Habari za Punde

Hotuba ya Bajeti Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais



HOTUBA YA BAJETI YA OFISI YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS

KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016



HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS MHESHIMIWA FATMA ABDULHABIB FEREJ
KUHUSU
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA OFISI YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016





UTANGULIZI

1.     Mheshimiwa Spika,  kwa ruhusa yako naomba  kutoa hoja  kwamba Baraza lako sasa likae kama Kamati ya matumizi ili liweze kupokea, kuzingatia, kujadili, kuchangia na hatimae kuidhinisha  Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mwaka wa fedha 2015/2016.

2.     Mheshimiwa Spika, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uzima na afya njema na kuweza kukutana kwa lengo la kujadili hotuba hii ya OMKR. Namuomba Mwenyenzi Mungu atuwezeshe kukamilisha vizuri miaka mitano ya awamu hii ya saba tukimalizia uwasilishaji wa hotuba ya bajeti kwa mwaka 2015/2016 mbele ya Baraza lako.

3.     Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohammed Shein kwa kuwa karibu nasi kwa muda wote katika utendaji wa kazi zetu za OMKR.  Hakika ukaribu wake huo tunauthamini sana maana umetuwezesha kutekeleza majukumu yetu ya kuwahudumia wananchi bila ya hofu na kwa mafanikio.

4.     Mheshimiwa Spika, vile vile  sina budi kuwapongeza  viongozi  wetu wa kitaifa Makamu wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa jitihada zao za kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuwatumikia wananchi wa Zanzibar.


5.     Mheshimiwa Spika, natoa shukurani na pongezi maalumu kwa Makamu wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad kwa uongozi wake imara.  Miongozo na ushauri wake anaotupa katika kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa masuala mtambuka yanayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais umekuwa ni chachu kwa mafanikio tuliyopata.  Kwa niaba ya wafanyakazi wote wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, tunaahidi kuendelea kushirikiana naye ili kuleta maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

6.     Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naomba nikupongeze wewe binafsi Mheshimiwa Spika pamoja na wasaidizi wako wakiwemo Naibu Spika na Wenyeviti wa Baraza kwa kuliongoza vyema.

7.     Mheshimiwa Spika, namshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitafifa Mheshimiwa Hamza Hassan Juma, pamoja na wajumbe wote wa Kamati yake kwa kushirikiana nasi bega kwa bega katika kuhakikisha tunafanikisha utekelezaji wa malengo ya OMKR.  Naishukuru pia Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Hesabu za Serikali chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Omar Ali Shehe, Mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Chake Chake kwa mashirikiano mema na OMKR.

8.     Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru wajumbe wenzangu wa Baraza hili la Wawakilishi, kwa mashirikiano yao ya dhati kwangu mimi binafsi pamoja na watendaji wa Ofisi yetu tukiwa ndani ya Baraza na hata katika majimbo yao. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie uchaguzi wa salama na atuwezeshe kukutana tena katika awamu ijayo.  Aidha, nachukua nafasi hii kuwatakiwa wote mafanikio mema katika uchaguzi unaokuja.

9.     Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa mashirikiano makubwa wanayonipa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi yetu. Vilevile, napenda kuwashukuru kwa dhati Afisa Mdhamini wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Wakurugenzi pamoja na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa juhudi, bidii na ustahamilivu katika kutekeleza majukumu yao ya kazi na kuleta ufanisi na tija kwa Taifa letu.

10.         Mheshimiwa Spika, katika mvua zinazoendelea za masika za mwaka huu ndani ya nchi yetu, mwanzoni mwa mwezi wa Mei tumeshuhudia mvua katika kiwango kikubwa ambacho hakijawahi kutokea kwa miongo ya hivi karibuni.

11.         Mheshimiwa Spika, mvua hizo zimesababisha maafa mbalimbali yakiwemo kupoteza maisha kwa wananchi wetu na uharibifu wa makaazi na miundo mbinu uliotokana na mafuriko katika maeneo mbalimbali.
12.         Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuwashukuru viongozi na wananchi wote kwa jumla kwa mashirikiano waliyoonesha katika kukabiliana na maafa hayo. Aidha, naomba nitoe mkono wa pole kwa wafiwa na waathirika, nawaomba wawe na moyo wa subira kwa mtihani huo nakufahamu kuwa hiyo ni kadari ya Alla. Serikali itaendelea kuwa pamoja na wananchi katika kukabiliana na changamoto hizo.

13.          Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais napenda kutoa mkono wa pole kwako Mheshimiwa Spika na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, familia pamoja na wananchi wa Jimbo la Magomeni kwa kuondokewa na Mwakilishi wao mpendwa marehemu Salmin Awadh Salmin.  Tunamuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala pema peponi Amin.

MALENGO MAKUU YA OFISI YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS

14.         Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ina jukumu la kusimamia na kuratibu Ofisi ya Faragha ya Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais, mipango, sera na utafiti, uendeshaji na utumishi, masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi, watu wenye ulemavu, udhibiti wa dawa za kulevya na muitiko wa Taifa wa kupambana na UKIMWI. Katika kutimiza jukumu hili, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imekuwa na malengo makuu yafuatayo:-

1.      Kuratibu na kusimamia shughuli za Makamu wa Kwanza wa Rais.
2.      Kuratibu mipango, sera na utafiti unaohusiana na maeneo ya majukumu ya OMKR.
3.      Kuimarisha usimamizi endelevu wa mazingira na kuratibu masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
4.      Kuimarisha na kutetea uzingatiaji wa haki na fursa sawa kwa watu wenye Ulemavu ndani ya jamii.
5.      Kuratibu na kudhibiti usafirishaji, uingizwaji, matumizi na biashara haramu ya dawa za Kulevya.
6.      Kuratibu Mwitiko wa Taifa juu ya kinga dhidi ya UKIMWI na kupunguza athari kwa jamii.

15.         Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inatekeleza majukumu yake kupitia Taasisi zifuatazo:-
1.      Ofisi ya Faragha
2.      Idara ya Mipango, Sera na Utafiti
3.      Idara ya Uendeshaji na Utumishi
4.      Idara ya Mazingira
5.      Idara ya Watu wenye Ulemavu
6.      Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Pemba
7.      Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya
8.      Tume ya UKIMWI

16.         Mheshimiwa Spika, kufuatia kupitishwa na kusainiwa kwa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2015, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mwaka 2015/2016 inategemea kuwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (Zanzibar Environmental Management Authority – ZEMA) ili kuongeza nguvu katika utekelezaji wa majukumu ya usimamizi wa mazingira, Zanzibar.

MUHTASARI WA MAFANIKO NA CHANGAMOTO ZA OMKR KWA MIAKA MITANO (5)

17.         Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imeanzishwa mwaka 2010 mara baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba, 2010.  Tokea kuanzishwa kwake, pamoja na kuendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya msingi, pia ilijikita katika kutayarisha nyenzo ambazo zitasaidia kufanyakazi kitaalamu na kwa ufanisi zaidi kwa miaka kadhaa ijayo.

18.         Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kipindi cha miaka mitano kimepita tokea kuanzishwa kwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, na hasa kwa vile tunamaliza bajeti ya awamu hii, naomba nieleze kwa muhtasari baadhi ya mafanikio ya msingi yaliyopatikana na OMKR.

19.         Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imeweza kuratibu kwa ufanisi mkubwa shughuli za Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais zikiwemo safari za ndani na nje ya nchi ambapo miongozo kwa taasisi mbali mbali imetolewa ikiwa ni sehemu ya kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya kijamii pamoja na kufanikisha usimamizi wa masuala yanayosimamiwa na OMKR.  Aidha, uratibu wa mikutano kati ya Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Mabalozi waliopo nchini, viongozi wa nchi na mashirika mbali mbali ya kimataifa ulifanyika kwa ufanisi mkubwa ambapo pamoja na mambo mengine mikutano hiyo imekuza mahusiano kati ya Zanzibar na nchi au mashirika hayo.

20.         Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, Ofisi ya Faragha imekuwa na changamoto ya msingi iliyodumu ndani ya kipindi cha miaka mitano ambayo ni kukosekana kwa makaazi rasmi ya Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais huko Dar-es-Salaam.  Hali hiyo imemlazimisha kufikia hotelini, jambo ambalo limepelekea kuwa na gharama zaidi.

21.         Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imeandaa Mpango Mkakati kwa kipindi cha 2014 – 2020 na Mpango Mkuu wa Utafiti kwa kipindi kama hicho kwa masuala yanayoratibiwa na OMKR.  OMKR pia imeandaa muongozo wa uzingatiaji pamoja na mfumo wa ufuatiliaji na tathmini kwa mambo mtambuka yanayosimamiwa na OMKR.

22.         Mheshimiwa Spika, ni jukumu la taasisi na wadau wengine kuutumia muongozo huo na mingine ya kisekta iliyoandaliwa katika kuhakikisha mambo mtambuka yakiwemo ya mazingira, masuala ya Watu wenye Ulemavu na UKIMWI yanazingatiwa katika mipango yao mbalimbali.

23.         Mheshimiwa Spika, katika sekta ya mazingira, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imeandaa sera ya mazingira ya mwaka 2013, Mkakati wa Zanzibar wa Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2014, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2015, Mkakati wa Mawasiliano ya Mazingira, Mkakati wa Mawasiliano wa Mabadiliko ya Tabianchi, Muongozo wa Uzingatiaji wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa sekta mbalimbali pamoja na kanuni za mifuko ya plastiki na maliasili zisizorejesheka.  Jumla ya Tathmini 71 za Athari za Kimazingira zimefanyika na kutolewa vyeti vya mazingira kwa miradi hiyo. Aidha, wananchi 8,000 wa kijiji cha Nungwi wamepatiwa maji safi na salama ambao kwa muda mrefu maji yao yalikuwa na chumvi-chumvi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

24.         Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine katika sekta ya mazingira ni kukua kwa uelewa wa masuala ya mazingira katika jamii ambapo kamati, vikundi na asasi zisizokuwa za Kiserikali (NGOs) mbalimbali zimeundwa ndani ya jamii kwa lengo la kusaidia usimamizi wa mazingira nchini.  Aidha, kupungua kwa matumizi ya mifuko ya plastiki ndani ya Zanzibar ni mafanikio ya kupigiwa mfano yaliyofikiwa na OMKR.

25.         Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, bado sekta ya mazingira inakabiliwa na changamoto za kuwepo kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu na uchafuzi wa mazingira kwa baadhi ya maeneo.

26.         Mheshimiwa Spika, katika masuala ya Watu wenye Ulemavu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imeweza kufanya usajili wa Watu wenye Ulemavu katika Mikoa yote mitano ambao utaiwezesha Serikali kuwatambua walipo pamoja na kuzingatia mahitaji yao katika mipango ya maendeleo.  Aidha, OMKR imeanzisha Mfuko wa Watu wenye Ulemavu kwa lengo la kudumisha utoaji wa huduma kwa watu hao, kuandaa rasimu ya sera ya Watu wenye Ulemavu ambayo inatarajiwa kuwasilishwa Serikalini hivi karibuni. Aidha, watu 281 wenye ulemavu (Unguja 150 na Pemba 131) wamepatiwa visaidizi na dawa ili pamoja na mambo mengine kurahisisha shughuli zao za maisha.

27.         Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi hizo, Serikali inakabiliwa na changamoto za kuwepo kwa udhalilishaji kwa Watu wenye Ulemavu hasa wenye ulemavu wa akili pamoja na baadhi ya wadau na jamii kutozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu katika mipango yao.

28.         Mheshimiwa Spika, katika sekta ya UKIMWI, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imetayarisha Mkakati wa Pili wa Taifa wa UKIMWI Zanzibar kwa kipindi cha 2011 – 2016 na Sheria ya Kukinga na Kusimamia Masuala ya UKIMWI ya mwaka 2013.  Sheria hii itaondoa unyanyapaa pamoja na kuimarisha haki za binadamu kwa kuwalinda walioambukizwa na wasioambukizwa na VVU.  Aidha, Tume imeandaa Mkakati wa Utafutaji wa Rasilimali kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa shughuli za UKIMWI.

29.         Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi hizo ambapo pia kumekuwa na kupungua kwa unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU, sekta hii ya UKIMWI inakabiliwa na changamoto ya kupungua kwa upatikanaji wa fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo hali inayokwaza juhudi za mapambano dhidi ya UKIMWI.

30.         Mheshimiwa Spika, katika kushughulikia tatizo la dawa za kulevya, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imefanya mapitio ya Sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya ya mwaka 2009 ambayo yamepelekea kuundwa kwa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya.  Aidha, OMKR imeandaa muongozo kwa ajili ya uanzishwaji wa nyumba za makaazi ya vijana walioacha matumizi ya dawa za kulevya.  Hivi sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa Kituo cha Tiba na Marekebisho ya Tabia kwa wanaotumia dawa za kulevya ambacho kinahitajika sana katika kukabiliana na tatizo la dawa hizo hapa nchini. 

31.         Mheshimiwa Spika, pamoja na kuimarika kwa mashirikiano miongoni mwa taasisi wadau katika suala la udhibiti wa dawa za kulevya, bado Serikali inakabiliwa na changamoto za kuwepo kwa uingizwaji na usambazwaji wa dawa hizo unaopelekea kuendelea kwa matumizi yake hapa Zanzibar.



UTEKELEZAJI WA MALENGO YA OMKR KWA MWAKA 2014/2015

OFISI YA FARAGHA

32.          Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Faragha ina jukumu la kuratibu shughuli za Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

 Kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Ofisi ya Faragha ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-

1.      Kusimamia na kuratibu shughuli zote za Makamu wa Kwanza wa Rais.
2.      Kuimarisha mazingira ya kazi katika kuleta ufanisi.

33.          Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi 2015, Ofisi ya Faragha imeweza kutekeleza yafuatayo katika malengo iliyopanga:-

34.          Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mashirikiano ya kijamii na kiuchumi, Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais amefanya ziara 4 za nje. Aidha, ziara mbali mbali za ndani ya nchi zilifanyika na ripoti za ziara hizo kuwasilishwa sehemu husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Kwa upande wa ziara za ndani miongozo mbali mbali imetolewa kwa taasisi na jamii zilizo tembelewa. 


35.         Mheshimiwa Spika, wageni 25 kutoka nje ya nchi walipata kuonana na Mheshimiwa Makamu wa Kwanza na kubadilishana mawazo juu ya mambo mbali mbali yanayohusu uchumi, kijamii na mazingira.  Vile vile, Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais ameonana na wageni wa ndani na kubadilishana mawazo juu ya mambo mbali mbali ya kijamii na ushauri wa mambo hayo umetolewa.  Sambamba na hayo, katika kusaidia shughuli za kiuchumi na kimaendeleo Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais amesaidia jumuiya na vikundi vya jamii.

36.          Mheshimiwa Spika, katika kukuza mawasiliano na upatikanaji wa taarifa kuhusiana na utekelezaji wa shughuli za Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais, jumla ya kalenda 2,000 za mwaka 2015 zenye ujumbe mbali mbali zimechapishwa na kusambazwa kwa wadau mbalimbali.  Ununuzi wa vifaa mbalimbali vya habari umefanyika na kuongeza utoaji wa habari za Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais. 

37.             Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mazingira ya kazi na ya wafanyakazi wa Ofisi ya Faragha, matengenezo madogo ya ofisi ya faragha na nyumbani kwa Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais yamefanyika. Vifaa mbali mbali kwa ajili ya matumizi ya ofisini na nyumbani vimenunuliwa.

38.          Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Faragha kwa mwaka wa fedha 2014/15 ilikadiria kutumia TZS 411,150,000/- kwa kuendeshea kazi. Hadi kufikia Machi, 2015 ilikwisha kuingiziwa TZS 143,902,500/- sawa na asilimia 35.

IDARA YA MIPANGO, SERA NA UTAFITI

39.          Mheshimiwa Spika, Idara hii ina jukumu la kuandaa na kusimamia utekelezaji wa sera na mipango  ya maendeleo; kuratibu shughuli za utafiti pamoja na kufuatilia  na kutathmini utekelezaji kwa taasisi zote zilizo chini ya Ofisi ya  Makamu wa Kwanza wa Rais.

Kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Idara ya Mipango, Sera na Utafiti ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-

1.      Kujenga uwezo wa utafiti kwa watendaji 20 na kufanya tafiti tatu katika maeneo ya OMKR (Mazingira, Watu wenye Ulemavu na Dawa za Kulevya).
2.      Kuratibu utekelezaji wa masuala mtambuka ya OMKR.
3.      Kuratibu shughuli za sera, mipango na miradi ya maendeleo.

40.         Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi 2015 Idara ya Mipango, Sera na Utafiti  imeweza kutekeleza yafuatayo katika malengo iliyopanga:-

41.         Mheshimiwa Spika, mafunzo ya utafiti ya siku tano kwa wafanyakazi wa OMKR yametolewa. Mafunzo hayo yaliwashirikisha watendaji 30 kutoka OMKR na yalilenga kuwawezesha watendaji kutumia matokeo ya utafiti katika kupanga na kufuatilia mipango ya kila siku.

42.          Mheshimiwa Spika, utafiti wa kimazingira unaohusu masuala ya athari na kiwango cha uingizaji wa vifaa chakavu vya umeme na elektroniki (e-waste) umefanyika na ripoti yake itawasilishwa kwa wadau hivi karibuni.

43.         Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha sekta zinazingatia masuala mtambuka yanayosimamiwa na OMKR ndani ya mipango yao ya kimaendeleo, mafunzo ya siku tatu ya wakufunzi (Unguja na Pemba) yalitolewa. Mafunzo hayo yalihusu utekelezaji wa muongozo wa mambo mtambuka ulioandaliwa na OMKR na kuwashirikisha watendaji 25 kutoka katika sekta mbali mbali za serikali.

44.         Mheshimiwa Spika, taarifa mbali mbali za utekelezaji za robo mwaka na za mwaka zimeandaliwa na kuwasilishwa sehemu husika ikiwemo Tume ya Mipango, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Wizara ya Fedha na taasisi nyengine kila ilipohitajika. 

45.         Mheshimiwa Spika, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti kwa mwaka wa fedha 2014/15 iliidhinishiwa kutumia TZS 146,065,000/- kwa kuendeshea kazi. Hadi kufikia Machi, 2015 ilikwisha kuingiziwa TZS 51,819,000/- sawa na asilimia 35.

UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

46.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Idara ya Mipango, Sera na Utafiti iliratibu utekelezaji wa miradi (2) ya maendeleo ifuatayo:- 

a)      Mradi wa kujenga Kituo cha Tiba na Marekebisho ya Tabia kwa watumiaji wa dawa za kulevya (Construction of Treatment and Rehabilitation center).

47.             Mheshimiwa Spika, mradi huu unatekelezwa kwa fedha za SMZ, kwa mwaka wa fedha 2014/15 ulilenga kukamilisha ujenzi wa sehemu ya chini, hadi kufikia Machi 2015 ujenzi wa msingi pamoja na uwekaji wa jamvi umekamilika.

48.            Mheshimiwa Spika, mradi huu kwa mwaka wa fedha 2014/15 uliidhinishiwa kutumia TZS 1,400,000,000/-. Hadi kufikia Machi, 2015 ilikwisha kuingiziwa TZS 250,000,000/- sawa na asilimia 18.

b)       Mradi wa kujenga uwezo wa utekelezaji wa masuala ya mazingira na                          mabadiliko ya tabianchi.

49.             Mheshimiwa Spika, mradi huu unatekelezwa kwa fedha za Washirika wa Maendeleo (UNDP) kupitia programu ya UNDAP. Mradi huu unatekelezwa kupitia malengo saba ambapo malengo manne kati ya hayo yanatekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais. Malengo hayo ni:-

i.        Kuhakikisha masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi yanaingizwa katika mipango ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa MKUZA II.
ii.      Kutayarisha Mkakati wa Zanzibar wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na kusaidia utekelezaji wake.
iii.    Kuimarisha muundo wa kitaasisi kwa ajili ya kusimamia masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
iv.    Kukuza kiwango cha upatikanaji wa taarifa na uelewa juu ya athari za mabadiliko na mikakati ya kukabiliana nayo miongoni mwa jamii na taasisi za Serikali.

50.            Mheshimiwa Spika, malengo mengine matatu ya mradi huu yanatekelezwa kupitia Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo na Maliasili na Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati.  Aidha, jumuiya ya Maendeleo ya Jamii na Uhifadhi wa Mazingira Zanzibar (COmmunity Deverlopment and Environmental COnservation in Zanzibar CODECOZ) nayo inashiriki katika utekelezaji wa mradi huu kwenye lengo moja la kukuza kiwango cha upatikanaji wa taarifa na uelewa juu ya athari za mabadiliko na mikakati ya kukabiliana nayo miongoni mwa jamii na taasisi za Serikali.

51.            Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi 2015 OMKR kupitia mradi huu imeweza kutekeleza yafuatayo:-

52.            Mheshimiwa Spika, rasimu za mipango kazi ya kisekta ya kuzingatia mabadiliko ya tabianchi zimetayarishwa.  Sekta zilizohusika na utayarishaji huo ni Uvuvi, Miundombinu, Utalii na Kilimo.

53.            Mheshimiwa Spika, hekta 30 za mikandaa/mikoko zimepandwa katika maeneo sita ya Unguja na Pemba. Maeneo hayo ni Kiongwe, Mafufuni na Kisakasaka kwa Unguja na Ndagoni, Wambaa na Pujini kwa Pemba.

54.            Mheshimiwa Spika, ripoti ya ukusanyaji  wa taarifa za msingi za kutayarisha  mpango wa jamii wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi  imetayarishwa  na inategemewa  kuwasilishwa kwenye vikao vya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mapitio na kuridhiwa.

55.            Mheshimiwa Spika, hatua za utayarishaji wa Mpango kazi wa Utekelezaji Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi zimeshaaza na utayarishaji wa mpango huo unategemewa kumalizika mwezi Januari, 2016 kwa hatua za uhamasishaji wa nyenzo za utekelezaji.

56.            Mheshimiwa Spika, watendaji wawili kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais waliwezeshwa kuhudhuria mkutano wa 20 wa Dunia wa mabadiliko ya tabianchi uliofanyika Lima, Peru na mashirikiano ya wadau mbalimbali wa mabadiliko ya tabianchi wa nje ya nchi yameongezeka.

57.            Mheshimiwa Spika, vipindi 6 vya elimu ya athari mabadiliko ya tabianchi vilitayarishwa na kurushwa kupitia redio jamii za Micheweni, Makunduchi na Tumbatu. Uelewa wa jamii juu ya masuala ya mabadiliko ya tabianchi umeongezeka.

58.            Mheshimiwa Spika, Wajumbe 5 kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Idara ya Ushirika na Asasi ya kiraia ya Community Forest Pemba (CFP) wamepatiwa safari ya kimasomo huko Arusha Tanzania bara kujifunza utayarishaji na utekelezaji wa mipango ya jamii ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi (Local Adaptation Plans of Action – LAPA).

59.            Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 mradi huu uliidhinishiwa kutumia TZS 577,500,000/-.  Hadi kufikia Machi, 2015 mradi ulikwisha kuingiziwa TZS 245,620,000/- sawa na asilimia 43.





IDARA YA UENDESHAJI NA UTUMISHI

60.             Mheshimiwa Spika, Idara hii ina jukumu la kusimamia shughuli za kila siku za uendeshaji na utumishi zikiwemo sheria na kanuni za utumishi, mafunzo, maslahi na maendeleo ya wafanyakazi.

Kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Idara ya Uendeshaji na Utumishi ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-

  1. Kusimamia, kukuza na kuimarisha mazingira ya utendaji kazi wa OMKR na kuleta ufanisi.
  2. Kuwajengea uwezo wafanyakazi na kuwapatia maslahi.

61.             Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi 2015,  Idara imeweza   kutekeleza yafuatayo katika malengo iliyopanga:-

62.             Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mazingira ya utendaji kazi vifaa mbali mbali vimenunuliwa pamoja na huduma mbali mbali za ofisi zimetolewa.

63.            Mheshimiwa Spika, katika kushiriki mikutano ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa, wafanyakazi 23 wamewezeshwa kushiriki katika mikutano ya ndani kwa ajili ya kufuatilia wa shughuli za Ofisi (Pemba, Dar-es-Salaam na Dodoma) na 9 wamewezeshwa kushiriki katika mikutano ya kikanda na kimataifa nje ya nchi (Kenya, Malaysia, Qatar, Lima na Singapore). Safari hizi zimeongeza mahusiano na washirika wa maendeleo.

64.             Mheshimiwa Spika, taarifa mbali mbali zinazohusiana na majukumu ya OMKR zimetolewa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, makala 2 zenye maudhui yanayohusu mabadiliko ya tabianchi na sheria ya mazingira zimetolewa katika gazeti la Zanzibar Leo. Aidha, filamu fundishi 2 kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi moja ikiwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiengereza zinazohusu mabadilko ya tabianchi zimetayarishwa.

65.            Mheshimiwa Spika, wafanyakazi 33 wamesaidiwa gharama za ada na vifaa na kupatiwa fursa za mafunzo katika ngazi za Cheti, Stashahada, Shahada ya kwanza na ya pili, pamoja na shahada ya uzamili katika fani tofauti (Angalia Kiambatanisho Nam. 1). 

66.            Mheshimiwa Spika, katika kusimamia ufanisi wa utendaji wa OMKR, vikao viwili vya kamati ya uongozi vimekaa na kujadili rasimu ya sera ya watu wenye ulemavu, mkakati wa mawasiliano ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji wa kazi za maabara ya utalii zinazotekelezwa na OMKR.  Aidha, kikao kimoja cha zabuni kilichojadili kumpata mkandarasi wa ujenzi wa kituo cha marekebisho ya tabia (Construction of treatment and rehabilitation center) kimefanyika. Vilevile, ripoti ya fedha ya mwaka 2013/2014 imetayarishwa na kuwasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Wizara ya Fedha.

67.            Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Idara ya Uendeshaji na Utumishi iliidhinishiwa kutumia TZS 1,610,084,000/-.  Kati ya fedha hizo, TZS 320,084,000/- kwa ajili ya matumizi mengineyo, na TZS 1,290,100,000/- kwa ajili ya mishahara.  Hadi kufikia Machi, 2015 Idara ya Uendeshaji na Utumishi ilikwisha kuingiziwa TZS 1,110,748,833/- zikiwemo TZS 173,444,933/- kwa matumizi mengineyo ambazo ni sawa na asilimia 54, na TZS 937,303,900/- kwa mishahara ambazo ni sawa na asilimia 73.

68.            Mheshimiwa Spika, Idara ya Uendeshaji na Utumishi ndio Idara pekee iliyoingiziwa fedha zaidi ya asilimia 50 kwa vile kazi zake nyingi zinajumuisha kuzihudumia Idara zote ikiwemo mafunzo kwa wafanyakazi wote, huduma za jingo na utekelezaji na usimamizi wa vikao vyote kwa misingi ya utawala bora.


IDARA YA MAZINGIRA

69.             Mheshimiwa Spika, Idara hii  ina jukumu la kukusanya na kuhifadhi taarifa za kimazingira, kutoa taarifa za kimazingira ili ziweze kusaidia katika kutayarisha na kutekeleza mipango na miradi ya kimaendeleo, kufuatilia mwenendo wa hali ya kimazingira, kukabiliana na matatizo ya kimazingira, kuhamasisha wadau kuchukua hatua za kuhifadhi mazingira pamoja na kutoa elimu ya mazingira kwa jamii.  Aidha, Idara hii pia inajukumu la kuratibu masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Idara ya Mazingira ilipanga kutekeleza   malengo yafuatayo:-

1.      Kuimarisha na kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria na Kanuni za Mazingira.
2.      Kusimamia uingizwaji wa masuala ya mazingira  katika miradi ya maendeleo.
3.      Kukuza uelewa wa elimu ya mazingira kwa jamii na wadau wengine.

70.             Mheshimiwa Spika, hadi kufikia  Machi 2015, Idara ya Mazingira imeweza   kutekeleza yafuatayo katika malengo iliyopanga:-

71.             Mheshimiwa Spika, jumla ya operesheni 33 za uzuiaji matumizi ya mifuko ya plastiki zimefanyika (Angalia Kiambatanisho Nam. 2).  Katika operesheni hizo, watu 23 wamekamatwa na kupelekwa mahakamani na kutozwa faini ya jumla ya TZS 3,170,000/-.  Aidha, wastani wa kilo 759 za mifuko ya plastiki zimekamatwa na kuangamizwa.  Vile vile, jumla ya operesheni 27 zimefanyika Unguja na Pemba za kuwakamata wanaovuna na kusafirisha maliasili kinyume na utaratibu.

72.             Mheshimiwa Spika, sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2015 imepitishwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika kipindi hiki cha 2014/2015.  Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa dhati kabisa Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza lako kwa kuipitisha Sheria hiyo. Ni imani ya OMKR kuwa sheria hiyo itasaidia sana kupunguza uharibifu na uchafuzi wa mazingira uliopo hivi sasa na kuongeza ufanisi wa kusimamia masuala ya mabadiliko ya tabianchi.  Aidha, naomba pia nichukue nafasi hii kuliarifu Baraza lako kuwa Mheshimiwa Rais ameshatia saini Sheria hiyo.

73.             Mheshimiwa Spika, jumla ya miradi kumi na tatu (13) imefanyiwa tathmini ya athari za mazingira na kijamii na tayari ripoti za tathmini hizo zimeshafanyiwa mapitio na wadau kwa uratibu wa Idara ya Mazingira.  Kufuatia mapitio hayo, miradi yote imepatiwa vyeti vya kimazingira na imetakiwa kuendelea na utekelezaji kwa kufuata masharti yaliyotolewa (Angalia Kiambatanisho Nam. 3).

74.             Mheshimiwa Spika, mafunzo ya aina mbili ya tathmini ya athari za kimazingira yamefanyika. Mafunzo hayo yaliwashirikisha watu 40 kutoka taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali ambayo yameongeza ujuzi na ufahamu wa Tathmini za Athari za Kimazingira na usimamizi na ufuatiliaji wa Tathmini hizo.

75.             Mheshimiwa Spika, jumla ya vipindi 13 (11 vya redio na 2 vya TV) vimetayarishwa na kurushwa kupitia ZBC Redio na TV (Angalia Kiambatanisho Nam. 4).  Vipindi 10 vya radio vilihusu matumizi ya majiko sanifu (2), umuhimu wa umeme wa jua (2),  marufuku ya mifuko ya plastiki (2), mmong’onyoko wa fukwe (2), kanuni ya maliasili zisizorejesheka (2) na matumizi endelevu ya maliasili zisizorejesheka (1).  Aidha, vipindi viwili vya TV vinavyohusu matumizi ya majiko sanifu na umeme wa jua vimerushwa hewani

76.            Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Idara ya Mazingira iliidhinishiwa kutumia TZS 113,284,000/- kwa ajili ya kuendeshea kazi.  Hadi kufikia Machi, 2015 Idara ya Mazingira ilikwisha ingiziwa TZS 44,2745,000/- sawa na asilimia 39.

77.             Mheshimiwa spika,  kwa kipindi cha mwaka 2014/2015 OMKR iliidhinishiwa kukusanya TZS 10, 500,000 kupitia Idara ya Mazingira. Fedha hizi zinatokana na ada ya hifadhi ya mazingira ikiwa ni pamoja na vyeti vya Mazingira. Kazi ambayo inategemea idadi ya miradi inayowasilishwa kutoka Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar au miradi ya maendeleo ambayo inastahili kufanyiwa tathmini. Hadi kufikia Machi 2015,  jumla ya TZS 8,700,000/- zimekusanywa ambazo ni sawa na asilimia  83.

IDARA YA WATU WENYE ULEMAVU

78.             Mheshimiwa Spika, Idara ya Watu Wenye Ulemavu ina jukumu la kuratibu,        kusimamia na kufuatilia masuala mbali mbali yanayohusu Watu wenye Ulemavu ili kuhakikisha ujumuishwaji katika shughuli zote za kimaendeleo zikiwemo za kiuchumi na kijamii.

Kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Idara ya Watu wenye Ulemavu ilipanga kutekeleza malengo yafuatayo:-

  1. Kuimarisha na kusimamia utekelezaji wa Sheria, kanuni Miongozo kwa Watu wenye Ulemavu.
  2. Kusimamia haki, fursa sawa na ujumuishwaji wa Watu wenye Ulemavu.
  3. Kuanzisha programu ya Makuzi ya Awali Maendeleo ya Mtoto (Early Childhood Development).

79.             Mheshimiwa Spika, hadi kufikia  Machi 2015, Idara ya Watu wenye Ulemavu imeweza kutekeleza yafuatayo katika malengo iliyopanga:-

80.             Mheshimiwa Spika, rasimu ya Sera ya Watu wenye Ulemavu imeandaliwa na taratibu za kukamilisha rasimu ya mpango kazi kwa ajili ya utekelezaji wa sera ya Watu wenye Ulemavu zinaendelea ili kwa pamoja ziweze kuwasilishwa Serikalini.

81.            Mheshimiwa Spika, kikao kimoja cha Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu kimefanyika kujadili taarifa mbali mbali zinazohusiana na maendeleo na changamoto zinazowakabili Watu wenye Ulemavu.

82.             Mheshimiwa Spika, kikao kimoja cha maafisa waratibu wa masuala ya Watu wenye Ulemavu kimefanyika.  Kupitia kikao hiki utekelezaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu katika sekta mbalimbali ulijadiliwa. Vilevile mafunzo juu ya uwezeshaji wa Watu wenye Ulemavu na Mkataba wa Kimataifa wa Haki na fursa za Watu wenye Ulemavu yametolewa kwa maafisa waratibu 14 wa wizara na waratibu 10 wa jumuiya zinazoshughulika na masuala ya watu wenye ulemavu.

83.            Mheshimiwa Spika, ziara kumi (10) zimefanywa katika taasisi za Serikali na binafsi kwa lengo la kuhamasisha masuala ya Watu wenye Ulemavu na Kuzungumzia Ujumuishwaji wa Watu wenye Ulemavu katika sekta hizo.  Vile vile safari moja imefanywa nchini Kenya na nne (4) za ndani ya nchi kwa lengo la kukuza mashirikino juu ya utekelezaji wa programu zinazohusu masuala ya Watu wenye Ulemavu.

84.             Mheshimiwa Spika, waandishi wa habari 20 wamepatiwa elimu na kujengewa uelewa juu ya masuala ya makuzi ya awali ya maendeleo ya mtoto mwenye ulemavu.

85.            Mheshimiwa Spika, mafunzo ya usimamizi wa fedha na uongozi kwa viongozi 35 (23 Unguja na 12 Pemba)  wa Jumuiya za Watu wenye Ulemavu yametolewa kwa lengo  la kuzijengea uwezo na kuleta ufanisi katika kazi.

86.              Mheshimiwa Spika, Watu wenye Ulemavu 225 (Pemba 131 na Unguja 94) wamepatiwa visaidizi vya aina mbali mbali ili pamoja na mambo mengine kurahisisha shughuli zao za maisha (Angalia Kiambatanisho Nam. 5).

87.              Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo, siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu imeadhimishwa ambapo maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika kisiwani Pemba kwa kufanyika shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuielimisha jamii juu ya haja ya kuzingatia haki za Watu wenye Ulemavu.

88.            Mheshimiwa Spika, Idara ya Watu wenye Ulemavu kwa mwaka wa fedha 2014/15 iliidhinishiwa kutumia TZS 278,442,000/- kwa kuendeshea kazi.  Hadi kufikia Machi, 2015 ilikwisha ingiziwa TZS 100,724,500/- sawa na asilimia 36.






OFISI KUU PEMBA

89.             Mheshimiwa Spika, Ofisi Kuu Pemba ina jukumu la kuratibu, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa shughuli zote za Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa upande wa Pemba.

Kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Ofisi kuu Pemba ilipanga kutekeleza   malengo yafuatayo:-

  1. Kuwajengea uwezo wafanyakazi na kuwapatia maslahi.
  2. Kuimarisha mazingira ya utendaji kazi.
  3. Kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za OMKR Pemba.
  4. Kukuza na kuimarisha mawasiliano ya habari.

90.            Mheshimiwa Spika, hadi kufikia  Machi 2015, Ofisi kuu Pemba imeweza   kutekeleza yafuatayo katika malengo iliyopanga:-

91.            Mheshimiwa Spika, ziara zote za Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais huko Pemba na ziara mbili za Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa zimeratibiwa.  Ziara hizo zimeweza kuishauri Ofisi juu ya utekelezaji wa majukumu yake pamoja na kukagua shughuli mbalimba zinazofanywa na jamii.

92.            Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kupunguza athari za uharibifu wa mazingira, ziara nane za ukaguzi zimefanywa kwenye maeneo yanayotumika kwa uchukuaji wa maliasili zisizorejesheka kama vile mchanga, mawe na kifusi. Maeneo yaliyokaguliwa ni Ging’ingi, Mwambe, Mkanyageni, Kiungoni, Ole, Pujini, Uwandani na Mvumoni Tundauwa.

93.            Mheshimiwa Spika, katika kuwajengea uwezo wafanyakazi gharama za mafunzo ya usimamizi wa mazingira zimelipiwa kwa mfanyakazi mmoja anayesoma katika chuo kikuu cha Dodoma ngazi ya shahada ya pili (Angalia Kiambatanisho Nam. 1).  Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kukuza na kuimarisha ufanisi wa kiutendaji.

94.            Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mazingira ya utendaji kazi, jengo la Idara ya Mazingira Pemba limeezekwa.  Ofisi Kuu Pemba pia imeweza kununua gari na vifaa mbali mbali kwa ajili ya matumizi ya Ofisi.

95.             Mheshimiwa Spika, Ofisi Kuu Pemba kwa mwaka wa fedha 2014/15 iliidhinishiwa kutumia TZS 369,575,000/-.  Kati ya fedha hizo, TZS 159,575,000/- kwa ajili ya matumizi mengineyo, na TZS 210,000,000/- kwa ajili ya mishahara.  Hadi kufikia Machi, 2015 Ofisi Kuu Pemba ilikwisha kuingiziwa TZS 251,169,450/- zikiwemo TZS 77,100,000/- sawa na asilimia 48 kwa matumizi mengineyo, na TZS 174,069,450/- kwa mishahara ambazo ni sawa na asilimia 83.


 
TUME YA KITAIFA YA KURATIBU NA UDHIBITI WA DAWA ZA KULEVYA

96.            Mheshimiwa Spika, Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya  ina jukumu la kuratibu mapambano dhidi ya matumizi, biashara na usafirishaji wa  dawa za kulevya kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, kutoa taaluma kwa jamii juu ya athari ya dawa za kulevya na kutoa huduma za tiba na  ushauri nasaha kwa watumiaji wa dawa za kulevya.

Kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za kulevya ilipanga kutekeleza   malengo yafuatayo:-

  1. Kupunguza matumizi ya dawa za kulevya.
  2. Kupunguza usafirishaji na usambazaji wa Dawa za Kulevya.
  3. Kuweka mazingira bora ya kazi na kuleta ufanisi katika mapambano dhidi 
           ya dawa za kulevya.

97.             Mheshimiwa Spika, hadi kufikia  Machi 2015, Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za kulevya imeweza   kutekeleza yafuatayo katika malengo iliyopanga:-

98.            Mheshimiwa Spika, jumla ya vipindi viwili vya redio vimerushwa kupitia ZBC Redio kwa lengo la kuelimisha jamii juu ya athari ya Dawa za Kulevya.  Ziara za utoaji taaluma kuhusu athari ya Dawa za kulevya zimefanywa kwenye skuli 42 (Angalia Kiambatanisho Nam. 6) ambapo wanafunzi 2,806 (1,716 wanawake; 1,090 wanaume) walipatiwa taaluma hiyo. Vile vile, ziara kama hizo zimefanyika kwa Shehia 39 Unguja na Pemba.  Aidha, nyumba kumi (10) za makaazi ya vijana walioacha matumizi ya Dawa za Kulevya zimepatiwa ruzuku (Angalia Kiambatanisho Nam. 7) ambapo viongozi wa nyumba hizo  walifanyiwa mikutano ya kupewa taaluma juu ya ugawaji  wa vifaa vya kutendea kazi vilivyotoka Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (UNODC).

99.            Mheshimiwa Spika, katika kupunguza usafirishaji na usambazaji wa dawa za Kulevya, Tume imetoa mafunzo ya sheria ya dawa za Kulevya kwa taasisi za Serikali za Unguja na Pemba zikiwemo Polisi, waendesha mashtaka, Mahakimu, Watumishi wa Uwanja wa ndege, Bandari, TRA, Mkemia, ZRB na Taasisi ya Kupambana na Kuzuwia Rushwa. Mafunzo hayo yalikuwa na lengo la kujadili mwenendo na changamoto wa kesi za dawa za kulevya na kuimarisha mahusiano ya kisekta.

100.       Mheshimiwa Spika, mkakati wa pamoja kati ya viongozi wa Tume, Wilaya, Shehia na wadau wengine juu ya kudhibiti uingizaji, usambazaji na matumizi ya Dawa za Kulevya katika Shehia umeandaliwa na utekelezaji wake umepelekea kuvunjwa kwa vijiwe na kusambaratisha maeneo yanayofanyiwa biashara ya dawa za kulevya yaliyomo kwenye shehia husika na kuunda kamati za Udhibiti wa Dawa za Kulevya za  Shehia. Pia Kikao kimoja kimefanyika ili kutathmini na kujadili changamoto na mafanikio mbalimbali yaliyojitokeza katika kufanikisha kazi ya uratibu na udhibiti wa dawa za kulevya.

101.       Mheshimiwa Spika, wafanyakazi watano wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi ya utunzaji wa kumbukumbu na mfanyakazi mmoja amelipiwa sehemu ya gharama za mafunzo ya utawala shahada ya pili.

102.       Mheshimiwa Spika, Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya kwa mwaka wa fedha 2014/15 iliidhinishiwa kutumia jumla ya TZS 364,000,000/-.  Kati ya fedha hizo, TZS 220,000,000/- kwa ajili ya matumizi mengineyo, na TZS 144,000,000/- kwa ajili ya mishahara.  Hadi kufikia Machi, 2015 Tume ilikwisha kuingiziwa TZS 269,920,950/- zikiwemo TZS 162,138,000/- kwa matumizi mengineyo ambazo ni sawa na asilimia 74, na TZS 107,782,950/- kwa mishahara ambazo ni sawa na asilimia 75.

TUME YA UKIMWI

103.        Mheshimiwa Spika, majukumu makuu ya Tume ya UKIMWI ni kuhakikisha kwamba sera na mikakati ya taifa ya kupiga vita UKIMWI zinatayarishwa  na kutekelezwa, kutafuta rasilimali zitakazotumika katika utekelezaji wa Muitiko wa Kitaifa wa Kupambana na UKIMWI, kuimarisha uwezo wa wadau katika kufanyia kazi programu za UKIMWI na kuratibu shughuli zao, kushajihisha utoaji wa huduma za tiba na matunzo kwa watu walioathirika na kuathiriwa, kufuatilia na kutathmini umakini na ufanisi wa utekelezaji wa mikakati, sera na muitiko wa kitaifa na kutoa taarifa zote zinazohusiana na UKIMWI.

Kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Tume ya UKIMWI ilipanga kutekeleza   malengo yafuatayo:-

  1. Kuongoza, kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria na Mkakati wa pili wa Kitaifa  wa UKIMWI kwa wadau wote.
  2. Kuimarisha  ubora wa taarifa zinazokusanywa pamoja na kufuatilia matumizi ya taarifa zinazotokana na  ufuatiliaji, tathmini  na utafiti wa pgrogramu  za UKIMWI.
  3. Kutoa miongozo na kuratibu  masuala ya habari, utetezi na mawasiliano  kuhusu UKIMWI  ili kuchochea  mabadiliko ya tabia katika jamii na makundi maalumu.
  4. Kuongoza pamoja  kuimarisha mazingira mazuri  ya kazi na wafanyakazi wa Tume  kwa ajili ya kuleta ufanisi  katika shughuli za uratibu wa masuala ya UKIMWI.

104.        Mheshimiwa  Spika, hadi kufikia Machi 2015 Tume ya UKIMWI  imeweza kutekeleza yafuatayo katika malengo iliyopanga:-

105.       Mheshimiwa Spika, katika kukuza mawasiliano na habari, nakala 5,000 za Toleo la 18 na 5,000 toleo la 19 la Jarida la JIHADHARI lenye ujumbe tofauti wa mapambano dhidi ya UKIMWI zimechapishwa na kusambazwa kwa wadau mbalimbali.

106.        Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Mkakati wa Pili wa Taifa wa UKIMWI (Zanzibar National Strategic Plan – ZNSP II), Tume imeiwezesha kifedha Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na Watoto  kwa ajili ya kutayarisha mpango wa utekelezaji (operational plan) wa miaka miwili (2015 – 2016) ambao utawezesha  kutekeleza  programu ya kuzuia udhalilishaji  wa kijinsia (Gender Based Violence – GBV).

107.       Mheshimiwa Spika, jumla ya watu 756 walio katika makundi maalumu wameweza kufikiwa na kupatiwa ushauri nasaha (342 wanaotumia dawa za kulevya, watu 6 wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga, 389 dada-poa na 19 kaka-poa).  Miongoni mwao 138 waliweza kupima VVU ambapo watano (5) kati yao (3 w’me na 2 w’ke) waligundulika kuishi na VVU.  Aidha, watu 62 walipatiwa rufaa na kupelekwa katika vituo vya tiba kwa uchunguzi zaidi.

108.       Mheshimiwa Spika, jumla ya vipeperushi 4,200 vimechapishwa na kusambazwa kwa waliofikiwa kupitia mikutano 16 iliyofanyika (Unguja 8 na Pemba 8).

109.        Mheshimiwa Spika, Zanzibar tumeungana na nchi nyengine Duniani kuadhimisha  Siku ya UKIMWI ambayo ni tarehe 1 Disemba ya kila mwaka.  Maadhimisho hayo yalifanyika kijiji  cha Machomane,  Wilaya ya Chake-Chake Pemba ambapo shughuli mbalimbali za kilele zilifanyika ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha jamii juu ya mapambano ya UKIMWI.

110.       Mheshimiwa Spika, wafanyakazi  watano wamelipiwa gharama za masomo katika ngazi ya shahada ya  pili na stashahada katika fani tofauti. Wafanyakazi wawili wamepatiwa  mafunzo ya muda mfupi  juu ya ufuatiliaji na tathmini (Angalia Kiambatanisho Nam. 1). Aidha, safari 6 za ndani za ufuatiliaji zimefanyika ambazo zimeongeza uratibu na ufanisi wa kazi za Tume.

111.       Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Tume ya UKIMWI iliidhinishiwa kutumia jumla ya TZS 811,000,000/-. Kati ya fedha hizo, TZS 533,208,700/- kwa ajili ya matumizi mengineyo, na TZS 277,791,300/- kwa ajili ya mishahara.  Hadi kufikia Machi, 2015 Tume ya UKIMWI ilikwisha kuingiziwa TZS 503,194,400/-.  Kati ya hizo TZS 258,789,946/- sawa asilimia 49 kwa ajili ya matumizi mengineyo, na TZS 244,404,454/- sawa asilimia 88 kwa ajili ya mishahara.



UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

112.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015 Tume ya UKIMWI  ilitekeleza kazi mbalimbali zilizopatiwa fedha na Washirika wa Maendeleo. Fedha hizo ni kutoka  UNFPA, UNDP na UNICEF. Shughuli zilizotekelezwa  kupitia fedha  hizo ni kama zifuatazo:-

a)      Utekelezaji wa kazi zilizofadhiliwa na UNFPA

113.       Mheshimiwa Spika, mikutano miwili ya wadau wa sheria kutoka taasisi mbali mbali imefanyika kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutetea masuala ya mapambano juu ya udhalilishaji wa kijinsia na kukinga maambukizi mapya ya UKIMWI na kuangalia mapungufu yaliyopo kiutekelezaji, kutoa mapendekezo na kuwezesha matumizi mazuri ya sheria zilizopo.
                                                                                                                                                                                                                                                                                             
114.       Mheshimiwa Spika, katika kupunguza vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, Tume imefanya mikutano 4 kwa viongozi wa dini yenye jumla ya washiriki 80 (40 Unguja, 40 Pemba) ambao walihamasishwa juu ya mbinu bora za kukinga na kudhibiti maambukizi ya  UKIMWI kwa vijana pamoja na kupunguza vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia.

115.        Mheshimiwa Spika, katika kufanya uhamasishaji katika jamii juu ya kupinga vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto na kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI, maigizo19 yalifanyika katika shehia 19 Unguja na Pemba.  Kwa Unguja Shehia hizo ni 10 ambazo ni Bumbwini Kiongwe, Mafufuni, Nyamanzi, Pwani Mchangani, Unguja Ukuu Kaebona, Kiwengwa, Mpapa, Chukwani (buyu), Unguja Ukuu Tindini na Mbuzini.  Kwa Pemba Shehia hizo ni 9 ambazo ni Wambaa, Wesha, Chumbageni, Pujini Dodo, Chachani, Bopwe, Mchangamdogo, Mzambarauni, Pujini Kibaridi. Jumla ya wananchi 1,592 kutoka Shehia kumi za Unguja wamefikiwa, kati ya hao 650 ni wanaume na 942 ni wanawake. Aidha, jumla ya wananchi 2,250 kutoka Shehia tisa za Pemba wamefikiwa kati ya hao 900 ni wanaume na 1350 ni wanawake.

116.       Mheshimiwa Spika, katika kuwasaidia watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI, vikundi vitano (3 Unguja na 2 Pemba) vya ujasiriamali vya wanawake wanaoishi na virusi vya UKIMWI vimepatiwa fedha na missada mbalimbali kwa ajili ya kujiendeleza (Angalia Kiambatanisho Nam. 8).

117.       Mheshimiwa Spika, jumuiya ya ZAYEDESA imepatiwa msaada wa kuimarisha kituo cha huduma rafiki cha vijana kilichoko Mkoani Pemba. Baada ya kuimarishwa kituo hicho, jumuiya hiyo imeweza kuwatumia waelimishaji rika wake katika kuwafikia walio katika makundi maalum 17 (dada poa 11, kaka poa 3 na watumiaji wa dawa za kulevya 3).

118.       Mheshimiwa Spika, kupitia mikusanyiko ya kidini yenye lengo la kuimarisha maadili mema na kurekebisha tabia ili kuweza kujikinga na maambukizo mapya ya UKIMWI pamoja na kupunguza vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, Tume imeiwezesha Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) kufanya ziara 9 (5 Unguja na 4 Pemba) za uhamasishaji ambapo wanashehia 270 Unguja na 214 kwa Pemba waliweza kufikiwa. 

119.       Mheshimiwa Spika, Vilevile vipindi 5 vya redio (3 ZBC na 2 redio Adhana) vilitayarishwa na kurushwa hewani kwa ajili ya kutoa elimu ya mwitiko wa taifa wa mapambano dhidi ya UKIMWI.

120.       Mheshimiwa Spika, mikutano 2 ya uratibu (1 Unguja na 1 Pemba) iliyowashirikisha viongozi wa dini (kiislamu na kikiristo) iliyolenga kukemea vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji ilifanyika. Jumla ya viongozi wa kidini 50 (25 Unguja na 25 Pemba) walishiriki.

121.       Mheshimiwa Spika, shehia 20 (Unguja 9, Pemba 11) zinazotekeleza mpango shirikishi wa kuziwezesha jamii (community capacity enhancement) zimefanyiwa ufuatiliaji.  Shehia hizo kwa Pemba ni Kiwani, Makombeni, Michezani, Chonga, Vitongoji, Nawara, Kiuyu Kigongoni, Msuka, Tumbe Mashariki, Tumbe Magharibi na Kizimbani.  Kwa upande wa Unguja Shehia hizo ni Tumbatu Jongowe, Tumbatu Uvivini, Tumbatu Gomani, Kiboje, Mkwajuni, Koani, Malindi, Mlandege na Nungwi.

b)     Utekelezaji wa kazi zilizofadhiliwa na UNDP

122.       Mheshimiwa Spika, mkutano mmoja wenye washiriki 40 kutoka kamati za UKIMWI za shehia, sekta kuu za Serikali, taasisi za kisheria, taasisi za kiraia, makundi maalum na taasisi za watu wenye ulemavu ulifanyika Pemba kwa lengo la kuhakikisha ufanisi katika kuongeza uwezo wa programu za habari utetezi na mawasiliano kwa kuchochea mabadiliko ya tabia katika masuala ya UKIMWI.


123.        Mheshimiwa Spika, mikutano miwili ya uratibu imeandaliwa (1 Unguja na 1 Pemba). Jumla ya washiriki 40 (20 Unguja na 20 Pemba) walishiriki katika mikutano hiyo ambao ni waratibu wa shughuli za UKIMWI katika ngazi za wilaya, sekta kuu za Serikali, jumuiya na sekta binafsi katika mapambano dhidi ya UKIMWI (ABCZ), Jumuiya ya Watu wanaoishi na VVU, taasisi za kiraia, mtandao wa waelimishaji rika katika makundi maalum.

c)      Utekelezaji wa kazi zilizofadhiliwa na UNICEF

124.       Mheshimiwa Spika, Tume ya UKIMWI ilifanya ziara za kuwapitia wadau wanaofanyakazi na makundi maalum kwa lengo la kutambua shughuli wanazofanya na changamoto wanazokabiliana nazo na kusaidia kupata ufumbuzi.  Miongoni mwa taasisi zilizotembelewa ni pamoja na kanisa la Anglikana, nyumba ya wanawake ya makaazi ya vijana walioacha matumizi ya dawa za kulevya, watu waliokuwa wakitumia dawa za kulevya na wamepata nafuu (Zanzibar recovery community), mtandao wa watu walio katika makundi maalumu (Key Population Network), mkusanyiko wa vijana wa Zanzibar kwa ajili ya kupambana na UKIMWI (Zanzibar Youth Forum), na jumuiya ya kidini ya mapambano dhidi ya UKIMWI (ZEYADA). Aidha mkutano wa robo mwaka kwa wadau wanaofanyakazi na makundi maalum ulifanywa kutathmini mafanikio na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo na namna wanavyozitatua.

125.       Mheshimiwa Spika, zoezi la kuzitambua na kuzifanyia uhakiki asasi za kiraia zinazowalenga vijana katika maeneo ya UKIMWI na Afya ya uzazi limefanyika kwa Unguja na Pemba. Jumla ya asasi za kiraia 68 (Unguja 51, Pemba 17) zimetambuliwa na kati ya hizo asasi  36 tu ndio zimeonekana kuwa na uwezo wa kufanyakazi kitaalamu.
     
126.       Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Tume ya UKIMWI iliidhinishiwa kutumia jumla ya TZS 1,369,000,000/- kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.  Hadi kufikia Machi, 2015 Tume ya UKIMWI ilikwisha kuingiziwa TZS 633,427,500/- sawa na asilimia 46.

127.       Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Tume ya UKIMWI iliidhinishiwa kutumia TZS 50,000,000/- ikiwa ni mchango wa Serikali katika kazi za maendeleo.  Hadi kufikia Machi, 2015 hakuna fedha zilizopatikana.


MALENGO YA OMKR KWA MWAKA 2015/2016

128.       Mheshimiwa Spika, kama ilivyokwishaelezwa kuwa kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Serikali inaendelea kutekeleza mageuzi ya mfumo wa bajeti kutoka katika bajeti inayotumia vifungu (line item) kwenda katika mfumo unaotumia programu (Program Based Budget – PBB).

129.       Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mwaka 2015/2016 inakusudia kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake kupitia Programu kuu saba (7) zifuatazo:-

A.    Programu ya Usimamizi wa Mazingira na Mabadiliko ya tabianchi;
B.  Programu ya Usimamizi wa masuala ya Watu wenye Ulemavu;
C.  Programu ya Mipango na Utawala;
D.    Programu ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya;
E.     Programu ya Mipango na Utawala wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu; Udhibiti wa Dawa za Kulevya;
F.      Programu ya Kuratibu Muitiko wa Taifa wa UKIMWI; na
G.    Programu ya Mipango na Utawala wa Tume ya UKIMWI
(Angalia Kiambatanisho Nam. 9).


  1. PROGRAMU YA USIMAMIZI WA MAZINGIRA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

130.       Mheshimiwa Spika, programu hii itatekelezwa kupitia programu ndogo mbili (2) na matarajio yake ya muda mrefu ni kuimarisha usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

A.1. Programu ndogo ya Usimamizi wa Mazingira
131.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo ina lengo kuu la kufikia mazingira endelevu ambapo huduma zinazotarajiwa kutolewa ni kuendeleza mazingira endelevu kwa jamii pamoja na kukuza uelewa wa jamii juu ya usimamizi wa mazingira.

132.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa programu hii ndogo yatapimwa kutokana na idadi ya kanuni na miongozo ya usimamizi wa mazingira itakayotayarishwa; idadi ya mikutano ya kimataifa ya mazingira itakayohudhuriwa; idadi ya miradi ya wahisani itakayoanzishwa; idadi ya misaada ya kitaalamu itakayopatikana; idadi ya operesheni za kimazingira zitakazofanywa; idadi ya ziara za ufuatiliaji na ukaguzi wa kimazingira zitakazofanywa; idadi ya miradi itakayokaguliwa; idadi ya miradi itakayofanyiwa tathmini ya athari za kimazingira; idadi ya miradi itakayofanyiwa ukaguzi wa kimazingira; idadi ya vipindi vya radio na vipindi vya TV vitakavyorushwa; idadi ya vipeperushi na vijarida vilivyotayarishwa na kusambazwa; pamoja na idadi ya mikutano ya uhamasishaji itakayofanyika

133.       Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Programu hii ndogo ya Usimamizi wa Mazingira utafanywa kwa pamoja kati ya Idara ya Mazingira na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (Zanzibar Environmental Management Auhtority – ZEMA).

134.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo inakadiriwa kutumia jumla ya TZS 174,076,000/- kutoka Serikalini.

A.2. Programu ndogo ya Usimamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi
135.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo ina lengo kuu la kuratibu na kusimamia masuala ya mabadiliko ya tabianchi ambapo huduma zinazotarajiwa kutolewa ni kutayarisha nyenzo na mipango ya usimamizi, kuratibu mikutano ya usimamizi, kujenga uwezo wa wadau, kukuza uelewa juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuzisaidia jamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

136.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa programu hii ndogo yatapimwa kutokana na kuwepo kwa mpango kazi wa utekelezaji wa Mkakati wa Mabadiliko ya tabianchi utakaotayarishwa, kuwepo kwa utaratibu maalumu wa kifedha kwa ajili ya kugharamia masuala ya mabadiliko ya tabianchi utakaoandaliwa,  kuwepo kwa mfumo wa utayarishaji wa mipango wa kijamii ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi utakaotayarishwa, idadi ya maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi yatakayoendelezwa, idadi ya taasisi zitakazosaidiwa kuingiza mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwenye programu za taasisi hizo, idadi ya taasisi zitakazosaidiwa kuanzisha vitengo vya mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwenye taasisi hizo, idadi ya mikutano ya Kamati za mabadiliko ya tabianchi itakayofanyika, idadi ya wafanyakazi watakaosaidiwa kushiriki mafunzo mafupi na mikutano ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi, idadi ya mikutano, vipeperushi na programu za TV na redio za kuelimisha jamii na wadau juu ya masuala ya mabadiliko ya tabianchi zitakazotayarishwa na idadi ya majiko sanifu yatakayotengenezwa na kutumika.

137.       Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Programu hii ndogo ya Usimamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi utafanywa na Idara ya Mazingira, Wizara ya Kilimo na Maliasili kupitia Idara ya Misitu na Maliasili zisizorejesheka, Wizara Fedha kupitia Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kupitia Idara ya Nishati na Madini na Jumuiya ya Maendeleo ya Jamii na Uhifadhi wa Mazingira Zanzibar (COmmunity Deverlopment and Environmental COnservation in Zanzibar CODECOZ) na utaratibiwa na Idara ya Mipango, Sera na Utafiti.

138.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo inakadiriwa kutumia jumla ya TZS 450,000,000/- kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.

139.       Mheshimiwa Spika, naliomba Baraza lako kuidhinisha jumla ya TZS           624,076,000/- kwa ajili ya utekelezaji wa Programu hii ya Usimamizi wa Mazingira na Mabadiliko ya TabianchiKati ya hizo TZS 174,076,000/- kutoka Serikalini na TZS 450,000,000/- kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.

  1. PROGRAMU YA USIMAMIZI WA MASUALA YA WATU WENYE ULEMAVU

140.       Mheshimiwa Spika, programu hii itatekelezwa kupitia programu ndogo moja (1) na matarajio yake ya muda mrefu ni kuimarisha ujumuishaji wa mahitaji ya Watu wenye Ulemavu katika Sera, Sheria na Mipango mbalimbali.

B.1. Programu ndogo ya Usimamizi wa Masuala ya Watu wenye Ulemavu
141.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo ina lengo kuu la kuhakikisha upatikanaji wa haki na fursa sawa kwa Watu wenye Ulemavu. Huduma zinazotarajiwa kutolewa ni kutetea ujumuishwaji wa Watu wenye Ulemavu; kukuza uelewa wa jamii juu ya masuala ya watu wenye ulemavu pamoja na uwezeshaji wa Watu wenye Ulemavu.

142.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa programu hii ndogo yatapimwa kutokana na sheria itakayofanyiwa mapitio; idadi ya nakala za sheria zitakazo chapishwa na kusambazwa; idadi ya miongozo na kanuni zitakazotayarishwa; idadi ya mikutano ya Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu; idadi ya mikutano ya waratibu wa masuala ya watu wenye ulemavu; idadi ya vipindi vya radio na vipindi vya TV; idadi ya mikutano ya uhamasishaji; idadi ya Watu wenye Ulemavu  waliopatiwa visaidizi na dawa; idadi ya jumuiya za Watu wenye Ulemavu zitakazosaidiwa; pamoja na idadi ya vikundi vya ujasiriamali vya Watu wenye Ulemavu vitakavyosaidiwa.

143.       Mheshimiwa Spika, programu hii ya Usimamizi wa Masuala ya Watu wenye Ulemavu inakadiriwa kutumia jumla ya TZS 155,460,000/- kutoka Serikalini, na utekelezaji wake utafanywa na Idara ya Watu wenye Ulemavu.  Hivyo, naliomba Baraza lako kuidhinisha jumla ya TZS 155,460,000/- kwa ajili ya utekelezaji wa Programu hii.

  1. PROGRAMU YA MIPANGO NA UTAWALA

144.       Mheshimiwa Spika, programu hii itatekelezwa kupitia programu ndogo tatu (3) na matarajio yake ya muda mrefu ni kuimarisha ufanisi na ubora katika utoaji wa huduma katika OMKR.

C.1. Programu ndogo ya Uongozi na Utawala
145.       Mheshimiwa Spika, programu hii ina lengo kuu la kuratibu shughuli za uongozi na rasilimali watu ambapo huduma zinazotarajiwa kutolewa ni kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi na uongozi; kuisaidia jamii katika kazi za maendeleo pamoja kuongeza uelewa wa jamii juu ya masuala yanayosimamiwa na OMKR.

146.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa programu hii yatapimwa kutokana na asilimia ya utekelezaji wa mpango wa manunuzi; idadi ya wafanyakazi waliopatiwa mafunzo; asilimia ya mahudhurio kazini; idadi ya wafanyakazi waliopatiwa stahiki; idadi ya vikundi vilivyopatiwa msaada; idadi ya mikutano na waandishi wa habari (press conference) na idadi ya vipindi vya redio na vipindi vya TV.

147.       Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Programu hii ndogo ya Uongozi na Utawala utafanywa na Idara ya Uendeshaji na Utumishi pamoja na Ofisi ya Faragha.

148.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo inakadiriwa kutumia jumla ya TZS 2,051,997,000/- kutoka Serikalini.

C.2. Programu ndogo ya Mipango, Sera na Utafiti
149.       Mheshimiwa Spika, programu hii lengo kuu ni kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa Sera, Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini kwa masuala yanayosimamiwa na OMKR ambapo huduma zinazotarajiwa kutolewa ni kuimarisha mfumo wa upatikanaji taarifa na kuzisambaza kwa wadau; kuratibu masuala mtambuka yanayosimamiwa na OMKR; na kutayarisha sera, mipango na bajeti za OMKR.

150.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa programu hii ndogo yatapimwa kutokana na idadi ya tafiti zitakazofanywa; idadi ya nakala za ripoti za utafiti zitakazochapishwa; idadi ya mikutano ya kuwasilisha taarifa za utafiti kwa wadau; idadi ya taasisi zenye mpango wa kujumuisha mambo mtambuka; idadi ya mikutano ya uratibu wa masuala mtambuka; idadi ya mikutano ya ufuatiliaji na tathmini; hotuba ya bajeti na Mfumo wa Matumizi wa Muda wa Kati (MTEF) itakayotayarishwa; na idadi ya nakala za sera ya Watu wenye Ulemavu zitakazochapishwa.

151.       Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Programu ndogo ya Mipango, Sera na Utafiti utafanywa na Idara ya Mipango, Sera na Utafiti.

152.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo inakadiriwa kutumia jumla ya TZS 93,719,000/- kutoka Serikalini.

C.3. Programu ndogo ya Uratibu wa masuala ya OMKR Pemba
153.       Mheshimiwa Spika, programu hii lengo lake kuu ni kuratibu shughuli za uongozi, rasilimali watu na shughuli za Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais Pemba ambapo huduma zinazotarajiwa kutolewa ni uimarishaji wa ufanisi wa utendaji kazi na uongozi pamoja na kuratibu, kufuatilia na kukuza mashirikiano kwa masuala ya OMKR Pemba.

154.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa programu hii ndogo yatapimwa kutokana na asilimia ya utekelezaji wa mpango wa manunuzi; idadi ya wafanyakazi watakaopatiwa mafunzo; asilimia ya mahudhurio kazini; idadi ya wafanyakazi watakaopatiwa stahiki; na idadi ya ziara za vijijini (field visits) zitakazofanywa kufuatilia shughuli za Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

155.       Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Programu hii ndogo utafanywa na Ofisi Kuu Pemba.

156.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo inakadiriwa kutumia jumla ya TZS 448,148,000/- kutoka Serikalini.

157.       Mheshimiwa Spika, naliomba Baraza lako kuidhinisha jumla ya TZS 2,593,864,000/- kwa ajili ya utekelezaji wa Programu hii ya Mipango na Utawala wa OMKR.

  1. PROGRAMU YA UDHIBITI WA DAWA ZA KULEVYA

158.       Mheshimiwa Spika, programu hii itatekelezwa kupitia programu ndogo mbili (2) na matarajio yake ya muda mrefu ni kuiwezesha jamii kuwa huru na athari ya dawa za kulevya.

D.1. Programu ndogo ya Uratibu wa Udhibiti wa Usafirishaji na Usambazaji wa dawa za kulevya
159.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo ina lengo kuu la kuzuia uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya ambapo huduma zinazotarajiwa kutolewa ni kudhibiti uingizaji na usafirishaji wa dawa za kulevya pamoja na kuzuia usambazaji wa dawa za kulevya.

160.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa programu hii ndogo yatapimwa kutokana na kuwepo muongozo wa utoaji taarifa; idadi ya mikutano ya kuhamasisha jamii; na idadi ya operesheni zitakazofanyika na maeneo yanayofanyiwa biashara ya dawa za kulevya yatakayosambaratishwa.

161.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo inakadiriwa kutumia jumla ya TZS 57,814,000/- kutoka Serikalini.

D.2. Programu ndogo ya Kinga ya msingi ya Mahitaji na Matumizi ya Dawa za Kulevya
162.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo ina lengo kuu la kupunguza tatizo la utegemezi wa dawa za kulevya katika jamii ambapo huduma zinazotarajiwa kutolewa ni uhamasishaji wa jamii juu ya athari ya dawa za kulevya pamoja na kuzijengea uwezo nyumba za upataji nafuu.

163.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa programu hii ndogo yatapimwa kutokana na idadi ya skuli, taasisi za binafsi na za Serikali zilizofikiwa; idadi ya nyumba zilizosaidiwa na idadi ya waliofaidika na programu za ujasiriamali.

164.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo inakadiriwa kutumia jumla ya TZS 33,250,000/- kutoka Serikalini.

165.       Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Programu ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya utaratibiwa na Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya, naliomba Baraza lako kuidhinisha jumla ya TZS TZS 91,064,000/- kwa ajili ya utekelezaji wa Programu hii ya Udhibiti wa dawa za kulevya.

  1. PROGRAMU YA MIPANGO NA UTAWALA WA TUME YA KITAIFA YA KURATIBU NA UDHIBITI WA DAWA ZA KULEVYA

166.       Mheshimiwa Spika, programu hii itatekelezwa kupitia programu ndogo mbili (2) na matarajio yake ya muda mrefu ni kuwezesha mazingira bora ya kazi ndani Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya.

E.1. Programu ndogo ya Utawala na Uendeshaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya
167.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo ina lengo kuu la kuongeza uwezo wa kufanya kazi na kuweka mazingira mazuri ya kazi ambapo huduma zinazotarajiwa kutolewa ni kujenga uwezo wa wafanyakazi katika uratibu wa mapambano ya dawa za kulevya.

168.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa programu hii ndogo yatapimwa kutokana na asilimia ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Tume; idadi ya wafanyakazi waliopatiwa mafunzo ndani ya kazi pamoja na asilimia ya bajeti ya utekelezaji wa mipango ya Tume.

169.       Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Programu hii ndogo utafanywa na Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya.

170.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo inakadiriwa kutumia jumla ya TZS 304,690,000/- kutoka Serikalini.

E.2. Programu ndogo ya Uratibu wa masuala ya Dawa za kulevya Pemba
171.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo ina lengo kuu la kuongeza uwezo wa kufanya kazi na kuweka mazingira mazuri ya kazi ambapo huduma zinazotarajiwa kutolewa ni uratibu wa shughuli za Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya kisiwani Pemba.

172.       Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Programu hii ndogo utafanywa na Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya ofisi ya Pemba na inakadiriwa kutumia jumla ya TZS 71,346,000/- kutoka Serikalini.

173.       Mheshimiwa Spika, naliomba Baraza lako kuidhinisha jumla ya TZS 376,036,000/- kwa ajili utekelezaji wa Programu hii ya Mipango na Utawala wa Tume Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya.

  1. PROGRAMU YA KURATIBU MUITIKO WA TAIFA WA UKIMWI

174.       Mheshimiwa Spika, programu hii itatekelezwa kupitia programu ndogo mbili (2) na matarajio yake ya muda mrefu ni kuwezesha kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU katika jamii.

F.1. Programu ndogo ya Mawasiliano na Utetezi.
175.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo ina lengo kuu la kuimarisha utekelezaji wa mipango ya  utetezi na uhamasishaji ili kupunguza maambukizi mapya ambapo huduma zinazotarajiwa kutolewa ni uhamasishaji na utetezi ili kupunguza mazingira ya hatari ya kuambukizwa VVU na kuchochea mabadiliko ya tabia kwa makundi maalum na jamii.

176.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa programu hii ndogo yatapimwa kutokana na idadi ya shehia zitakazofikiwa kwa njia ya sanaa za maonyesho; idadi ya programu za jamii zitakazofanyika kwa makundi maalum; idadi ya watu wa makundi maalum watakaofikiwa; idadi ya vipeperushi na majarida yatakayochapishwa na kusambazwa kwa walengwa; idadi ya vipindi vya redio na TV vitakavyorushwa; idadi ya mikoa itakayohamasishwa na kuchukua hatua za kupunguza mazingira hatarishi; idadi ya mikutano ya kuziratibu taasisi  zinazotekeleza shughuli za utetezi na uhamasishaji; idadi ya taasisi zitakazojengewa uwezo; na asilimia ya fedha zitakazotolewa kwa utekelezaji wa programu ya stadi za maisha  na afya ya uzazi kwa vijana nje ya skuli.

177.       Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Programu hii ndogo utafanywa na Tume ya UKIMWI, na unakadiriwa kutumia jumla ya TZS 1,034,381,000/- zikiwemo TZS 51,981,000/-kutoka Serikalini, TZS 932,400,000/- kutoka kwa washirika wa maendeleo na TZS 50,000,000/- ikiwa ni mchango wa Serikali katika kazi za maendeleo.

F.2. Programu ndogo ya Uratibu wa muitiko wa Taifa wa UKIMWI.
178.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo ina lengo kuu la kuongoza, kuratibu, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miongozo ya kitaifa, sera na sheria ya kukinga na kusimamia masuala ya UKIMWI ambapo huduma zinazotarajiwa kutolewa ni utafutaji wa rasilimali kwa ajili ya muitiko wa UKIMWI; kuelimisha jamii juu ya Sheria ya  Kusimamia na Kudhibiti UKIMWI ya mwaka 2014; kuandaa Mkakati wa Tatu wa Taifa wa UKIMWI; kuongeza uwezo wa Tume, jamii, wizara na sekta binafsi kupambana na UKIMWI; na kufanya ufuatiliaji na mikutano ya kuratibu shughuli za UKIMWI kwa sekta za serikali, wilaya, sekta binafsi, asasi za kiraia na shehia.

179.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa programu hii ndogo yatapimwa kutokana na kuwepo kwa Mfuko wa Taifa wa UKIMWI; idadi ya mapendekezo ya miradi; idadi ya vipindi vya redio na TV vitakavyorushwa; kuwepo Mkakati wa tatu wa Taifa wa UKIMWI; idadi ya shehia zitakazowezeshwa na zitakazopatiwa mafunzo; idadi ya mikutano ya uhamasishaji kwa ABCZ; idadi ya wizara zitakazopatiwa muongozo wa kufanya mapitio ya mipango ya UKIMWI; kuwepo ripoti ya Tathmini ya hali halisi na mahitaji ya huduma za UKIMWI kwa maeneo ya masoko na usafiri wa daladala; idadi ya mikutano ya uratibu; kuwepo kwa ripoti ya mwaka ya ufuatiliaji; idadi ya mikutano ya Kamati ya Kitaalamu ya Ufuatiliaji; kuwepo kwa mpango wa utafiti wa Tume; na idadi ya wadau wanaotekeleza shughuli za UKIMWI watakaofuatiliwa.

180.       Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Programu hii ndogo utafanywa na Tume ya UKIMWI, na unakadiriwa kutumia jumla ya TZS 100,833,000/- kutoka Serikalini.

181.       Mheshimiwa Spika, naliomba Baraza lako kuidhinisha jumla ya TZS 1,135,214,000/- kwa ajili ya utekelezaji wa Programu hii ya Kuratibu Muitiko wa Taifa wa UKIMWI, zikiwemo TZS 152,914,000/- kutoka Serikalini, TZS 932,400,000/- kutoka kwa washirika wa maendeleo na TZS 50,000,000/- ikiwa ni mchango wa Serikali katika kazi za maendeleo.

  1. PROGRAMU YA MIPANGO NA UTAWALA WA TUME YA UKIMWI

182.       Mheshimiwa Spika, programu hii itatekelezwa kupitia programu ndogo mbili (2) na matarajio yake ya muda mrefu ni kuwezesha mazingira bora ya kazi ndani ya Tume ya UKIMWI Unguja na Pemba.

G.1. Programu ndogo ya Utumishi na Uendeshaji wa Tume ya UKIMWI
183.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo ina lengo kuu la kuwa na mazingira wezeshi kwa Tume ya UKIMWI kutimiza majukumu yake ambapo huduma zinazotarajiwa kutolewa ni kuweka mazingira mazuri ya kazi; kujenga uwezo wa wafanyakazi; na kusimamia matumizi mazuri ya fedha, uwazi na uwajibikaji.

184.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa programu hii ndogo yatapimwa kutokana na asilimia za utekelezaji wa mpango wa manunuzi na matengenezo ya ofisi yaliyofanyika; idadi ya wafanyakazi watakaopatiwa mafunzo pamoja na idadi ya wafanyakazi na familia zao watakaoshiriki Siku ya Afya (wellness program).

185.       Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Programu hii ndogo utafanywa na Tume ya UKIMWI na unakadiriwa kutumia jumla ya TZS 383,386,000/-.

G.2.Programu ndogo ya Uratibu wa masuala ya UKIMWI Pemba.
186.       Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo lengo lake kuu ni kuratibu shughuli za UKIMWI Pemba kwa wadau wote,

187.       Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa programu hii ndogo yatapimwa kutokana na idadi ya mikutano ya uratibu kwa Taasisi za Serikali, taasisi binafsi na Shehia itakayofanyika, na idadi ya wafanyakazi watakaopatiwa mafunzo.

188.       Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Programu hii ndogo utafanywa na Tume ya UKIMWI ofisi ya Pemba na unakadiriwa kutumia jumla ya TZS 184,900,000/-.

189.       Mheshimiwa Spika, naliomba Baraza lako kuidhinisha jumla ya TZS 568,286,000/- kwa ajili ya utekelezaji wa Programu hii ya Mipango na Utawala wa Tume ya UKIMWI.

SHUKURANI

190.       Mheshimiwa Spika, naomba kukushukuru tena, pamoja na Wajumbe wote wa Baraza lako kwa kunisikiliza kwa utulivu na umakini wa hali ya juu. Ni dhahiri kwamba mashirikiano yenu, umoja, upendo na nidhamu ndio siri kubwa ya mafanikio tuliyoyapata.

191.       Mheshimiwa Spika, naomba kuchukuwa nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza Makatibu wote wa Baraza wakiongozwa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi kwa umakini wao katika kulisaidia Baraza, Kamati za Baraza na Wajumbe wa Baraza katika kutekeleza majukumu yao.  Aidha, naomba niwashukuru Waandishi wote wa habari waliopata nafasi ya kushuhudia yale yaliyofanyika hapa Barazani kwa vipindi tofauti vya mwaka lakini na wale tuliokuwa pamoja nje ya Baraza kwa safari na mikutano mbalimbali katika jamii.  Wote wamekuwa na mchango adhimu wa kuwafikishia wananchi taarifa na miongozo mbalimbali ya masuala yanayohusu nchi yao.

192.       Mheshimiwa Spika, naomba pia kwa namna ya pekee kuchukuwa nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza kwa dhati kabisa Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuanzia Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugezi, Afisa Mdhamini pamoja na Maafisa wa ngazi zote kwa kufanya kazi bila kuchoka zilizotuwezesha kutekeleza malengo na majukumu yetu kwa ufanisi katika kipindi cha mwaka 2014/2015.

193.       Mheshimiwa  Spika, natoa  shukrani za dhati  kwa nchi marafiki, mashirika ya Kimataifa na watu binafsi kwa kuendelea kutusaidia katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais. Nchi hizo ni pamoja na Marekani, Finland, Norway, Uingereza, Uholanzi, Australia, China, Brazil, India na Falme za nchi za Kiarabu na Oman. Pia mashirika ya kimataifa yakiwemo  UNDP, UNICEF, UNFPA,UNAIDS, UNEP, UNODC, UNFCCC, WHO, World Bank, CDC, THPS, IOC, UNESCO, DFID, IIED, Save the Children international pamoja na nchi na mashirika  mengine ambayo sikuyataja, lakini kwa njia moja au nyengine yanatuunga mkono katika shughuli zetu za maendeleo. Juhudi na michango yao tunaithamini sana.

194.        Mheshimiwa Spika, shukurani za pekee ziwaendee wote walioshiriki kwa njia moja au nyengine katika kufanikisha utekelezaji wa kazi za Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais. Mwisho napenda kuwashukuru wananchi wote kwa ujumla kwa kufanikisha kazi za maendeleo ya nchi yetu.

195.    Mheshimiwa Spika, kwa  namna  ya  pekee napenda kuishukuru familia yangu kwa ustahamilivu wao na msaada mkubwa wanaonipa katika kunijengea utulivu ili niweze  kutekeleza majukumu yangu, nawaombea heri na baraka katika maisha yao.

196.    Mheshimiwa Spika, mwisho napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wananchi wote kwa ujumla kwa kudumisha amani katika kipindi hichi chote cha miaka mitano chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, sote tunaelewa amani ni nyenzo muhimu ya kutufikisha katika maendeleo endelevu na ustawi wa jamii yetu, nawaomba wanasiasa na wananchi wote kwa ujumla kuhakikisha tunadumisha amani katika kipindi hichi cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu hadi kufikia kukamilisha uchaguzi kwa salama na amani namuomba Mwenyezimungu atuwezeshe kuitunza amani ndani ya nchi yetu.

HITIMISHO

197.    Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa sasa nachukuwa nafasi hii kuwaomba Wajumbe wa Baraza lako waipokee, waijadili, washauri, waelekeze na hatimae kuidhinisha matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ya jumla ya shilingi Bilioni tatu, milioni mia tatu na sabini na tatu na laki nne (T.Shs. 3,373,400,000/-) kwa mwaka wa fedha 2015/2016, zikiwemo  shilingi Bilioni mbili, milioni mia tisa na ishirini na tatu na laki nne (TZS 2,923,400,000/-) kutoka Serikalini na shilingi Milioni mia nne na hamsini (T.Shs. 450,000,000/-) kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.  Kati ya fedha hizo, shilingi Milioni mia moja na sabini na nne, na elfu sabini na sita (T. Shs. 174,076,000/-) kutoka Serikalini pamoja na shilingi Milioni mia nne na hamsini (T.Shs. 450,000,000/-) kutoka kwa Washirika wa Maendeleo zitakuwa kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Usimamizi wa Mazingira na Mabadiliko ya tabianchi; shilingi Milioni mia moja na hamsini na tano, laki nne na elfu sitini (T. Shs. 155,460,000/-) kutoka Serikalini kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Usimamizi wa masuala ya Watu wenye Ulemavu; na shilingi Bilioni mbili, milioni mia tano na tisini na tatu, laki nane na elfu sitini na nne (T. Shs. 2,593,864,000/-) kutoka Serikalini kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Mipango na Utawala (Angalia Kiambatanisho Nam. 10).

198.    Mheshimiwa Spika, aidha, naliomba Baraza lako liidhinishie Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya matumizi ya jumla ya shilingi Milioni mia nne na sitini na saba na laki moja (T.Shs 467,100,000/-) kutoka Serikalini kwa mwaka wa fedha 2015/2016. Kati ya fedha hizo, shilingi Milioni tisini na moja na elfu sitini na nne (T.Shs 91,064,000/-) kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya; na shilingi Milioni mia tatu na sabini na sita na elfu thelathini na sita (TShs. 376,036,000/-) kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Mipango na Utawala wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu; Udhibiti wa Dawa za Kulevya (Angalia Kiambatanisho Nam. 10).

199.    Mheshimiwa Spika, aidha, naliomba Baraza lako liidhinishie Tume ya UKIMWI matumizi ya jumla ya shilingi Milioni mia saba na ishirini na moja na laki moja (T.Shs. 721,100,000/-) kutoka Serikalini, shilingi Milioni mia tisa na thelathini na mbili na laki nne (T.Shs. 932,400,000/- kutoka kwa Washirika wa Maendeleo, na shilingi Milioni hamsini (T. Shs. 50,000,000/-) ikiwa ni mchango wa Serikali katika kazi za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2015/2016.  Kati ya fedha hizo, shilingi Milioni mia moja na hamsini na mbili, laki tisa na elfu kumi na nne (T.Shs. 152,914,000/-) kutoka Serikalini, shilingi Milioni mia tisa na thelathini na mbili na laki nne (T.Shs. 932,400,000/- kutoka kwa Washirika wa Maendeleo, na shilingi Milioni hamsini (T. Shs. 50,000,000/-) ikiwa ni mchango wa Serikali katika kazi za maendeleo, zitakuwa kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Kuratibu Muitiko wa Taifa wa UKIMWI; na shilingi Milioni mia tano na sitini na nane, laki mbili na elfu themanini na sita (TShs 568,286,000/-) kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Mipango na Utawala wa Tume ya UKIMWI (Angalia Kiambatanisho Nam. 10).

200.    Mheshimiwa Spika, aidha, naliomba Baraza lako likubali mchango wa jumla ya T. Shs. 34,712,000/- ikiwa ni mapato yaliyokadiriwa kukusanywa na OMKR kwa mwaka 2015/2016.

201.     Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima, naomba kutoa hoja.


Kiambatanisho Nam. 1:
WAFANYAKAZI WALIOPATIWA FURSA ZA MAFUNZO KWA MWAKA 2014/2015
NA
JINA
CHUO
FANI
DARAJA
MWAKA ALIONZA
MWAKA ANAOMALIZA
MFADHILI
Idara ya Uendeshaji na Utumishi
1
Nd. Waziri Abbas Sheha
Chuo cha Utawala wa Umma
Utawala wa Umma
Stashahada
2013
2015
OMKR
2
Nd. Ali Msellem Khamis
Chuo kikuu huria Tanzania
Uhusiano wa Kimataifa
Shahada ya pili
2014
2016
OMKR
3
Nd. Asya Mmanga Said
Institute Counting Professional  Studies
Uwekaji kumbu kumbu
Cheti
2014
2015
OMKR
4
Nd. Jokha  Nossor Mvinja
Chuo cha Ununuzi Ugavi
Ununuzi na Ugavi
Shahada ya kwanza
2012
2015
OMKR
5
Nd. Khamis Makame Ali
Chuo cha Ununuzi Ugavi
Ununuzi na Ugavi
Shahada ya kwanza
2013
2016
OMKR
6
Nd. Bakari Shaban Bakar
Chuo Kikuu cha Zanzibar - Tunguu
Uchumi na Fedha
Shahada ya pili
2014
2016
OMKR
7
Nd. Abdillah Mussa Mshandete
Chuo Kikuu Mzumbe
Uongozi wa Biashara
Shahada ya pili
2014
2016
OMKR
8
Nd. Asha Rashid Juma
India
Kiingereza na Teknoloj
Kozi Fupi
2014
2014
INDIA
9
Nd. Saada Mussa Said
China
Mabadiliko ya Tabianchi
Kozi Fupi
2014
2014
CHINA
10
Nd. Zena Mussa Mwinyi
Chuo cha kumbu. Mwalim Nyerere
Uwekaji kumbu kumbu
Kozi Fupi
2014
2014
OMKR
Idara ya Mipango, Sera na Utafiti

11
Nd. Suleiman Kheir Suleiman
Chuo cha Mipango Dodoma
Usimamizi wa miradi
Stashahada ya Uzamili
2014
2015
OMKR
12
Nd. Jabu Sharif Haji
Chuo kikuu huria Tanzania
Uchumi
Shahada ya pili
2014
2016
OMKR
Idara ya Watu wenye Ulemavu
13
Nd. Kombo Muhidin Ame
Chuo kikuu huria Tanzania
Rasilimali watu
Shahada ya pili
2013
2015
OMKR
14
Nd. Asma Adam Ali
KIU
Uhasibu na Fedha
Shahada ya kwanza
2012
2015
OMKR
15
Nd.Abushir  Said Khatib
Chuo kikuu huria Tanzania
Uchumi
Shahada ya pili
2014
2016
OMKR
Ofisi ya Faragha
16
Nd. Moh`d Ibrahim Mikuto
Chuo cha Utalii
Upishi
Stashahada
2013
2015
OMKR
17
Nd. Hassan Hamad Kombo
India
Uandishi wa habari
Kozi Fupi
2014
2014
INDIA
Idara ya Mazingira
18
Nd. Makame Haji Khamis
Chuo cha Mipango Dodoma
Mipango ya Mazingira
Shahada ya pili
2014
2016
UDHAMINI BINAFSI
19
Nd.Mtoro Abdalla Salim
Institute Counting Professional  Studies
Uhasibu
Stashahada
2014
2016
OMKR
20
Nd. Khadija Othman Juma
Chuo Kikuu cha Zanzibar - Tunguu
Uchumi
Shahada ya kwanza
2013
2016
OMKR
21
Nd. Chiku Ali  Moh`d
Dar. Institute of Arts Media  Communiction
Vedio, Film and TV production
Stashahada
2014
2016
HIMA
22
Nd. Ali Vuai Pandu
Chuo cha Mipango Dodoma
Mipango ya Mazingira
Shahada ya pili
2014
2016
UDHAMINI BINAFSI
23
Hassan Hamad Hassan
Chuo Kikuu cha Dodoma
Bioanuai
Shahada ya pili
2012
2014
UDHAMINI BINAFSI
24
Nassor Jamal Nassor
Chuo Kikuu cha SUZA
Sayansi ya Mazingira
Shahada ya pili
2012
2014
COSTECH
25
Salma Moh’d Aboud
Chuo Kikuu cha Zanzibar - Tunguu
Sheria
Shahada ya pili
2012
2014
UDHAMINI BINAFSI
26
Mgeni Mwalim Khamis
Chuo Kikuu cha Bagamoyo
Mfumo wa Habari
Shahada ya pili
2014
2015
BODI YA MIKOPO
27
Alawi H. Hija
Chuo kikuu cha SUZA
Sayansi ya Mazingira
Shahada ya pili
2014
2016
UDHAMINI BINAFSI
28
Mwalim Khamis Mwalim
Chuo Kikuu Huria- Tanzania
Usimamizi wa Miradi
Shahada ya pili
2013
2015
HIMA
29
Juma Shaame Salim
Chuo Kikuu Huria- Tanzania
Elimu ya Mazingira
Shahada ya pili
2013
2015
UDHAMINI BINAFSI
30
Nassor Majid Nassor
Chuo Kikuu cha Dar es salaam
Tathmini na Usimamizi wa Mazingira
Shahada ya pili
2013
2015
BODI YA MIKOPO
31
Mussa Khamis Khamis
Chuo Kikuu Huria- Tanzania
Kazi za kijamii
Shahada ya pili
2015
2017
UDHAMINI BINAFSI
32
Zuwena Juma Bilal
Chuo cha Hotel na Uongozi - Dar es salaam (Tawi la Pemba)
Ununuzi
Stashahada
2015
2017
UDHAMINI BINAFSI
33
Zuhura Msabaha Khamis
Chuo cha Uandishi wa Habari (Time) - Pemba
Uandishi wa Habari
Stashahada
2015
2017
UDHAMINI BINAFSI

Ofisi Kuu Pemba
34
Ali Othman Mussa
Chuo cha Mipango- Dodoma
Mipango na Usimamizi wa Mazingira
Shahada ya pili
2013
2015
HIMA
Tume ya UKIMWI
35
Nd. Yahya Abeid Ali
Chuo cha Utawala wa Umma
Teknolojia ya habari
Stashahada
2013
2014
TUME
36
Nd. Juma Mohammed Ahmed
Chuo cha Utawala wa Umma
Uhasibu
Stashahada
2013
2014
TUME
37
Nd. Fatma Khamis Ali
Chuo Kikuu cha Zanzibar - Tunguu
Uongozi wa Biashara
Shahada ya pili
2013
2014
TUME
38
Nd. Nassor Ali Abdalla
Chuo Kikuu Morogoro
Utekelezaji wa sera kuzishirikisha taasisi za kiraia
Shahada ya pili
2013
2014
TUME
39
Nd. Mohammed Said Mohammed
INDIA
Ufuatiliaji na Tathmini
Kozi fupi
2014
2014
TUME
Kiambatanisho Nam. 2:
OPERESHENI ZA KUDHIBITI MATUMIZI YA MIFUKO YA PLASTIKI ZILIZOFANYWA KWA MWAKA 2014/2015
Namb.
Mwezi
Idadi ya Operesheni
Idadi ya Watu waliokamatwa
Kiwango cha Mifuko kilichokamatwa (Kgs)
1.       
Julai, 2014
5
0
0
2.       
Agosti,2014
3
3
2
3.       
Septemba, 2014
3
0
0
4.       
Oktoba,2014
12
14
694
5.       
Novemba, 2014
-
-
-
6.       
Disemba, 2014
-
-
-
7.       
Jnuari, 2015
-
-
-
8.       
Februari, 2015
10
6
63
9.       
Machi, 2015
-
-
-

JUMLA
33
23
759
Kiambatanisho Nam. 3:
MIRADI ILIYOFANYIWA TATHMINI YA ATHARI ZA KIMAZINGIRA (EIA) NA KUPEWA VYETI VYA KIMAZINGIRA KWA MWAKA 2014/2015
Namb.
Jina la Mradi
Mahali Ulipo
Nambari ya Cheti
1.       
Amber Golf and Beach Resort
Mbuyu Tende-Matemwe
IM/EIA/51
2.       
Construction of New Port Project Phase 1 Zanzibar
Maruhubi
IM/EIA/52
3.       
Zanzi Gas Co Limited, Zanzibar
Welezo - Makufuli
IM/EIA/50
4.       
Construction of Terminal II of Abeid Amani Karume International Airport
Kisauni
IM/EIA/53
5.       
Island Paradise Inn Hotel
Mlandege - Zanzibar
IM/EIA/03
6.       
Upgrading of 62.6 km of Road in Unguja Island to Bitumen standards Zanzibar
North, South and west district of Zanzibar
IM/EIA/54
7.       
Zas Villa Luxury and Resort

Kiwengwa Kumba Urembo North B district
IM/EIA/55
8.       
Tulia resort (nature safari lodge)
Pongwe Pwani
IM/EIA/56
9.       
Beach resort Project at Makunduchi (Fard company)
Shungi Makunduchi
IM/EIA/57
10.   
Uzuri Zanzibar Resort Project
Kendwa
IM/EIA/58
11.   
Ujamaa Beach Resort
Makunduchi
IM/ER/05
12.   
Internet Data Center
Fumba
IM/ER/03
13.   
Trade Wind Hotel
Matemwe
IM/ER/04









Kiambatanisho Nam. 4:
VIPINDI VYA REDIO NA TV VILIVYORUSHWA HEWANI KWA MWAKA 2014/2015
NAMBA
MADA YA KIPINDI
IDADI
KITUO
IDARA HUSIKA
1
Marufuku ya mifuko ya plastiki
1
ZBC Redio
Idara ya Mazingira
2
Matumizi ya majiko sanifu
2
ZBC Redio 
Idara ya Mazingira
3
Umuhimu wa umeme wa jua
2
ZBC Redio 
Idara ya Mazingira
4
Tangazo la marufuku ya mifuko ya plastiki
1
ZBC Redio 
Idara ya Mazingira
5
Kanuni za Mali Asili zisizorejesheka
2
ZBC Redio 
Idara ya Mazingira
6
Matumizi endelevu ya Mali Asili zisizorejeseka
1
ZBC Redio 
Idara ya Mazingira
7
Mmong’onyoko wa fukwe
2
ZBC Redio 
Idara ya Mazingira

Matumizi ya majiko sanifu
1
ZBC TV
Idara ya Mazingira

Matumizi ya umeme wa jua
1
ZBC TV
Idara ya Mazingira

JUMLA
13




Kiambatanisho Nam. 5:
AINA NA IDADI YA VISAIDIZI VILIVYOTOLEWA KWA WATU WENY ULEMAVU WA AINA MBALIMBALI KWA MWAKA 2014/2015
PEMBA
Wilaya
Aina ya kisaidizi
Wanawake
Wanaume
CHAKE CHAKE
Kiti cha magurudumu mawili
3
1
Fimbo nyeupe
4
5
Miwani + Kofia
6
3
Magongo ya kutembelea
2
3
MKOANI
Kiti cha magurudumu mawili
1
3
Fimbo nyeupe
4
5
Miwani + Kofia
6
3
Magongo ya kutembelea
1
2
WETE
Kiti cha magurudumu mawili
4
0
Fimbo nyeupe
4
8
Miwani + Kofia
5
3
Magongo ya kutembelea
6
10
MICHEWENI
Kiti cha magurudumu mawili
3
3
Fimbo nyeupe
6
9
Miwani + Kofia
3
6
Magongo ya kutembelea
0
9
JUMLA
58
73
UNGUJA
KASKAZINI A
Kiti cha magurudumu mawili
1
6
Fimbo nyeupe + miwani
0
0
Miwani +Kofia
4
2
Magongo ya kutembelea
0
0
Fimbo nyeupe
0
0
KASKAZINI B
Kiti cha magurudumu mawili
1
1
Fimbo nyeupe + miwani
0
0
Miwani +Kofia
0
1
Magongo ya kutembelea
0
0
Fimbo nyeupe
0
2
MJINI
Kiti cha magurudumu mawili
3
6
Fimbo nyeupe + miwani
0
0
Miwani +Kofia
3
1
Magongo ya kutembelea
0
4
Fimbo nyeupe
1
3
MAGHARIBI
Kiti cha magurudumu mawili
1
1
Fimbo nyeupe + miwani
0
1
Miwani +Kofia
3
2
Magongo ya kutembelea
0
3
Fimbo nyeupe
4
1
KATI
Kiti cha magurudumu mawili
3
2
Fimbo nyeupe + miwani
4
6
Miwani +Kofia
1
1
Magongo ya kutembelea
1
5
Fimbo nyeupe
1
1
KUSINI
Kiti cha magurudumu mawili
2
3
Fimbo nyeupe + miwani
1
0
Miwani +Kofia
0
0
Magongo ya kutembelea
2
0
Fimbo nyeupe
2
4
JUMLA
38
56

Kiambatanisho Nam. 6:
IDADI YA SKULI ZILIZOPATA ELIMU YA ATHARI YA DAWA ZA KULEVYA UNGUJA NA PEMBA KWA MWAKA 2014/2015
UNGUJA
1
JINA LA SKULI
IDADI YA WANAWAKE
IDADI YA WANAUME
2
K/SAMAKI
34
27
3
DARAJANI
40
21
4
RAHALEO
30
22
5
AL-HARAMAYN
43
27
6
JANG’OMBE B MSINGI
56
30
7
NYERERE SEK
33
29
8
KIDONGO CHEKUNDU B MSING
40
31
9
JANG’OMBE SEK.
39
24
10
JANG’OMBE A MSINGI
36
20
11
K/CHEKUNDU A MSINGI
50
30
12
CHUKWANI
49
28
13
MFENESINI
49
20
14
MIKUNGUNI
56
26
15
M’KWEREKWE. A
40
32
16
M’KWEREKWE G
32
20
17
KITOPE
48
29
18
CHWAKA
50
24
19
KIANGA
40
28
20
NUNGWI
49
30
21
MTONI
50
27
22
E/MBADALA
50
18
23
MPENDAE
49
30
24
M’KWEREKWE. E
40
28
25
BUBUBU SEK.
55
38
26
MWERA
30
20
27
MACHUI
40
23
28
MUYUNI
39
30
29
VIKOKOTONI
38
20

JUMLA
1245
758
PEMBA
1
CHANJAMJAWIRI SEK
40
27
2
CHANJAANI SEK
47
20
3
UWONDWE SEK
49
37
4
MICHEWENI MS
38
30
5
JADIDA MSINGI
37
20
6
OLE SEK
38
28
7
SHUNGI SEK
29
20
8
CHWAKA TUMBE SEK
37
34
9
TIRONI MSINGI
19
17
10
WINGWI SEK
18
19
11
MZAMBARAUNI SEK
37
30
12
CHAMBANI SEK
45
30
13
CHAMBANI MSINGI
37
20

JUMLA
471
332
Jumla ya Unguja na Pemba
1,716
1,090









Kiambatanisho Nam. 7:
NYUMBA ZA MAKAAZI (SOBER HOUSES) ZILIZOPEWA RUZUKU KWA MWAKA 2014/2015
                                                     MAELEZO
KIASI (TSH)
SEPTEMBA 2014

  1. LIMBANI SOBER HOUSE (PEMBA)
1,500,000
  1. KIFOE SOBER HOUSE (PEMBA)
1,500,000
  1. MTOFAANI SOBER HOUSE (UNGUJA)
1,500,000
OKTOBA 2014

  1. FREE AT LAST RECOVERY HOME (UNGUJA)
1,500,000
  1. TAWWABIINA SOBER HOUSE (UNGUJA)
1,500,000
NOVEMBA 2014

  1. DETROIT SOBER HOUSE (UNGUJA)
1,500,000
  1. TRENT SOBER HOUSE (UNGUJA)
1,500,000
  1. Z’BAR YOUTH FORUM (UNGUJA)
1,500,000
DISEMBA 2014

  1. NYARUGUSU SOBER HOUSE (UNGUJA)
1,500,000
  1. MKOROSHONI SOBER HOUSE (PEMBA)
1,500,000
JUMLA
15,000,000

Kiambatanisho Nam. 8:
VIKUNDI  VYA WAJASIRIAMALI KUTOKA ZAPHA+ VILIVYOPATIWA FEDHA NA MISAADA MBALI MBALI KWA MWAKA 2014/2015
Jina la kikundi
Kazi za kikundi
Msaada waliopata
Pahala kilipo
Umoja ni nguvu
Kuweka na kukopa
Mafunzo na shs . 890,000/- za kuendeleza mradi
Welezo, Unguja

Female Individual Entrepreneurship group
Kushona, kutengeneza sabuni na biashara ndogo ndogo
Mafunzo na shs . 890,000/- za kuendeleza mradi
Bububu, Unguja
Umoja ni nguvu Micheweni
Kilimo cha mazao ya chakula na mboga mboga
Mafunzo na shs . 890,000/- za kuendeleza mradi
Micheweni - Pemba
Lengo letu moja
Ufugaji wa kuku
Mafunzo na shs . 890,000/- za kuendeleza mradi
Chake chake - Pemba
Jipe moyo
Utengenezaji wa sabuni
Mafunzo na shs . 890,000/- za kuendeleza mradi
Welezo, Unguja




Kiambatanisho Nam. 10:
MCHANGANUO WA FEDHA ZINAZOOMBWA KWA PROGRAMU ZA OMKR, TUME YA UKIMWI NA TUME YA KITAIFA YA KURATIBU NA UDHIBITI ZA DAWA ZA KULEVYA KWA MWAKA 2014/2015
PROGRAM KUU
PROGRAMU NDOGO
Fedha Zinazoombwa kwa mwaka 2015/2016
Matumizi ya Kawaida
Mchango wa SMZ katika kazi za maendeleo
Washirika wa Maendeleo
Jumla TZS
Usimamizi wa Mazingira na Mabadiliko ya tabianchi
Usimamizi wa Mazingira
174,076,000
0
0
174,076,000
Usimamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi
0
0
450,000,000
450,000,000
Jumla kwa Programu 1
174,076,000
0
450,000,000
624,076,000
Usimamizi wa masuala ya Watu wenye Ulemavu
Usimamizi wa masuala ya Watu wenye Ulemavu
155,460,000
0
0
155,460,000
Jumla kwa Programu 2
155,460,000
0
0
155,460,000
Mipango na Utawala
Uongozi na Utawala
2,051,997,000
0
0
2,051,997,000
Mipango, Sera na Utafiti
93,719,000
0
0
93,719,000
Uratibu wa masuala ya OMKR Pemba
448,148,000
0
0
448,148,000
Jumla kwa Programu 3
2,593,864,000
0
0
2,593,864,000
JUMLA YA OMKR - TZS
2,923,400,000
0
450,000,000
3,373,400,000
Udhibiti wa Dawa za Kulevya
Uratibu wa Udhibiti wa Usafirishaji na Usambazaji wa dawa za kulevya
57,814,000
0
0
57,814,000
Kinga ya msingi ya Mahitaji na Matumizi ya Dawa za Kulevya
33,250,000
0
0
33,250,000
Jumla kwa Programu 4
91,064,000
0
0
91,064,000
Mipango na Utawala wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu; Udhibiti wa Dawa za Kulevya
Utawala na Uendeshaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya
304,690,000
0
0
304,690,000
Uratibu wa masuala ya Dawa za kulevya Pemba
71,346,000
0
0
71,346,000
Jumla kwa Programu 5
376,036,000
0
0
376,036,000
JUMLA YA TUME YA KITAIFA YA KURATIBU NA UDHIBITI WA DAWA ZA KULEVYA - TZS
467,100,000
0
0
467,100,000
Kuratibu Muitiko wa Taifa wa UKIMWI
Mawasiliano na Utetezi.
51,981,000
50,000,000
932,400,000
1,034,381,000
Uratibu wa muitiko wa Taifa wa UKIMWI.
100,833,000
0
0
100,833,000
Jumla kwa Programu 6
152,914,000
50,000,000
932,400,000
1,135,214,000
Mipango na Utawala wa Tume ya UKIMWI
Utumishi na Uendeshaji wa Tume ya UKIMWI
383,386,000
0
0
383,386,000
Uratibu wa masuala ya UKIMWI Pemba.
184,900,000
0
0
184,900,000
Jumla kwa Programu 7
568,286,000
0
0
568,286,000
JUMLA YA TUME YA UKIMWI - TZS
721,100,000
50,000,000
932,400,000
1,703,500,000



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.