Na Takdir Ali-Maelezo Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshauriwa kufanya juhudi za kuwahamisha Ombaomba waliozagaa katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Mji wa Zanzibar.
Hayo yameelezwa na Mjumbe wa Kamati ya Katiba,Sheria na Utawala ya Baraza la Wawakilishi Wanu Hafidhi Ameir wakati alipokuwa akiwasilisha Maoni ya Kamati hiyo katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Amesema kumekuwa na Ongezeko kubwa la watu wanaokaa katika Maeneo mbali mbali ya Mji wa Zanzibar na kuomba, jambo ambalo halitoi Taswira nzuri kutokana na Maadili ya Wananchi wa Zanzibar.
Wanu amefafanua kuwa Mila na Silka za Zanzibar haziruhusu Watu kukaa kwa ajili ya kuomba Wapita njia na hivyo kuiomba Serikali kuweka mikakati makini ya kuondosha Tatizo hilo linaloongezeka siku hadi siku.
Akielezea kuhusu kuwepo kwa Nyumba za Wageni (Baa) Wanu amesema Nyumba hizo zimekuwa zikiathiri Maadili ya watoto wa Zanzibar hususan kwa Wanafunzi wa Skuli.
Ameweka wazi kwamba Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi haina budi kuchukua juhudi za kufanya utafiti wa kina ili kuzuia tatizo hilo lisiendelee.
Akitolea mfano wa Baa zinazolalamikiwa Wanu amesema ni pamoja na Baa ya Chukwani ambayo amedai baadhi ya Wanafunzi huacha muda wa masomo na kwenda katika Baa hiyo kufanya vitendo viovu.
Wanu amesema wakati umefika kwa Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi kufanya Utafiti ili kulijua kwa undani suala hilo na kulitafutia ufumbuzi kabla halijaleta athari kubwa kwa Wananchi.
No comments:
Post a Comment