Habari za Punde

MAITI MOJA YAPATIKANA..........BADO 2

 MAITI ya marehemu Ali Mbarouk (55) mkaazi wa Mitamani wilaya ya Chake Chake Pemba, ikiizingizwa hospitali ya Chake Chake kwa ajili ya kufanyiwa uchunguuzi, akiwa ni miongoni mwa wavuvi watatu ambao walipotea juzi baada ya chombo chao kupigwa na doruba kwenye kisiwa cha Misali na hadi jana wenzake wawili hawajaonekana
Na Haji Nassor, Pemba                    
HATIMAE mvuvi mmoja kati ya watatu waliohofiwa kufa maji baada ya wenzao watano kuokolewa wakiwa hai, ameonekana jana akiwa ameshafariki dunia, eneo la bahari ya    Mkubuu wilaya ya Chake chake.
Marehemu huyo alitambulika kwa jina la Ali Mbaruok mkaazi wa Mitamani, akikisiwa kuwa na umri wa miaka (54), ambapo wenzake wawili, wanaohifiwa kwamba wameshafariki dunia, na hadi jana majira ya saa 8:40 jioni, wakiwa hawajaonekana ni Omar Najim mkaazi wa Gombani na Rashid Zahoro mkaazi wa mkoroshoni wote Wilaya ya Chake chake Pemba.
Wavuvi watano, kati ya nane waliookolewa baada ya kutokezea dhahma hiyo ni Abdalla Ameir Khami (22), mtoto Omar Haji Ali (16), Rashid Salim Abeid (38), Mbarouk Mohamed Mbarouk (65) Hadi Ahmed Nassor wote wakaazi wa mji wa Chake chake, ingawa aliebakia hospitali ni Rashid Salim pekee akiendelea na matibabu.
Taairifa zinaeleza kuwa wavuvi hao, waliondoka bandari ya Wesha majira ya asubuhi, kwa ajili ya kwenda kwenye kazi yao ya uvuvi, ingawa walipokaribia kwenye kisiwa cha Misali walipigwa na wimbi kali na kusababisha maji kuingia ndani.
Ilifahamika kuwa baada ya kutokezea hali hiyo, siuntafahamu kwa wavuvi hao waliosadikiwa kuwa na boti aina ya ‘fiber’ iliwakumba na wapo waliofanikiwa kupata vitu vinavyoelea hadi walipofanikiwa kuokolewa na kufikishwa hospitali.
Daktari dhama wa hospitali ya Chake chake dk, Yussuf Hamad Idd alithibitisha kuupokea mwili wa marehemu huyo jana majira ya saa 5:55 na kuufanyia uchunguuzi ingawa ulionekana na michubuko baadhi ya sehemu za mweili wake.
Aidha alisema juzi majira ya saa 10:00 jioni aliwapokea majeruhi wanne na kuwapa matibabu ingawa watatu baada ya kutibiwa waliruhusiwa.
Daktari huyo alisema walilazimika kuwaruhusa majeruhi hao kutokana na hali zao kuendelea vyema na hasa kwa vile hawakupata madhara yoyote, isipokuwa Rashid aliepata michubuko sehumu za tumboni.
“Unajua kwa mujibu wa mwenyewe alisema baada ya kutokezea dhoruba hiyo, alimwagikiwa na mafuta ya petrol na ndio maana akapata michubuko kwenye tumbo, lakini anaendelea vyema’’,alifafanua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa kusini Pemba Juma Yussuf Ali alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kusema lilitokea baina majira ya 6:30 mchana na 7:00 kwenye bahari ya kisiwa cha Misali.
Alisema baada ya kupokea taarifa hizo, Jeshi hilo likisaidiana na vikosi vyengine lilifika eneo la tukio na kuanza zoezi la kuwatafuta wavuvi watatu, ingawa hadi juzi (Mei, 2) hawakufanikiwa kuwapata.
“Unajua tulianza kuwatafuta hadi usiku ukatuingilia ingawa kwa juzi hatukufanikiwa kuwaona wavuvi hao na zoezi hilo likaendelea tena (Mei 3) na kufanikiwa kuupata mwili wa marehemu Ali Mbarouk’’,alifafanua.
Mara baada ya kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba Mhe: Mwanajuma Majid Abdalla viongozi mbali mbali chama na serikali walifika hospitali ya Chake chake na kuwafariji majeruhi wa tukio hilo.

Hili ni wastani wa tukio la nne kutokea kwa mwaka huu, kwa Mkoa wa kusini Pemba kwa watu kufa baharini, ambapo la wiki iliopita ni la mpagazi aliefariki baada ya kujirusha kutoka melini na kujaribu kuogolea kurudi gatini ingawa alifariki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.