Na Masanja Mabula –Pemba
SHIRIKA la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) limewatoa hofu wakulima wa karafuu kwamba hakuna mkulima ambaye atauza karafuu zake katika vituo vya Shrika hilo na kutolipwa fedha zake taslimu .
Ofisa Mdhamini wa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) Pemba Abdalla Ali Ussi amesema kuwa Shirika hilo lina uwezo wa kununua karafuu zote kutoka kwa wakulima na kuwalipa fedha zao hapo hapo .
Akizungumza kwenye kikao cha wadau kwa karafuu cha kupanga njia ya kukabiliana na wanunuzi wa karafuu kwa njia ya kikombe na Pishi , amewataka wananchi hususani wakulima wa karafuu kupuuza kauli za kwamba Shirika limeanza kuwakopa wakuluma .
Alisema kwamba taarifa hizo hazina ukweli na kufahamisha kwamba kitendo cha wakulima kutolipwa fedha zao kilijitokeza siku moja katika kituo cha ununuzi Bandarini Wete kulikosababishwa na matatizo ya kibenki na sio Shirika .
“Naomba nuitumia fursa hii kuwafahamisha wakulima wa karafuu kwamba hakuna mkulima ambaye atakopwa karafuu zake na Shirika kwani tunazo fedha za kutosha kuweza kununua karafuu zote kutoka kwa wakulima ”alifahamisha .
“Tatizo la kutolipwa wakulima lilitokea siku moja na lilisababishwa na matatizo ya benki na sio Shirika naomba sana wakulima waelewa hivyo ”aliongeza Abdalla .
Aidha Mdhamini alikanusha taarifa kwamba Shirika limeishiwa na fedha baada ya sehemu kubwa ya akiba yake kutumika kwa ajili ya uchaguzi Mkuu uliofutwa na kusema kwamba Shirika linajitegemea .
Kuhusu suala la biashara ya haramu ya kikombe , Mdhamini amesema kuwa dawa yake ni kuwazuia wanaohusika na uuzaji wa karafuu mbichi na kuahidi kuitumia sheria namba 2 ya mwaka 2014 kuwabana wanaohusika na vitendo hivyo .
Akizungumza kwenye kikao hicho Katibu Tawala Wilaya ya Micheweni Hamad Omar Small amesema kwamba katika kufanikisha udhibiti wa wanunuzi wa karafuu kwa njia ya kikombe kunahaitajika ushirikiano kati ya taasisi zote pamoja na Serikali kuu .
Small alisema kwamba pamoja na Shirika kufikia uwezo wa kununua karafuu tani 53 kwa siku , lakini uwezekano wa kuongezeka zaidi upom iwapo kila mmoja atawajibika kusimamia na kuzuia biashara ya kikombe na karafuu mbichi .
“Hili linahitaji nguvu ya pamoja kati ya taasisi na Serikali kuu , uwezekano wa kuongeza idadi ya tani upo kinachohitajika ni ushirikiano tu ”alieleza Small .
Mwenyekiti wa kikoa hicho Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Omar Khamis Othman ameagiza Shirika kuondoa muhali na kutaka kutumika kwa sheria ya karafuu ili kudhibiti wanunuzi wa karafuu mbichi .
Aidha ni vyema vyombo vya ulinzi navyo kuwachukulia hatua wananchi waliofikishwa ktika vyombo hivyo kwa tuhuma za kuuhujumu mkarafuu pamoja na karafuu ili iwe fundisho kwa wanaotekeleza vitendo hivyo katika mashamba ya wakulima .
“Pamoja na uwepo wa Sheria lakini kinachotakiwa kupewa kipaombele ni kuondoa muhali anayekamatwa akituhumiwa kufanya hujuma lazima ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria nah ii ndio dawa pekee ya biashara ya karafuu mbichi ”alifahamisha .
Taarifa zaidi zinasema kwamba wakulima wa karafauu wamechoshwa na matendo ya wizi unaofanywa na watu wasiojulikana na kusababisha baadhi ya wakulima kuajiri walinzi wa kimasai katika mashamba yao .
No comments:
Post a Comment