STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 5 Juni, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Maonesho ya Muziki wa Afrika nchini Ujerumani kuwa ni tukio muhimu linaloutangaza utajiri na urithi mkubwa wa utamaduni wa bara hilo katika ramani ya utamaduni wa dunia.
Akifungua rasmi Tamasha hilo linalofanyika kila mwaka katika mji wa Wursburg nchini Ujerumani jana, Dk. Shein amesema Maonesho hayo yamefanikiwa kuwaunganisha watu wa rangi tofauti lakini wenye dhamira moja ya kuendeleza urithi na ubunifu katika muziki wa Afrika.
Aliwaeleza maelefu ya washiriki wa maonesho hayo kuwa Zanzibar imeshiriki katika maonesho hayo ikiwa ni fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kihistoria na urafiki kati yake na Ujerumani na watu wa nchi hiyo.
Aidha alieleza kuwa Maonesho hayo ni fursa nyingine kwa kikundi cha Taarab kutoka Zanzibar kujifunza katika ngazi ya kimataifa na kuonesha utamaduni wa Zanzibar ambao ni moja ya kivutio kikubwa cha utalii.
Kwa hivyo alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Ujerumani kuzidi kutembelea Zanzibar kujionea vivutio vingi vya kitalii ikiwemo muziki ambao huoneshwa katika hoteli nyingi za kitalii huko Zanzibar.
Dk. Shein amesema kikundi hicho cha Taarab kutoka Skuli ya Muziki ya Nchi za Majahazi huko Zanzibar kinajumuisha wasanii vijana wenye vipaji ambao wanaendeleza vipaji vyao kwa kujifunza na kuendeleza muziki wa kale wa Zanzibar kwa vijana.
Aliwaeleza washiriki wa Maonesho hayo kuwa Zanzibar katika historia ya utamaduni wake ilibahatika kutoa wasanii waliotajika ulimwenguni wakiwemo waimbaji Siti binti Saad na Bi Fatma binti Baraka maarufu Bi. Kidude ambaye katika uhai wake alishiriki katika matamasha mengi ya muziki nchini Ujerumani.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliishukuru taasisi ya Afro Project waandaji wa Maonesho hayo kwa kuipa Zanzibar nafasi ya pekee katika maonesho ya mwaka huu ambapo mbali ya kushiriki kikundi cha Taarab lakini pia kufanyika maonesho ya Zanzibar yaliyopewa jina “Zanzibar –Traditions at the gate to Africa”.
Miongoni mwa maonesho hayo ni picha kuhusu historia ya Zanzibar na watu wake yaliyoandaliwa na wapigapicha mashuhuri wa kijerumani Mario Gerth and Joachim Schmeisser.
Aliwapongeza waandaji wa Maonesho hayo kwa mafanikio makubwa kwa kuweza kuwakusanya wasanii kutoka bara la Afrika na sehemu nyingine ulimwenguni ambapo ushiriki wao unaongeza na kuimarisha maelewano miongoni mwa mataifa na wasanii hao wanapata kujifunza kutoka miongoni mwao.
Dk. Shein aliwataka wasanii wanaoshiriki Maonesho hayo kupenda muziki wa wenzao na kubadilishana uzoefu na kuongeza kuwa watakachojifunza katika muziki kitachangia kuleta maelewano na amani duniani.
Dk. Shein anatarajiwa kuendelea na ziara yake nchini Ujerumani leo kwa kutembelea Idara ya Magonjwa ya Kitropiki katika Taasisi ya Afya ya Wurzburg. Aidha atatemebela Ofisi za jiji la Warzburg na kuonana na viongozi mbalimbali wa wakiwemo Wenyeviti wa Kamati za Bunge la Halmashauri ya jiji la Wurzburg na wabunge wa Bunge la jimbo la Bavaria. Baadae atashiriki katika chakula cha jioni kilichoandaliwa na wenyeji wake.
Katika ziara hiyo Dk. Shein amefuatana na mke wake Mama Mwanamwema Shein,Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk, Waziri wa Kilimo na Maliasili Dk. Sira Ubwa Mamboya, Naibu waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dk. Mahadhi Juma Maalim na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Wengine ni Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, Katibu Mkuu wizara ya Biashara,Viwanda na Masoko Julian Banzi Raphael na Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho Dk. Amina Ameir Issa.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment