Habari za Punde

Ufunguzi wa Kongamano la Kibiashara la Urusi na Tanzania katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Dar es salaam.

 Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Tanzania Mh. Charles Mwijage kulia amkimshindikiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuingia katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Mjini Dar es salaam kufungua Kongamano la Biasharfa kati ya Tanzania na Shirikisho la Urusi.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Kongamano la Kimataifa baina ya Shirikisho la Urusi na Tanzania lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere Jijini Dar es salaam.
  Waziri wa Viwanda na Biashara wa Shirikisho la Urusi Bwana Denis Manlurov akielezea nia ya Wafanyabiashara wa Urusi wanavyoshawishika kutaka kuwekeza miradi yao Nchini Tanzania kwenye Kongamano la Urusi na Tanzania.
  Baadhi ya Wafanyabiashara wa Shirikisho la Urusi na wale wa Tanzania wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi Balozi Seif hayupo pichani wakati akilifungua Kongamno la Biashara vkati ya Pande hizo mbili.
  Baadhi ya Wafanyabiashara wa Shirikisho la Urusi na wale wa Tanzania wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi Balozi
Seif hayupo pichani wakati akilifungua Kongamno la Biashara vkati ya Pande hizo mbili.
 Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wakuu wa Kongamano la Biashara kati ya Urusi na Tanzania mara baada ya kulifungua rasmi.

Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Vianda na Biashara wa Urusi Bwana Denis Manlurov na kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Biashara,Viwanda na Uwekezaji wa Tanzania Mh. Charles Mwijage, Waziri wa Biashara wa Zanzibar Balozi Amina Salim Ali na Mwenyekiti wa IPP Dr. Reginal Mengi.
  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akifafanuja jambo mbele ya Wana Habari mara baada ya kulifungua Kongamano la Kimataifa la Biashara kati ya Tanzania na Urusi.

 Mwenyekiti wa IPP Dr. Reginal Mengi kulia akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzikbar Balozi
Seif mara baada ya ufunguzi wa Kongamano la Kibiashara la Urusi na Tanzania katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Dar es salaam.

Picha na – OMPR – ZNZ.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Shirikisho la Urusi kulitumia soko la Kiuchumi liliopo Tanzania katika kuwekeza miradi yao
ya Kiuchumi itakayosaidia kuimarisha zaidi uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Nchi mbili hizo rafiki.



Alisema kutokana na mabadiliko ya mfumo wa dunia uliojikita zaidi katika masuala ya Teknolojia ya Kisasa  uhusiano wa Tanzania na Shirikisho hilo unastahiki kwa sasa kuelekezwa zaidi katika Nyanja za uwekezaji badala ya Siasa na utamaduni.



Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akilifungua Kongamano la Kibiashara kati ya Shirikisho la Urusi na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius K. Nyerere Jijini Dar es salaam.



Alisema Tanzania hivi sasa imebahatika kuwa kituo maarufu katika kuimarisha Biashara, Uchumi na uwekezaji ndani ya Mwambao wa Afrika Mashariki na eneo la Ukanda wa Nchi za Sahara fursa ambayo inaweza kutumiwa  vyema na wawekezaji wa Shirikisho la Urusi ambao Taifa lao tayari limeshapiga hatua kubwa ya maendeleo katika sekta za Nishati,madini, mafuta pamoja na anga.



Balozi Seif alisema katika kuendelea kuimarisha uhusiano wa pande hizo mbili Watanzania watafarajika kuona wawekezaji wa Shirikisho hilo wanatumia fursa ya kuanzisha miradi yao katika sekta ya Kilimo, nishati, viwanda, usafiri pamoja na utalii.



Alifahamisha kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imeshatenga eneo kubwa la ardhi lenye  zaidi ya Hekta Milioni 43 kwa ajili ya shughuli za uwekezaji  wa sekta ya kilimo cha umwagiliaji.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara hao wa Shirikisho la Urusi waliongozwa na Waziri wao wa Viwanda na Biashara kwa uamuzi wao wa kutembelea Tanzania kuangalia
fursa za uwekezaji.



Alisema uwekezaji wa wafanyabiashara wa Urusi unaweza kufanikiwa kwa kiwango kizuri kwa vile kundi kubwa la wasomi wa Tanzania wamepata taaluma ya Juu Nchini Urusi jambo ambalo wanaweza kutumiwa vyema na
Wafanyabiashara hao katika uanzishwaji wa miradi ya uwekezaji.



Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na uamuzi wa pande hizo mbili kufanya  Kongamano la Biashara Mjini Dar es salaam kitendo ambacho kitaongeza kasi ya ushirikiano kati ya Urusi na Tanzania katika kupanua kasi ya biashara na uwekezaji.



Akizungumzia sekta ya Utalii inayoonekana kuongoza katika uchumi wa Dunia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Tanzania imebahatika kuwa na vivutio vingi vya utalii vinavyoweza kuwashawishi watalii wa
Urusi wakaamua kuitembelea Tanzania.



Yapo maeneo ya Kihistoria hasa Zanzibar, Misitu  pamoja na hifadhi za Taifa zenye wanyama tofauti zinazoweza kutumiwa katika masuala ya uwekezaji ambapo wafanyabiashara wa Nchi hiyo wanakaribishwa kuwekeza
kwenye eneo hilo muhimu.



Balozi Seif aliwahakikishia wawekezaji hao kutoka Urusi kwamba Tanzania bado salama yenye utulivu na amani unaoweza kuwaletea tija na mafanikio wataoamua kuanzisha miradi yao.



Mapema Waziri wa Viwanda na Biashara wa Shirikisho la Urusi Bwana Denis Manlurov alisema Tanzania na Urusi zina uhusiano wa Kihistoria wa muda mrefu uliojengeka katika uimarishaji wa Taaluma katika sekta tofauti.



Bwana Denis alisema uhusiano huo ulitoa fursa kwa Watanzania wengi waliomaliza masomo yao ya sekondari kupendelea kuongeza elimu yao ya juu katika vyuo mbali mbali vikuu vya Urusi.



Waziri huyo wa Shirikisho la Urusi aliwahakikishia Watanzania kwamba Nchi yake kupitia Makongamano  yanayoandaliwa kila Mwaka baina ya Urusi na Mataifa ya Bara la Afrika {Russian – African Forum } itaendelea kuunga mkono Nchi za Afrika katika harakati zake za kujinasua na ukali wa maisha hasa kwa wananchi wao wa kipato cha chini.



Akitoa salamu katika Kongamano hilo la  Kibiashara kati ya Shirikisho la Urusi na Mwenyekiti wa IPP  Dr. Reginal Mengi alisema Watanzania  wana fursa ya kuingia ubia na Wawekezaji wa Urusi katika sekta za
Madini, Nishati, Kilimo, Utalii na hata Anga maeneo ambayo bado yana rasilmali ya kutosha.



Dr. Mengi alisema ubia huo ambao umekuwa ukitangazwa mwa muda mrefu katika azma ya kuimarisha uchumi wa Taifa utasaidia kuongeza pato la Serikali na Wananchi sambamba na kuongeza fursa za ajira.



Mwenyekiti huyo wa IPP alielezea matumaini yake kwamba Tanzania inatarajia kuwa ya Viwanda ili kuingia vyema katika uchumi wa kati kati ifikapo mwaka 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.