Habari za Punde

Dk Shein: Ahadi zangu zina lengo la kuwasaidia wananchi na kuwaletea maendeleo endelevu.


 
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                30.12.2015
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo ametembelea miradi ya Maendeleo ukiwemo mradi wa gati mpya pamoja na mradi wa maji safi na salama huko Wilaya ndogo Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja na kueleza kuwa ahadi zake zina lengo la kuwasaidia wananchi na kuwaletea maendeleo endelevu.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kutembelea miradi hiyo Dk. Shein alisema kuwa amefurahishwa kwa kiasi kikubwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo ambayo itakuwa ni mkombozi mkubwa katika kuwaletea maendeleo sambamba na kuimarisha huduma za kijamii.

Dk. Shein alisema kuwa  ujenzi wa gati mpya   umejengwa kwa kitaalamu zaidi kwani gati hiyo itahimili vishindo vya vyombo vyote kwani juhudi hizo zote ni kwa ajili ya usafiri wa uhakika wa wananchi wa kisiwa cha Tumbatu pamoja na bidhaa zao hasa ikizingatiwa kuwa wananchi hao wa Tumbatu wao wenyewe ndio waliokuwa mafundi chini ya usimamizi wa Shirika la Bandari.

Katika maelezo yake  Dk. Shein alisema kuwa ujenzi huo wa gati ni miongoni mwa maendeleo makubwa yaliokusudiwa kwa ajili ya wananachi wa Tumbatu ambapo kabla ya kuwepo kwa gati hiyo wananchi hao walikuwa wakipata usumbufu mkubwa.


Akieleza kuhusu mradi mpya wa maji safi  na salama, Dk. Shein alisema kuwa kutokana na kuwa maji ni uhai na hakuna maisha ya mwanaadamu bila ya kuwepo kwa huduma ya maji ndipo Serikali ikaona haja ya kuwaongeza huduma hiyo wananchi wa Tumbatu kwa kuanzisha mradi huo mpya wa maji.

Dk. Shein alisema kuwa lengo na madhumuni ya mradi huo ni kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wa Tumbatu hivyo aliwataka wananchi hao kuutunza mradi huo ili uwasaidie zaidi wao na vizazi vyao vijavyo.

Aidha, Dk. Shein aliwaahidi wananchi wa Tumbatu kuwa matangi kwa ajili ya maji yatajengwa  kisiwani humo na Serikali kwani uwezo huo inayo.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka wananchi wa Tumbatu kuwapuuza wale wote watakaobeza miradi hiyo kwani hulka hizo ni miongoni mwa hulka za baadhi ya wanaadamu na kusisitiza kuwa mwanaadamu yeyote anaepata neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni vizuri akashukuru.

Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa Tumbatu kwa kushiriki vyema katika ujenzi wa miradi hiyo na kuwaadi kuwa Serikali yao itaendelea kuwaunga mkono katika kuwapelekea miradi ya maendeleo.

Akitoa shukurani kwa wazee wa Tumbatu, Dk. Shein alipokea ombi lao la kutaka kuimarishiwa zaidi kituo chao cha Polisi kwa lengo la kuongezewa ulinzi wanachi hao pamoja na mali zao huku akiwaahidi kuwa juhudi zitachukuliwa na Serikali katika kukiimarisha zaidi kisiwa cha Tumbatu kwa kujenga barabara pamoja na taa maalum za muangaza wa jua kwa mashirikiano ya pamoja Serikali na uongozi wa Jimbo hilo.

Nae Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu Mhe. Haji Omar Kheir alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa juhudi zake za makusudi za kuhakikisha wananchi wa Tumbatu wanapata huduma bora maendeleo zikiwemo huduma za afya, maji safi na salama,umeme, elimu ujenzi wa gati na huduma nyenginezo.

Aidha, Mwakilishi huyo wa Tumbatu ambaye pia, ni Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ alitoa pongezi kwa Wizara ya  Miundombinu na Mawasiliano pamoja na Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kwa kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Zanzibar Abdalla Juma alimueleza Dk. Shein kuwa ujenzi wa gati hiyo mpya ni kutekeleza agizo la Serikali na kusema kuwa kwa upande wa Tumbatu umekamilika na kilichobaki ni mambo madogo madogo huku akieleza kuwa kwa upande wa gati ya Mkokotoni ujenzi wake unatarajiwa kuanza mapema mwaka ujao.

Mkurugenzi Juma alisema kuwa ujenzi wa gati hiyo mpya kwa upande wa Tumbatu ambayo tayari imeshaanza kutumika hadi kumaliza kwake utagharimu Shilingi 374 ambapo kwa upande wa gati ya Mkokotoni ambayo tayari michoro yake ipo, itagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni moja na wakati wowote tenda yake itatangazwa.

Alisema kuwa kwa upande wa gati ya Tumbatu ni kwa ajili ya vyombo yote vidogo vidogo vikiwemo vile vya kienyeji ambapo pia, limejengwa eneo maalum kwa ajili ya mizigo na kwa upande wa Mkokotoni bandari hiyo mpya itatumiwa na hata boti kubwa.

Nae Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Dk. Mustafa Ali Garu kwa upande wake alisema kuwa mradi huo mpya wa maji safi na salama kisiwani unaotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umeshaanza kutoa huduma huku akieleza kuwa mchango mkubwa umetolewa na wananchi wa Tumbatu, Mwakilishi wa pamoja na Washirika wa Maendeleo wakiwemo Ubalozi wa Marekani na Iran.

Garu alisema kuwa mradi huo unatarajiwa kuwa na visima vitatu ambapo tayari hivi sasa kisima kimoja kimeshaanza kazi kilichochimbwa huko Donge Kipange na vyengine vinaendelea na kueleza kuwa kukamilika kwa visima hivyo na kuunganishwa kwake kutaondosha kabisa upatikanaji wa maji kwa mgao kama ilivyo hivi sasa na badala yake yatapatikana kwa muda wote wa masaa 24.

Garu alisema kuwa Mradi huo unatekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia ZAWA ikiwa ni pamoja na kulaza mabomba baharini na  uchimbaji visima na kueleza kuwa gharama za Mradi huo ni T. Shilingi Bilioni moja na nusu na kwa hivi sasa tayari Shilingi milioni 700 zimeshatumika.

Nao wazee wa Tumbatu walitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa juhudi za makususdi anazozichukuwa za kuwapelekea maendeleo wananchi wa kisiwa hicho sambamba na kutekeleza kwa vitendo ahadi anazowaahidi.

Sambamba na hayo, Wazee hao walimueleza Dk. Shein kuwasaidia kukiimarisha kituo chao cha polisi kwa lengo la kuimarisha hali ya usalama katika kisiwa chao.  

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.