

Alifahamisha kwamba upo muelekeo unaoonyesha kuwepo kwa nishati hiyo hapa Zanzibar kutokana na kujitokeza kwa Wataalamu na Makampuni  ya Mafuta na Gesi yanayotaka kushirikiana na Zanzibar katika kufanya utafiti wa nishati hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.