STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
6.10.2015
WANANCHI wa Zanzibar wametakiwa kuheshimu sheria za uchaguzi ziliopo kwa wakati
wote hasa wakati huu wa Kampeni, siku ya kupiga kura, siku ya kutangaza matokeo
pamoja na siku za baadae.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika uzinduzi wa jengo jipya
la Wizara ya Katiba na Sheria lilioko Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Dk. Shein aliendelea kuwasisitiza
wananchi kuheshimu misingi ya Katiba na Sheria ziliopo na kuwaeleza kuwa Sheria
za uchaguzi zipo na zinalindwa na Katiba ya Zanzibar.
Katika hotuba yake hiyo ya uzinduzi wa
jengo jipya la Wizara ya Katiba na Sheria lililopewa jina la ‘Nyumba ya Sheria’,
Dk. Shein aliwahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa Zanzibar itafanikiwa
kufanya uchaguzi huru na wa haki.
Dk. Shein aliwataka wananchi daima
wasikubali mifarakano ambayo ni chanzo cha kusababisha maafa kama wanavyoshuhudia
hivi sasa katika mataifa mbali mbali duniani.
“Nachukua fursa hii leo kwa mara nyengine
tena kusisitiza umuhimu wa mshikamano na umoja wetu..tutafanikiwa kufanya
uchaguzi huru na wa haki”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa wananchi
wanawajibu wa kushikamana ili kutekeleza wajibu wa kikatiba na kisheria wa
kuwachagua viongozi wa kuongoza kila baada ya miaka mitano kwa mafanikio.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaeleza
wananchi historia ya katiba ya Zanzibar na kusema kuwa kabla ya kuja kwa
wageni, Zanzibar ilikuwa na utawala wa wenyeji ambapo na sheria zilikuwepo na
zilikuwa kwa ajili ya kuongoza na kusimamia mfumo wa maisha uliokuwepo wakati
huo.
Alisema kuwa leo wananchi wa Zanzibar
wamefanikiwa kwa kuwa na Katiba yao ambayo mwaka 2010 ilifanyiwa marekebisho
ambayo yalileta Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa.
Alisema kuwa katika mfumo wa utawala wa kidemokrasia
duniani kote, Katiba ni kitu muhimu na cha lazima ambapo pia, ni kieleezo au
nembo ya utawala na mamlaka ya nchi na kuwataka wananchi kuiheshimu na kuitii
katika yao ya Zanzibar ambayo ni msingi wa utawala wao.
Licha ya hayo alieleza kuwa kuwa na
Katiba tu peke yake haitoshi kuwaletea
nafuu watu bali utekelezaji wa Katiba
ndiyo jambo muhimu na kusisitiza kuwa utii wa Sheria ndio msingi wa maendeleo
kwa nchi yoyote duniani.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa
Wizara hiyo ina jukumu la kusimamia masuala yote ya katiba na Sheria katika
kipindi hiki ambacho Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika Muundo wa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa jengo
hilo la ghorofa saba ni wazo la kimaendeleo kwa matumizi bora ya ardhi na
utekelezji kwa vitendo wa Mipango Miji iliyopitishwa na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar hivi karibuni.
Alisema kuwa katika kuimarisha mazingira
ya kufanyia kazi, Serikali itaendelea kujenga majengo ya kisasa yanayopendeza
na kuvutia sambamba a kuweka vifaa vya kufanyia kazi vinavyoendana na
mabadiliko, pamoja na mahitaji ya wakati huu.
Nae Waziri wa Katiba na Sheria Abubakar
Khamis Bakary alisema kuwa ni ukweli usiopingika kwamba jengo hilo limetatua
changamoto kubwa ya ufinyu wa nafasi kwa wafanyakazi wa taasisi za Wizara hiyo
pamoja na wananchi wanaopatiwa huduma na taasisi hizo.
Waziri Bakary alitoa shukurani kwa Dk.
Shein kwa nia yake njema ya kuitakia mema Zanzibar kwa kudumisha amani na
utulivu na kuongoza gurudumu la maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri Bakary
harakati za mradi wa jengo hilo zilianza mwaka 2011 na mkataba wa ujenzi
ulifungwa mwezi April 2012 ambapo kazi hiyo ilitarajiwa kuchukua kipindi cha
miezi 18 hadi kukamilika kwake mwezi Novemba 2013 lakini kutokana na changamoto
jengo lilihamiwa Jaulai 2015.
Alisema kuwa jengo hilo litaiwezesha
Wizara hiyo pamoja na Idara zake saba kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu zake na kujenga mifumo
ya kielektroniki itakayarahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa
wananchi.
Jengo hilo limejengwa na Kampuni ya China Railways JiangChang Engineering (CRJE)
na Mshauri ni Kampuni ya The National Estate Development Company Ltd
(NEDCO) ambapo Mhandisi Mkaazi ni Bwana
Ali Othman ambapo gharama za ujenzi wa
jengo hilo ni Tsh.Bilioni 8.3.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment