Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Makamo wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Korea Kusini "KOICA GLOBAL" Bw.Kwon Taemyon akiwa na ujumbe wake walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo pamoja na mwenyeji wa Ujumbe huo Waziri wa Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi Mhe,Hamad Rashid Mohamed(hayupo pichani),[Picha na Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Makamo wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Korea Kusini "KOICA GLOBAL" Bw.Kwon Taemyon akiwa na ujumbe wake walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo pamoja na mwenyeji wa Ujumbe huo Waziri wa Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi Mhe,Hamad Rashid Mohamed(hayupo pichani),[Picha na Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akizungumza na Makamo wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Korea Kusini "KOICA GLOBAL" Bw.Kwon Taemyon (wa pili kushoto) akiwa na ujumbe wake walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo pamoja na mwenyeji wa Ujumbe huo Waziri wa Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi Mhe,Hamad Rashid Mohamed(wa pili kulia) akiwepo Katibu Mkuu Kiongozi Dkt.Abdulhamid Yahya Mzee(kulia),[Picha na Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akiagana na Makamo wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Korea Kusini "KOICA GLOBAL" Bw.Kwon Taemyon baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar leo (katikati) Waziri wa Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi Mhe,Hamad Rashid Mohamed,[Picha na Ikulu.]
STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 14.4.2016
JAMHURI ya Korea Kusini imeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali
mbali ya maendeleo kwa kutambua juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wake.
Akizungumza na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Makamo wa Rais wa Shirika
la Maendeleo la Korea ya Kusini (KOICA), Bwana Kwon Taemyon aliyasema hayo leo
huko Ikulu Mjini Zanzibar akiwa ameambatana na ujumbe wake kutoka Shirika hilo.
Katika mazungumzo hayo viongozi hao
walitumia fursa hiyo kuzungumza na kutilia mkazo juu ya ushirikiano wa muda
mrefu uliopo kati ya Korea ya Kusini na Tanzania ikiwemo Zanzibar na viongozi wote
hao kwa pamoja waliahidi kuuimarisha uhusiano na ushirikiano huo.
Bwana Taemyon alimueleza Dk. Shein kuwa Jamhuri
ya Korea inathamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar na
itaendelea kuiunga mkono katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo
miradi ya kilimo, ufugaji, uvuvi, mifugo pamoja na sekta nyenginezo iliyopo
sambamba na kuanzisha miradi mengine mipya hapa Zanzibar.
Makamo huyo wa Rais wa Shirika hilo la
Maendeleo la (KOICA), alisema kuwa miongoni mwa nchi katika bara la Afrika
ambazo nchi hiyo imeziwekea kipaumbele katika kuimarisha miradi ya maendeleo na
kuanzisha miradi mengine mipya ni Tanzania ambapo na Zanzibar nayo itafaidika
kwa kiasi kikubwa katika kipaumbele hicho.
Aidha, katika mazungumzo hayo Makamu huyo
wa Rais wa (KOICA) alimueleza Dk. Shein azma ya Shirika hilo la kusaidia mradi
mkubwa wa ufugaji wa samaki ambao utawasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi ikiwa
ni pamoja na kutoa elimu pamoja na kusaidia nyenzo nyengine muhimu za ufugaji
huo hatua ambayo itaongeza soko la ajira
sambamba na kipato kwa wananchi na Taifa kwa jumla.
Kiongozi huyo alimuhakikishia Dk. Shein
kuwa Serikali ya nchi yake pamoja na wananchi wa nchi hiyo wako Tayari
kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na watu wake.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa upande wake alitoa shukurani na
pongezi kwa Serikali ya Korea ya Kusini kwa mashirikiano makubwa sambamba na
kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi yake mbali mbali ya
maendeleo.
Dk. Shein alisema kuwa pande mbili hizo
zina historia kubwa katika mashirikiano na uhusiano wake hatua ambayo imeweza
kusaidia na kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo kilimo, ufugaji
wa wanyama, uvuvi, mazingira na ufugaji wa samaki, elimu pamoja na sekta
nyenginezo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliipongeza Jamhuri
ya Korea kwa kusaida miradi kadhaa ukiwemo mradi mkubwa wa kilimo cha
umwagiliaji maji na kuimarisha eneo la hekta 2,105 za miundombinu ya
umwagiliaji maji katika mabonde ya Cheju, Kilombero na Chaani kwa Unguja na
Mlemele na Makwararani kwa Pemba, hatua
itakayosaidia katika kupambana na umasikini na kukuza uchumi hapa nchini.
Aidha, Dk. Shein alieleza juhudi za
makusudi zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kuimarisha kilimo cha
umwagiliaji maji ambacho mafanikio yake yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika
kuharakisha ukuaji uchumi wa Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein
hakuchelea kumueleza Makamo huyo wa Rais wa (KOICA) azma ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uvuvi wa bahari kuu ambapo juhudi
maalum zimekuwa zikichukuliwa katika kutafuta wawekezaji na tayari wapo
walioonesha nia ya kuekeza huku akipongeza azma ya (KOICA) ya kuanzisha mradi
mkubwa wa ufugaji samaki hapa Zanzibar.
Sambamba na hilo Dk. Shein alimueleza
kiongozi huyo azma ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya kuaanzisha viwanda vya uvuvi hatua ambayo itasaidia
kwa kiasi kikubwa kuinua kipato cha wananchi pamoja na kukuza pato la taifa.
Dk. Shein alilipongeza Shirika hilo
katika juhudi zake za kuunga mkono
kilimo hicho cha umwagiliaji maji hapa Zanzibar ambapo lengo kubwa la
Serikali ni kuhakikisha kiwango cha uagiziaji wa mchele kutoka nje ya nchi
kinapungua kwa kuzalisha nusu ya mchele unaoagiziwa kutoka nje kuazia mwaka
2018 hadi 2019.
Ujumbe huo wa Makamu wa Rais wa Shirika
la Maendeleo la Korea Kusini (KOICA) uliofika Ikulu kufanya mazungumzo na Rais
pia, uliongozana na Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mhe. Hamad Rashid
Mohammed pamoja na viongozi wa Wizara hiyo.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment