Habari za Punde

Mawaziri wa Nishati wajadili kuhusu nishati endelevu kwa wote

  Sehemu  ya Wajumbe wa Mkutano wa Mawaziri kuhusu nishati,  mkutano ambao ulifunguliwa na   Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw.  Jan Eliasson siku ya  Jumatano.
Naibu Waziri wa Nishati  na Madini, Mhe. Charles Kitwanga akiwa katika Ukumbi wa Mikutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, unapofanyika mkutano wa Mawaziri wa Nishati kutoka  mataifa mbalimbali duniani, mkutano ambao pia unawashirikisha wadau na wataalamu    wanaohusika  sekta ya  nishati.

Na  Mwandishi Maalum, New York

Naibu  Waziri wa  Nishati na  Madini,  Mhe.Charles   Kitwanga ( Mb),  ni  miongoni mwa  mawaziri kutoka  mataifa mbalimbali duniani wanaohudhuria mkutano wa kila mwaka   kuhusu Nishati Endelevu kwa Wote  (SE4All)

Mkutano huu  unafanyika  hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,  ambao siku ya   jumatano mawaziri  wameanza kujadili na kubadilisha uzefu kuhusu eneo hilo la nishati ambalo  linaelezwa kuwa ni muhimu kwa maendeleo endelevu   kijamii,  kiuchumi na  mazingira .

Mhe. Kitwanga  ambaye  anatarajiwa  kuelezea  msimamo wa Tanzania katika eneo hili la nishati  endelevu siku ya alhamisi ( leo). Ameambatana na   Kaimu Katibu  Mkuu,  Bw. Ngosi Mwihava pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Madini.

Akifungua  mkutano wa  Mawaziri,  Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliasson, amesema  mkutano huo wa mawaziri na ambao ulitanguliwa na  mijadala mbalimbali iliyofanyika nje na Makao Makuu,  kuwa Mawaziri hao wanakutana katika wakati muafaka na hasa kwa kuzingatia kwamba mwaka huu wa 2015 ni  muhimu sana kwa Umoja wa Mataifa na Nchi wanachama.

 Akasema ,   viongozi wa dunia wametambua kwamba,  njia sahihi ya kufikia mafanikio ya pamoja   sasa na baadaye ni kuwa na  uwiano  uliosawa kiuchumi, kijamii na  kimazingira.


Naibu  Katibu Mkuu,  ameongeza kuwa kwa  muda mrefu,  jumuiya ya kimataifa imekuwa ikifuata njia za ukuaji wa pamoja pasipo  kuheshimu mipaka   baina ya   mazingira ya dunia na  haja  ya kuishi kwa kuzingatia uwiano bora na viumbe wengine.

 Na kwa sababu hiyo,  Bw. Jan Eliasson amewaeleza  Mawaziri hao na wadau wengine  wanaoshiriki mkutano huu kuwa,    mwaka huu Jumuiya ya Kimataifa itakuwa na  mikutano mitatu muhimu na ambayo itatoa mwelekeo mpya  na ajenda mpya  kuhusu maendeleo endelevu kwa wote.

Ameitaja mkutano hiyo mitatu na muhimu kuwa ni , Mkutano  utakaofanyika mwezi Julai Addis Ababa, Ethiopia, mkutano  ambao dhumuni lake kuu  litakuwa ni  kujadili na kukubaliana kuhusu mfumo wa fedha  kwaajili ya  utekelezaji wa maendeleo endelevu.

Mkutano wa pili  ambao ameutaja  ni ule utakofanyika mwezi Septemba hapa  New York, mkutano ambao Wakuu wa Nchi na Serikali watapitisha ajenda na malengo ya  Maendeleo Endelevu baada ya 2015.

Aidha  mkutano wa tatu ni ule utakaofanyika Jijini  Paris, Ufaransa mwezi Desemba,  ambapo makubaliano yanatarajiwa kufikia kuhusu  mabadiliko ya Tabia  Nchi.

Akizungumzia kuhusu nishati endelevu, Naibu Katibu Mkuu, ameeleza kwamba Nishati endelevu ndio msingi  mkuu wa maendeleo na mageuzi katika sekta zote ziwe za viwanda,  kilimo au ustawi wa jamiii na kuongeza  kuwa katika dunia ya sasa ambayo inakabiliwa na changamoto nyingi,  ufumbuzi wa changamoto hizo unahitaji ushirikiano wa pamoja  baina ya  serikali,  sekta binfasi na makundi mengine ya kijamii

Akasisitiza kuwa  mpango  kuhusu nishati endelevu kwa wote, umeonyesha kwamba ushirikiano  miongoni  wa wadau mbalimbali umeweza kusaidia  kusukuma mbele ajenda hiyo ya   nishati endelevu kwa wote.

Ameongeza kuwa  kizazi kijacho kitakichangaa kizazi cha  sasa kwa kutoweka mipango madhubuti kwaajili yao.

Naibu  Katibu Mkuu wa Umoja wa  Taifa akabainisha pia kwamba,   Nchi zaidi ya 80 zinazoendelea zimejiunga mpango huo wa nishati endelevu kwa wote. Na kwamba  Ahadi zenye thamani ya mabilioni ya dola tayari zimepatikana.


Ripoti  kuhusu kuhusu mchakato wa kuelekea nishati endelevu  ambayo ilitolewa kwa washiriki wa mkutano huo   Mei 18,  inaonyesha kwamba watu  1.1 bilioni duniani kote wanaishi bila nishati ya umeme.  Huku  karibu  wengine  3 bilioni wakiendelea kupika  kwa  kutumia    nishati  ambazo si salama kwao na  mazingira, nishati hizo ni pamoja na  mkaa, kuni,  mafuta ya  taa na  samadi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.