Habari za Punde

Filamu za Bi Kidude kuoneshwa kumbukumbu ya kifo chake

Na Salum Vuai, MAELEZO
14/04/2016
KATIKA kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa tatu tangu kufariki kwa msanii mkongwe aliyeitangaza sana Zanzibar duniani Fatma Baraka ‘Bi. Kidude’, filamu mbili zinazohusu maisha na kifo chake zitaoneshwa mjini Zanzibar.

Mohammed Bajbeir, mmiliki na Mkurugenzi wa ukumbi wa sinema uliopo mjini Zanzibar, ZANCINEMA, amewaambia waandishi wa habari jana, kwamba maonesho ya filamu hizo yanalenga kuwapa fursa Wazanzibari na wageni, kumjua kwa undani nyakanga huyo wa sanaa ya uimbaji na unyago.

Marehemu Bi. Kidude, alifariki dunia Aprili 17, 2013 baada ya kuugua maradhi ya kisukari yaliyochangiwa na umri mkubwa, na kuzikwa kijijini kwao Kwambani katika mazishi yaliyoweka rekodi miongoni mwa wasanii kwa kuhudhuriwa na watu wengi wakiwemo viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Bajbeir amezitaja filamu hizo kuwa ni ‘As old as my tongue’ inayoelezea kwa urefu maisha ya msanii huyo katika tasnia ya muziki, pamoja na ‘I shot Bi. Kidude’ (Kifo cha Bi. Kidude), ambayo inaelezea kuumwa kwake hadi pumzi zake za mwisho.

Filamu hizo zimeandaliwa na kutengenezwa na Andy Jones, raia wa Uingereza, ambaye alikuwa akimsoma na kumfuatilia marehemu Bi, Kidude kwa miaka kadhaa hadi akamudu kuandika filamu hizo zinazogusa mtima wa kila anayeziangalia.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa ZANCINEMA ulioko Funguni mjini Zanzibar kuelekea siku ya kumbukumbu ya Bi, Kidude, Jones alisema Wazanzibari wana kila sababu ya kumuenzi gwiji huyo wa sanaa ambaye amefanya kazi kubwa kuitangaza nchi yake ulimweguni, kisanii na kiutamaduni.

Aidha, alieleza kwamba, kwa namna Bi. Kidude alivyokuwa mtu wa watu wa kila rika, mcheshi, na mwenye imani asiyeangalia kipato, anastahili kukumbukwa kwa namna ya pekee.   

“Wapo watu wa mataifa ya nje ambao hawakuwa wakimfahamu, lakini waliposikia kazi zake, walisafiri hadi Zanzibar kwa ajili ya kumjua na kumshuhudia jukwaani akionesha uwezo wake,” alisema Muingereza huyo.

Alifahamisha kuwa tayari filamu hizo zimeshaoneshwa katika nchi mbalimbali duniani, lakini maonesho ya Zanzibar yatakuwa ya kipekee.

Aidha, alisema zimewahi kuoneshwa katika matamasha ya Zanzibar, Sauti za Busara na lile la filamu (ZIFF), ambapo watu wengi walivutiwa nazo.

Andy Jones, alifika Zanzibar kwa mara ya kwanza mwaka 2000, na kuendelea kuja kila mwaka hadi 2006 alipokamilisha filamu ya kwanza, ‘As old as my tongue’ kuhusu historia ya Bi. Kidude.

Alieleza kuwa, alitumia pauni 15,000 za Kiingereza (sawa n ash. 51,000,000 kwa thamani ya sasa), kutengeneza filamu ya ‘Kifo cha Bi. Kidude’ (I shot Bi, Kidude), iliyochukua miaka miwili na nusu hadi kukamilika.

Jones alisema, wakati wa uhai wake, marehemu Bi, Kidude alikuwa akilipwa asilimia kumi ya mauzo kila ilipouzwa, na sasa fedha hizo ameamua kuzigawa kwa Akademi ya Muziki wa Nchi za Jahazi (DCMA) ya Zanzibar kwa ajili ya kuwaendeleza wasanii wa kike wanaochipukia.   

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.