
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 2.12.2015

RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ujenzi wa
bandari mpya ya Mpigaduri unaotarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwaka 2016 ni hatua
muhimu ya kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi sambamba na kuharakisha maendeleo
ya kiuchumi na kijamii Zanzibar.
Akijibu
maswali ya waandishi wa habari wakati wa ziara yake fupi ya kutembelea eneo
litakalojengwa bandari hiyo leo, Dk. Shein alieleza kuwa mradi huo pamoja na
ule wa upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume itafungua milango
zaidi ya kiuchumi kwa Zanzibar.
“Huu
ni mradi mkubwa kwa uchumi wetu hivyo wananchi watarajie maendeleo makubwa na
yenye kasi zaidi ya uchumi wetu” Dk. Shein alieleza.
Aliwaambia
waandishi wa habari na viongozi waliokuwepo kuwa mradi wa ujenzi wa bandari ya
Mpigaduri si mradi mpya ulianza tangu Awamu ya Tano iliyoongozwa na Dk. Salmin
na kuendelea kushughulikiwa katika Awamu ya Sita hadi ndani ya miaka mitano ya Awamu
ya Saba ndio ilipofanikiwa kufikia hatua hii ya utekelezaji.
“Sisi
awamu hii tumekwenda mbele zaidi,tumetafuta fedha na tumefanikiwa kutokana na
urafiki wetu na serikali ya Jamhuri ya Watu wa China tutapata mkopo wa kujenga
bandari hii” Dk. Shein alidokeza.
Alifafanua
kuwa mazungumzo yake na Rais Xi Jinping wa China wakati wa ziara yake nchini
Tanzania na baadae alipofanya ziara nchini China suala hilo lilizungumzwa kwa
kirefu na matokeo yake ndio utekelezaji wa mradi huo.
Kuhusu
wananchi wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo litakalojengwa bandari Dk
Shein aliwaeleza wizara na mamlaka husika kuhakikisha kuwa kunakuwepo na mpango
maalum wa kuwapatia eneo ambalo litakuwa na miundombinu ya kisasa kufanya
shughuli zao na kusisitiza kuwa ni vyema suala hilo likashughulikiwa haraka
iwezekanavyo kuepusha migogoro na wananchi hao.
Akijibu
swali kuhusu hatua za serikali kuendana na kasi ya kupambana na maovu katika
jamii hasa ufisadi, Dk. Shein alisema katika miaka mitano iliyopita Serikali
imepitisha sheria nyingi na kali kama vile za uhujumu uchumi na sheria ya
maadili ya viongozi hivyo ipo haja ya
kutekelezwa ipasavyo na si suala la kuelezwa kila mara”.
Awali
akitoa maelezo kwa Mheshimiwa Rais, Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na
Mawasiliano Dk. Juma Malik Akil alieleza kuwa ujenzi utakuwa wa awamu tatu
tofauti ambapo awamu ya kwanza itakayogharimu Dola za kimarekani milioni 231.4
itaanza mwezi Januari, 2016.
Alifafanua
kuwa awamu ya kwanza ambayo inatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu
itakuwa bandari kamili yenye kila huduma zitakiwazo kwa bandari za kisasa na
awamu nyingine zitatekelezwa kulingana na kuongezeka kwa mahitaji ya miaka
ijayo.
Kuhusu
suala la wananchi wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo Dk. Akil alieleza
kuwa wao wamejulishwa hivi majuzi tu na mkandarasi kuwa ujenzi utaanza mapema
mwezi Januri 2016 lakini alieleza “watakutana na wizara ya Ardhi kulijadili
suala hilo na kuchukua hatua zifaazo mara moja”
Kwa
maelezo ya Muhandisi Mkuu wa Shirika la Bandari, Bwana Mbarouk Hamad Mbarouk
alisema kuwa, Kampuni ya CHEC kutoka nchini China ndio inayotarajiwa kufanya
ujenzi wa bandari hiyo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment