Hassan Khamis, Pemba
WATU wawili mama na mwanawe wa kike (14), wamefariki dunia na mmoja kuokolewa, baada ya kuzama baharini, wakati walipokua wakivua chaza, kwenye bahari ya Mtambwe Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Kamishna msaidizi wa Polisi Sheikhan Mohamed Sheikhani amethitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema lilitokea majira ya saa 5:00 asubuhi.
Alisema tukio hilo lilitokea juzi Mei 1, mwaka huu katika bahari ya Kidundo Mtambwe katika eneo linalofahamika kwa jina la Dundani Mtambwe ambapo ndipo wanawake wawili walipofariki dunia.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Mrisho Othman Juma (35) ambae ni mama mzazi wa mtoto Saada Omar Haji (14) wote wakaazi wa Chekea Mtambwe, ambapo aliyeokolewa ni Siti Othman Hassan (30) nae mkaazi wa Chekea.
Alifafanua siku hiyo ya tukio majira ya saa 3:00 asubuhi bibi Mrisho akiwa na mwanawe Saada waliondoka nyumbani kwao wakiwa wamefuatana na Siti Othman, kwa lengo la kwenda baharini kuvua chaza ambapo wakati huo maji yamekupwa (kutoka).
Kamanda Sheikhan alisema wakati wavuvi hao wakiendelea kuvua, ghafla mtoto Saada aliteleza na kuanguka kwenye mto mdogo wa bahari, uliokua karibu yao ambapo baada ya tukio hilo, mama mzazi (bi Mrisho) aliamua kumuuokoa mwanawe kwa kujaribu kumpa mkono ili kutaka kumvuta.
“Huyu mama alifanya wajibu wake ili kutaka kumuokoa mwanawe (Saada) ingawa kwa bahati mbaya mama huyo nae alianguka na kutumbukia katika mto huo na kuanza kusombwa na maji, na ndipo Siti Othaman alipoanza kupiga kelele za kuomba msaada”,alifafanua.
Baada ya muda walifika wavuvi wa samaki wakiwa na vidau na kufanikiwa kuuokoa mwili wa Mrisho Othman akiwa ameshafariki na baada ya muda wa takriban saa moja nao mwili wa Saada ulionekana akiwa ameshafariki tayari wakati huo Siti akiwa amepata mshituko na alichukuliwa hadi ufukweni.
Hata hivyo Kamanda huyo ametoa wito kwa wavuvi kuwa na tahadhari wakati wanapokwenda kwenye shughuli zao mbali mbali zikiwemo za uvuvi ili kuepusha maafa.
Daktari Mohamed Nassor wa hospitali ya Wet, ambae ameufanya uchunguzi wa miili ya marehemu hao amesema wamefariki baada ya kunywa maji mengi na kukosa msaada wa haraka ingawa alieokolewa ametibiwa na kuruhusiwa.
No comments:
Post a Comment