Habari za Punde

Eka 150 za miwa iliopea zachomwa moto na watu wasiojulikana

 Meneja wa Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda  Bwana Tushar Mehta wa kwanza kutoka Kushoto akimkaguza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye eneo la shamba la miwa lilitotiwa moto hapo Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.

 Baadhi ya miwa iliyopea katika shamba la Kiwanda cha Sukari Mahonda ambapo eka150 zilitiwa moto.

 Bwana Tushar  Mehta akimueleza Balozi Seif hasara iliyopatitaka kutokana na  Eka 150 za shamba la Miwa Mahonda  zilizotiwa moto mchana wa Jumatatu.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akielezea masikitiko yake kutokana na tabia ya baadhi ya Watu kufanya hujuma za kutia moto kwenye shamba la Miwa Mahonda.
Eneo la Shamba la Miwa la ekari 150 lililotiuwa Moto na watu wasiojuilikana na kukisababishia hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.5 Kiwanda cha Sukari Mahonda.

Picha na – OMPR – ZNZ


Othman Khamis Ame, OMPR

Eka Mia 150 za miwa iliyopea zilizotiwa moto na watu wasiojuilikana  katika eneo la kusini Magharibi ya Mashamba ya Miwa ya Kiwanda cha Sukari Mahonda zinakadiriwa kuleta hasara ya  Dola za Kimarekani Laki  947,475.72  sawa na shilingi za Kitanzania Bilioni 1,832,242,500.00/-.

Moto huo ulioshambulia  mashamba hayo jana majira ya saa sita mchana  ulizimwa kwa ushirikiano kati ya wapiganaji wa Kikosi cha Zima moto na Uokozi Zanzibar, JKU, Wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda pamoja na Wananchi   na kufanikiwa kuudhibiti  mnamo majira ya saa Tisa Jioni.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika katika eneo hilo la maafa na kujionea hali halisi ya hasara iliyopatikana ambapo Meneja wa Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda  Bwana Tushar Mehta alisema eneo hilo la Eka 150 lililotiwa moto pekee lilikuwa na uwezo wa kuzalisha Sukari Tani Mia 750 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.5.


Bwana Tushar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Uongozi wa Kiwanda hicho umesikitishwa na kitendo cha watu waliofanya hujuma hiyo licha ya  nia njema ya  Kiwanda hicho kuwekeza mradi huo wenye lengo la kuongeza Mapato kwa Serikali sambamba na kuongeza fursa za ajira kwa wakaazi wa maeneo jirani yanayokizunguuka Kiwand hicho.

Hata hivyo Bwana Tushar alimuhakikishia Balozi Seif  kwamba Uongozi wa Kiwanda hicho bado umeonyesha nia ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa ya sukari kwa kutoa mapendekezo ya kupatiwa mashamba zaidi ya kilimo cha miwa katika Maeneo ya Bumbwi Sudi na Bambi.

Alisema hatua hiyo imekuja kutokana na mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa Kiwanda cha Sukari ambapo kwa sasa kimekuwa katika harakati za matengenezo ya kuwekewa mashine  kubwa zitakazokuwa na uwezo mkubwa zaidi wa uzalishaji  wa Sukari.

Akielezea masikitiko yake kutokana na kitendo cha hujuma ya moto katika shamba hilo la miwa Mahonda Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema huo ni uharibifu mbaya ambao hauitakii mema Nchi hii.

Balozi Seif alisema kitendo hicho cha uhalifu kinachopaswa kulaaniwa vikali na uuma kimeleta sura mbaya na kuisababishia ukosefu wa mapato Serikali Kuu iliyoamua kukaribisha uwekezaji wa Viwanda hapa Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda  kutovunjika moyo kutokana na kitendo hicho na kuahidi kwamba Serikali kupitia vyombo vyake vya Dola inaendelea na uchunguzi kumbaini Mtu au kikundi kilichohusika na vitendo hicho na kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria.

Hata hivyo Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali Kuu itajitahidi kuendelea kuuelimisha Wananchi juu ya umuhimu wa uwekezaji vitenga uchumi nchini wenye lengo la kuimarisha ustawi wa Jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.