Habari za Punde

Amani, utulivu ipigiwe chapuo uchaguzi wa marejeo


Na Mwandishi wetu, Pemba

OKTOBA 28, mwaka 2015 Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC, Jecha Salim Jecha, alitangaaza rasmi kuyafuta matokeo ya uchaguzi mkuu ngazi ya udiwani, uwakilishi na urais wa Zanzibar.

Kila mmoja ni shahidi wa hili, na wala sina nia ya kukumbushia pakubwa, maana wapo waliofurahia wakiwa na sababu kadhaa, lakini pia wengine walinuna nao wakiwa na sababu tunasema zenye akili.

Yote kwa yote ndio tumeshashuhudia kwamba matokeo hayo yamefutwa, na mfutaji akiwa na sababu kadhaa, ikiwemo uchaguzi huo kutawaliwa na ghilba.

Kisha ufutaji huo ukasindikizwa kisheria zaidi kwa taarifa hiyo, kuingizwa kwenye gazeti rasmi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wengine kufikiria kwamba ni Gazeti la Zanzibar leo, kumbe silo hili ni maalum hilo.

Niende mbele kwanini uchaguzi ulifutwa……hapana kila mmoja anaelewa sababu kadhaa, na kisha Mwenyekiti wa ZEC kutangaza kwamba uchaguzi huo, utarejewa na vyama kuingia tena dimbani.
Wala sio siri…. na wala sioni aibu kusema kuwa Chama kikuu cha upinzani Zanzibar CUF walishatangaaza mara kwa mara na kwa hati nyeusi kwamba, wao hawafahumu kufutwa huko na wala hawana habari na uchaguzi wa marejeo.

Huku chama kinachotetea kiti chake cha utawala cha CCM kwanza kikikubaliana na ufutwaji huo, na kisha kimeshajipanga ili kuingia tena kwenye marejeo ya uchaguzi huo.

Na hii ndio demokrasia, kwamba mmoja akisema hii nguo ni nyeusi, basi atokea mwengine aseme sio  nyeusi, bali ina rangi tu nyeusi, lakini wote wanasema hayo sio kwa utashi bali kwa nguvu ya hoja tena nzito.


Kama ZEC ilishatangaaza kwamba kuna uhakika wa kurejea kwa uchaguzi, akina mimi na yule tumekuwa tukisema kila mara kwamba, lazima amani na utulivu katika uchaguzi huo, ipigie chapuo.

Walishasema wazee kwamba ‘hakuna harusi ndogo wala isio na gharama, basi tusema kwa pamoja kwamba, na lolote kwenye uchaguzi laweza kujichomoza.

Wiki tatu kabla ya uchaguzi wa mwanzo Oktoba 25 mwaka 2015, viongozi wa dini zote unazozijua wewe, makababila, vyama vya siasa, wanawake, vijana na mashirika kadhaa yalismama na kuomba amani na utulivu hadi nykati za usiku.

Sasa tumekwama wapi kwa uchaguzi huu ambao vyombo vyenye mamlaka vinasimama na kusema utarejewa, na kauli za hivi karibuni kwamba ni mwezi wa Januari 2016 au hata kabla ya kumalizika kwa mwezi wa Febuari.

Nakumbuka sana mikutano yote ya kamapeni iliofanywa kabla ya kuhitimishwa pale oktoba 24 mwaka 2015, hakuna kiongozi wa chama cha siasa, ambae hakuna neneo amani na utulivu kwenye hutba yake.

Kumbe kila mmoja aliona umuhimu wa kudumisha na kuendelea amani na utulivu, tena kabla, wakati na baada ya uchgauzi, tukiamini kuwa kumbe bila ya vitu hivyo hakuna linalofanyika.

Mgombea urais wa chama cha CUF maalim Seif Sharif Hamad kwenye mkutano wake wa kampeni alioufanya katikati ya kijiji alichozaliwa cha Mtambwe, alisisitiza umuhimu wa amani na utulivu.

“Ndugu wananchi nasema Jeshi la Polisi sasa limeshatufahamu sisi CUF nini lengo letu, sasa lazima tuhakikishe tunatunza amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu’’,alisema.

Kwani alikuwa yeye tu….. hata Mgombea wa nafasi kama hiyo kutoka AFP Said Soud Said, yeye alisema lazima kila mmoja neno amani na utulivu liwe mbele kisha ndio chama.

Alikwenda mbali zaidi kwamba, hakuna umuhimu wa uwepo wa chama chochote Zanzibar, kwamba hakitozingatia amani kwa wananchi, maana urais, umakamu na uwaziri hautafanyika kama amani haitotawala.

Lakini Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai wakati akimuombea kura mgombea wa chama hicho Dk Ali Mohamed Shein, kwenye mkutano uliofanyika Kiwani, alisema chama hicho hakijapanga vijana kufanya fujo.

“CCM ni mwalimu wa demokrasia, CCM ndio chama mama, hakina haja ya kuvunja amani, maana chenyewe kinatetea amani na utulivu’’,alisisitiza.

Sasa iwe wewe unaeshiriki au uko kando kwenye uchaguzi wa marejeo, ni vyema suala la amani na utulivu likapigiwa chapuo, maana hakuna asietaka utulivu na anaewania fujo.

Kama vyombo vyenye mamlaka vimeshasema uchaguzi unarejewam mbona hatuoni shamra shamra za hutuba za viongozi wa dini na vyama vya siasa kusimama kidedea juu ya amani na utulivu.

Maana hapa narejea tena iwe wewe ni mshiriki wa uchaguzi au wa kukaa kando, lakini je amani na utulivu huna shida navyo tena, naamini jawabu sio, sasa tuipige chapuo.

Kijana Omar Kombo Daudi (22) wa Mkoani, anasema chakuhubiri 
kwa sasa kama mamlaka zimeshamua kurejea uchaguzi, ni amani na utulivu maana bado wananchi wanahitaji hilo milele.

“Hakuna hata kiongozi mmoja wa dini, chama, au NGOs na wengine asietaka amani na uutulivu, sasa lazima tuone yale maombi kadhaa yaliofanywa yarejewe’’,alifafanua.

Bibi Asha Hassan Makame (50) wa Chakechake, anasema lazima kila mmoja apigie chapuo suala la amani na utulivu, maana  hakuna uchaguzi uliohakikishiwia amani na utulivu kwa asilimia mia moja.

“Inawezekana kuna vyama havitoshiriki uchaguzi wa marejeo, lakini bado vinastahili kuomba amani na utulivu, maana hata wao watakaobakia majumbani wanahitaji amani’’,alisema.

Ingawa Mwanaidi Mbarawa Hija (35) anasema suala la amani na utulivu sio tu kwenye mambo ya kisiasa pekee, bali hata wakati wowote kila mmoja aombe amani na utulivu.

“Unajua suala la amani ni wakati wote, lakini kama kuna shughuli za kisiasa kama uchaguzi, lazima kila kiongozi kwa nafasi yake akemee, maana amani ni kwa sote na machafuko pia’’,aliweka wazi.

Bado upo umuhimu kwa kila mmoja, iwe wakati huu wa kuelekea uchaguzi wa marejeo au hata katika maisha ya kila siku, suala la amani na utulivu pia ni sehemu ya maisha.


 Yote kwa yote suala la amani na utulivu, ambalo dini zote inalikubali lazima kwa Zanzibar kuelekea uchgauzi wa marejeo iwe ndio ajenda kuu, maana athari na faida ni kwa wote.

1 comment:

  1. Mimi si mwanachama wa chama chochote, ila ni mpigania maendeleo katika visiwa vyetu, napenda sana kuona kiongozi mwenye kuleta amani na maendeleo ya kweli katika nchi yake.
    Nilikuwa mfatiliaji mzuri tangu vyama vyote vilivyoanza kampeni hadi siku ya Uchaguzi, lakini kwa mtazamo wangu wa kawaida nahisi CCM Zanzibar hawapo tayari kwa demokrasia ya kweli.
    Naamini hata wapinzani wakiweza kutawala nchi haitokuwa na machafuko kwani wazanzibari ni watu wenye kupenda amani na utulivu.
    CCM zanzibar lazima wakubali matakwa ya wananchi wakubali kuwa wazanzibari sasa wanataka kuona mabadiliko katika nchi yao, naamini hata wapinzani hawataweza kuleta maendeleo ya mara moja lakini mabadiliko yanahitajika Zanzibar, Miaka zaidi ya 40 ya CCM ni kipimo kikubwa kama ni chama cha kuleta maendeleo, sasa imefika muda wa wapinzani kuongoza Zanzibar alau kwa miaka5 iwe Chadea, iwe Chauma iwe JahaziAsilia au hata Cuf.
    Mabadiliko yanahitajika Zanzibar hata Muandishi unalijua hilo kwani katika wakati wa kampeni uliweka katika Blog yako kura za maoni ni ushahidi tosha kuwa waZanzibari wanataka mabadiliko ya kweli kwa njia ya AMANI NA UPENDO.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.