HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA KUSIMAMIA OFISI ZA
VIONGOZI WAKUU WA KITAIFA KUHUSIANA NA BAJETI YA OFISI YA MAKAMO WA KWANZA WA
RAIS KWA MWAKA 2015/2016.
Mhe. Spika,
Nianze
kwa kutanguliza jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambae kwake tunamtegemea na
kumuomba msamaha wa makosa yetu makubwa na madogo. Pia tunamshukuru kwa kuweza
kutukutanisha hapa tukiwa wazima na wenye Afya njema, katika kuwatumikia
wananchi wetu waliotuchagua kwa mapenzi makubwa.
Mhe. Spika,
Pili
naomba pia kukushuru wewe mwenyewe binafsi kwa kuweza kuliongoza Baraza lako
tukufu hili la Wananchi wa Zanzibar, kwa kipindi chote cha uhai wa Baraza hili
la nane kwa umahiri mkubwa na kwa kushirikiana na wasaidizi wako bila ya
matatizo yoyote bila ya kuonyesha upendeleo kwa upande wowote.
Pia nachukua nafasi nyingine ya kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa neema yake ya mvua aliyotupa nchini mwetu, ambayo bila ya
kutuneemesha neema hii, maisha yetu hayataweza kuendelea. Aidha, kwa kuwa mvua
zinazoendelea kunyesha zimeleta maafa kwa baadhi ya wananchi wetu, nachukua
nafasi hii kuwapa pole wale wote ambao wameathirika na mvua hizo na nawaomba
sana waendelee kuwa na subira na kuchukua hatua madhubuti ya kuepuka madhara
makubwa ya mvua hizo, lakini waendelee kuiamini Serikali yao kwani imeonesha
mashirikiano makubwa na kuwasaidia katika maafa haya na mengine yanayotokea
katika nchi yetu.
Mhe Spika,
pia katika hili tunaendelea tena kuwapongeza viongozi wetu wote wakuu wa Nchi
kwa kuonysha moyo wa kuwafariji wananchi wetu waliopatwa na maafa ya mafuriko
ya Mvua kubwa ya Masika iliyonyesha hivi karibuni, kwa kweli tuliwaona viongozi
wetu hawa walitoka maofisini mwao na kuwemo mitaani kuwafariji watu wetu hawa
kwa niaba yao tunawashukuru na tunawaomba waendelee na moyo huo huo wa kuwa
karibu na jamii kwa hali na mali.
Mhe. Spika,
Kwa
heshima kubwa kamati yangu tunampongeza sana Mhe Makamo wa Kwanza wa Rais, kwa
kuendelea kuiongoza Afisi yake ya Makamo wa Kwanza wa Rais kwa umahiri mkubwa
na pia kuendelea kumshauri vizuri Mhe Rais wa Zanzibar katika kuiongoza nchi
yetu sote tunaamini mafanikio yote tunayoyapata ya maendeleo hapa Zanzibar basi
ni mashauriano ya pamoja baina ya Mhe Rais wetu wa Zanzibar, Makamo wa kwanza
wa Rais na Makamo wapili wa Rais, kwa kukaa pamoja na kuangalia mustakbal wa nchi
yetu katika kuwaletea maendeleo hapa Zanzibar, tunawaomba viongozi wetu
waendelee kukaa pamoja kwa kushauriana na tumuombe Mwenyeenzi Mungu awajaalie
waendelee kuelewana kwani wakielewana wao ndipo Nchi yetu itakapopata Baraka na
neema ili wananchi wetu wafaidike na matunda ya Nchi yetu.
Mhe Spika,
Pia
kamati yangu inampongeza sana Mhe Waziri wa Nchi Afisi ya Makamo wa Kwanza wa
Rais, kwa kuweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa kwa kumsaidia
Makamo wa kwanza wa Rais katika shughuli zake, Mhe Spika, Waziri huyu ni mwanamke
shupavu asiyeyumba wala kuterereka katika kutekeleza majukumu yake, na ndio
maana ameweza kubeba sifa ndani na nje ya nchi yetu, kamati yangu katika
kipindi chote cha miaka mitano imeweza kupata mshirikiano makubwa kutoka kwa
Waziri huyu, kwani pia hakusita kutaka msaada wetu pale alipokua akikwazwa na
utekelezaji wa shughuli zake na bila kusita kamati yangu iliweza kutoa msaada
mkubwa ili kufanikisha majukumu yake , ndio maana leo tunajivunia alau kuweza
kupata eneo la kujenga nyumba za kurekebishia tabia za vijana wetu
walioathirika na madawa ya kulevya( Rehabilitation Centre) huko kidimni Mkoa wa
Kusini Unguja, hayo ni baadhi tu kati ya mafanikio hayo.
Mhe Spika,
kwa kuwa Mhe Waziri yeye ni (Hajat) na katika hotuba yake ametuombea Dua sote
turudi tena hapa Barazani ili kuliendeleza gurudumu hili tuliloliacha basi
Mweneenzi Mungu aikubali dua yake ili tuweze kuwa pamoja mwakani kuja
kuisimamia Bajet yake hii. Amin.
Mhe Spika,
pia kamati yangu inaungana na Waziri kutoa mkono wa pole kwa Familia ya aliyekua
mjumbe mwenzetu Marehem Salmin Awaadh Salmin. Sote basi tumumbe Mwenyenzi Mungu
aiweke roho ya mwenzetu peponi Amin.
Mhe Spika,
Kamati
yangu inatoa shukrani zetu za dhati kwa Katibu Mkuu wa Afisi hii kamati yangu
pamoja na kuisimamia Afisi hii lakini imeweza kuchota mengi kutoka kwa Katibu
Mkuu huyu Senior katika SMZ, Naibu
Katibu wake ,Wakurugenzi, Makamishna pamoja na watendaji wote wa Afisi hii ya
Makamo wa Kwanza.
Nichukue
tena nafasi hii kuwapongeza Wajumbe wote wa Baraza hili la Nane la Wawakilishi,
lililoanza uhai wake Novemba 2010, kwa Mashirikiano na kufanya kazi kwa pamoja
baina ya Wajumbe hawa, bila ya kujali tofauti zao za kisiasa kwa kweli kumenipa
faraja sana na kujiamini kwa kusimama tena leo hii katika kikao cha mwisho cha
Bajeti ya Ofisi hii ya Makamo wa Kwanza wa Rais. Niendelee kuwaomba Wajumbe
kudumisha mapenzi na mashirikiano ya pamoja katika kujenga nchi yetu hii ya
Zanzibar, ambayo ni utegemezi wake, ni nguvu za pamoja za watu wake, ambao ndio
sisi na wananchi wa Majimbo yetu yote.
Mhe Spika,
Baada
ya shukrani nyingi kwa watu mbali mbali tulioshirikiana nao sasa naomba niingie
katika kuichangia Hotuba ya Mhe Waziri afisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, kama
hivi ifuatavyo;-
Mhe Spika,
Kwa
kweli kwa niaba ya kamati tumpe pole sana Mhe Waziri, kwani majukumu yote
aliyopewa kuyasimamia katika Afisi yake ni masuala magumu ambayo yanachangamoto
nyingi kwani karibu yote wao hawana uwezo wa kuyashulikia moja kwa moja
isipokua inabidi yashughulikiwe na taasisi nyingine chini ya isimamizi wenu
inawezekana wakati mwingine hamuridhiki na uharaka au kwa kasi mnayoitarajia
lakini mnabakia kusikitika, au kusononeka lakini pamoja na hayo tunawapomngeza
kwa kuwasimamia kwa karibu na kutoa ushauri pale inapobidi ili kuhakikisha
kwamba ufumbuzi unapatikana.
Mhe Spika,
Kamati
yangu inaipongeza Idara ya Uratibu ya shughuli za Makamo wa Kwanza wa Rais kwa
kuweza kuratibu shughuli zake zote za kitaifa pamoja na zile zinahusu masuala
ya nje ya nchi ya Makamo wa kwanza , lakini bado kamati yangu inaungana na Mhe
Waziri kwa idara hii kuendelea kukabiliana na changamoto wa ukosefu nyumba za
makaazi kwa Makamo wa Kwanza wa Rais hapa Unguja, bado tunakodi nyumba ya mtu
binafsi, vil;e vile Pemba tunakodi na Dar-es- Salaam ndio kabisaaa anafikia Hoteli, Mhe Spika, Kamati yangu kwa
kweli hairidhiki kabisa na hali hii kwani huyu ni kiongozi mkubwa katika Nchi
yetu, lakini pia inaigharimu Serikali kutumia pesa nyingi sana kulipia majengo
hayo pesa ambazo zingeliweza kuwahudumia wananchi wetu kwa shughuli zao mbali mbali
za kijamii na kimaendeleo. Kwa hiyo tunaiomba Serikali katika muhula ujao
kupitia Tume ya Mipango tunaitaka Serikali kuhakikisha inampatia Makamo wa
Kwanza wa Rais Makaazi ya kudumu Unguja, Pemba na Dar-es Salaam, ili awe na
utulivu lakini vile vile kuokoa pesa za wananchi.
Mhe Spika,
Jukumu
jingine ambalo Afisi hii ya Makamo wa Kwanza ni usimamizi wa Mazingira, kama
nilivyoeleza hapo mwanzo miongoni mwa changamoto zilipo katika eneo hili la
uharibifu wa Mazingira kwa kweli hali yetu sio nzuri katika usimamizi wa jambo
hili, kwani ukizingatia nchi yetu ni visiwa lakini bado uelewa wa wananchi wengi
katika uhifadhi wa Mazingira hapa Zanzibar ni mdogo sana kwani ukiangalia
kuanzia katika miradi mikubwa mingi hapa Zanzibar huwa haifanyiwi tathmini ya
kimazingira kabla ya kuanzisha miradi hiyo jambo ambalo hasa katika fukwe zote
za Zanzibar kuna uharibifu mkubwa wa Mazingira na wakati mwingine sisi viongozi
ndio tunaowakingia vifua watu hao bila ya kujua kuwa tunaliangamiza taifa letu,
na waswahili wanamsemo wao kua hili gogo tulilokalia ndio tunalolikata yaani.(
VISIWA VYA UNGUJA NA PEMBA) hali hii kwa kweli inasikitisha sana kwani athari
kubwa tumeanza kuziona, leo hii tusije kushangaa siku moja tiamka Kisiwa cha Kisiwa
Panza kikiwa kimezama chote kwa maji ya Bahari.(Mwenyenzi Mungu atuepushie
mbali)
Mhe Spika,
Leo
hii wananchi wengi hasa katika kisiwa cha Pemba wameingia katika umaskini
mkubwa waliokua hawakuutarajia katika maisha yetu kwani yale maeneo waliyokua
wakilima mpunga na mazao mengine tangu enzi za mababu zetu hivi sasa yamevamiwa
na maji ya Bahari na hawawezi tena kuyatumia kwa ajili ya Kilimo, jambo ambalo
walikua kilimo wakikitegemea kwa chakula, kusomesha watoto wao, pamoja na mahitaji
mengine, hii yote inatokana na uharibifu wa mazingira hasa kwenye maeneo ya
fukwe unayofanywa na katika maeneo mengine. Kwa hiyo nitoe wito kwa sisi sote
tuungane katika kupiga vita uharibifu wa mazingira.
Mhe Spika,
Kutokana
na kuokoa muda nimetoa mfano mmoja tu katika uharibifu wa mazingira ambapo eneo
hili ndilo linaloongoza katika kuwatia umasikini watu wengi kwa hiyo nawaachia
wajumbe wengine ili waongelee maeneo mengine ya yenye uharibifu wa Mazingira.
Mhe Spika,
Pamoja
na hayo lakini kamati yangu tunatoa pongezi kwa Serikali kwa kusikia kilio
chetu cha muda mrefu kwenye eneo hili kwa kuleta Sheria itakayoanzisha taasisi
maalum itakayosimamia masuala ya mazingira tunaamini ikiweza kusimamia vizuri
Basi athari hiyo haitoweza kuendelea kua mbaya zaidi na kutoa miongozo ya
kudhibiti Pale palipokwisha kuharibika.
Mhe Spika,
Kamati
yangu inaipongeza Serikali kupitia Idara ya watu wenye Ulemavu kwa kazi nzuri
wanayoifanya ya kuratibu masuala yote yanayohusu watu wenye ulemavu na pia
kuweza kukamilisha Data base ya kuwatambua watu wote wenye ulemavu kwani hii
itasaidia kuwatambua ili kuweza kurahisisha upatakanaji wa mahitaji muhimu kwa
wakati ya watu hao, lakini pia nitoe pongezi maalum kwa mkurugenzi wa Idara hii
kwa kazi kubwa anayoifanya katika kupigania haki za watu wenye ulemavu, kwa
hiyo tunawaomba waendelee na utendaji wao bora , kwa hiyo natoa wito kwa
Mkurugenzi wa Idara hii kuanza mikakati ya kutafuta Wawakilishi na Wabunge wao
wenyewe watakaokuja kuwawakilisha katika chombo hiki cha Baraza la Wawakilihi
na Bunge ili kuja kutetea fursa, maslahi na huduma bora kwa kundi lao ndani ya
vyombo vya kutunga Sheria baada ya Katiba mpya kupitishwa. Pia tunawapongeza
kwa kuanzisha mfuko wa watu wenye ulemavu mfuko ambao utaweza kusaidia shughuli
zao mbali mbali za kujiongezea kipato na kuwaletea maendeleo.
Mhe Spika,
Kama
nilivyoeleza hapo mwanzo Waziri amekabidhiwa mambo mazito mingoni mwao ni
mapambano dhidi ya maradhi thakili yanayoangamiza wananchi wetu, yaani maradhi
ya ukimwi, tunampongeza Mkurugenzi wa Tume ya Ukimwi kwa kazi kubwa ya
kueleimisha jamii katika mapambano dhidi ya maradhi ya Ukimwi, lakini kamati
yangu inasikitika sana pale inaposikia kua washirika wa Maendeleo wameanza
kupunguza misaada yao katika mapambano dhidi ya Maradhi ya Ukimwi.
Kwa
hiyo kamati yangu inaitaka Serikali pamoja na kuongeza fungu katika mapambano
dhidi ya maradhi ya ukimwi lakini bado fungu hilo ni dogo halitoshi kwa
kulingana na gonjwa lenyewe, pia kamati yangu inawapongeza viongozi wa ZAPHA +
Kwa jitihada zao za kujikusanya na kuweza kutoa misaada mbali mbali kwa wale waliopata
maambukizi ya maradhi hayo pia na kwa wale ambao tayari wameathirika, kwani
bila ya jitihada zao basi hali ingelikua mbaya zaidi. Kutokana na elimu
wanayoendelea kuitoa kwa jamii basi hata hali ya unyanyapaa imepungua kwa kiasi
kikubwa ingawa bado kuna mnaeneo mengine unyanyapaa bado upo, kwa hiyo bado
jitihada ya kuwafikia watu katika maeneo hasa ya vijijini iendelee na kwa hiyo
iko haja kwa Serikali kuandaa utaratibu wa kuisaidia fungu la fedha ZAPHA+ hasa
baada ya hao wahisani kupunguza kwa kiasi kikubwa misaada kwa masuala ya
Ukimwi.
Mhe. Spika,
Kamati
yangu imeendelea kujadili na kutafakari kwa kina bajeti za Wizara tatu
inazozisimamia, ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais.
Kamati
yetu imepokea bajeti kwa Wizara zote hizo katika mfumo mpya wa Programu, ambao
unaitwa Program Based Budget (PBB). Mfumo huu kama ulivyokwisha elezwa na Mhe.
Waziri na kama Wajumbe wako walivyopata mafunzo yake kupitia Semina ya tarehe 14
-15 Mwezi huu, unatofautiana sana na ule tuliouzoea wa Line Budget, ambao
Wajumbe walikuwa wanajadili kifungu kwa kifungu, lakini sasa wanalazimika
kujadili Progamu kubwa na ndogo.
Mhe. Spika,
Pamoja
na kutolewa semina kwa Wajumbe wote tarehe 14 -15/05/2015, na pamoja na ukweli
kuwa mabadiliko haya yalianza kuelezwa na Wajumbe kupata maelezo yake takriban
miaka miwili nyuma, utakubaliana na mimi kuwa, kabla ya Kamati zetu kupitia
bajeti za Wizara husika, ama kabla ya Kamati ya Wenyeviti kupitia bajeti kuu ya
Serikali, ilipaswa kwanza Wajumbe wote wawe na uelewa mpana zaidi na hasa kwa
namna ulivyowasilishwa katika vitabu vya bajeti.
Kwa
hiyo kamati yangu inaenedelea kuitaka Serikali kwa kushirikiana na Afisi yetu
ya Baraza la Wawakilishi mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu kutoa mafunzo upya kwa
Wajumbe wako wa Baraza hili tukufu la Wawakilishi ili kuweza kuisimamia Bajeti
hii tunayoipitisha hapa Barazani.
Mhe. Spika,
Kamati
yangu ilifanya uchambuzi wa bajeti ya Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, pamoja
na kukosa elimu ya matendo kabla ya bajeti hiyo na imelazimika kujifunza haraka
sana wakati huo huo wa upitishaji wa bajeti. Katika kuipitia bajeti hiyo,
Kamati yangu itaizungumza Ofisi hii katika maeneo matatu makuu kama ifuatavyo:
OFISI YA MAKAMO WA KWANZA WA RAIS ZANZIBA
Mhe Spika,
Bado
Ofisi hii inaendelea na makusanyo ya mapato yake kupitia Idara ya Mazingira,
ambayo inategemea kupata mapato hayo kupitia ada ya hifadhi ya mazingira ambayo
kwa mwaka jana ilikadiriwa kukusanywa Tsh. 10,500,000,
na ilipofikia Machi 2015, Idara ilifanikiwa kukusanya Tsh. 8,700,000, sawa na asilimia 83 ya makadirio. Sasa Idara hii kwa
mwaka huu wa 2015/2016 imekadiriwa kukusanya Tsh. 23,100,000, kwa nyongeza ya Tsh. 12,600,000, ambayo ni sawa na asilimia 220 ya makadirio ya mwaka
uliopita, fedha ambayo kwa namna ambavyo haikuweza kukusanywa kamili kwa miaka
iliyopita ambapo Idara hii kwa mfano mwaka 2012/2013 ilikadiriwa kukusanya Tsh.
8,130,000 na ulipotimia mwaka iliweza
kukusanya Tsh. 7,618,000 sawa na
asilimia 94 ya makadirio. Ni wazi kuwa, kwa mwaka huu pamoja na ukweli kuwa
Idara na Wizara kwa ujumla wanategemea kupata mafanikio makubwa baada ya
kusainiwa kwa Sheria mpya ya Mazingira, bado kuna changamoto kubwa ya
kupatikana makusanyo kamili ya yaliyokadiriwa.
Mhe. Spika,
Ofisi
ya Makamo wa Kwanza wa Rais kupitia Idara ya Mazingira, imekisia kukusanya Tsh.
11,612,000 kupitia chanzo kipya cha
ada ya ukaguzi wa mazingira. Chanzo hiki kimeelezwa kwa Kamati kuwa kinatokana
na Sheria mpya ya usimamizi wa Mazingira ambayo itaipa Idara ya Mazingira
ruhusa kamili ya kukagua miradi ya mazingira na hivyo taasisi zinazohusika na
ukaguzi wa mazingira kupitia miradi yao mbali mbali, watatakiwa kufanyiwa
ukaguzi huo. Chanzo hiki kinaifanya Ofisi hii kuwa na dhima ya makusanyo ya
Tsh. 34,712,000.
Hata
hivyo, Kamati haina pingamizi na chanzo hicho wala kima kilichokisiwa
kukusanywa, kwani kula uhondo kwataka matendo na asiye na matendo hula uvundo.
Hivyo, hatupendi kuona fedha hizo zilizokadiriwa zinashindwa kukusanywa, mbali
na kuelezwa kwenye vitabu hivyi vya bajeti. Ni lazima Idara ya Mazingira kwa
muongozo wa Ofisi hii ya Makamo wa Kwanza wa Rais, ikajifanya juhudi kubwa
katika kukusanya fedha hizo, ili mwaka ujao iweze kupatiwa kima cha juu zaidi
katika makusanyo yake. Kamati yangu inaamini kua ikiwa Mamlaka hii ya usimamizi
wa itafanya kazi yake ipasavyo basi watakusanya zaidi ya kiwango hicho
kilichowekwa kwani kuna adhabu nyingi kwa wale watakao kiuka sheria na kukiuka
sheria ya Mazingira jambo ambalo limekua ni utamaduni wa wazanzibari pamoja na
wawekezaji kukiuka kwa makusudi taratibu za uhifadhi wa mazingira.
Mhe. Spika,
Ofisi
hii sasa inatambuliwa matumizi yake kupitia fungu kuu la B01, ambapo jumla ya
fedha zinazohitajika kwa matumizi ya kazi za kawaida ni Tsh. Bil, 2,923,400,000 na fedha zinazohitajika
kwa matumizi ya maendeleo ni Tsh. 450,000,000.
Fedha hizo zinatarajiwa kutumika kwa program kuu tatu na program ndogo sita
kama ifuatavyo:
Programu
Kuu ya Usimamizi wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, yenye program ndogo
mbili ambazo ni Usimamizi wa Mazingira na Usimamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi.
Programu
Kuu ya Pili ni Usimamizi wa Masuala ya Watu wenye Ulemavu ambayo ina program
ndogo moja ya Usimamizi wa Masuala ya Watu wenye Ulemavu, na
Program
Kuu ya Tatu ni Mipango na Utawala yenye program ndogo tatu ambazo ni Uongozi na
Utawala, Mipango, Sera na Utafiti na Uratibu wa masuala ya Ofisi ya Makamo wa
Kwanza wa Rais, Pemba.
Mhe. Spika,
Program
Kuu zote hizi zimeelezwa huduma zake zinazotarajiwa kutolewa pamoja na
viashiria vya mafanikio yanayotarajiwa kufikiwa kwa mwaka wa 2015/2016. Aidha,
kwa program ndogo ya Usimamizi wa Mazingira inatarajiwa kutumia Tsh. 174,076,000 ambapo Tsh. 161,376,000 zinatarajiwa kutumika kwa
kuendeleza mazingira endelevu kwa jamii na Tsh. 12,700,000 zitatumika kwa kukuza uelewa wa kimazingira kwa jaimii.
Mhe. Spika,
Jumla
ya Tsh. 155,460,000 zinahitajika kwa
matumizi ya Tsh. 73,060,000
zinazotarajiwa kutumiwa kwa ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu, Tsh. 2,400,000 zinahitaji kwa kukuza uelewa
wa jamii juu ya masuala ya watu wenye ulemavu, huku Tsh. 80,000,000 zikihitajika
kwa uwezeshaji wa watu wenye ulemavu.
Mhe. Spika,
Kamati
yetu pia iliridhika kwa Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais kuidhinishiwa Tsh. 2,593,864,000 kwa Tsh. 2,051,997,000 kutumika kwa kuimarisha
ufanisi wa utendaji kazi na uongozi, kusaidia jamii katika kazi za maendeleo na
kuongeza uelewa wa jamii juu ya masuala yanyaosimamiwa na Ofisi ya Makamo wa
Kwanza wa Rais.
Mhe. Spika,
Kamati
imeelezwa na kuridhika kuwa Tsh. 53,744,000
zitumike kwa kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa taarifa na kuzisambaza kwa wadau,
Tsh. 17,527,000 zitumike kwa
kuratibu masuala mtambuka yanayosimamiwa na Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais,
huku utayarishaji wa sera na mipango ya maendeleo utumie Tsh. 22,448,000.
Mhe. Spika,
Program
ndogo ya uratibu wa masuala ya Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Pemba
unahitaji fedha za kutosha, hali iliyoifanya Kamati yangu kuridhishwa na
kuidhinishwa matumizi ya Tsh. 448,148,000
ambapo jumla ya Tsh. 426,480,000
zitumike kwa kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi na uongozi na Tsh. 21,668,000 zitumike kwa kuratibu,
kufuatilia na kukuza mashirikiano kwa masuala ya Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa
Rais, kisiwani Pemba.
Mhe. Spika,
Jumla
ya Tsh. 450,000,000 zimekadiriwa na
Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais kwa miradi ya maendeleo chini ya program ya
Usimamizi wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, ambapo program hii kubwa
chini ya program ndogo ya Usimamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi inakusudiwa kuratibu
na kusimamia masuala ya mabadiliko ya tabianchi ambapo kazi kuu ni kutayarisha
nyenzo na mipango ya usimamizi, kuratibu mikutano ya ya usimamizi, kujenga
uwezo wa wadau na kukuza uelewa juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja
na kuzisaidia jamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko hayo.
Mhe. Spika,
Fedha
hizo za maendeleo zinazoombwa zitasimamiwa na Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais
chini ya Idara ya Mazingira , Wizara ya Kilimo na Maliasili kupitia Idara ya
Misitu na Maliasili zisizorejesheka, kwa mfano kuna Tsh. 37,000,000 zimekadiriwa kutumiwa kwa kuimarisha mazingira wezeshi
kwa kuongeza matumizi mbadala ya misitu Zanzibar. Aidha, utekelezaji wa program
ndogo hii ya Usimamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi utafanywa kwa mashirikiano na
Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji
na Nishati kupitia Idara ya Nishati na Madini na Jumuiya ya CODECOZ na
kuratibiwa na Idara ya Mipango, Sera na Utafiti.
Mhe. Spika,
Fedha
zote hizo Tsh. 450,000,000
zinakadiriwa kupatikana kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ambao ni UNDP huku
fedha hizo ama zikiwa ni ruzuku ya nje na fedha za ndani. Aidha, pamoja na
ukweli kuwa, katika vitabu vya bajeti vilivyowasilishwa kwa Kamati, Serikali
haikuonekana kuchangia fedha yoyote, imeelezwa na Mhe. Waziri kupitia ripoti
yake kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajiwa kuchangia Tsh. 174,076,000 kwa ajili ya utekelezaji wa
program hii. Kwa hiyo katika eneo hili
kamati yangu inaomba ufafanuzi mpaka kufikia sasa jee iyo fedha kwa upande wa
Serikali jee zimeshaingizwa?
TUME YA KITAIFA YA KURATIBU NA UDHIBITI WA DAWA ZA
KULEVYA ZANZIBAR
Mhe. Spika,
Tume
ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar inakadiriwa
kutumia Tsh. 166,091,000 kwa ajili
ya mishahara, Tsh. 134,680,000 kwa
matumizi ya maposho na Tsh. 166,329,000
zitatumika kwa matumizi ya uendeshaji wa Ofisi, na hivyo kwa pamoja fedha
zinazoombwa ili ziidhinishwe na Baraza hili ni Tsh. 467,100,000. Fedha zote hizo zimeombwa chini ya program kuu mbili,
Programu ya Dawa za Kulevya yenye program ndogo mbili ya Udhibiti wa
usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya na program ndogo ya Kinga ya
Msingi ya Mahitaji ya Dawa za Kulevya. Na program kuu ya pili ni Utawala na
Uendeshaji wa Tume ya Dawa za Kulevya ambayo program yake ndogo ni hiyo hiyo ya
Utawala na Uendeshaji wa Tume ya Dawa za Kulevya.
Mhe. Spika,
Bado
tukumbuke kuwa, Zanzibar imeendelea kuwa sehemu hatarishi ya Uingizaji na
Usambazaji wa dawa za kulevya. Vijana wetu wanaendelea kuathirika na matumizi
haya ya dawa za kulevya hali inayolipelekea Taifa hili kukosa nguvu kazi na
kurudi nyuma kimaendeleo. Hivyo, ili kukabiliana na tatizo sugu la dawa za
kulevya, Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais kupitia Tume hii imeweka program
ndogo ya kudhibiti usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya Zanzibar,
ambapo jumla ya Tsh. 30,908,000
zinahitajika kwa kudhibiti uingizaji na usafirishaji wa dawa za kulevya na Tsh.
26,906,000 zinahitajika kwa kuzuia
usambazaji wa dawa za kulevya.
Mhe. Spika,
Pamoja
na kima hicho kilichotengwa kwa shughuli hizo za udhibiti na usambazaji wa dawa
za kulevya, ilivyokuwa malalamiko makubwa ya wananchi dhidi ya matumizi ya
madawa ya kulevya yanalegwa katika uingizwaji na usambazaji wa dawa hizo kwa
watumiaji mbali mbali na kwa kuzingatia ukweli kuwa Serikali hufanikiwa zaidi
kuwashughulikia watumiaji kuliko waletaji na wauzaji wa dawa hizo, fedha
zilizotengwa katika kutekeleza porgramu ndogo hii ni chache sana na inaonesha
bado Serikali kwa ujumla inahitajika iwe makini sana na jukumu hili zito ambalo
ndio chanzo cha kuenea matumizi ya madawa ya kulevya Zanzibar.
Mhe. Spika,
Jumla
ya Tsh. 376,036,000 zinahitajika kwa
program ya Utawala na Uendeshaji wa Tume ya Dawa za Kulevya kwa kujenga uwezo
wa wafanyakazi katika uratibu wa mapambano ya Dawa za Kulevya ambapo jumla ya
Tsh. 304,690,000 zinahitajika na kwa ajili ya Uratibu wa Shughuli Tume ya Dawa
za Kulevya Pemba, fedha zinazohitajika ni Tsh. 71,346,000. Aidha, kwa ujumla utekelezaji wa program ya Udhibiti wa
Dawa za Kulevya unaoratibiwa na Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa
za Kulevya unakadiriwa kutumia Tsh. 91,064,000/-.
TUME YA UKIMWI ZANZIBAR
Mhe. Spika,
Kwa
mwaka wa fedha 2015/2016, Tume ya Ukimwi inahitaji kupatiwa Tsh. Bil. 1,703,600,000, ambazo fedha
zitakazotumika kwa kazi za kawaida ni Tsh. Mil. 721,200,000 na fedha za maendeleo ni Tsh. Mil 982,400,000. Fedha hizo zinatarajiwa kutumika chini ya program kuu
mbili, program ya Kuratibu Muitiko wa Taifa wa Ukimwi ina program ndogo mbili
ya Mawasiliano na utetezi wa masuala ya Ukimwi na Uratibu wa muitiko wa Taifa
wa Ukimwi, na program kuu ya pili ni Utawala na Uendeshaji wa Tume ya Ukimwi
ambayo program yake ndogo ni Utumishi na Uendeshaji wa Tume ya Ukimwi.
Mhe. Spika,
Ofisi
ya Makamo wa Kwanza wa Rais kupitia Tume ya Ukimwi, imeahidi mbele ya Kamati
kuwa, kwa kutekeleza program zote mbili na program ndogo zilizomo, itakapofika June
30 ya mwaka 2016, itakuwa imeshatekeleza mambo yafuatayo:
·
Imezifikia Shehia 20
kwa maonesho.
·
Imefanya program 150
za jamii kwa makundi maalum.
·
Imewafikia watu 1400
wa makundi maalum.
·
Imechapisha na
kusambaza vipeperushi, vijarida 5000 kwa walengwa.
·
Imetoa vipindi 36 vya
redio na TV.
·
Imehamasisha mikoa
mitano kwa kuitaka kuchukua hatua za kupunguza mazingira hatarishi ya Ukimwi.
·
Imetoa mikutano 16 ya
kuziratibu taasisi zinazotekeleza shughuli za utetezi na uhamasishaji wa
masuala ya ukimwi.
·
Imezijengea uwezo
taasisi 30 zinazojishughulisha na masuala ya Ukimwi, na
·
Imetoa asilimia 100 ya
fedha kwa utekelezaji wa program za maisha na afya ya uzazi kwa vijana nje ya
Skuli.
Mhe. Spika,
Inatarajiwa
sana kwa Serikali sikivu kuwa mbali na kusema maneno na kuacha wananchi wake
watende matendo. Serikali sikivu siku zote hutenda matendo na kuwaacha wananchi
wake na watu wengine kusema maneno. Hii ni kwa sababu, tendo hukidhi haja
maridhawa kuliko neno. Na haja ikishughulikiwa kwa matendo hupatikana upesi,
lakini ikishughulikiwa kwa maneno, huchelewa kama sadaka.
Mhe. Spika,
Kwa
muda mrefu Serikali yetu husema maneno ikiwa ni pamoja na haja ya kuleta
mabadiliko ya mfumo wa bajeti katika kipaumbele cha program za kila Taasisi
zake, na kuwaacha wananchi wake waje waipime na kuzipima taasisi hizo katika
utekelezaji wa program hizo na viashiria vyake, leo tunaisifu kwa kutendo
matendo ya waliyouyasema muda mrefu wa nyuma. Hata hivyo, hatua hii bado
haijakidhi shida ya maneno ya wananchi na dhiki kubwa inayoipa taasisi zake,
nayo ni kupatiwa na kuingiziwa fedha kamili za matumizi kama vile
yalivyokadiriwa na Baraza hili katika mikutano mbali mbali ya bajeti.
Mhe. Spika,
Serikali
yetu pamoja na ahadi nyingi za mfumo huu mpya wa bajeti, iwapo tutashindwa
kukushanya kama tulivyopanga na ikiwa itaacha kufanya matendo ya kuziingiza
fedha inazoahidi leo na katika kikao hiki cha bajeti kwa Wizara na taasisi
zake, itaendelea zaidi kutoa mzigo mzito kwa Taasisi hizo na hatimae kwa
wananchi.
Mhe Spika,
kwa upande wa mambo ya kiujula naomba kuishauri Serikali kuangalia matatizo
yanayowakabili hasa wananchi katika kisiwa cha Pemba kwa kuvamiwa na maji ya
Bahari kwenye maeneo yao ya kilimo ambayo wanayategemea kwa kuendeshea maisha
yao, kwa hiyo uvamizi huo umewaacha wananchi hao katika umasikini mkubwa kwani
hawana njia nyingine yeyote ya kuendeshea maisha yao, kwa hiyo ni lazima
Serikali kuandaa mradi maalum kwa kuyahami maeneo hayo ambayo kila siku
yanaongezeka bila ya kuweka utaratibu basi umasikini utakua unaongezeka siku
hadi siku na baadae utakua ni mzigo mkubwa kwa Serikali yetu.
Mhe. Spika,
Mwisho
kabisa wa hotuba yangu hii fupi, naomba nitoe shukurani zangu za dhati kwako
wewe na Waheshimiwa Wajumbe wote, bila ya kuwasahau Wajumbe wa Kamati yangu na Makatibu
Kamati. Aidha, naomba ruhusa yako niendelee kuwatambua kama ifuatavyo:
1.
Mhe Hamza Hassan Juma
Mwenyekiti
2. Mhe. Saleh Nassor Juma Makamo Mwenyekiti
3. Mhe. Ali Mzee Ali Mjumbe
4. Mhe. Ashura Sharif Ali Mjumbe
5. Mhe.Shadya Mohammed Suleiman Mjumbe
6. Mhe. Makame Mshimba Mbarouk Mjumbe
7. Mhe. Subeit Khamis Faki Mjumbe
8. Ndg.Rahma Kombo Mgeni Katibu Kamati
9. Ndg.Othman
Ali Haji Katibu Kamati
Mhe. Spika,
Naendelea
kumshukuru Mhe. Waziri, Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Katibu Mkuu wa Ofisi
hii na watendaji wake wote kwa mashirikiano mema waliyoipatia Kamati kwa muda
wote wa uhai wa Kamati yetu.
Mhe. Spika,
Kama
sitakosea kutoa nasaha zangu kwa Katibu Mkuu na watendaji wake, huku nikijua
kuwa sisi viongozi wa siasa huongoza Taasisi hizi kwa muda na wao ni waajiriwa
wa kudumu, niendelee kuwaeleza kuwa, wao ndio roho ya Ofisi hii ya Makamo wa
Kwanza wa Rais. Kutekeleza kwao kwa majukumu yao kwa kuzingatia Katiba na
Sheria ni matarajio makubwa sana ya wananchi wa nchi hii. Aidha, wao ni
wataalamu na ni wajuzi wa mambo mbali mbali, lakini wenye dhamana ya kuwaletea
maendeleo na kuimarisha ustawi wa wananchi wa Zanzibar kupitia Ofisi yao hii.
Mhe. Spika,
Tunaendelea
kuwanasihi watendaji hawa waendelee kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu
mkubwa. Dhamana hii waliyonayo ni mzigo mzito mbele ya Muumbaji wao. Kutekeleza
kwao kwa majukumu yao, kusishawishike na tamaa ya mali, kwani mioyo mingi
haitoshwi na mali. Walakini, kwa kweli fikira ya mali isiyo kadiri, ni mzigo
usiochukulika.
Mhe. Spika,
Sasa
niwaombe Waheshimiwa Wajumbe watumie vipawa vyao na uwezo wao mkubwa katika
kuijadili bajeti ya Ofisi hii. Watumie elimu na uzoefu wao walioupata katika
miaka yote mitano ya uhai wao na uhai wa Baraza hili la Nane, huku wakijua
kuwa, zaidi ya nusu ya hasara za wanaadamu hutokea kwa sababu wenyewe hawataki
kutumia vipawa vyote walivyopewa. Tusipotumia vipawa na elimu tuliyopewa katika
kujadili na kuchambua bajeti kama hii, ambapo ndio moja kati ya majukumu manne
makuu yaliyoelezwa na kifungu cha 88 cha Katiba ya Zanzibar, tutawanyima sana
wananchi wetu waliotutuma kuwawakilisha katika chombo hiki, haki yao ya
uwakilishi bora. Kwahiyo, tuijadili kwa busara na upeo wa elimu na juhudi zetu
kwa kutoa michango kwa lengo la kuiboresha.
Mhe. Spika,
Naomba
kuwasilisha.
............................
Hamza
Hassan Juma,
Mwenyekiti,
Kamati
ya Kusimamia Afisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa,
Baraza
la Wawakilishi,
Zanzibar.
No comments:
Post a Comment