Habari za Punde

Balozi Seif aiasa Zantel kuongeza kasi ya utendaji

Na Othman Khamis Ame, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Viongozi na Watendaji wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel wanapaswa kuongeza kasi ya utendaji ili waendelee kuwa watoa huduma bora hapa Nchini licha ya kasoro ndogo ndogo zinazoweza kurekebishwa kwa wakati muwafaka.

Alisema Zantel kwa kipindi cha miaka Minane mfululizo imekuwa ikitunukiwa zawadi ya mlipa kodi bora katika kundi la walipa kodi wakubwa, zawadi  ambayo hutolewa kila mwaka na Mamlaka ya Kodi Tanzania { TRA }.

Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa huduma mpya ya mtandao wenye kasi zaidi wa G Nne { 4G } kwa upande wa Zanzibar iliyofanyika katika Bustani ya Mnara wa Kumbu kumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Michenzani Mjini Zanzibar.

Alisema ushindi huo ni fahari kubwa kwa Zantel pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye hisa zake ambayo ilipata changamoto kubwa na hatimae kufanikiwa kupata kibali cha kuanzishwa kwa Kampuni hiyo mwaka 1999.

Balozi Seif alieleza kwamba kodi zinazolipwa na Zantel zilizofikia zaidi ya shilingi Bilioni 18 kwa mwaka 2015 pekee zinasaidia Taifa katika kuweka urari wa nakisi ya Bajeti yake.

“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawakilishwa katika Bodi ya Wakurugenzi ya Zantel, ambacho ni chombo kikuu cha Kampuni cha kuweka mikakati ya Sera. Tunao Wawakilishi Wawili katika Bodi ya Zantel tokea kuasisiwa kwake mwaka 1999 ”. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameupongeza Uongozi wa Zantel kwa kutoa ajira kwa Wazanzibari walio wengi tokea kuanzishwa kwake ambapo wananchi kadhaa ikiwa ni pamoja na wataalamu wa fani mbali mbali walipata ajira ya kudumu.


Alifahamisha kwamba Kituo cha huduma kwa wateja pekee tayari kimeshatoa ajira kwa Vijana wasiopungua Mia Mbili.
Hata hivyo Balozi Seif alitanabahisha kwamba yapo matatizo yanayolalamikiwa na Wananchi kuhusu kukatika kwa mawasiliano kwa baadhi ya wakati jambo ambalo huleta usumbufu unaochangia baadhi ya wanandoa kutoaminiana.

Alisema ni vyema tatizo hilo likazingatiwa hasa kipindi hichi ambacho Kampuni hiyo kwa hapa Zanzibar tayari imeshaingia katika matumizi ya mtandao unaokwenda kwa kasi wa 4G.

Mapema Meneja Mkuu wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel Tanzania Bwana Benoit Janin alisema Uongozi wa Kampuni hiyo umekusudia kuimarisha zaidi huduma zake ili kuhakikisha unapatikana mtandao wa kasi utakaorahisisha ukuaji wa teknolojia hapa Zanzibar.

Bwana Benoit alisema tokea Kampuni ya Millicon iliponunua asilimia 85 ya hisa za Kampuni hiyo kutoka Kampuni ya Etisalat, Zantel imejikita katika safari mpya ya uwekezaji mkubwa katika kupanua na kuboresha mtandao na huduma kwa watumiaji wa mtandao huo.

Alisema matumizi ya teknolojia hiyo mpya ya mtandao wenye kasi zaidi wa G Nne { 4G } utasaidia watumiaji kupata huduma zenye  ubora na uhakika pamoja na kuwepo kwa ongezeko la kasi la matumizi ya mtandao kama vile huduma za skype, You Tube na mitandao mengine ya Kijamii.

“ Kampuni ya simu ya Zantel mara zote imekuwa ya kwanza kuleta ubunifu mpya kwa Wananchi wa Zanzibar, na kwa uzinduzi wa huduma hii ya 4G inadhihirisha dhamira yake ya kuendelea kutoa huduma bora na za kipekee kwa wakaazi wa Zanzibar ”. Alisema Bwana Benoit Janin.

Meneja Mkuu huyo wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel alieleza kwamba sambamba na uzinduzi wa huduma ya G4 Zantel imefanikiwa kupanua wigo wa mtanado wake kwa upande wa Tanzania Bara na kuwapa fursa wateja wake wa Zanzibar kutumia huduma hiyo katika mkoa wowote wa Bara.

Alisema upanuzi huo utaendelezwa zaidi  kwa lengo la kuwafaidisha hata wananchi wa vijiji vya mbali ili wafaidike na kufurahia huduma za teknolojia hiyo inayokwenda kwa kasi Duniani.

Alifahamisha kwamba Mteja anayejiunga na Mtandao wa 4G kupitia hata simu yake ya mkononi unamuwezesha kupokea au kupeleka taarifa kwa kasi zaidi, kuunganishwa na mtandao wa Internet, wanaowasiliana kuonana { Video call au skype }, kuona michezo ya sinema na Video pamoja na huduma ya TV.

Uzinduzi huo wa Mtandao wa 4G ulishuhudiwa pia na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Balozi Ali Abeid Aman Karume watendaji wa Wizara hiyo pamoja na Waziri wa Afya Mh. Mahmoud Thabit Kombo.

Msanii wa Bongo Flavour Banabas aliimba wimbo maalum wa uzinduzi huo ambapo wateja pamoja na baadhi ya watu walioshuhudia hafla hiyo walipata muda wa kujimwaga kwenye ukumbi maalum ndani ya Banda lililojengwa kwa shughuli hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.