Habari za Punde

Dk Shein ushirikiano wa skuli zetu ni kielelezo cha urafiki wa kweli wa nchi zetu

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                             08 Juni, 2015
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ushirikiano kati ya skuli ya Mwanakwerekwe ya mjini Unguja na skuli ya Bruno-H-Burgel ya mjini Postdam Ujerumani sio tu ni kielelezo cha urafiki na ukaribu wa wananchi wa Zanzibar na Ujerumani bali pia unadhihirisha dhamira ya kweli waliyonayo wananchi wa nchi hizo ya kuimarisha uhushirikiano wao kihistoria.

Akizungumza na jumuiya ya Skuli ya Bruno-H-Burgel wakati alipoitembela skuli hiyo jana mjini Postdam Ujerumani, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alisema kuwa ushirikiano kati ya skuli hizo ni miongoni mwa jitihada za kila upande za kuhakikisha kuwa ushirikiano wa nchi mbili hizo unazidi kuwekewa misingi imara ya kuuimarisha zaidi na zaidi.

Dk. Shein aliwapongeza walimu wa skuli hiyo kwa kuwajenga watoto katika misingi ya kujiamini na kujenga matumaini ya mafanikio katika masomo yao.

Aliwaeleza walimu na wanafunzi hao kuwa amevutiwa na kutiwa moyo sana programu ya kuhifadhi mazingira kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwapa moyo kuendelea na programu hiyo kwa kuwa ina umuhimu mkubwa katika maisha ya kila siku.

Katika skuli hiyo Dk. Shein alipokelewa na walimu na wanafunzi na kupata fursa ya kuangalia baadhi ya shughuli zinazofanywa na wanafunzi ikiwemo michezo maalum pamoja na kushiriki katika moja ya darasa ambapo aliangalia mchezo maalum wa kuelezea historia ya skuli na baadae alijibu maswali kutoka kwa baadhi ya wanafunzi.

Aidha Dk. Shein na ujumbe wake ulipata fursa ya kuangalia filamu ndogo iliyotengenezwa na skuli hiyo inayozungumzia uhifadhi wa mazingira kwa upande wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akitoa maelezo ya filamu hiyo, meneja wa mradi huo bibi Cordine Lippert alisema mradi huo unalenga kuwaelimisha watoto umuhimu wa kuhifadhi mazingira ikiwemo recycling ya vitu kama karatasi na chupa za plastiki na hata kuzitumia kwa matumizi mengine.


Alisema skuli yao ina ari ya kuimarisha ushirikiano na Zanzibar na kujifunza zaidi masuala ya mazingira na kuisifu Zanzibar kwa kufanikiwa kupiga marufuku mifuko ya plastiki kitendo ambacho wanakiona kuwa ni hatua nzuri kwa manufaa ya kuhifadhi mazingira.

Bibi Lippert alieleza pia uongozi wa skuli umefurahishwa na ziara ya Mheshimiwa Rais na kubainisha kuwa mwalimu Rukia kutoka skuli ya Mwanakwerekwe alitembelea skuli yao na walifurahia pia ziara yake hiyo.  

Dk. Shein anatarajiwa kumaliza ziara yake ya siku nane nchini Ujerumani leo kwa kuzungumza na Chama cha Wafanyabiashara wa Ujerumani wanaofanya shughuli zao katika nchi za Afrika.  
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.