STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 7 Juni, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Idadi ya watalii kutoka Ujerumani na nchi za Ulaya wanaotembelea Zanzibar inatarajiwa kuongezeka kufuatia jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kuitangaza Zanzibar katika masoko ya utalii ulimwenguni.
Akizungumza katika mahojiano maalum na waandishi habari mjini Wurzburg, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohmed Shein alisema mbali ya kutangaza vivutio vya utalii Serikali inaongeza nguvu katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya utalii nchini.
Dk. Shein alisema kuwa utalii mbali ya kuchangia katika pato la taifa lakini ni sekta ambayo inaimarisha uhusiano, urafiki na na ushirikiano baina ya watu wa mataifa mbalimbali kama ambavyo Tamasha la Muziki na Utamaduni wa Afrika linalofanyika mjini hapa.
Aliwaambia waandishi hao kuwa Zanzibar ina sifa ya pekee ulimwenguni na kufafanua kuwa visiwa hivyo sio tu kuwa ni maarufu kwa historia yake bali pia sifa za utamaduni, silka na mila za watu wake.
Alitoa mfano kuwa wageni wengi wanaofika Zanzibar wanavutiwa na ukarimu wa watu wake, mila na desturi za watu wake ikiwemo vyakula ambavyo ni nadra kupatikana katika sehemu nyingine za duniani.
Aliongeza kuwa hata muziki wa visiwa hivyo ni kitu kinachowavutia sana wageni ambapo mbali kuwa ni burudani lakini pia unawaunganisha watu wa mataifa mbalimbali na kuimrisha urafiki wao.
Alibainisha kuwa ni jambo la kufurahisha kuona wananchi kutoka Ujerumani wanatembelea sana Zanzibar na Tanzania kwa jumla hivyo matuaini yake kuwa ushiriki wa Zanzibar katika Tamasha la Muziki wa Afrika mwaka 2015 litatoa hamasa kwa wageni wengi zaidi kutembelea Zanzibar.
Hata hivyo alisema ushiriki wa Zanzibar katika tamasha hilo ni mwanzo tu wa hatua nyingi ambazo serikali imepanga kuchukua kuongeza kasi ya kuitangaza Zanzibar ikiwemo kuangalia namna bora zaidi Znzibar inaweza kufaidika kutangaza vivuio vyake vya utalii kupitia tamasha hilo.
Katika mahojiano hayo Dk. Shein alitaja baadhi ya changamoto zinazioikabili sekta ya utalii kuwa ni pamoja na miundombinu ya utalii hasa idadi ndogo ya hoteli za madaraja ya juu isiyolingana na mahitaji ya utekelezaji wa malengo ya sekta hiyo.
Sambamba na kuimarisha miundombinu katika sekta hiyo, Dk. Shein alisema suala la amani na utulivu ni moja ya vipaumbele vya serikali ili kuhakikisha wakati wote kunakuwepo na utulivu kwa wageni na wenyeji.
Katika ziara yake nchini humu hapo juzi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitembelea idara ya magonjwa ya tropiki katika hospitali ya Chuo cha Tiba cha Misheni ya Wurzburg na kuona baadhi ya shughuli zinazofanywa na hospitali hiyo.
Katika maelezo yake kwa Rais, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Profesa August Stich alisema chuo hicho kinashirikiana na taasisi za afya na hospitali nyingi barani Afrika ikiwemo Hospitali za Bugando ya huko Mwanza na KCMC huko Moshi Tanzania.
Alifafanua kuwa wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa ebola katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi taasisi yake ilitoa mafunzo maalum kwa karibu watumishi wa afya 200 waliokuwa wakifanyakazi kukabiliana na ugonjwa huo katika nchi hizo.
Siku hiyo jioni Dk. Shein na ujumbe wake walishiriki katika chakula cha jioni kilichoandaliwa na Serikali ya Jimbo la Bavaria ambapo hafla hiyo ilipambwa na burudani ya Taarab iliyoporoshwa na kikundi cha Taarab kutoka Zanzibar.
Dk. Shein anaendelea na ziara yake ya siku nane nchini Ujerumani leo kwa kusafiri hadi mji wa Berlin ambako ndiko makao makuu ya serikali ya Ujerumani ambako anarajiwa kuonana na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na Chama cha Wafanyabiashara wa nchi hiyo.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment