Habari za Punde

Vibali vya kuchimba mchanga hutolewa bila ya ubaguzi

Takdir Ali-Maelezo 

Serikali kupitia Idara ya Mazingira na Maliasili zisizorejesheka haijawahi wala haina sababu za kufanya ubaguzi wa kutoa ruhusa ya mtu yeyote kuchimba mchanga katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Fatma Abdul-habib Fereji wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Wawi Saleh Nassor Juma katika Baraza la Wawakilishi linaloendelea Chukwani nje kidogo ya Mji wa  Zanzibar.

Amesema Serikali kupitia Idara ya Maliasili zisizorejesheka ambayo ni Taasisi yenye dhamana ya kutoa vibali vya Mchanga/Udongo kwa baadhi ya Maeneo kwa miradi maalum ya maendeleo ambayo hutowa vibali hivyo bila ubaguzi wa aina yeyote kitu cha muhimu ni kufuata Taratibu na Sheria za nchi.

Amesema Maeneo hayo hutolewa baada ya kufuata Taratibu zote za nchi ikiwa ni pamoja na kufanya Ukaguzi Shirikishi wa Wadau na kwa kuzingatia mahitaji maalum ya aina ya Mchanga inayohitajika kwa ajili ya Shughuli za Mradi husika.


Aidha amesema uchunguzi wa Kimaabara wa kuangalia aina ya Mchanga/Udongo hufanywa ili kubaini eneo linalofaa kuchimbwa Mchanga.

Amefafanua kuwa kwa ujumla uchimbaji wa Mchanga/Udongo na wanaohusika kuchukua Mchanga/Udongo kwenye Maeneo hayo ni wale tu wanaohusika na shughuli za  Mradi husika.

Akielezea kuhusu eneo linalohusika  kwa kazi maalum ya Ujenzi wa nyumba za JWTZ ambazo zinajengwa katika eneo la Ngerengere kwenye kambi ya Jeshi la Wawi Fereji amesema Mkandarasi wa Ujenzi wa nyumba hizo alihitaji kupata Mchanga maalum ili kufikia Masharti ya Ujenzi wa nyumba hizo.

Ameendelea kusema kuwa kutokana na hali hiyo na baada ya kufanya uchunguzi wa kimaabara wa mchanga (soil test) katika maeneo mbali mbali ndio mchanga wa eneo hilo unaonekana kuwa unafaa kwa mahitaji ya ujenzi wa nyumba hizo.

Mbali na hayo amesema baada ya uchunguzi huo kuthibitika hali hiyo,ndipo taratibu ziliopo za maombi zikafuatwa na baada ya taratibu hizo kukamilika ndipo Idara ya Misitu na Maliasili zisizorejesheka ikatoa kibali cha uchimbaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.