Habari za Punde

Afariki baada ya kugongwa na gari Wete Pemba

Hassan Khamis, Pemba
MTU mmoja amefariki dunia baada ya kugongwa na gari wakati alipokua akiendesha baiskeli eneo la Mwane wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba .
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba kamishna Msaidizi wa Polisi Sheikhan Mohamed Sheikhan amethibitisha kutokea kwa tukio hilo wakati alipokuwa akitoa tarifa kwa waandishi wa habari afisini makao makuu ya jeshi hilo mjini Wete.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 3, mwaka huu majira ya saa 5:20 asubuhi Mwane wilaya wakati gari ya abiria yenye namba za usajili Z 524  ya Wete-Chake ikitokea Mzambarau Takao kuelekea Madenjani ilimgonga mpanda baiskeli.
 Kamanda huyo alieleza kuwa gari hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na dereva Khamis Juma Omar (30) mkaazi wa Kiuyu Minungwini, ndio iliomgonga mpanda baiskeli huyo Kassim Salim Issa (40) mkaazi wa Chwale Madenjani Wete ambae alikua anatokea Madenjani kuelekea Mzambarau Takao .
Kamanda huyo ameongeza kuwa mara baada ya kutokea kwa ajali hiyo Kassim alikimbizwa hadi katika Hospitali ya Wete kwa matibabu ingawa baadae majira ya 9:45 jioni alifariki dunia katika hospitali hiyo.

Nae Daktari Omar Salim ambae ameufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, alisema marehemu alikatika mikono yote yote miwili pamoja na kukatika mguu wa kulia na kuumia sememu ya kichwa .
Daktari huyo ameongeza pia maerhemu alivuja sana damu kichwani na jambo ambalo lilipelekea kukosa nguvu za kawaisda na kusababisha kifo chake .
Nao wananchi walioshudia tukio hilo wamelitaka jeshi la polisi mkoa wa Kaskazini Pemba kuhakisha askari wa usalama Barabarani wanakuwepo barabarani muda wote ili kuthibiti mwendo kasi kwa madereva.
Wametoa wito kwa jeshi hilo pia kutowafumbia macho madereva wakorofi na wazembe ambao wamekua wakigharimu maisha ya watu kila siku kutokana na mwendo kasi na udereva usiojali sheria na taratibu za barabara.

Nae kamanda Shehani ametoa wito kwa madereva kujali uhai wa watu wengine kwani ajali zimekua zikiacha watoto yatima wengi mitaani na kuzifanya familia nyingi kuyumba kiuchumi kutokana na kuondoka kwa wategemezi wao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.