Habari za Punde

Ravia ashinda kwa kishindo uchaguzi wa ZFA


Na Mkubwa Shadhil, ZANZIBAR


KAMA ilivyotarajiwa na wadau wengi wa mpira wa miguu hapa Zanzibar, Ravia Idarous Faina ameshinda nafasi ya urais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).

Katika uchaguzi wa chama hicho uliofanyika leo kwenye ukumbi wa uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, Ravia amepata kura 47 na kumbwaga mpinzani wake Salum Bausi Nassor aliyeambulia kura sita, kati ya 53 zilizopigwa.

Aidha, sahibu mkubwa wa Ravia, Ali Mohammed Ali, aliyewania tena nafasi ya Makamu Rais ofisi ya Pemba, naye amereejea tena kukalia kiti hicho baada ya kuvuna kura 46.
Mohammed amemshinda Sued Hamad aliyekuwa akipambana naye, ambaye ameondoka na kura saba.

Ravia Idarous ametetea kiti chake cha Urais Chama cha Soka Zanzibar (ZFA)Nafasi ya Makamu Rais upande wa Unguja, imechukuliwa na Mzee Zam Ali aliyepata kura 37, akiwashinda Mohammed Masoud Rashid na Ali Salum Mkweche walioramba kura 11 na tano mtawalia.

Zam alikuwa Katibu Mkuu wa ZFA Taifa kwa miaka mingi kabla kustaafu kwa mujibu wa sheria za utumishi serikalini, kwa vile anayeshika  nafasi hiyo huteuliwa na Serikali ya Zanzibar akiwa mwajiriwa wake.

Akizungumza na BIN ZUBEIRY ONLINE kutoka kisiwani Pemba, Bausi amesema kwa matokeo hayo ni wazi safari ya Zanzibar kupata maendeleo katika soka, bado ni ndefu na imejaa miiba.

Amefahamisha kuwa, alipogombea nafasi ya urais, alikuwa amesukumwa na hali mbaya katika uongozi ambayo imekisababishia chama hicho migogoro mingi isiyokwisha, hata kushtakiwa mahakamani.

Ameeleza pamoja na wajumbe wa mkutano mkuu kutumia haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka, lakini anaamini uamuzi wa kuwarejesha madarakani viongozi wanye kashfa ya kutafuna fedha za chama, hautasaidia kuleta mabadiliko.

Kwa upande mwengine, Bausi amemlaumu Mrajis wa Vyama vya Michezo Zanzibar Said Malik, kwa kukubali kuhudhuria na kubariki mkutano mkuu huo, huku akijua kwamba viongozi hao wameivuruga ZFA kwa kiasi kikubwa hata kumchosha Rais wa Zanzibar, ambaye mara kwa mara amekuwa akisikitikia hali mbaya ya soka la Zanzibar.

Hata hivyo, amesema baada ya hayo yaliyotokea Gombani, kwa sasa hatajaribu tena kutaka kugombea nafasi yoyote katika chama hicho, akisema tayari waliopo wamejijengea himaya na kuwateka wajumbe wa mkutano mkuu.

Uchaguzi huo umefanyika huku aliyekuwa Makamu Rais (Unguja) Haji Ameir Haji, akiendelea na mapambano nje ya ofisi kuhakikisha uongozi huo uliorejea unang’oka haraka iwezekianavyo.

Itakumbukwa kuwa, Ameir ndiye aliyewashtaki Ravia na Mohammed, pamoja na Katibu Mkuu wa ZFA Kassim Haji Salum mwaka 2014, kwa madai ya ufisadi wa fedha za chama pamoja na kukiuka katiba.

Jitihada za BIN ZUBEIRY ONLINE kumpata Ameir ili atoe maoni yake juu ya uchaguzi huo, hazikufanikiwa kwa siku ya leo, kwani kila alipogiwa simu, ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.