Habari za Punde

Uzinduzi wa Baraza Jipya la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Fatma Abdulhabib Ferej akizindua Baraza jipya la Taifa la Watu wenye Ulemavu katika Ofisi ya Elime Mbadala Rahaleo, (kulia) Katibu Mkuu katika Ofisi hiyo Omar Dadi Shajak na (kushoto) Mwenyekiti wa Baraza hilo Haidar Hasham Madoeya.
Waziri Fatma Ferej akimkabidhi cheti Mjumbe aliemaliza muda wa kulitumika Baraza hilo Nd. Salah wakati wa uzinduzi wa Baraza jipya.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar Ndg.Haidar Hassham Madoeya akitoa hutuba yake baada ya uzinduzi wa Baraza hilo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Mhe Fatma Abdulhabib Ferej, akiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya Viongozi Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar.(Picha na Ramadhani Ali Maelezo)

Na Ramadhani Ali /Maelezo Zanzibar.
Familia zenye watu wenye ulemavu zimeshauriwa kutovifumbia macho vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji na kuacha tabia ya kuyatatua matatizo hayo kienyeji ili kukomesha vitendo hivyo vilivyokithiri hivi sasa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Mh. Fatma Abdulhabib Ferej ametoa wito huo wakati akizindua Baraza jipya la Taifa la Watu wenye Ulemavu katika jengo la Elimu Mbadala Rahaleo.

Amesema vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa Watu wenye Ulemavu vimekuwa vikiongezeka kwa kasi hivyo aliliagiza Baraza  kusimamia suala hilo na kuwapeleka katika vyombo vya sheria watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar amezishauri Jumuiya za Watu wenye Ulemavu na jamii kwa ujumla kusaidia kutoa elimu juu ya udhalilishaji wa Watu wenye Ulemavu ili kuhakikisha vitendo hivyo vinaondoka.

Amelipongeza Baraza lililomaliza muda wake kwa kazi nzuri iliyofanya na kulitaka Baraza jipya kuziangalia  changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu na kuzipatia ufumbuzi unaofaa.

“Baadhi ya changamoto ambazo ningependa muzifanyie kazi ni huduma za afya, matunzo, elimu, mafunzo ya awali, makaazi, ajira binafsi na usafiri,”alieleza Waziri Fatma.

Katika kutekeleza majiku yake, ameliagiza Baraza kurekebesha Sheria Namba 9 ya mwaka 2006 ili kusaidia kufanikisha utekelezaji mzuri wa sheria hiyo utakaoenda sambamba na Mkataba wa Kimataifa na Haki za Watu wenye Ulemavu.

Aidha amelitaka kutoa ushauri unaofaa kwa Serikali ili maendeleo ya Watu wenye Ulemavu yapatikane kwani itasaidia kukumbusha na kutoa mwamko utekelezaji wa sheria.

Mwenyekiti mpya wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Haidar Hasham Madoeya ameahidi watafanyakazi kwa bidii na uweledi kwa mashirikiano makubwa na Taasisi zenye kutoa huduma kwa Watu wenye Ulemavu ili kufikia malengo ya kuwapatia maendeleo endelevu wahusika.

Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar linaundwa na baadhi ya wajumbe kutoka  Jumuiya za watu wenye ulemavu na Makatibu wakuu wa Wizara ya Afya, Elimu, Ustawi wa jamii na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais pamoja na Chama cha Waajiri na Shirikisho la Wafanyakazi.                                                 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.