STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 23 Agosti, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyeikiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ili kuhakikisha kunakuwepo na maendeleo ya kiuchumi na kijamii suala la amani na utulivu ni la kipambele kwa Chama cha Mapinduzi-CCM na Serikali zake.
Akizungumza katika halfa ya kuchangia Mfuko wa Maendeleo wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba iliyofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam jana, Dk. Shein aliwaeleza washiriki wa hafla hiyo ambao miongoni mwao ni wafanyabiashara na wawekezaji kuwa milango ya Zanzibar iko wazi kwao kushirikiana na serikali na wananchi wake kuimarisha uchumi na maendeleo.
Katika hafla hiyo jumla ya shilingi milioni 637.795 zilikusanywa ikiwa ni ahadi na fedha taslim.
“Zanzibar itajengwa na wazanzibari wenyewe lakini tumejidhatiti kikamilifu kuimarisha uchumi wetu kwa kushirikiana na wenzetu wanaotuunga mkono kama nyinyi” Dk. Shein alisema.
Alibainisha kuwa Zanzibar hivi sasa inatilia mkazo mkubwa katika kujenga uchumi wake kwa kuimarisha miundombinu ya uchumi ikiwemo usafiri wa anga na baharini pamoja na ujenzi wa miji mipya kwa kushirikiana na sekta binafsi.
“Tunatarajia si kipindi kirefu kushuhudia mabadiliko makubwa katika shughuli zetu za kiuchumi hasa pale tutakapokamilisha ujenzi na uimarishaji wa kiwanja chetu cha ndege Zanzibar pamoja na ujenzi wa bandari mpya ya Mpigaduri” Dk. Shein alibainisha.
Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar aliwapongeza na kuwashukuru wananchi wa Tanzania Bara kwa ushirikiano wao mkubwa katika kufanikisha michango mbalimbali kwa Chama cha Mapinduzi Zanzibar na kueleza kuwa hatua hiyo inadhihirisha udugu na mapenzi ya kweli kati wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara.
“Ni matarajio yangu na wana CCM wote kuwa huu ni mwanzo tu na ushirikiano wetu huu na tutauendeleza” Dk. Shein alieleza.
Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi wa Mkoa wa Kusini Pemba kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyowekwa na ambayo ndio yaliyowavutia wachangiaji hao kukichangia chama hicho.
“Viongozi wa Mkoa wawe makini katika matumizi ya fedha zilizokusanywa kwa malengo yaliyokusudiwa ambapo kwa kufanya hivyo mtawapa moyo wachangiaji wetu kuendelea kukiunga mkono chama chetu kama wanavyofanya mara zote tunapowaomba kufanya hivyo” Dk. Shein.
Dk. Shein aliwathibitishia wachangiaji hao kuwa imani yake inamtuma kuwa viongozi hao watazitumia fedha hizo kwa malengo yale yale yaliyokusudiwa.
Akizungumza katika hafla hiyo kumkaribisha Dk. Shei, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mheshimiwa Mohamed Aboud alimpongeza Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake za kuimarisha amani na utulivu hali iliyopelekea wawekezaji na wafanyabiashara kujenga imani na kuanzisha miradi yao Zanzibar.
Katika mnasaba huo Mheshimiwa Mohamed Aboud ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya hafla hiyo alieleza kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM umekuwa wa mafanikio makubwa ambapo katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Saba uchumi imeimarika na kuvutia uwekezaji mkubwa.
Katika hafla hiyo Dk. Shein alichangia milioni 20 na Mkwe wake Mama Mwanamwema shilingi milioni 10. Wengine waliochangia walikuwa ni mapoja na Makampuni ya Bakhresa shilingi milioni 100, Kampuni ya SuperDoll milioni 50, Kampuni ya Park Hyatt Zanzibar milioni 50 na Kampuni ya Home Shopping Centre shilingi milioni 25.
Mbali ya wafanyabiashara na wawekezaji hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa CCM na Serikali wakiwemo viongozi wastaafu kama Waziri Mkuu Mstaafu Balozi Salim Ahmed Salim na Waziri Kiongozi Mstaafu Shamsi Vuai Nahodha.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment