Habari za Punde

Ravia Ateuwa Wajumbe Watatu Kuingia Kamati ya Mpito.

 Na Mwandishi Wetu.

Rais wa Chama Cha Soka Zanzibar (ZFARavia Idarous ameteuwa wajumbe watatu watakaoingia katika kamati ya muda ya chama hicho, inayosimamia soka la Zanzibar kwa sasa.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni kutekeleza maazimio yaliyofikiwa baina ya pande mbili zilizokuwa zikivutana kupitia kikao kilichofanyika jijini Dar es 
Salaam chini ya rais wa TFF Jamal Emil Malinzi.

Hayo yamebainishwa na Afisa Habari wa chama hicho Ali Bakari Cheupe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Hoteli ya Zanzibar Ocean View iliyopo Kilimani mjini hapa.

Alisema kuwa katika kikao hicho Ravia alitakiwa kuteuwa wajumbe wasiozidi watatu ambao watakuwemo katika kamati ya muda inayosimamia soka la Zanzibar kwa sasa chini ya Mwenyekiti wake Hussein Ali Ahmada.

Cheupe aliwataja wajumbe hao kuwa ni Katibu wa timu ya Malindi Mohammed Masoud, Haji Issa Kidali na Abdalla Thabit ‘Dulla Sande wakiwa ni wajumbe watatu wa kuingia katika kamati hiyo inayosimamia ligi.

Afisa huyo alifahamisha kuwa mvutano ulikuwa mkubwa mpaka kufikia hatua ya kupatikana kwa maazimio hayo yaliyotokana na kufanyika kwa vikao mbali mbali vya maridhiyano .


Mgogoro huo wa ZFA ulitokana baada ya Makamo wa Rais wa ZFA  Unguja Alhaj Haji Ameir kufunguwa kesi mahakamani ambayo ilifutwa kutokana na kufikiwa kwa muafaka huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.